KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, May 17, 2010

Rekodi na matukio muhimu Kombe la Dunia

BAO la mapema zaidi kufungwa katika fainali za Kombe la Dunia ni lile la Vaclav Masek wa Czechoslovakia, ambalo alilifunga sekunde la 16 wakati timu hiyo ilipomenyana na Mexico mwaka 1962.

Bao lililochukua dakika nyingi ni lile lililofungwa na David Pllatt wa England. Alifunga bao hilo dakika ya 119 wakati timu hiyo ilipomenyana na Ubelgiji katika fainali za mwaka 1990.

Mabao mengi yaliyofungwa haraka na kwa muda mfupi ni yale ya mwaka 1982. Mabao hayo yalifungwa na Laszlo Kiss wa Hungary. Alifunga mabao hayo dakika ya 70, 74 na 77.

Mchezaji mwenye umri mkubwa kufunga bao katika fainali za michuano hiyo ni Roger Milla wa Cameroon. Alifunga bao hilo katika fainali za mwaka 1994 dhidi ya Russia akiwa na umri wa miaka 42 na siku 39.

Mchezaji pekee aliyefunga bao na kujifunga katika mechi moja ni Ernie Brandts wa Uholanzi. Alijifunga na baadaye kufunga bao wakati Uholanzi ilipomenyana na Italia mwaka 1978. Katika mechi hiyo, Uholanzi iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Goli la kwanza la kujifunga lilikuwa la Ramon Gonzalez wa Paraguay katika fainali za mwaka 1930. Alijifunga bao hilo wakati Paraguay ilipochapwa mabao 3-0 na Marekani.

Mchezaji aliyezifungia mabao nchi mbili tofauti katika fainali za kombe hilo ni Robert Prosineck. Aliichezea Yugoslavia mwaka 1990 na kuipachikia bao dhidi ya Falme za Kiarabu. Pia aliichezea Croatia katika fainali za mwaka 1998 na kuifungia bao dhidi ya Jamaica.

Wachezaji waliofunga mabao katika fainali mbili tofauti za kombe hilo ni Vava wa Brazil (1958 na 1962), Pele wa Brazil (1958 na 1970) na Paul Breitner wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi (1974-1982).

Mchezaji mwenye umri mdogo kufunga bao katika fainali hizo alikuwa Pele wa Brazil. Alifunga bao hilo katika fainali za mwaka 1958 timu hiyo ilipomenyana na Wales, akiwa na umri wa miaka 17.

Mchezaji aliyefunga bao katika kila mechi alizocheza katika fainali hizo ni Jairzinho wa Brazil mwaka 1970 na Alcide Ghiggia wa Uruguay mwaka 1950.

Je Wajua?

Miji 23 imewahi kutumika mara mbili kwa fainali za Kombe la Dunia. Miji hiyo ni Berlin, Dortmund, Frankfurt, Gelsenkirchen, Hamburg, Hanover, Munich, Stuttgart na miji mingine minane katika nchi za Mexico na Ufaransa na miji saba ya Italia.

Miji saba iliyoandaa fainali za mwaka 1974 pia ilitumika tena katika fainali za mwaka 2006 zilizofanyika Ujerumani. Mji pekee ulioachwa ni Dusseldorf. Miji mipya ilikuwa Cologne, Kaiserslautern, Leipzig na Nuremberg.

Kombe la mwanzo la dunia lililoitwa Jules Rimet, lilizawadiwa moja kwa moja kwa Brazil mwaka 1970 baada ya kushinda fainali hizo mara tatu. Kombe hilo lililotengenezwa kwa madini ya dhahabu, liliibwa nchini humo na kuyeyushwa.

Kombe la pili liliibwa mwaka 1966 nchini England, lakini liligunduliwa baadaye likiwa limefukiwa ardhini chini ya mti. Aliyeligundua alikuwa mbwa mdogo aliyejulikana kwa jina la Pickles.

Licha ya kuwa majirani, vyama vya soka vya Argentina na Uruguay vilikuwa vikitumia mipira tofauti na kusababisha ubishani mkali katika mechi ya fainali kati ya timu hizo mwaka 1930 kuhusu mpira upi utumike. Mwamuzi Jean Langenus kutoka Ubelgiji aliamua mpira mwepesi wa Argentina utumike kipindi cha kwanza na mpira mzito wa Uruguay utumike kipindi cha pili.

