KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 10, 2014

BUSHIRI KOCHA BORA LIGI KUU ZANZIBAR

Makamu Mwenyekiti wa BMZ Khamis Said, kushoto akimkabidhi Cheki ya shilingi milioni moja Kocha Bora wa Ligi Kuu ya Grand Malt, Ali Bushiri wa Timu ya KMKM.

DRFA YAOMBOLEZA KIFO CHA JIMMY MHANGO


CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kimetuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Mjumbe wa Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi, Jimmy Mhango aliyefariki juzi katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam kutokana na presha.


Katibu Mkuu wa DRFA, Msanifu Kondo amesema leo (Oktoba 22) kwamba wamepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mjumbe huyo, ambaye pia aliwahi kuwa mchezaji mahiri katika timu ya Ushirika ya Moshi katika miaka ya tisini chini ya Kocha Dan Korosso.

Marehemu pia aliwahi kuzichezea timu za Pan Africans ya Dar es Salaa pamoja na timu ya Mkoa wa Kilimanjaro ‘Kilimanjaro Stars.

“DRFA imepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Jimmy Mhango na inatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na wanafamilia wote wa mpira wa miguu, tunawaomba wawe na subira katika kipindi hiki kigumu,” alisema.

Kamati ya Nidhamu na Usuluhishi ya DRFA ambayo marehemu alikuwa mjumbe, inaongozwa na Roman Masumbuko (Mwenyekiti), Fahadi Kayuga (Makamu Mwenyekiti), Mohamed Mpili (Mjumbe) na Peter Nkwera (Mjumbe).

Marehemu anatarajiwa kuzikwa leo (Jumanne)katika makaburi ya Ilala Mchikichini, Dar es Salaam saa kumi jioni. Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema

Imetolewa na Mohamed Mharizo
Ofisa Habari
Chama Cha Mpira Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA)
Oktoba 22, 2013

TWANGA PEPETA YAINGIA MKATABA NA PRAIN PROMOTIONS


BENDI ya muziki wa dansi nchini ya African Stars 'Twanga Pepeta',
wameingia mkataba maalumu na kampuni ya Prain Promotions
Limited kwa ajili ya utengenezaji wa kazi zao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Mkurugenzi wa Twanga Pepeta, Asha Baraka, alisema mkataba
huo una manufaa kwa bendi hiyo kutokana na kutaka
kuwanufaisha wanamuziki na wasanii wa nchini kwa ujumla.

Baraka alisema kampuni hiyo ambayo awali ilikuwa
ikijishughulisha na usambazaji wa kazi za filamu, imeamua kuingia
mkataba na bendi yake kutokana na ubora wao.

Alisema wasanii nchini wanatakiwa kunufaika na kazi
wanayoifanya, na Prain wameihakikishia Twanga kuwa kazi zao
sasa zimetengenezwa kwa ubora wa hali ya juu kiasi cha
kumshinda mtu yeyote kuirudufu.

"Tunataka maendeleo ya wasanii, tumekuwa tukiwakumbatia
zaidi wasanii wa nje, lakini muunganiko wetu sasa utasaidia kuinua
hali ya kipato sahihi kwa wanamuziki tulionao," alisema Baraka.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Prain Promotions, Evance
Steven, alisema kampuni yao imeamua kuingia kwenye muziki na
kuichagua Twanga Pepeta kuwa bendi ya kwanza kutokana na
kazi yao wanayofanya katika burudani.

Steven alisema kazi kubwa waliyoanza nayo katika albamu ya
Twanga Pepeta ya Dunia Daraja ni kuhakikisha kuwa haiwezi
kunakiliwa (kurudufiwa) upya na maharamia wa kazi za kisanii
nchini kama ilivyozoeleka.

"Tumewahakikishia wenzetu wa Twanga Pepeta kuwa kazi zao
sasa ziko salama kuuzwa kihalali kutokana na kuziwekea programu
maalumu ya kushindwa kunakilika, hivyo kila mtu atanunua
kihalali kazi za bendi hii za Dunia Daraja," alisema ofisa huyo.

Twanga itaanza kuuza kazi hizo katika kila maonesho yao huku
zikionekana kufungwa katika ubora wa hali ya juu alipokuwa
akiwaonesha waandishi wa habari utofauti mkubwa uliofanywa
na Prain, ambapo pia zina stika maalumu za TRA (Mamlaka ya
Mapato Tanzania).

Wednesday, April 9, 2014

TFF YAWAPONGEZA MSHUJAA WA BRAZIL





Tunaipongeza timu ya Tanzania ya Watoto wa Mitaani kwa kutwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani baada ya jana (Aprili 6 mwaka huu) kuifunga Burundi mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Ushindi kwa timu hiyo ni fahari kwa Tanzania, lakini kubwa ni kwa kituo cha Mwanza ambacho ndicho kinachoiendesha pamoja na wadhamini na wafadhili walioiwezesha kushiriki fainali hizo kwa mara ya pili mfululizi.

Vilevile ushindi huo unatoa changamoto kubwa kwa wadau wa mpira wa miguu kuwa watoto wa mitaani ni sehemu tu ya vipaji vilivyotapaa nchini, hivyo iliyopo ni kuvisaka na kuvibaini vipaji hivyo kwa ajili ya ustawi wa mchezo huo nchini.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) tutaendelea kushirikiana na kituo hicho cha Mwanza, na vingine vyote ambavyo vinajishughulisha na mchezo huu, lengo likiwa ni kuundeleza na hata kutoa ajira kwa vijana hapo baadaye kupitia mpira wa miguu.

Timu hiyo inarejea nchini Alhamisi (Aprili 10 mwaka huu) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 jioni kwa ndege ya Emirates

NGORONGORO HEROES KUINGIA KAMBINI LEO


Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngongoro Heroes) imereja nchini leo mchana (Aprili 7 mwaka huu) kutoka Kenya mechi ya michuano ya Afrika dhidi ya wenyewe, na itaingia kambini Alhamisi.


Ngorongoro Heroes ambayo imewasili saa 8.25 kwa ndege ya Kenya Airways ilitoka suluhu na Kenya katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kanyetta uliopo katika mji wa Machakos.

Kocha John Simkoko amesema benchi lake la ufundi linafanyika kazi upunguzi uliojitokeza ili wafanye vizuri kwenye mechi ya marudiano itakayochezwa Aprili 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Iwapo Ngorongoro Heroes itaitoa Kenya, raundi inayofuata itacheza na Afrika Kusini. Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 zitafanyika mwakani nchini Senegal.

Monday, April 7, 2014

NGORONGORO HEROES KUREJEA LEO


Timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngongoro Heroes) inarejea nchini leo (Aprili 7 mwaka huu) kutoka Kenya ambapo jana (Aprili 6 mwaka huu) ilicheza mechi ya michuano ya Afrika.

Ngorongoro Heroes ambayo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 8.25 mchana kwa ndege ya Kenya Airways ilitoka suluhu na wenye Kenya katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kanyetta uliopo mji wa Machakos.

Timu hizo zitarudiana jijini Dar es Salaam wiki tatu baadaye ambapo itakayofuzu itacheza raundi ya pili dhidi ya Afrika Kusini. Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 20 zitachezwa mwakani nchini Senegal.

WATOTO WA MITAANI WA TANZANIA WATWAA UBINGWA WA DUNIA



Timu ya Taifa ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imetwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani baada ya jana (Aprili 6 mwaka huu) kuilaza Burundi mabao 3-1 katika mchezo wa fainali uliochezwa jijini Rio de Janeiro, Brazil.

Mshambuliaji Frank William alifunga mabao matatu katika mechi hiyo iliyochezwa uwanja mkongwe na maarufu wa klabu ya Fluminense huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Fedha wa Uingereza, George Osborne.

Tanzania ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuitandika Marekani mabao 6-1 ambapo hadi mapumziko ilikuwa mbele kwa mabao 4-0.

Burundi ilipata tiketi ya kucheza fainali baada ya kuifunga Pakistan mabao 4-3 katika mechi ya nusu fainali ya pili.

Timu ya Tanzania inarejea nchini Alhamisi (Aprili 10 mwaka huu) ambapo itatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) saa 10 jioni kwa ndege ya Emirates


Tanzania boys win 2014 Street Child World Cup

Tanzania boys won the 2014 Street Child World Cup producing a powerful performance to beat their neighbours Burundi 3-1. After the game both teams joined together to stress that the Street Child World Cup was more than just a game, and to congratulate the players from all teams at the tournament.


Tanzania and Burundi had already faced each other in the 2014 Street Child World Cup in the opening fixture of the group stages. Tanzania had looked on course for an impressive opening victory, taking a two-goal lead, only for Burundi to demonstrate their remarkable resilience to mount a second half comeback and get a draw.

