'
Saturday, September 26, 2015
TANZANIA MWENYEJI WA KOZI YA KIMATAIFA YA WAAMUZI
Jumla ya waamuzi chipukizi 29 wasiokua na beji za FIFA kutoka nchi 28 barani Afrika wanatarajiwa kuhudhuria kozi ya waamuzi inayoandaliwa na FIFA kwa kushirikiana na CAF itakayofanyika kuanzia kesho Jumamosi tarehe 26 –30 Septemba mwaka huu jijini Dra es salaam.
Kozi hiyo itaendeshwa na wakufunzi kutoka katika nchi za Afrika Kusini, Malawi, Misri na Mauritius itafanyika katika hoteli ya Holiday Inn iliyopo jijini Dar es salaam ambapo waamuzi chipukizi kutoka Tanzania watakohudhuria ni Abdallah Kambuzi (Shinyanga) na Shomari Lawi (Kigoma).
Lengo la kozi hiyo ni kuwaanda waamuzi wanaochipukia ili baadae kuweza kuwa waamuzi wa FIFA ambao watatumika kwa michuano mbalimbali.
TFF YATUMA RAMBIRAMBI BAKWATA
Rais wa Shrikisho la Mpira wa Migu nchini (TFF), Jamal Malinzi ametuma salam za rambirambi kwa Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakary Zubeiry kufuatia vifo vya mahujaji zaidi ya 700 vilivyotokea Maka wakati wa kuhiji.
Katika salam zake kwenda kwa mufti mkuu, Malinzi amewapa pole waislam wote duniani kufuatia vifo vya mahujaji hao zaidi ya 700 vilivyotokea juzi na majeruhi zaidi ya 400 wakati wa ibada ya hija.
Malinzi amesema kwa niaba ya familia ya mpira wa miguu nchini TFF inawapa pole wafiwa wote, ndugu jamaa na marafiki na kuwatakia majeruhi afya njema na kusema ipo pamoja nao katika kipindi hichi kigumu cha maombelezo.
Wednesday, September 23, 2015
KUZIONA SIMBA NA YANGA BUKU SABA
Viingilio vya mchezo wa watani wa jadi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania utakaochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam vimetangazwa leo ambapo kiingilio cha chini kitakua ni shilingi elfu saba (7,000).
Katika mchezo huo kiingilio cha juu kitakua ni shilingi Elfu Thelathini (30,000) kwa viti vya VIP A, Elfu Ishirini (20,000) kwa viti vya VIP B & C, huku kiingilio cha shilingi Elfu Saba (7,000) kikiwa ni kwa viti vyenye rangi ya Blu, Kijani na Orange.
Tiketi za mchezo ho zitaanza kuuzwa siku ya Ijumaa saa 2 kamili asubuhi katika vituo vifuatavyo: Karume – Ofisi za TFF, Buguruni – Oilcom, Dar Live – Mbagala, Uwanja wa Taifa, Luther House – Posta, Ferry – Kivukoni, Mnazi Mmoja, Ubungo – Oilcom na Makumbusho – Standi ya mabasi ya daladala.
TFF inawaomba wapenzi, wadau na washabiki wa mpira wa miguu nchin kununua tiketi katika magari yaliyopo kwenye vituo vya kuuzia tiketi ili kuondokana na kuuziwa tiketi zisizo sahihi.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi wa kimataifa mwenye beji ya FIFA, Israel Nkongo (Dsm) akisaidiwa na Josephat Bulali (Tanga), Ferdinand Chacha (Mwanza) mwamuzi wa akiba Soud Lila (Dsm) wakati kamisaa wa mchezo huo atakua Charles Mchau kutoka Kilimanjaro.
Michezo mingine ya Ligi Kuu ya Vodacom siku hiyo ya Jumamosi itakua ni kati ya Coastal Union dhidi ya Mwadui FC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Maafande wa jeshi la Magereza (Tanzania Prisons) watawakaribisha maafande wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Maafande wa JKT Ruvu watakuwa wenyeji wa Stand United katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, huku wakata miwa wa Turiani Mtibwa Sugar watawakaribisha Majimjaji ya Songea katika uwanja wa Manungu wakati Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Toto Africans katika uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
Ligi hiyo itaendelea siku ya Jumapili kwa michezo miwili ambapo waoka mikate wa Azam FC watawakaribisha Mbeya City katika uwanja wa Chamazi Complex, huku African Sports wakiwa wenyeji wa Ndanda FC kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
TWIGA STARS KUJIPIMA NA MALAWI
Timu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania (Twiga Stars) inatarajiwa kucheza mchezo wa kirafiki na timu ya Taifa ya Wanawake ya Malawi tarehe 24 Oktoba, mwaka huu nchini Malawi.
