KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, April 30, 2015

BURIANI MUTOMBO LUFUNGULA AUDAX, MZIZI WA MWISHO WA MAQUIZ ULIOKUWA UMEBAKIA






MUTOMBO Lufungula  'Audax (kushoto), akiwa na Kasongo Mpinda 'Clayton' katika moja ya maonyesho ya Bana Maquiz.

NA PETER ORWA

WIKI chache kabla ya kifo chake, mwaka 2010, mwimbaji mahiri wa muziki wa dansi, Kasaloo Kyanga, alieleza changamoto aliyokumbana nayo wakati anajiunga na bendi ya Maquiz Original mwanzoni mwa miaka ya 1980, kwamba:“Nilikutana na ‘Predezshee saba’… Nikasema hapa ‘taweza’ kweli? “

Ujumbe wake ni kwamba, wakati huo anajiunga akiwa na umri wa miaka 24, alikutana na magwiji saba waimbaji unaomjumuisha Mutombo Lufungula Audax, akishirikiana na wengine kama vile Mbuya Makonga ‘Adios, Kasongo Mpinda ‘Clyton’ na Kikumbi Mwanza Mpango au King Kiki.

Leo hii ‘Predeshee’ huyo, Mutombo Lufungula Audax, hayupo tena kwa wiki moja sasa na alizikwa  katika nyumba ya milele wiki moja iliyopita, tukio lililotetemesha anga ya muziki nchini… Ni pigo kubwa ambalo limeacha masikitiko!

Marehemu huyo ambaye ndiye mwanahisa na muasisi aliyebaki katika bendi ya Maquiz Du Zaire, kati ya wenzake tisa waliounda zaidi ya miaka 50 iliyopita, nyumbani kwao, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), wakati huo ikiitwa taifa hilo Congo na baadaye Zaire.

Muasisi mwingine aliye hai, lakini aliondoa hisa zake mapema kabla ya bendi kufilisika ni mpiga solo mahiri, Nguza Vikings, ambaye baadaye alijiunga na Sambulumaa, kisha akaanzisha bendi yake ya Achigo, kabla ya kukutwa na matatizo yaliyompeleka gerezani kwa maisha yote.

Baadhi ya wanahisa wengine ni Ilunga  Lubaba, Mwema Mujanga,’ Chibangu Katai, Robert Otrish na Chinyama Chiyaza, aliyekuwa kiongozi wa bendi.

Audax alizikwa Jumapili mchana iliyopita katika makaburi ya Kinondoni, baada ya kutanguliwa na shughuli ya heshima za mwisho zilizofanyika katika Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam.

Ni kifo kinachotia simanzi katika tasnia ya muziki wa dansi, kwani gwiji mwingine ninayethubutu kumtaja aliongeza ushindani katika mchuano kati ya Maquiz na wapinzani wao, Orchestra Safari Sound, Kabeya Badu (65), naye alifariki mwaka jana na kuzikwa katika makaburi hayo hayo ya Kinondoni.

Katika historia yake, marehemu Kabeya aliwahi kupitia Maquiz kabla ya kujiunga na OSS na kisha wakati fulani bendi ya Tancut Almasi Orchestra. 

Mwimbaji mkongwe, Tshimanga Kalala Assosa, ana maelezo ya ziada kuhusiana na kifo cha Audax, ambacho kilitokana na maradhi ya kupooza yaliyomsumbua sana kwa miaka mitano iliyopita.

“Ameteseka sana,”anatamka Assosa, huku akifafanua kwamba kifo hicho kilitokea nyumbani kwa marehemu Kimara King’ong’o, alikokuwa akiugua na hafichi kumtambulisha kuwa ni mtu wake wa karibu.

Watu hao wamefahamiana kwa takriban maisha yao yote, tangu zama za miaka ya 1950, wakiwa kijijini kwao, Kamina Nsobongo, katika jimbo la Katanga, wakati huo ikiitwa Jamhuri ya Congo na baadae ikawa Zaire mwaka 1965.

“Hata mara ya mwisho nilipoenda nyumbani Congo (DRC), mama yake alikuja nyumbani,”anasimulia Assosa na kufafanua kwamba marehemu Audax ana dada anayeishi nchini, anayeitwa Kaiba.        