So when Tanzania were 2-0 up at half time in the final they were very aware that the game was far from over. But instead of letting Burundi back into the game, this time Tanzania scored the first goal of the second half, completing a hat-trick for Frank, to put the game out of Burundi’s reach. Although Burundi got a consolation goal, it was too late to change the outcome of the game.

In the first half despite having the better of the opening exchanges Burundi failed to get a shot on target. Burundi moved the ball around with familiarly impressive passing, but failed to test the Tanzania keeper. Then after seven minutes a clever sidestep by Frank left him in space and he fired home into the top corner. The goal against the run of play began a passage of end-to-end action, which only ended when Frank bagged his second goal from a tight angle.

After the game the Tanzania team were quick to congratulate the Burundi team for their performance, and Tanzania captain Deograutis said it was a demonstration of the bonds developed between squads throughout the Street Child World Cup: “We are friends and neighbours with the Burundi team, and know what it is like to lose the final, so we wanted to show them our support.

“We’re happy because in 2010 we were in the final but didn’t win the cup. We’re representing all the children in Tanzania, and we hope we’ve made them proud.”

Team Tanzania is organised by Tanzania Street Children Sports Academy which works with around 300 street children. TSCSA works in three areas; outreach through street-based work, using sport as an educational tool through work in schools and running a football academy.

TSCSA President Altaf Hirani thinks all the Street Champions have demonstrated their talents and exuberance throughout the tournament: “These children have shown what they can do if they are given opportunities and the chance to flourish. The Street Child World Cup has been a great way to raise awareness of the global campaign to protect children. We would like to thank the organisers and the volunteers, who have been fantastic right from the start.”

Tanzania coach Suleiman Jabir added that TSCSA hope winning the Street Child World Cup will be a vehicle to increasing their deliver of support to children: “We hope we can use this as a stepping stone, to help more children in Tanzania and to campaign to the government to pass policies to support children. But this isn’t just about Tanzania, this is about children everywhere.”

Team Burundi is organised by New Generation, which is fostering relations between boys from different ethnic backgrounds in a country scarred by civil war. The players are former street children, who New Generation are working to get back into the community and education.

Burundi coach Teddy Bright thinks his team demonstrated the values New Generation tries to foster in its players: “It’s important to play together, to know each other as friends and trust each other. We’re really happy to be at this event to raise awareness for street children, not just in Burundi but all over the world.”

Sunday, April 6, 2014

WATOTO WA MITAANI WATINGA FAINALI BRAZIL


Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania imefanikiwa kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Dunia yanayofanyika Rio de Janeiro nchini Brazil baada ya jana kuifunga Indonesia kwa jumla ya mabao 5-3.

Hadi muda wa kawaida wa mchezo huo unamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2 ndipo ikatumia mikwaju ya penalti kuamua mshindi. Tanzania ilipata penalti tatu dhidi ya moja ya wapinzani wao.

Kwa matokeo hayo, Tanzania sasa itacheza mechi ya nusu fainali leo dhidi ya Marekani ili kupata timu zitakazocheza mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu. Mechi za fainali na kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa kesho (Aprili 6 mwaka huu).

Timu nyingine zilizoingia nusu fainali na mechi zake zinachezwa leo (Aprili 5 mwaka huu) ni Burundi itakayocheza na Pakistan.

Katika mechi zilizopita, Tanzania ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi, ikaitandika Argentina mabao 3-0 ikailaza Nicaragua mabao 2-0 na ikafungwa na Philippines mabao 2-0.

TAIFA STARS, BURUNDI KUCHEZA APRILI 26



Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) itacheza mechi ya kirafiki na Burundi (Intamba Mu Rugamba) Aprili 26 mwaka huu ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager tayari ipo kambini Tukuyu mkoani Mbeya ikijiandaa kwa ajili ya mechi hiyo ikiwa na wachezaji waliopatikana katika programu maalumu ya kusaka vipaji.

Baadaye wachezaji wengine wa Taifa Stars ambao wapo nje ya programu ya kusaka vipaji wataungana na wenzao kabla ya kutengeneza kikosi cha mwisho kitakachoivaa Burundi.
Mechi hiyo itakayofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachezeshwa na waamuzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kutoka nchini Kenya.

21 KUCHEZA RCL


Timu 21 kati ya 27 zitakazocheza Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kutafuta tiketi ya kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao tayari zimejulikana.

Timu hizo ni Abajalo SC (Dar es Salaam), AFC (Arusha), African Sports (Tanga), Bulyanhulu FC (Shinyanga), Geita Veterans (Geita), JKT Mafinga (Iringa), JKT Rwamukoma (Mara), Kariakoo SC (Lindi), Kiluvya United (Pwani), Milambo SC (Tabora) na Mshikamano FC (Dar es Salaam).

Nyingine ni Mvuvumwa FC (Kigoma), Navy SC (Dar es Salaam), Njombe Mji (Njombe), Pachoto Shooting Stars (Mtwara), Panone FC (Kilimanjaro), Singida United (Singida), Tanzanite (Manyara), Town Small Boys (Ruvuma), Ujenzi FC (Rukwa) na Volcano (Morogoro).

WATANO WAFANYA MTIHANI WA UWAKALA WA WACHEZAJI
Watanzania watano wamefanya mtihani wa uwakala wa wachezaji wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao ulifanyika jana (Aprili 3 mwaka huu) duniani kote.

Watahiniwa katika mtihani huo ambao ulikuwa na maswali kutoka FIFA na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) walikuwa Godlisten Anderson, Jesse Koka, Lutfi Binkleb, Rwechungura Mutahaba na Silla Yalonde.

NAVY SC, ABAJALO, MSHIKAMANO KUIWAKILISHA DAR LIGI YA MABINGWA WA MIKOA


CHAMA Cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), kimetangaza timu tatu zilizofanikiwa kucheza Ligi ya Mabingwa wa Mikoa baada ya kufanya vizuri katika Ligi Daraja la Pili Mkoa wa Dar es Salaam iliyomalizika Jumapili iliyopita.

Ofisa Habari wa DRFA Mohamed Mharizo amesema timu hizo ni Navy SC ya Temeke iliyokua vinara baada ya kujizolea pointi 34 ikifuatiwa na Abajalo ya Sinza iliyojikusanyia pointi 31 na Mshikamano ya Temeke iliyokua na pointi 30.

“Ligi yetu naweza kusema ilikua bora nay a ushindani kwa sababu tulianza raundi ya kwanza tukiwa na timu 32 na baadae zikabaki timu 16 ambazo katika hizo tatu ndio zimefanikiwa kuwakilisha mkoa wetu wa Dar es Salaam katika Ligi ya Mabingwa wa mikoa inayotarajia kuanza Aprili 20 mwaka huu.

“Kwa niaba ya uongozi wa DRFA, tunazipongeza timu hizi na tunaamini kwa dhati kabisa kuwa zitatuwakilisha vyema katika Ligi ya Mabingwa wa mikoa na hatimaye kufuzu kucheza Ligi Daraja la Kwanza,” alisema Mharizo.

Imetolewa Aprili 4, 2014
Mohamed Mharizo
Ofisa Habari
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).

Thursday, April 3, 2014

KOCHA AZAM ATAMBA UBINGWA NI WAO



KOCHA Mkuu wa Azam FC, Joseph Marius Omog amewataka wachezaji wake kutobweteka kwa ushindi wa jana dhidi ya Simba SC, kwani vita ya ubingwa bado ni kali na Mbeya City na Yanga SC nao pia wote wana nafasi ya kubeba taji.

Azam FC jana iliifunga Simba SC mabao 2-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kufikisha pointi 53 baada ya kucheza mechi 23 mbele ya Yanga SC yenye pointi 46 za mechi 22 na Mbeya City yenye pointi 45 za mechi 23.

Omog ambaye ni raia wa Cameroon amewataka wachezaji wake kuendelea kupambana kuhakikisha wanashinda mechi zote zilizosalia kama wanataka kusherehekea ubingwa. “Hakuna mechi nyepesi katika hatua hizi, hata timu inayotaka kushuka daraja inaweza kukufunga, lazima tutilie mkazo mechi zote,”alisema Omog.

Kocha huyo wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon amewapongeza wachezaji wake kwa ushindi wa jana katika mchezo mgumu na akawataka sasa kuhamishia fikra zao katika mchezo ujao dhidi ya Ruvu Shooting Aprili 6, Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.

Ikitoka Mlandizi, Azam FC itakwenda Mbeya kucheza na Mbeya City Aprili 13 Uwanja wa Sokoine kabla ya kumalizia Ligi Kuu msimu huu kwa kumenyana na JKT Ruvu Aprili 19, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

YANGA YAKANA KUWATIMUA KASEJA, CHUJI NA YONDANI



Young Africans itashuka dimbani siku ya jumapili kucheza na JKT Ruvu katika muendelezo wa michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara mzunguko wa pili raundi ya 23 mchezo utakaofanyika katika dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.


Ligi Kuu ya Vodacom inaelekea ukingoni na sasa kila timu ikijitahid kufanya vizuri ili kuweza kujiweka katika mazingira mazuri aidha ya kubakia Ligi Kuu, kupata Ubingwa au kujinusuru kutoshuka daraja.

Young Africans yenye pointi 46 imebakisha michezo minne ambapo ikiweza kushinda yote itafikisha pointi 58 ambazo zinaweza kupitwa na vinara wa Ligi Kuu ya Vodacom Azam FC peke kama itashinda michezo yake yote miatatu iliyosalia.

Baada ya kupoteza mchezo wake dhidi ya Mgambo JKT mwishoni mwa wiki jijini Tanga, Kikosi cha mhoalanzi Hans Van der Pluijm kimeingia kambini jana jioni katika Hoteli ya Kiromo huku kikiendelea kufanya mazoezi katika Uwanja wa Boko Beach Veterani.

Mlinda mlango Deoragtias Munish "Dida" aliyekua majeruhi kwa takribani wiki mbili kwa sasa ameshapona majeraha aliyokuanayo na ameungana na wenzake kambini tayari kwa maandalizi ya mchezo huo wa siku ya jumapili.

Katika mchezo wa awali wa mzunguko wa kwanza timu hizi zilipokutana, Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 4-0

Aidha taarifa zinazosambazwa na baadhi ya vyombo vya kawamba wachezaji Athuman Idd, Kelvin Yondani na Juma Kaseja wamesimamishwa kutokana na timu kufungwa mchezo dhidi ya Mgambo JKT hazina ukweli, wachezaji hao hawajafukuzwa na wapo wanaendelea na mazoezi pamoja na wenzao.

Tunaomba vyombo vya habari kuwa wanatoa taarifa za ukweli na sio kupotosha jamii na mwisho wa siku kuwapa usumbufu viongozi kufanya kazi ya kukanusha.

KAPOMBE AANZA KUFANYA MAZOEZI NA AZAM




Mshambuliaji Shomari Kapombe amejiunga rasmi na klabu ya Azam FC na kufanya nayo
mazoezi ili kujiweka fiti kwa wakati huu, ambao hana timu baada ya kugoma kurejea klabu
yake ya Daraja la Nne Ufaransa, AS Cannes.

Tovuti ya Azam FC imemnkukuu Kapombe akisema kwamba ameamua kuja kufanya
Azam FC kwa sababu kwanza ni jirani na eneo analoishi na pia wana vifaa vyote vya vya
mazoezi vitakavyosaidia kumuweka fiti.

Hata hivyo, Kapombe hakutaka kuzama ndani juu ya mustakabali wake wa baadaye,
akisema; “Nimekuja Azam kufanya mazoezi kujiweka fiti tu, basi,”alisema.

Tayari kuna habari kwamba, Kapombe anataka kucheza klabu ya Tanzania ambayo
itashiriki michuano ya Afrika mwakani.

Kiungo huyo anayeweza kucheza nafasi za ulinzi pia, anamaliza Mkataba wake Simba
SC mwezi huu, lakini alikwishaingia Mkataba wa miaka minne na AS Cannes ya
Ufaransa mwaka jana.

Na Simba SC imekubaliana na klabu ya Daraja la Nne Ufaransa, kuununua Mkataba wa
mchezaji huyo arejee kufanya kazi Msimbazi baada ya kushindwa kuendelea kucheza
Ulaya.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alizungumza na
AS Cannes mwezi uliopita na kufikia makubaliano ya kuuziana Mkataba huo, ili
Kapombe arejee Msikmbazi.

Poppe alisema kwamba Simba SC imekubali kuilipa Cannes kiasi cha Euro 33, 000
ambazo sawa na Sh. Milioni 66 ili kurejeshewa mchezaji wake huyo.

Kapombe alitolewa bure kwenda AS Cannes katikati ya mwaka jana akiwa bado ana
Mkataba na klabu hiyo ya Msimbazi, unaomalizika Aprili mwaka huu.

Baada ya kuwa Ufaransa kwa zaidi ya miezi mitatu, Kapombe alirejea nchini Novemba
mwaka jana kwa ruhusa maalum ya kuja kuichezea timu ya taifa katika mchezo wa
kirafiki dhidi ya Zimbabwe.

Baada ya mchezo huo, mchezaji huyo akaamua kubaki moja kwa moja nyumbani akidai
halipwi mishahara.

IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY

VYAMA KUMI VYA MIKOA VYATUMA WAWAKILISHI WAKE RCL


Vyama kumi vya mpira wa miguu vya mikoa vimewasilisha majina ya mabingwa wao
watakaoshiriki Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL).

Mabingwa hao ni Arusha (AFC), Kilimanjaro (Panone FC), Lindi (Kariakoo SC),
Manyara (Tanzanite SC), Mara (JKT Rwamukoma), Morogoro (Volcano FC), Mtwara
(Pachoto Shooting Stars), Pwani (Kiluvya United), Shinyanga (Bulyanhulu FC), Singida
(Singida United) na Tanga (African Sports).

Mikoa ambayo haijawasilisha mabingwa wake ni Dar es Salaam, Dodoma, Geita, Iringa,
Kagera, Katavi, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Njombe, Rukwa, Ruvuma, Simiyu na
Tabora wakati mikoa ya Dodoma na Mwanza imeomba kuongezewa muda kutokana na
sababu mbalimbali.

Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliagiza kuwa
mikoa yote iwe imemaliza ligi na kuwasilisha jina la bingwa wake Machi 30 mwaka huu.

WACHEZAJI NGORONGORO HEROES WAAHIDI USHINDI



Nahodha wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Aishi Manula amesema wamejipanga kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mechi dhidi ya Kenya itakayochezwa Jumapili (Aprili 6 mwaka huu) katika mji wa Machakos.

Akizungumza leo (Aprili 2 mwaka huu) kwenye hafla ya kukabidhiwa bendera kwa timu hiyo kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Manula ambaye pia anaidakia timu ya Azam alisema lengo lao ni kufanya vizuri kwenye mechi hiyo.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yasoda akikabidhi bendera hiyo, aliwataka wachezaji hao kujituma na kutanguliza uzalendo mbele bila kusahau kuwa mchezo wa mpira wa miguu ni ushirikiano.

Alisema Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji, hivyo waliopata fursa ya kuwemo Ngorongoro Heroes wakati huu wajue kuwa wamepata bahati, na wanatakiwa kufahamu kuwa wao ni wawakilishi wa Tanzania, na Watanzania wana kiu ya kusikia matokeo ya mechi hiyo.

Ngorongoro Heroes inayofundishwa na John Simkoko inaondoka kesho (Aprili 3 mwaka huu) saa 4.30 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways, na mara baada ya kuwasili itakwenda moja kwa moja kwenye hoteli ya Garden iliyopo Machakos ambayo ndiyo imepangiwa kufikia na Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF).

Wachezaji waliopo kwenye msafara huo unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF), Ayoub Nyenzi ni Abrahman Mohamed, Aishi Manula, Ally Idd, Ally Mwale, Athanas Mdamu, Ayoub Semtawa, Bryson Raphael na Edward Manyama.

Wengine ni Gadiel Michael, Hamad Juma, Hassan Mbande, Ibrahim Ahmada, Idd Ally, Kelvin Friday, Michael Mpesa, Mohamed Ibrahim, Mudhathir Yahya, Pato Ngonyani, Peter Manyika na Salum Mineli.

TIMU YA WATOTO WA MTAANI YACHACHAFYA BRAZIL


Timu ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania kutoka Kituo cha Mwanza inaendelea vizuri katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani yanayoendelea Rio de Janeiro nchini Brazil ambapo katika mchezo wake wa kwanza ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi.

Juzi (Machi 31 mwaka huu), timu hiyo inayoongozwa na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutoka Mkoa wa Mwanza, John Kadutu ilicheza mechi mbili. Katika mechi ya kwanza iliifunga Argentina mabao 3-0 na baadaye ikailaza Nicaragua mabao 2-0.