Mechi hiyo kati ya Twiga Stars dhidi ya Malawi itachezwa jijini Lilongwe kufuatia mwaliko wa chama cha soka nchini Malawi (FAM) kuialika Twiga Stars kwenda nchini Malawi kwa ajili ya mchezo huo
Mchezo huo wa kirafiki ni sehemu ya maandalizi ya vikosi vya timu zote mbili za Wanawake Tanzania na Malawi kwa ajili ya michuano mbalimbali.
MALINZI AFUNGA KOZI YA MAKOCHA
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi amefunga kozi ya makocha ya leseni C inayotolewa na CAF, iliyowashirikisha makocha 31 kutoka mikoa mbalimbali nchini.
Akifungua kozi hiyo iliyoandaliwa na Chama cha Soka mkoa wa Dar es salaam (DRFA), Malinzi amewaomba washiriki wa kozi hiyo kwenda kutumuia ujuzi walioupata kwa kufundisha timu na vituo vya vijana vilivyopo seheu mbalimbali.
“Naimani wote hapa mlioshirki kozi hii ni watu wa mpira, ombi langu kwenu ni kwenda kufundisha mpira na sio kwenda kuviweka vyeti hivi hivi makabatini, mtusaidie kuandaa vijana kama tulivyo TFF na mipango mziuri ya kuendeleza vijana kwa ajili ya ushirki wa vijana kwenye fainali za Mataifa Afrika kwa vijaa wenye umri chini ya miaka 17 mwaka 2017 nchini Madagascar, mwaka 2019 Tanzania na baadae tuweze kushiriki fainali za Olimpiki mwama 2010 Tokyo nchini Japan.
Aidha Mwenyekiti wa DRFA Almasi Kasongo akiongea wakati wa kumkaribsisha Rais wa TFF, alisema DRFA wamejitahid kuendesha kozi hiyo yenye washiriki 31 lakini chnagamoto kubwa ni gharama za uendeshaji kwani kozi moja kama hiyo inahitaji fedha zaidi ya shilingi milioni 15 za Kitanzania jambo ambalo vyama vingine vya mikoa vinashindwa kumudu.
STAR TIMES KUDHAMINI LIGI YA FDL
Kampuni ya StarTimes Media ya jijini Dar es salaam leo imeingia mkataba wa udhamini na TFF kudhamini Ligi Daraja la Kwanza nchini (FDL) inayoshirikisha timu 24 kutoka katika mikoa 16 ya Tanzania bara.
Akiongea na waandishi wa habari wakai uwekaji sahihi mkataba huo, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi ameshukuru kituo cha Star Times kwa kuamua kuwekeza katika mpira wa miguu na hasa kwenye chimbuko la vipaji na wachezaji wengie nchini.
Malinzi amesema udhamini huo wa shilingi milioni 900 kwa kipindi cha miaka mitatu, unatarajiwa kuongezeka wiki ijayo baada ya kuingia mkataba na mdhamini mwingine wa kurusha matangazo ya ligi hiyo kwa shilingi milioni 450 na kufikia jumla ya udhamini wa shilingi bilioni 1.3.
Aidha Malinzi amesema TFF inaendelea na mipango ya kuhakikisha inavisaidia vilabu vya madaraja ya chini, timu za wanawake na vijana kuona vinapata udhamini na kuweza kushirki vyema michuano mbalimbali.
Naye Mkurugenzi wa StarTimes Media nchini, Lanfang Liao amepongeza ushirikiano mpya ulioanzishwa kati ya kampuni yake na TFF na kuahidi kudumisha ushirkiano huo kwa faida ya maendeleo ya mpira wa Tanzania.
Mwenyekiti wa timu ya Kinondoni Municipal Council (MKC), John Njunde akiongea kwa niaba ya vilabu vya ligi daraja la kwanza, amesema anaishukru TFF kwa kuweza kuvitafutia udhamini vilabu na sasa wataweza kushiriki vizuri ligi hiyo inayotoa timu tatu zitakazopanda ligi kuu msimu ujao.
VYAMA VYA MIKOA VYATAKIWA KUANZISHA LIGI ZA WANAWAKE
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TF) limeviagiza vyama vya mpira wa miguu vya mikoa (FA’s) kuendesha mashindano ya ligi ya mabingwa wa mikoa kwa wanawake (Region Womens Champion League) kabla ya tarehe 31, Disemba mwaka huu.
Kila chama cha mkoa cha mpira wa miguu nchini kinapaswa kuwasilisha jina la bingwa wa mkoa mwishoni wa mwezi Disemba mwaka huu, kwa ajili ya maandalizi ya Ligi ya Taifa ya Wanawake inayotarajiwa kufanyika mwakani.
Ligi ya Taifa ya Wanawake inatarajiwa kuanza mapema mwakani baada ya kupatikana mabingwa wa mikoa 27 nchini ikijumuisha mkoa wa Dar es salaam utakaokuwa na timu tatu za Ilala, Kinondoni na Temeke.
Jumla ya timu 10 zinatarajiwa kupanda Ligi Kuu ya Wanawake Taifa baada ya timu za mikoa 27 kucheza ligi ya mabingwa na kupata timu 10 zitakazoanza kwenye ligi hiyo ya wanawake mwakani.
Tuesday, September 22, 2015
MALINZI AFUNGA KOZI YA MAKOCHA, AWAPA ANGALIZO
RAIS wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Jamal Malinzi, amefunga kozi ya wiki mbili ya makocha lesseni C inayotambuliwa na Shirikisho la soka barani Afrika (CAF) na kuwataka wahitimu hao kufanyia kazi mafunzo waliyoyapata.
Akizungumza kwenye hafla fupi ya kufunga mafunzo hayo, Malinzi amesema kuwa anasikitika kuona makocha wanapata mafunzo kama hayo lakini wanaenda kuweka vyeti vyao ‘makabatini’ na kuacha kufanyia kazi walichojifunza.
“Hiki mlichokipata kwenye mafunzo haya mnatakiwa muende mkafanyie kazi kwa kutafuta timu za kufundisha na baada ya mwaka mmoja ni vizuri mkajiendeleza zaidi ya hapa,” alisema Malinzi
Amesema kuwa Shirikisho lake limepanga kuhakikisha baada ya muda litafuta utaratibu wa makocha wenye lesseni C kuwa kwenye benchi la ufundi la timu za daraja la kwanza na kuwa wasaidizi kwenye benchi la ufundi la timu za ligi kuu.
“Kwa sasa hivi makocha wa ligi kuu wanatakiwa kuwa na leseni ya daraja B na wasaidizi angalau leseni daraja C, ila kuanzia msimu wa 2017-2018 mambo yatabadilika na lessen I C aizataruhusiwa kwenye mabenchi ya ufunzi kwa timu za ligi kuu, mambo yataendelea hivyo mpaka mwisho tutakuwa na leseni za daraja A,” alisema Malinzi.
Aidha, aliwataka wahitimu hao ambao wengi wao wanatoka kwenye klabu za daraja la kwanza na wengine wakiwa makocha wasaidizi kwenye klabu za ligi kuu, kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata kwenye mafunzo hayo kuzisaidia timu zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha soka mkoa wa Dar es Salaam, Almas Kasongo, ameishukuru TFF kwa jitihada za kuendeleza mchezo wa soka nchini na kuelelezea changamoto wanazokutana nazo katika kuandaa kozi kama hizo kwa vyama vya soka vya mikoa nchini.
“Sisi DRFA tumefanikiwa kuendesha kozi hii kwa sababu ya uwepo wa timu za Simba, Yanga na Azam kwenye ligi kuu ambazo ni sehemu ya mapato kwa chama chetu, ila kwa vyama vingine hali inakuwa ngumu kuandaa na kuendesha mafunzo kama hayo,” alisema Kasongo.
Kozi hiyo ya wiki mbili ilikuwa ikifanyika kwenye ukumbi wa TFF na kuendeshwa na mkufunzi anayetambulika na CAF, Salum Madadi ambaye pia ni Mkurugenzi wa ufundi wa TFF.
TFF YAISHITAKI ETOILE DU SAHEL FIFA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) limefungua kesi kwenye Kamati ya Nidhamu ya FIFA dhidi ya klabu ya Etoile Sportive du Saleh ya Tunisa kutokana na klabu hiyo kushindwa kuilipa klabu ya Simba SC ya Tanzania pesa za mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi.
Kwa mujibu wa barua ya FIFA kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Tunisia (FTF) na nakala yake kwenda TFF, klabu hiyo inashitakiwa kwa kuvunja kanuni kwa mujibu wa ibara ya 64 ya kanuni za nidhamu za FIFA (Fifa Disciplinary Code).
Kwa kuzingatia hilo, agenda hii itakuwa kwenye kikao kijacho cha kamati ya nidhamu.
Etoile Sportive du Sahel wametakiwa kulipa mara moja kiasi cha dola za kimarekani laki 3 na riba ya asilimia 2% kwa kila mwaka kama ilivyoelekezwa na maamuzi ya Jaji mmoja wa Kamati ya Nidhamu za Wachezaji mnamo tarehe 20 Novemba 2014.
Tangu wakati huo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limekua likiwasiliana na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Tunisia (FTF) na FIFA kwa niaba ya klabu ya Simba amabye ni mwanachama wa TFF.
Ikiwa klabu hiyo ya Tunisia itafanya malipo kwa klabu ya Simba na kupelekea ushahidi wa malipo kwa FIFA basi suala hilo litafutwa.
Aidha klabu hiyo iko kwenye hatari ya kushushwa daraja au kupokwa alama kwenye ligi (League Point) iwapo haitalishughulikia suala hilo mara moja.
MALINZI AFUNGA FAINALI ZA AIRTEL RISING STARS
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi leo amefunga fainali za michuano ya kombe la Airtel Rising Stars katika uwanja Karume jijini Dar es salaam.
Akiongea kwakati wa ufungaji michuano ya airtel mbele ya halaiki ya vijana walioshirki michuano hiyo, Malinzi ameishukuru kampuni ya simu ya Airtel kwa kuendelea kudhamini michuano hiyo ambayo inawapa nafasi vijana ya kucheza mpira na kuonekana na baadae kujipatia ajira.
“Lengo la TFF ni kushirki fainali za Olimpiki za Dunia mwaka 2020 Tokyo –Japan hivyo wachezaji wenye vipaji kutoka kwenye michuano hii ya Airtel na vijana wengine wataendelea kutunzwa kwa ajili ya timu ya Taifa ya baadae” Alisema Malinzi.
Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel ambao ndio wadhamini wakuu wa michuano hiyo, amesema airtel wataendelea na program hiyo ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 kwa wanawake na wanaume, na kuahidi kuendelea koboresha michuano hiyo kila mwaka.
Michuano ya Airtel Rising Stars iliyomalizika leo, ilizisihirkisha timu za wanaume na wanawake kutoka mikoa saba nchini, huku mashindano hayo yakiwa yanafanyika kwa msimu wa tano sasa tangu kuanzishwa mwaka 2011.
Kwa upande wa wanaume, timu ya Ilala imeibuka mabingwa baada ya kuifunga Mbeya kwa mabao 4-0 katika mchezo wa fainali ulochezewa jioni ya leo, huku timu ya wanawake ya Temeke wakiibuka washindi baaada ya kuibwaga Kinondoni mwa mikwaju ya penati 5-4.
Monday, September 21, 2015
SIMBA YAITUMIA SALAMU YANGA, YAICHAPA KAGERA SUGAR MABAO 3-1
TIMU kongwe ya soka nchini, Simba jana iliendelea kuchanua katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuitandika Kagera Sugar mabao 3-1.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mshambuliaji Hamisi Kiiza ndiye aliyeibeba Simba baada ya kuifungia mabao yote matatu.
Kutokana na kuzitikisa nyavu za Kagera Sugar mara tatu, Kiiza sasa ameweka rekodi ya kuifungia Simba mabao matano katika mechi tatu ilizocheza za ligi hiyo.
Simba sasa imefikisha pointi tisa sawa na Yanga na Azam, lakini zinatofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa. Yanga inaongoza kwa mabao mengi ya kufunga.
Kiiza alifunga bao la kwanza katika kipindicha kwanza, alipounganisha wavuni kwa kichwa mpira wa krosi uliopigwa na Awadh Juma. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipa Manyika Peter wa Simba alistahili pongezi kutokana na kuzuia mipira mingi ya hatari iliyopigwa na washambuliaji wa Kagera Sugar.
Kiiza aliiongezea Simba bao la pili dakika ya 46 baada ya kumalizia krosi safi kutoka kwa beki wa kushoto, Mohamed Hussein Tshabalala.