Anafafanua uhusiano wake na Audax kuwa, licha ya kutoka kijiji kimoja, walisoma shule moja na anamfahamu kwamba katika maisha yake yote, Audax alikuwa mpenzi na mchezaji mahiri wa mpira wa miguu, lakini akazama zaidi katika muziki kulikomfanya aache soka na masomo.

“Mama zetu pia walikuwa wanafahamiana sana,” anasema Assosa na kuongeza “Mara ya mwisho nilipoenda Congo (DRC), mama yake alikuja nyumbani.”

Assosa anajitambulisha kuwa na umri mdogo kwa marehemu Audax kwa wastani wa miaka miwili na alikuwa anasoma madarasa ya chini yake, lakini binafsi hakubobea katika soka. Mapenzi yake binafsi yaliozama kwenye masomo na kuimba kanisani.

Kwa mujibu wa John Kitime, mwanamuziki mwingine mkongwe aliyewahi kupigia gita la rhythm na besi kwa bendi kama Vijana na Tancut, marehemu Audax alizaliwa tarehe 9 ya mwezi Oktoba ya mwaka 1945..

Assosa anasimulia kwa hatua kisa cha Audax na baadhi ya wenzake ambao ndio wakawa wanamuziki  waasisi wa Maquiz, kwamba kijijini kwao Kamina kulizuka makundi mengi ya vijana wanaobobea katika muziki na kuunda bendi ndogo ndogo kijijini.

Moja ya kumbukumbu alio nao Assosa ni kwamba, wakati wa harakati za kuelekea uhuru wa Congo, yeye na marehemu Audax walikuwa katika kundi la vijana waliioonekana wanaimba vizuri na waliteuliwa kwenda nchini Ubelgiji kumuimbia Mfalme wa taifa hilo lilokuwa likiwatala.

Wakati huo Audax alishakuwa ametawaliwa na muziki na kuacha masomo tangu kipindi kirefu.

“Tuliporudi na sisi wengine ndio ukawa mwisho wa shule na hawa (vijana wenzake wa kijijini akiwemo Audax) ndio walitufanya shule ikawa basi… ndio watu waliotufanya tuvunje kalamu,” anasema Assosa.

Anafafanua kwamba, hali ya kuzingirwa na vijana wanamuziki kijijini, ndio kulimteka naye azame katika muziki na kuacha shule akiwa miongoni mwa vijana ambao awali walipenda mno masomo.   

Mwanamuziki huyo anawataja wakongwe wa muziki nchini anaotoka pamoja kijijini Kamina Nsabongo, ni pamoja na Mbombo wa Mbomboka na marehemu Issa Nundu, ambao katika nafasi tofauti waliwahi kupitia bendi kama Makassy, Super Matimila, OSS na Maquiz.

Assosa anawataja wengine waliokuwa Maquiz ni, Nguza Vikings, Mbuya Makonga Adios na Chinyama Chiyaza na anaongeza kuwa Adios alikuwa mwanakwaya mwenzake katika kanisa analolitaja la Mtakatifu Bavo, akiwa mpiga kinanada na yeye mwimbaji wa sauti ya pili, aliyodumu nayo hadi sasa katika dansi.

Kundi hilo lililounda Maquiz likiwa na bendi yao kijijini lilianza na mkakati wa kuvuka mpaka kwenda Uganda mwaka 1963, jambo ambalo Assosa hakukubaliana nalo na akaamua kurudi nyumbani kutoka mpakani mwa nchi na baadaye alielekea Kinshasa alikovuma kimuziki baada ya muda mfupi.

Lile kundi lilounda Maquiz, wakati huo likiwa na jina la Super Gaby, baada ya kukaa Uganda, lilihamia Tanzania mwaka 1972, ambapo Nguza na Audax walikuwa wamebaki huko na muda mfupi walikuja kujiunga na wezao nchini.

Ikumbukwe, mwaka 1971 taifa la Uganda utawala wake ulipinduliwa na kuchukuliwa na Rais Iddi Amin Dada.