Michuano hiyo ya siku kumi inashirikisha timu kumi. Mbali ya Tanzania, nyingine ni Argentina, Burundi, India, Kenya, Liberia, Marekani, Mauritius, Misri na Pakistan. Kwa wasichana ni Afrika Kusini, Brazil, El Salvador, Indonesia, Msumbiji, Nicaragua, Philippines, Uingereza na Zimbabwe.

Tuesday, April 1, 2014

SIMBA, AZAM ZAINGIZA MIL 26/-


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Azam na Simba iliyochezwa jana (Machi 30 mwaka huu) Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam imeingiza sh. 26,455,000.

Watazamaji 4,741 walikata tiketi kushuhudia pambano hilo ambapo Azam iliibuka na ushindi wa mabao 2-1. Viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 15,000 na sh. 20,000.

Mgawanyo kwa mapato ulikuwa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 4,035,508.47, gharama za kuchapa tiketi sh. 3,908,686 wakati kila klabu ilipata sh. 5,460,687.63.

Uwanja sh. 2,776,620.83, gharama za mechi sh. 1,665,972.50, Bodi ya Ligi sh. 1,665,972.50, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 832,986.25 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 647,878.19.

TFF YATUMA RAMBIRAMBI MSIBA WA DK MZIRAY



SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko kifo cha daktari wa tiba ya michezo, Dk. Hemed Mziray kilichotokea juzi jijini Dar es Salaam.

Dk. Mziray ambaye alikuwa mfanyakazi wa Hospitali ya Manispaa ya Temeke na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Chama cha Tiba ya Michezo Tanzania (TASMA) amesafirishwa kwenda kwao mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.

Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu kwani kwa nyakati tofauti Dk. Mziray ameshirikiana na TFF na wadau wengine wa mpira wa miguu katika masuala ya tiba na uongozi.

Alikuwa kiungo kati ya Uwanja wa Taifa ambapo mechi za kimataifa, za ligi na za kirafiki zimekuwa zikichezwa na Hospitali ya Temeke kwa wagonjwa wanaohitaji huduma zaidi, hivyo mchango wake tutaukumbuka daima.

TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Dk. Mziray, TASMA na wafanyakazi wa Hospitali ya Temeke na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito. Pia TFF inatoa ubani wa sh. 200,000 kwa familia ya marehemu kama rambirambi zake.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Amina

WANACHAMA TFF KUANDALIWA KATIBA ZA MFANO

Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF imekutana Machi 30 mwaka huu kujadili utekelezaji wa maagizo ya TFF kwa wanachama wake kurekebisha Katiba zao ili ziendane na Katiba ya TFF pamoja na ile ya FIFA kabla ya Machi 30 mwaka huu.

Vyama vya mikoa Lindi na Dar es Salaam na Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake (TWFA) viliomba kuongezewa muda wakati vingine vimeomba Katiba mama kama angalizo lao la mabadiliko hayo. Klabu ya Simba Sports ndiye mwanachama pekee aliyewasilisha mabadiliko ya Katiba. TFF inawapongeza viongozi na wanachama wa klabu hiyo kwa kufanya mkutano wao kwa utulivu.

Kamati itatangaza nyongeza ya muda wa kufanya mabadiliko hayo baada ya kuviandalia vyama vya mikoa na vyama shiriki katiba mfano kwa ajili ya kurahisisha shughuli hiyo.

Baada ya kupitia uamuzi wa wanachama wa Simba S.C. Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeamua ifuatavyo:

(i) Kwa kuwa pendekezo la wanachama wa Simba kubadili kipengele na 26 kuhusu sifa za mgombea kinapingana na kipengele na 29 (4) cha Katiba ya TFF, hivyo basi Kamati imeagiza kipengele cha Katiba ya Simba kibaki vilevile bila kubadilishwa.

(ii) Vipengele vingine vyote vimepitishwa na vitapelekwa kwa Msajili wa Klabu na Vyama vya Michezo kwa ajili ya kusajiliwa.

(iii) Mchakato wa uchaguzi wa Klabu ya Simba uendelee kama ulivyopangwa wakizingatia uamuzi huu wa Kamati. TFF inaitakia Klabu ya Simba uchaguzi mwema.

Pia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji imeshauri TFF kuwasiliana na FIFA kupata mwongozo kuhusu katazo la watu wenye rekodi ya kifungo kugombea.

TFF imepokea ushauri huo na itaufanyia kazi na kama kuna mabadiliko yoyote kiutaratibu yataanzia katika Katiba ya TFF kupitia Mkutano Mkuu.