Kagera Sugar ilipata bao la kujifariji dakika ya 50 lililofungwa na Mbaraka Yussuf baada ya mabeki wa Simba kujichanganya katika eneo lao la hatari.
Kiiza alihitimisha karamu ya magoli dakika ya 90 baada ya kuifungia Simba bao la tatu kwa shuti kali, baada ya kupokea krosi kutoka kwa Mwinyi Kazimoto.
Simba wanatarajiwa kushuka tena dimbani Septemba 26, mwaka huu, kuvaana na mahasimu wao Yanga katika mechi inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini.
Sunday, September 20, 2015
YANGA HII WEEE ACHA TU, YAIBAMIZA JKT RUVU 4-1
YANGA SC imetoa onyo kwa mahasimu wao, Simba SC kuelelea mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuwatandika JKT Ruvu mabao 4-1 jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo wa tatu mfululizo unaifanya Yanga SC itimize pointi tisa na kujiimarisha kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inayoonyeshwa moja kwa moja na Azam TV.
Hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma dakika ya 30 akimalizia pasi fupi ya Amissi Tambwe baada ya kazi nzuri ya kiungo wa kulia Deus Kaseke.
Yanga SC ilitawala mchezo kipindi cha kwanza, lakini haikuweza kutengeneza nafasi nyingi za kufunga mabao, wakati JKT walicheza kwa kujihami zaidi kipindi hicho.
Kipindi cha pili, Yanga SC walirudi na kasi ya kusaka mabao zaidi na iliwachukua dakika tatu tu kupata bao la pili, lililofungwa na Mrundi, Amissi Tambwe aliyemalizia krosi ya Kaseke.
JKT wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi dakika ya 49, kupitia kwa beki na Nahodha wake, Geogre Minja aliyetumia mwanya wa wachezaji wa Yanga SC kuzubaa baada ya kupata bao la pili.
Mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara misimu miwili iliyopita, Amissi Tambwe akaifungia Yanga SC bao la tatu dakika ya 62 kwa kichwa akimalizia krosi ya Simon Msuva.
Kiungo Mzimbabwe, Thabani Kamusoko akahitimisha sherehe za mabao Yanga SC kwa kufunga bao la nne, dakika ya 87 kwa shuti la nje ya boksi baada ya kukutana na mpira uliookolewa na Michael Aidan kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na Mbuyu Twite baada ya Msuva kuangushwa.
Katika mechi nyingine za ligi hiyo jioni ya leo, Stand United imeshinda 2-0 dhidi ya African Sports ya Tanga Uwanja wa Kambarage, Shinyanga mabao yote yakifungwa na Elias Maguri, wakati Uwanja wa Mkwakwani, Tanga bao pekee Fully Maganga limeipa Mgambo Shooting ushindi wa 1-0 dhidi ya Majimaji FC na Uwanja wa Sokoine, Mbeya Prisons imeshinda 1-0 dhidi ya Mbeya City bao pekee la Jumanne Elfadhil.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi nne, Mwadui FC na Azam FC Uwanja wa Mwadui Complex, Mtibwa Sugar na Ndanda FC Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro, Simba SC na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Coastal Union na Toto Africans Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Hajji, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Thabani Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Salum Telela dk78, Amksi tambwe, Donald Ngoma na Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya dk61.
JKT Ruvu; Tony Kavishe, Michael Aidan, Napho Zuberi, Martin Kazila, Ramadhani Madenge, George Minja, Ismail Aziz/Abdulrahman Mussa dk57, Nashon Naftali, Samule Kamuntu/Gaudence Mwaikimba dk57, Saad Kipanga/Emmanuel Pius dk77 na Mussa Juma.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BIN ZUBEIRY
Saturday, September 19, 2015
VIJANA WALIOKWENDA ORLANDO PIRATES WAREJEA
Kufuatia safari ya vijana watano wa U15 Asaad Ali Juma, Maziku Aman, Issa Abdi, Kelvin Deogratias, Athumani Maulid waliokwenda kufanya mazoezi kwenye klabu ya Orlando Pirates kufuatia mwaliko uliotolewa na TFF na klabu hiyo, safari hiyo ilikamilika na vijana wamerejea nyumbani.
Vijana hawa waliongozana na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi wakiwa Afrika Kusini walifanya mazoezi ya wiki moja kuanzia Septemba Mosi mpaka tarehe 7 Septemba, 2015 chini ya uangalizi wa Augusto Placious ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Orlando Pirates.
Idara ya ufundi ya Orlando Pirates imejiridhisha na kiwango kilichoonyeshwa na vijana hao.
Hatua inayofuata ni mawasiliano kati ya shule wanazosoma hao vijana hapa Tanzania na klabu ya Orlando Pirates ili kutafutiwa nafasi za masomo kwenye shule za Afrika Kusini.
Jambo hili likikamilika vijana hao watakwenda nchini Afrika Kusini kwa ajili ya masomo na kufundishwa mpira.
TFF inamshukuru Dr. Irvin Khoza Rais na mmiliki wa klabu ya Orlando Pirates kwa ushirkiano na kutoa nafasi kwa vijana wa U15 Tanzania kwenda kufanya mazoezi kwenye klabu hiyo kongwe nchini Afrik Kusini na kuendelezea
Wednesday, September 16, 2015
AZAM YAENDELEA KUCHANUA
AZAM FC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada kuwalaza mabao 2-0 wenyeji Stand United Uwanja wa Kambarage, Shinyanga jioni ya leo.
Shukrani kwao, wafungaji wa mabao hayo, mshambuliaji wa Kenya, Alan Watende Wanga na kiungo mzalendo Frank Rymond Domayo.
Huo ushindi wa pili mfululizo kwa Azam FC ya kocha Muingereza Stewart Hall, baada ya awali kuichapa Prisons ya Mbeya 2-1 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Katika mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Yanga SC imeialza 3-0 Prisons Dar es Salaam, Simba SC imeifunga 2-0 Mgambo JKT Tanga, Majimaji FC imeifunga 1-0 Kagera Sugar Songea, Mbeya City imeichapa 3-0 JKT Ruvu Mbeya, Toto Africans imefungwa 2-1 na Mtibwa Sugar Mwanza, Ndanda FC imeialza 1-0 Coastal Union Mtwara na Mwadui FC imeshinda 2-0 dhidi ya African Sports.
MATOKEO MECHI ZA LIGI KUU TZ BARA LEO
Yanga SC 3-0 Prisons
Mgambo JKT 0-2 Simba SC
Majimaji FC 1-0 Kagera Sugar
Mbeya City 3-0 JKT Ruvu
Stand United 0-2 Azam FC
Toto Africans 1-2 Mtibwa Sugar
Ndanda FC 1-0 Coastal Union
Mwadui FC 2-0 African Sports
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY
YANGA MBELE KWA MBELE LIGI KUU
YANGA SC imeendelea kung’ara katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuichapa mabao 3-0 Prisons ya Mbeya Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jioni ya leo.
Mabingwa hao watetezi, sasa wanafikisha pointi sita na mabao matano, baada ya awali kushinda pia nyumbani 2-0 dhidi ya Coastal Union.
Hadi mapumziko, Yanga SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na kiungo Mkongo, Mbuyu Twite dakika ya 27 baada ya kipa wa Prisons, Mohammed Yussuf kushindwa kuokoa mpira wa adhabu uliopigwa na Simon Msuva, kufuatia Deus Kaseke kuangushwa nje ya boksi.
Mrundi Amissi Tambwe aliifungia Yanga SC bao la pili dakika 45 akiumalizia mpira uliopanguliwa na kipa wa Prison, Yussuf baada ya mpira wa adhabu wa kiungo wa Rwanda, Haruna Niyonzima kufuatia Msuva tena kuangushwa.
Mshambiliaji wa Prisons Jeremiah Juma alipoteza nafasi nzuri ya kufunga kipindi cha kwanza baada ya kupia juu la lango. Kipindi cha pili, kocha wa Prisons, Salum Mayanga alianza kwa kumpumzisha kipa Yussuf na kumuingiza Aron Kalambo
Refa Alex Mahagi wa Mwanza alimtoa kwa kadi nyekundu James Josephat dakika ya 59 baada ya kumdondosha Msuva kwenye boksi na Mzimbabwe Donald Ngoma akaifungia Yanga SC bao la tatu kwa penalti dakika ya 60.
Kikosi cha Yanga SC kilikuwa: Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, Mwinyi Haji Mngwali, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondan, Thabani Kamusoko, Deus Kaseke/Salum Telela dk66
Simon Msuva, Haruna Niyonzima Geoffrey Mwashiuya dk79, Amissi Tambwe/Malimi Busungu dk84, Donald Ngoma na Deus Kaseke.
Prisons: Mohammed Yussuf/ Aron Kalambo dk46, Salum Kimenya, Laurian Mpalile, James Josephat, Nurdin Chona, Jumanne Elfadhil, Lambert Sabianka, Juma Seif, Mohammed Mkopi/Cosmas Ader dk47, Boniface Hau Ally Manzi dk64 na Jeremiah Juma.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY
SIMBA YAIBANJUA MGAMBO SHOOTING 2-0
SIMBA SC imetimiza dhamira ya kukusanya pointi zote sita katika mechi zake mbili za awali za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara- baada ya jioni ya leo kuilaza mabao 2-0 JKT Mgambo.
Huo ni mwanzo mzuri kwa kocha Muingereza Dylan Kerr Simba SC, kwani sasa Wekundu wa Msimbazi nao wamo kwenye mbio za ubingwa.
Hadi mapumziko, tayari Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililofungwa na kiungo Mzimbabwe Justuce Majabvi dakika ya 27 baada ya krosi ya Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ kuzua kizazaa langoni mwa Mgambo
Mgambo walikosa bao la wazi dakika ya 19 baada ya shuti la Salim Aziz Gillah kupaa juu kidogo ya lango.
Said Ndemla alikaribia kufunga dakika ya 35 kwa kichwa akimaizia krosi ya Hassan Kessy lakini mpira ukatoka nje kidogo ya lango.
Mgambo tena wakakosa bao la wazi baada ya shuti la Nassor Gumbo aliyeingia akichukua nafasi ya Salim Gillah kugonga mwamba na kurudi uwanjani dakika tano baaadye.
Mganda Hamisi Kiiza ‘Diego’ aliifungia Simba SC bao la pili dakika ya 73 akimalizia pasi Ibrahim Hajibu baada ya gonga safi baina yao.
Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Simba SC baada ya awali kuifunga African Sports 1-0, bao pekee la Kiiza.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Peter Manyika, Mohamed Hussein, Hassan Ramadhani, Murushid Juuko, Hassan Isihaka, Justuce Majabvi, Awadh Juma, Said Ndemla/Abdoulaye Pape N’daw dk69, Mussa Mgosi/Ibrahim Habib dk67, Mwinyi Kazimoto/Hamisi Kiiza dk46 na Peter Mwalianzi.
Mgambo JKT; Said Abdi, Bashiru Chanache, Salim Mlima, Salim Kipaga, Ramadhani Malima/Athanas Chacha, Bakari Mtama, Salim Gillah, Mohammed Samatta, Helbert Charles, Fullu Zulu Maganga/Bolly Shaibu dk68 na Chande Magoja.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY
TFF YAFANYA MABADILIKO YA KAMATI NDOGO
Kikao cha Kamati ya Utendaji cha Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kilichofanyika Septemba 06, mwaka huu kilifanya mabadiliko madogo ya kamati zake ndogo ndogo.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Blassy Kiondo aliyekua Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Wanawake ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Ufukweni na Sakafuni (Beach Soccer and Futsal).
Amina Karuma ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Wanawake nchini (TWFA) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji aliteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Soka la Wanawake.
Mashindano ya Copa Coca Cola yanayodhaminiwa na Kampuni ya Vinywaji ya Coca Cola yaliyokuwa yafanyike katikati ya mwaka huu, sasa yatafanyika mapema mwakani mwezi Februari kuanzia ngazi ya Wilaya na fainali zake kufanyika mwezi Juni na Julai 2016.
Michuano hiyo ambayo hushirikisha timu za mikoa yote Tanzania kuanzia katka ngazi ya Wilaya, hufanyika kila mwaka kwa kuwashirkisha vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15).
Taarifa ya Idara ya Masoko ya Coca Cola imesema kampuni hiyo imeahirisha kufanyika kwa michuano hiyo wa mwaka huu, na sasa itafanyika mwakani ili waweze kupata nafasi ya kuandaa vizuri mashindano hayo.
Tuna uzoefu na mashindano hayo, ni vyema tukaifanya wakati wa likizo wakati vijana wakiwa mapumziko, sababu wachezaji wote wa michuano ya Copa Coca Cola ni wanafunzi hivyo ni vizuri tukaandaa mashindano hayo wakati wanafunzi wakiwa likizo.
Michuano ya Copa Coca Cola ilianza mwaka 2007 kwa kushirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17 (U17) na baadae mwaka 2012 kubadilishwa na kuwa mashindano ya vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U15).
Baadhi ya wachezaji waliopatikana katika mashindano hayo kwa sasa wanacheza katika vilabu vikubwa vya Ligi Kuu ya Vodacom nchini na wengine wamepata naafasi ya kucheza soka nje ya nchi.
LIGI YA FDL KUANZA SEPT 19
Ligi Daraja la Kwanza nchini (FDL) inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Jumamosi Septemba 19 kwa michezo 10 kuchezwa katika viwanja mbalimbali nchini, ambapo jumla ya timu 24 zinashirki ligi hiyo ambayo washindi wa tatu watapanda ligi kuu ya Vodacom msimu ujao.
Kundi A, Polisi Dar watakuwa wenyeji wa Friends Rangers kwenye uwanja Mabatini mkoani Pwani, Mjii Mkuu ya Dodoma watapambana na Polisi Dodoma kwenye uwanja wa Jamhuri mjini humo.
Kundi B, Polisi Morogoro watacheza na Burkina Faso uwanja wa Jamhuri Morogoro, Njombe Mji FC watacheza na Kurugenzi uwanja wa Amani mjini Njombe, Lipuli ya Iringa watawaribisha Kimondo FC uwanja wa Wambi- Iringa na JKT Mlale watakua wenyeji wa Ruvu Shooting katika uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma.
Kundi C, Mbao FC watawakaribisha Geita Gold uwanja wa CCM Kirumba, Rhino Rangers watacheza dhidi ya Polisi Tabora uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Panone FC watawakaribisha JKT Oljoro katika uwanja wa Ushirka mjini Moshi na Polisi Mara watakua wenyeji wa JKT Kanembwa kwenye uwanja wa Karume mkoani Mara.
YANGA KUCHAGUA VIONGOZI WAPYA BAADA YA UCHAGUZI MKUU
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limepokea maombi ya klabu ya Young Africans (Yanga SC) ya kutaka kufanya uchaguzi wake mkuu wa viongozi wa klabu hiyo kwa nafasi za Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na wajumbe wa kamati ya Utendaji.
TFF imeiomba klabu hiyo kufanya mkutano wake wa Uchaguzi wa viongozi baada ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Rais, Wabunge na Madiwani) utakaofanyika Oktoba 25, 2015.
Hii ni kutokana na unyeti wa uchaguzi wa klabu ya Yanga yenye matawi nchini kote.
TFF KUFANYA MAREKEBISHO YA KANUNI ZAKE
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limebaini kuwepo kwa vitendo vyaa wanafamilia wa mpira wa miguu Tanzania kujihusisha na masuala ya Siasa wakiwa katika mavazi rasmi ya mpira ambayo yana nembo za vilabu na wadhamini wa Ligi.
Katiba ya TFF ibara ya I (4) inatamka “TFF is neutral in matters of politics and religion. Discrimination of any kind against a country, private person or group of people on account race, skin colour, ethnic, national or social origin, gender, language, religion, political opinion or any other opinion, wealth, birth or any other status is strictly prohibited and punishable by suspension or expulsion.”
Aidha kanuni za Ligi, Kanuni ya 14(40) inatamka: “ Hairuhusiwi kwa mchezaji, mwamuzi au kiongozi wa timu kuonyesha kwa njia yeyote tangazo au ujumbe unaohusiana na dini yeyote au ulio na madhumuni maalum bila idhini ya TFF/TPLB”.
TFF inachukua fursa kuwakumbusha wana familia wote wa mpira wakiwemo viongozi, wachezaji, waamuzi, makocha na madaktari wa michezo kuwa ni marufuku kuelezea hisia zao za kisiasa au kujihusisha katika kampeni za kisiasa wakiwa katika mavazi rasmi ya mpira zikiwemo jezi na track suites zenye nembo za TFF, vilabu wadhamini na ligi, Taifa stars au za washirika wa TFF wakiwemo wadhamini.
Aidha ni marufuku kwa mashabiki wa mpira kutumia fursa ya mechi za mpira wa miguu kubeba mabango au kusambaza ujumbe wa kisiasa.
Hatua kali zitachukuliwa kwa wataokiuka mahitaji ya katiba na kanuni za mashindano. TFF inatambua haki za wanamichezo kushiriki katika siasa ili mradi ushiriki wao hazikiuki kanuni na mahitaji ya katiba za TFF na FIFA
Subscribe to:
Posts (Atom)

