Nchi zilizofuzu kucheza mara nyingi mechi ya fainali ya Kombe la Dunia ni Brazil, Ujerumani, Italia na Argentina. Brazil imemcheza fainali mara saba na kushinda mara tano. Ujerumani imecheza fainali mara saba na kushinda mara tatu. Italia imecheza fainali mara tano na kushinda mara nne. Argentina imecheza fainali mara tatu na kushinda mara mbili.

Brazil ndiyo nchi pekee iliyofuzu kucheza fainali zote 18 za kombe la dunia, ikifuatiwa na Italia na Ujerumani, zilizofuzu kucheza fainali 16 na Argentina iliyofuzu kucheza fainali 14.

Haijawahi kutokea kwa bingwa mtetezi kufanya vibaya katika fainali za kombe la dunia kama ilivyokuwa kwa Ufaransa mwaka 2002. Si tu kwamba ilishindwa kuvuka raundi ya kwanza, bali pia haikushinda hata mechi moja.

Wachezaji waliocheza mechi nyingi za fainali za Kombe la Dunia ni kipa Antonio carbajal wa Mexico (1950-66) na Lothar Matthaus wa Ujerumani (1982-98). Wachezaji hao walicheza fainali tano za kombe la dunia kila mmoja.

Norman Whiteside wa Ireland Kaskazini alikuwa mchezaji wa kwanza mwenye umri mdogo kucheza fainali za Kombe la Dunia mwaka 1982. Alicheza fainali hizo akiwa na umri wa miaka 17 na siku 41 wakati timu hiyo ilipomenyana na Yugoslavia.

Wanasoka wawili waliweka rekodi ya kutwaa Kombe la Dunia wakiwa wachezaji na makocha. Mario Zagallo wa Brazil alitwaa kombe la dunia akiwa mchezaji mwaka 1958 na 1962 na pia akiwa kocha 1970. Franz Beckenbauer wa Ujerumani alitwaa kombe hilo akiwa mchezaji mwaka 1974 na akiwa kocha 1990.

Oliver Kahn wa Ujerumani alikuwa kipa wa kwanza kupewa tuzo ya ya mpira wa dhahabu akiwa mchezaji katika fainali za mwaka 2002 zilizofanyika Japan na Korea Kusini.

Pele wa Brazil ni mchezaji pekee aliyecheza fainali tatu za kombe hilo na nchi hiyo kutwaa ubingwa. Alicheza fainali za mwaka 1958, 1962 na 1970. Hakucheza fainali za mwaka 1966 kutokana na kuwa majeruhi. Cafu wa Brazil pia alicheza fainali tatu mfululizo za mwaka 1994, 1998 na 2002.

Bora Milutinovic wa Serbia ndiye kocha pekee aliyeziongoza nchi tano katika fainali tano tofauti za kombe la dunia kati ya mwaka 1986 hadi 2002. Alizifundisha nchi za Mexico, Costa Rica, Marekani, Nigeria na China.

Carlos Alberto Parreira wa Brazil ameziongoza nchi nne katika fainali nne tofauti za kombe hilo. Nchi hizo ni Brazil, Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu na Kuwait.

Makocha watano waliziwezesha nchi zao kucheza fainali za kombe hilo mara mbili. Makocha hao ni Pozzo wa Italia (1934 na 1938), Schon wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi (1966-1970), Zagallo wa Brazil (1970-1998), Beckenabauer wa iliyokuwa Ujerumani Magharibi (1986-1990) na Bilardo wa Argentina (1986-1990).

Mechi 16 ziliamuliwa kwa penalti kuanzia mwaka 1982 wakati Ujerumani ilipoishinda Ufaransa katika mechi ya nusu fainali. Mechi maarufu ilikuwa ya fainali ya mwaka 1994wakati Brazil ilipoichapa Italia kwa penalti 3-2 baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa suluhu. Italia pia ilifungwa mara mbili kwa njia ya penalti na Argentina na Ufaransa katika fainali za 1990 na 1998.

No comments:

Post a Comment