Bendi hiyo ilipewa jina la Maquiz Du Zaire mwaka 1973, huku wakijozolea umaarufu, wakipiga muziki  katika ukumbi wa Mikumi Tours iliyopo eneo la TAZARA,  lililomilikiwa na aliyekuwa mfanyabiashara maarufu wa Dar es Salaam, Mzee Batenga

Hata hivyo hawakudumu sana, kutokana na eneo la ukumbi huo kuchukuliwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya stesheni ya TAZARA na walipata mkataba mwingine wa kupiga katika ukumbi wa Tours and Hunters, eneo la Ubungo. Ulikuwa unamilikiwa na Hugo Kisima, ambaye baadaye  alimiliki bendi ya OSS na ukumbi wa Safari Resort.

Mwanamuziki Kitime, anamsifu Audax kwamba alikuwa mtunzi mahiri na mwalimu wa muziki katika bendi ya Maquiz, iliyopitia mitindo mbalimbali kama vile Kamanyola Bila jasho, ulioasisiwa na Kingi Kiki mwaka 1973, Sendema na Zembwela.

Naye Assosa, anamwagia sifa kwamba, mbali na kuwa mtunzi, alikuwa mahiri katika kuchangia mawazo bora kwenye tungo za ndani ya bendi na hata muundo wa sauti, akitoa mfano kuna wakati alitoka na kujiunga na bedi ya Legho, lakini Audax aliwashawishi wakurugenzi wenziwe hadi wakamrudisha.

“Alikuwa mtu wangu wa karibu na alinipenda sana. Waliniita na hata nikasikia ile wanasema ‘nyongo ilitumbukia’ nikarudi Maquiz,” anasema Assosa. 

Kwa mujibu wa Kitime, marehemu aliuhusudu sana utunzi wake wa kibao cha Mpenzi Luta, ingawaje kuna mingine mingi aliozitunga  ikiwemo kibao ‘Nani Atanitetea.’

Wakati fulani, Audax alitunga kibao Kisebengo, kilichobeba ujumbe wenye kijembe kwa mwezake kutoka kijijini Kamina – Nguza Vikings, aliyeamua kuichukua hisa zake za Maquiz, katika dakika za mwisho baada ya safari ndefu ya kuunda bendi na maisha ya pamoja kimuziki.

Ikumbukwe, kuna wakati bendi ya Maquiz Du Zaire ilifikia kilele cha mafanikio, ambapo wakurugenzi wake wakiwemo, kina Audax mbali na kupiga muziki, waliunda kampuni iliyoitwa OMACO.

Assosa anasema, wakati wanaendeleza mafanikio ya muziki kupitia Maquiz, upenzi wa Audax katika soka hakuwahi kukoma, na ncjini alikuwa shabiki mkubwa wa klabu ya Yanga na hata ulipotokea mgawanyiko ukiozaa timu ya Pan African, alijiunga nayo na kuwa na kadi ya uanachama.

Hata baada ya kusambaratika, Audax kwa kushirikiana na wenzake kama vile Mwema Mujanga na Adios waliasisi bendi ya Bana Maquiz, iliyokuwa na makao makuu katika baa ya Savoy, eneo la Tabata na baadaye walimuongeza mwenzao, Assosa.

Hata hivyo, Assosa ana simulizi ya simanzi kwamba kwa bahati mbaya bendi hiyo ilifilisika vyombo, huku Adios akiwa ameshafariki. Katika mihangaiko Audax na Asosa walifanikiwa kupata msaada wa vyombo kwa mkopo wa shilingi milioni nane, ambao mfanyabiashara mmoja aliyetoa sharti la hisani wamlipe kidogo kidogo.

Assosa anasema, tukio ambalo hatolisahau na ni la kumsikitisha,   lililotokea miaka mitano iliyopita,  kwamba siku ambayo aliahidiwa kukabidhiwa vyombo na yeye akiwa katika mchakato wa kuvichukua, ni kwamba muda mfupi baadaye alipigiwa simu ya kufahamishwa Audax amepatwa na kiharusi, yuko hospitalini Muhimbili.

Anasema, tangu wakati huo amekuwa mgonjwa na kamwe hakuwahi hata kuviona vyombo ambavyo alishiriki katika mchakato wote wa kuvipata, jambo ambalo Assosa hafichi hisia zake akisema ‘inamuuma sana.’

Ni historia itayakayobaki kuwa ya kudumu, marehemu Audax ni nembo ya kudumu ya bendi ya Maquiz, akiwa mwanahisa muasisi wa mwisho aliyekuwa amebaki. 

MUNGU AMBARIKI APUMZIKE KWA AMANI.

1 comment: