KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Tuesday, September 15, 2015

MALINZI AZINDUA KAMBI YA U-13



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi leo amezindua rasmi kambi ya kikosi cha timu ya Taifa umri chini ya miaka 13 ambacho kitakua pamoja kuelekea fainali za Afrika za vijana umri chini ya miaka 17  (U17) zitakazofanyika nchini Tanzania mwaka 2019.

Kikosi hicho ni cha vijana 20 ambao waliteuliwa tokana na mashindano ya vijana ya umri chini ya miaka 13 (U13) yaliyofanyika Mwanza mwezi Juni mwaka huu.

Malinzi amezindua kambi hiyo itakayodumu kwa muda wa miaka mitano hadi mwaka 2019. Kambi hiyo itakuwa  kwenye shule ya kulea na kukuza vipaji vya mpira ya Alliance iliyopo jijini Mwanza.

Wakiwa Alliance vijana hao gharama za masomo, matunzo na vifaa zitatolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF).

Akizindua kambi hiyo Malinzi aliongea na wazazi wa watoto hao na kuwaahidi kuwa TFF kwa kushirikiana na shule ya Alliance itahakikisha vijana hao wanapewa elimu nzuri itakayozingatia maadili.

Wazazi wa watoto wametoa shukrani kwa uteuzi huu wa watoto wao na Mkurugenzi wa shule ya Alliance Bw James Bwire ameahidi kutoa elimu bora na mafunzo mazuri kwa vijana.

Jumla ya vijana 455 toka mikoa yote ya Tanzania walishiriki mashindano hayo

Sunday, September 13, 2015

OLE GABRIEL AFUNGUA MICHUANO YA AIRTEL RISING STAR



Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Elisante Ole Gabriel leo Jumapili, Septemba 13, amezindua rasmi michuano ya Airtel Rising Stars kitaifa kwenye uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa michuano hiyo, Ole Gabreil ameipongeza kampuni ya simu za mkononi ya Airtel nchini kwa kuendesha michuano hiyo, ambayo inawapa nafasi vijana wa kike na kiume kuonyesha vipaji vyao vya kucheza mpira wa miguu.

Ole Gabriel ameiomba Airtel kuendelea kudhamini michuano hiyo na kutanua wigo zaidi kwa mikoa mingi kuweza kushiriki kwenye mashindano hayo.

Aidha Ole Gabriel ameiitaka TFF kuwasiliana na Wizara yake pindi wanapoagiza vifaa vya michezo nje ya nchi mapema, ili ofisi yake iweze kulisadia Shirikisho katika suala la ushuru wa vifaa vya michezo vinapoingia nchini.

Naibu katibu mkuu huyo aliyasema hayo wakati akijibu ombi la Makamu wa Rais wa TFF, Wallace Karia aliyeiomba Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo kuisaidia TFF kupata msamaha wa kodi pindi inapoingiza vifaa vya michezo nchini kwa ajili ya maendeleo ya mpira wa miguu.

Jumla ya timu saba za vijana wa kike na kiume zinashiriki fainali hizo za Taifa za Airtel Rising Stars zinazodhaminiwa na kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, ambapo vijana wenye vipaji huchaguliwa na kupata nafasi ya kujiunga na vituo vya michezo (Academy) za Dakara – Senegal na Doha – Qutar zinazomilikiwa na kampuni hiyo.

Mikoa inayoshiriki fainali hizo ni Arusha, Ilala, Kinondoni, Temeke, Mbeya, Morogoro, Mwanza na Mbeya

KING MAJUTO YUKO HIJJA MAKKA

MSANII maarufu wa filamu na vichekesho nchini, Amri Athumani 'King Majuto' (kulia) akiwa na mahujaji wenzake katika mji wa Madina juzi kabla ya kwenda Makka, ikiwa ni mwendelezo wa ibada ya hija.

NGOMA, MSUVA WAIUA COASTAL UNION




NA AMINA ATHUMAN
MABAO mawili yaliyofungwa na Simon Msuva na Donald Ngoma yameiwezesha Yanga kuibuka na ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Coastal Union.
Katika mchezo huo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliandika bao lake la kwanza dakika ya saba kupitia kwa Msuva aliyeachia shuti kali akiunganisha pasi ya Kelvin Yondan.
Bao la pili lilipatikana dakika ya 42 baada ya Ngoma kuunganisha mpira uliorudi uwanjani baada ya kipa wa Coastal Union kupangua mpira wa krosi iliyochongwa na Msuva.
Katika mchezo huo, Yanga ilianza mchezo kwa kasi na kushambulia lango la wapinzani wao kama nyuki ikitafuta mabao ya kufunga.
Dakika ya 12 Coastal Union ilibadilisha mfumo wa uchezaji na wachezaji wake kurudi nyuma kwa ajili ya kuzuia mashambulizi.
Hali hiyo ilisaidia kupunguza kasi ya Yanga lakini dakika ya 18 Niyonzima alibaki na kipa Sebwato Nicholas, lakini shuti alilopiga lilitoka pembeni kidogo ya goli.
Coastal Union ilijibu shambulizi hilo dakika ya 23 ambalo halikuzaa matunda kabla ya kufanya mabadiliko na kumtoa Adeyum Ahmed na kuingia Twaha Ibrahim
Mabadiliko hayo yaliamsha ari ya wachezaji wa Coastal Union ambapo dakika ya 29 Ali Ahmed alipata nafasi ya kufunga na kuachia shuti kali lililopaa mita chache na kutoka nje.
Coastal Union ilipata nafasi nyingine dakika ya 76 kupitia kwa Patrick Protas baada ya kubaki na kipa lakini mpira aliopiga ulitoka pembeni kidogo ya goli.
Timu zote ziliendelea kushambuliana kwa zamu lakini hadi dakika 90 zinamalizika Yanga ndiyo iliyoondoka uwanjani na kicheko baada ya kupata pointi tatu.

Ali Mustapha, Mbuyu Twite, Haji Mwinyi, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Thaban Kamusoko, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amis Tambwe/Malimi Busungu, Donald Ngoma na Godfrey Mwashiuya/Deus Kaseke.
Coastal Union:Sebwato Nicholas, Hamad Juma, Yasin Mustapha, Ernest Joseph, Tumba Sued, Said Jeilan/Patrick Protas , Ali Ahmed, Yousoufa Sabo, Nasoro Kapama, Godfrey Wambura na Adeyum Ahmed.

MABAO 10 YATINGA MECHI ZA AWALI LIGI KUU, AZAM YAILAZA PRISONS 2-1


MABAO 10 tu yametinga nyavuni katika mechi  saba za ufunguzi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo, huku kipa mpya wa Mbeya City, Juma Kaseja akianza vibaya Uwanja wa Sokoine.
Kaseja amefungwa bao moja  na timu yake mpya ikilala 1-0 nyumbani mbele ya Kagera Sugar kutoka Bukoba na hakuna timu iliyoshinda kwa wastani wa zaidi ya bao 1-0 dhidi ya wapinzani wake.
Timu zote zote zimeshinda 1-0 na 2-1 baada ya mechi zote saba leo.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga Simba SC imewafunga bao 1-0 wakati Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara, Ndanda FC imelazimishwa sare ya 1-1 na Mgambo Shooting ya Tanga.
Uwanja wa Majimaji, Songea  wenyeji Majimaji FC wameshinda 1-0 dhidi ya JKT Ruvu, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Azam FC imeshinda 2-1 dhidi ya Prisons wakati Toto Africans imeshinda 1-0 dhidi ya Mwadui FC.
Timu zilizoanza kwa ‘mikosi’ zaidi Ligi ya msimu huu ni Stand United iliyofungwa 1-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Kambarage, Shinyanga na Mbeya City iliyofungwa 1-0 na Kagera Sugar Uwanja wa Sokoine, Mbeya.
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania itaendelea kesho wakati mabingwa watetezi, Yanga SC watakapomenyana na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
IMETOLEWA KUTOKA BLOGU YA BINZUBEIRY

SIMBA YAANZA VYEMA LIGI KUU, YAICHAPA AFRICAN SPORTS 1-0


SIMBA SC imeanza vyema Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji African Sports Uwanja wa Mkwakwani, Tanga jioni ya leo.
Shukrani kwake mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Hamisi Friday Kiiza ‘Diego’ aliyefunga bao hilo pekee dakika ya 56, akimalizia kwa kichwa krosi maridadi ya Nahodha Mussa Hassan Mgosi.
Simba SC ilicheza vizuri tangu mwanzo wa mchezo na kukaribia lango la wapinzani mara kadhaa, lakini uhodari wa kipa wa zamani wa Yanga SC, Yussuf Abdul uliwanyima mabao zaidi Wekundu hao wa Msimbazi.
Pamoja na kwamba imepanda msimu huu, African Sports maarufu kama Wana Kimanumanu walionyesha upinzani kwa Simba SC
Mshambuliaji Boniphace Maganga aliyesajiliwa msimu huu kutoka Marsh Academy ya Mwanza, alikosa bao la wazi baada ya kuunganishia juu ya lango krosi nzuri ya Simon Sserunkuma dakika ya 89.
Hussein Amir aliinyima Sports bao la kusawazisha dakika ya 90, baada ya kuunganishia juu ya lango krosi nzuri ya Ayoub Masoud.
Katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu leo, Azam FC imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Prisons ya Mbeya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Shukrani kwake Farid Mussa aliyefunga bao la ushindi dakika ya 86 baada ya Jeremiah kuisawazishia Prisons dakika ya 60, kufuatia
Kipre Herman Tchetche kuanza kuifungia Azam FC dakika ya 42.
Kikosi cha African Sports kilikuwa; Yusuph Yusuph, Ayubu Masoud, Mwaita Gereza, Juma Shemvuni, Rahm Abdallah, Novat Lufungo, Jemes Mendi/Ally Ramadhani dk83, Husein Amiri, Hasani Matemema, Omary Issa, Pera Mavuo/Bakari Masoud dk53.
Simba SC; Peter Manyika, Mohamed Husei ‘Shabalala’ Hassan Kessy, Jjuko, Majabvi, Awadh Juma, Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto/Simon Sserunkuma dk89, Mussa Hassan ‘Mgosi’,Hamisi Kiiza/Boniphace Maganga dk75 na Peter Mwalinyanzi.
IMETOLEWA BLOGU YA BINZUBEIRY

DK. FEENELLA KUZINDUA MICHUANO YA AIRTEL RISING STAR



 Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dr. Fenella Mkangara leo Jumapili, Septemba 13, 2015 saa 8 kamili mchana anatarajiwa kuzindua rasmi fainali za michuano ya Airtel Rising Star katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam.

Jumla ya timu sita zinatarajiwa kushiriki michuano hiyo ambayo imekua ikifanyika kila mwaka nchini kwa udhamini wa kampuni ya simu za mkononi ya Airtel, ambapo vijana wenye vipaji huchaguliwa na kupata nafasi ya kujiunga na vituo vya michezo (Academy) za Dakara – Senegal na Doha – Qutar zinazomilikiwa na kampuni hiyo.

Katika uzinduzi huo wa leo, timu za mkoa wa Ilala, Kinondoni, Mbeya, Morogoro, Mwanza na Temeke zinatarajiwa kupambana kusaka mshindi kwa fainali hizo za kitaifa.

Shirikisho la Mpira Miguu nchini (TFF), limetuma salamu za rambirambi kwa familia za Lubawa,  kufutia kifo cha mwamuzi mstaafu na kamishina wa TFF Saleh Lubawa kilichotokea jana jioni.

Katika salam zake kwenda kwa familia ya marehemu, TFF imesema inawapa pole wafiwa, ndugu jamaa na marafiki na kwa niaba ya familia ya mpira miguu nchini wapo pamoja na familia katika kipindi hichi cha maombolezo.

Mazishi ya marehemu Saleh Lubawa yanatarajiwa kufanyika leo jioni nyumbani kwake eneo la Kongowe – Kibaha.

MALINZI KUKUTANA NA WAZAZI WA U-13


Rais wa Shirikisho la Mpira Miguu nchini (TFF), Jamal Malinzi anatarajiwa kukutana wazazi wa vijana wenye umri chini ya miaka 13 (U-13) waliochaguliwa kujiunga na kituo cha michezo cha Alliance kilichopo jijini Mwanza.

Malinzi anatarajiwa kukutana na wazazi wa vijana hao siku ya jumatatu ya tarehe 14, Septemba 2015 saa 5 kamili asubuhi katika shule ya Alliance, kabla ya taratibu za kuwakabidhi vijana hao kwa uongozi wa kituo hicho.

Mapema mwezi Juni mwaka huu TFF iliendesha mashindano ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 13 (U-13) yaliyofanyika jijini Mwanza, ambapo jopo la makocha liliweza kuchagua wachezaji 20 wenye vipaji ambao watajiunga na kituo hicho kwa ajili ya masomo ya kawaida na kufundishwa michezo.

Mpango huo wa kuwaweka vijana katika kituo cha Alliance una lengo la kuandaa timu bora ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 17, itakayoshiriki kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Vijana wenye umri huo zitakazofanyika nchini Tanzania mwaka 2019.

DRFA YAZINDUA KOZI YA UKOCHA LESENI C




Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam,DRFA kwa kushirikiana na shirikisho la soka nchini TFF,leo imezindua rasmi kozi ya ukocha wa leseni C’ inayotambuliwa na shirikisho la kandanda barani afrika CAF.

Kozi hiyo ya wiki mbili inaendeshwa na mkufunzi, Salum Madadi ambaye ni mkurugenzi wa ufundi wa Tff,ikiwa na jumla ya washiriki 31 wengi wao wakiwemo makocha wa vilabu vya ligi daraja la pili,daraja la kwanza na ligi kuu.

Miongoni mwa washiriki hao ni pamoja na kocha msaidizi wa Simba,Suleiman Matola,katibu mkuu wa zamani wa Simba Muhina Kaduguda,kocha wa Ruvu shooting Tom Olaba,kocha wa makipa wa Yanga Juma Pondamali,nyota wa zamani wa Taifa Stars,Ally Mayai na Peter Tino.

Mgeni rasmi katika ufunguzi wa kozi hiyo ni mjumbe wa kamati ya utendaji ya Tff,Msafiri Mgoy,ambaye amewapongeza washiriki kwa uamuzi wao wa kutaka kujiongezea maarifa ya ufundishaji wa soka ,kwa kuwa Tanzania inakabiliwa na upungufu mkubwa wa makocha ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika ambayo yamepiga hatua kisoka.

Aidha amesema Tff imeweka mpango maalum wa kutunza kumbukumbu za makocha hao na wengine watakaopatikana,pamoja na kufuatilia kazi zao kwenye vilabu mbalimbali watakavyofundisha ili iwe rahisi kuwatengenezea mazingira mazuri ya kufanya kazi zao.

Naye mwenyekiti wa DRFA,Almasi Kasongo wakati akimkaribisha mgeni rasmi,amesema chama chake kinataraji pia kuendesha kozi za madaktari pamoja na kuendeleza mpango wake wa kuinua soka la vijana,ili taifa liwe na wachezaji wenye uwezo wa kushindana na mataifa mengine.

Kasongo amesema licha ya chama chake kuwa na mikakati ya kuhakikisha soka la mkoa wa Dar es salaam na nchi kwa ujumla linanyanyuka,lakini bado nguvu kumbwa inahitajika kutoka Tff pamoja na wadau wenye mapenzi mema na mpira wa nchi hii.

Friday, September 11, 2015

TASWA KUMUAGA JK OKTOBA 10


CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), kitatoa tuzo kwa Rais Jakaya Kikwete pamoja na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi katika miaka 10 akiwa Rais wa Tanzania.
Tukio hilo ambalo pia litahudhuriwa na Rais Kikwete, litafanyika Oktoba 8, mwaka huu ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam likiwa na lengo la wanamichezo kumuaga Rais Jakaya Kikwete.
TASWA itakabidhi tuzo maalum kwa Rais ikiwa ni kuthamini mchango wake kwa maendeleo ya michezo wakati wa miaka 10 ya uongozi wake na imebariki tukio hilo kama  ‘JK na Wanamichezo’.
Licha ya kutoa tuzo kwa Rais na wanamichezo 10 waliofanya vizuri zaidi, pia TASWA itatoa vyeti maalum kwa kampuni mbalimbali zilizosaidia kwa kiasi kikubwa kudhamini michezo katika miaka 10 ya Rais Kikwete.
Maandalizi muhimu yamekamilika kuhusiana na tukio hilo, ambapo wawakilishi kutoka vyama vyote vya michezo hapa nchini pamoja na wanamichezo wataalikwa kuhudhuria tukio hilo la kihistoria.
TASWA inamshukuru Rais Kikwete kwa kukubali kujumuika nasi siku hiyo ili kuagana na wanamichezo, ambao wameshuhudia mambo mazuri akiwafanyia katika uongozi wake, ambao utafikia tamati baada ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Pia TASWA inaishukuru Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa ushirikiano mkubwa iliotoa kuhakikisha tukio hilo linafanikiwa.
Tayari wadhamini mbalimbali wamejitokeza kusaidia na tunaomba wengine watuunge mkono, ambapo Jumanne Oktoba 15, TASWA itafanya mkutano na waandishi wa habari kutangaza mdhamini mshiriki mmoja, mkutano utakaofanyika ukumbi wa City Sports Lounge, Dar es Salaam.
TASWA imeona kuna haja ya wanamichezo kuagana na Rais Kikwete na kumpa tuzo kutokana na masuala mbalimbali aliyofanya kwa miaka yake 10 katika kusaidia kukuza michezo na sanaa hapa nchini.
Baadhi ya mambo hayo ni serikali yake ilivyolipia  makocha wa michezo ya soka, netiboli na ngumi na pia serikali ilipeleka wanariadha wetu China, Ethiopia na New Zealand kwa maandalizi ya mashindano ya kimataifa.
Pia tutamkumbuka Rais Kikwete kwa uamuzi wa kurejesha michezo shuleni pamoja na mashindano ya michezo kwa shule za msingi na sekondari (UMISHUMTA na UMISETA).
Yapo mambo mengi ambayo tukiyataja yote aliyofanya kuhusu michezo yatachukua nafasi kubwa, hivyo tuna kila sababu wanamichezo kujitokeza na kuagana na Rais wetu.

Ahsanteni,
Juma Pinto
Mwenyekitii TASWA
11/09/2015.

TFF, AZAM ZAREJESHA KOMBE LA SHIRIKISHO



Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kwa udhamini wa kampuni ya Azam Media kupitia Azamtv Sports leo wamezindua kombe la Shirikisho litakalofahamika kama Azam Sports Federation Cup (ASFC) ambalo litaanza kutimua vumbi mwezi Novemba mwaka huu kwa kushirikisha timu 64 nchini.

Kurudishwa kwa michuano hii imekua ni faraja kwa wapenzi na wadau wa mpira miguu nchini baada ya kukosekana kwa takribani miaka 13 michuano hiyo, ambapo sasa Bingwa wa kombe la Shirikisho ataiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika (CAFCC).

Akiongea na waandishi wa habari wakati wa uzindizi wa michuano hiyo na kuchezeshwa droo ya awali, Rais wa TFF Jamal Malinzi amemshukuru Mkurugenzi wa Azam Media Rhys Thorrington kwa kuweza kudhamini michuano ambayo itongeza ushindani zaidi nchini.

Malinzi amesema anaviomba vilabu vitakavyoshiriki michuano ya kombe la hilo, vionyeshe ushindani mkubwa kwani ndio nafasi pekee ya kuweza kuitangaza na kuonekana kwa kuwa michuano hiyo itakua ikionyeshwa moja moja na luninga ya Azamtv.

Aidha Malinzi amesema kila timu inayoshiriki michuano hiyo itapata fedha ya usafiri shilingi milioni 3, na vifaa vitakavyotolewa na mdhamini kampuni ya Azam Media.

Naye Mkurugenzi wa Azam media Rhys Thorrington amesema uhdmaini huo wa miaka mine una thamani ya fedha za kitanzania bilioni 3.3  ambapo timu zitakazoshiriki michuano hiyo zitapata nafasi ya kuonekana moja moja katika nchi zaidi ya saba barani Afrika kupitia kituo chao cha azamtv.

Mshindi wa Kombe la ASFC linalodhaminiwa na kampuni ya Azam kupitia Azamtv Sports, atajinyakuliwa kitita cha shilingi milioni hamsini (TZS 50,000,000), jumla ya timu 64 kutoka Ligi Kuu (VPL), ligi daraja la kwanza (FDL) na ligi daraja la pili (SDL) zitashirki katika kombe hilo.

Timu zote 24 za ligi daraja la pili na 8 za ligi daraja la kwanza 3, zilizopanda daraja na 5 zilizoshika nafasi za chini kwenye makundi yote zitashiriki katika raundi ya kwanzamwezi Novemba kwa kucheza mechi 16 na kupata washindi 16 ambao wataingia raundi ya pili.

Timu 16 zilizoshinda raundi ya kwanza na 16 zilizofanya vizuri ligi daraja la kwanza zitachanganywa na kupangwa kucheza mechi 16 nyingine za raundi ya pili mwezi Desemba.

Washindi wa raundi ya pili wataingia raundi ya tatu ambapo watachanganywa na timu 16 zilizopo ligi kuu na kuchezwa mechi 16 nyingine ambazo washindi wake wataingia raundi ya nne. Raundi hii ya tatu itafanyika mwezi Januari 2016.

Timu 16 zilizoshinda raundi ya tatu zitaingia raundi ya nne zitapangwa ili kucheza hatua hii ambayo itakuwa na mechi  8 na washindi 8 wataingia katika hatua inayofuata ambayo ni raundi ya tano au robo fainali. Raundi hii ya nne itachezwa Februari 2016.

Washindi wa raundi ya nne watapata nafasi ya kuingia raundi ya 5 ambayo pia ni robo fainali, droo itapangwa. Raundi hii ya tano itachezwa mwezi Machi 2016.

Washindi wa raundi ya tano au robo fainali watapangwa kucheza nusu fainali au raundi ya 6 mwezi Aprili.

Washindi wa nusu fainali watapambana katika fainali na kumpata bingwa wa Azam Sports Federation Cup 2015/16. Mechi ya fainali itachezwa wiki moja baada ya ligi kuu kumalizika na Bingwa atakabidhiwa kombe na zawadi ya fedha tasilimu shilingi milioni 50.

Mechi za raundi ya kwanza na raundi ya pili kama mshindi hatapatikana ndani ya dakika 90 basi mshindi atapatikana kwa kupigiana penati moja kwa moja. Mechi za raundi ya tatu na nne kama mshindi hatapatikana ndani ya dakika 90 mechi itarudiwa katika uwanja wa timu iliyokuwa mgeni mechi ya awali.

Mechi za robo fainali au raundi ya tano kama mshindi hatapatikana ndani ya dakika 90 hatua ya penati tano tano itaamua mshindi.

Kwa mechi za nusu fainali na fainali kama mechi itaisha kwa sare ndani ya dakika 90, dakika 30 za nyongeza zitachezwa, na kama hakutakuwa na mshindi penati zitaamua mshindi.

Ratiba ya raundi ya kwanza:

AFC -Arusha Vs Polisi Mara, Polisi -Tabora Vs Green Worries -Dar es salaam, Karikoo Lindi Vs Changanyikeni -Dar es salaam, Mkamba Rangers –Morogoro Vs Mvuvuma - Kigoma, Rhino Tabora Vs Allicane - Mwanza, Panone Kilimanjaro Vs Coca Cola Mbeya, Polisi Morogoro Vs Mshikamo Dar es salaam, Sabasaba Morogoro Vs Abajalo Tabora.

Magereza Iringa Vs Polisi Dar es salaam, Milambo Tabora Vs Town Small Ruvuma, Abajalo Dar es salaam Vs Transit Camp Dar es salaam, Ruvu Shooting Vs Cosmopolitan Dar es salaam, JKT Rwamkoma Mara Vs Villa Sqaud (Dar es salaam), Wenda FC Mbeya Vs Madini Arusha, Pamba FC Mwanza Vs Polisi Dom, Singida United Vs Bulyanhulu FC Shinyanga.

Wednesday, September 9, 2015

BIMA YA AFYA KUDHAMINI LIGI KUU BARA



MFUKO wa Bima ya Afya nchini (NHIF) umeingia makubaliano ya udhamini wa bima ya afya kwa wachezaji na viongozi wa benchi la ufundi kwa vilabu 16 vya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Akiongea na waandishi wa habari katika mkutano uliofnayika leo ofisi za TFF zilizopo Karume, Katibu Mkuu wa TFF Mwesigwa Selestine amesema wanaishukuru NHIF kwa kuwapa udhamini huo ambao utavisaidia vilabu vya Ligi Kuu katika matibabu ya wachezaji na bechi ka ufundi.

Tumekua na kilio cha muda mrefu juu ya vilabu vya Ligi Kuu kuwa na Bima za afya kwa wachezaji, kitu ambacho kipo kikanuni lakini vilabu vilikuwa vinashindwa kutimiza hitaji hilo la kikanuni na sasa TFF kwa kushirikian na NHIF tutakua tumeiondoa tatizo hilo.

Naye Mkuu wa Mawasiliano wa NHIF, Sungi amesema udhamini huo wa bima ya matibabu kwa wachezaji na benchi la ufundi utatolewa kwa matibabu yote yatakayofnayika ndani ya nchi.

Mchezaji au kiongozi pindi atakapopata tatizo la kuumwa, basi ataweza kutibiw akatika hospitali yoyote yenye huduma ya Bima katika eneo alilopo, lengo ni kuhakikisha wanakua na afya njema kwa ajili ya kushiriki vizuri mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Vodacom.

Lengo letu ni kuona wachezaji wanapata huduma ya afya popote wanapokuwa na kuweza kushiriki vizuri katika michuano ya Ligi Kuu, na kuweza kuzitumikia vyema timu zao kwenye mashindano.

Ofisa Mtendaji wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura kwa niaba ya vilabu vya Ligi Kuu amesema wanashukuru kupata udhamini huo wa bima ya afya, uwepo wa NHIF umevipunguzia vilabu mizigo wa matibabu na sasa vilabu vitaweza kushiriki vizuri kwenye michuano ya msimu huu.

'MAPROO' WAPIGWA 'STOP' LIGI KUU




NA VICTOR MKUMBO
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limesema kuwa ni marufuku kwa klabu za ligi kuu kuwachezesha wachezaji wa kimataifa katika michuano ya ligi kuu msimu huu iwapo hazitawalipia ada ya Dola za Kimarekani 2,000 (sawa na sh. milioni 4.6).
Katika mkutano wa Kamati ya Utendaji uliofanyika mwaka huu, Zanzibar, kamati ilikubaliana kuwa kila mchezaji ambaye atasajiliwa na klabu ya ligi kuu msimu huu, atalipiwa ada ya Dola 2,000 kabla ya kuanza kwa ligi hiyo.
Hata hivyo, baadhi ya klabu zimeshatangaza kugomea kulipa ada hiyo kwa madai kuwa uamuzi huo umechukuliwa kwa kushtukiza.
Kamati ya Utendaji ya TFF ilifikia makubaliano hayo ili wachezaji wa kimataifa waliosajiliwa Tanzania, waweze kuchangia fedha hizo kwa ajili ya maendeleo ya soka ya wanawake na vijana.
Akizungumza Dar es Salaam, jana, Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto, alisema wameamua kuzikumbusha klabu zote zilizosajili wachezaji wa kigeni ili kuwalipia ada hiyo.
Alisema katika ligi kuu msimu huu, wapo wachezaji 27 wa kigeni, waliosajiliwa na timu mbalimbali, zikiwemo Simba, Yanga  na Azam. Klabu hizo zimesajili wachezaji saba kila moja.
Kizuguto alisema  wachezaji wengine wa kigeni wamesajiliwa katika timu za Mbeya City, Stand United, African Sports na Coastal Union.
“Tunazikumbusha klabu za Ligi Kuu Bara zilizosajili wachezaji kutoka nje ya nchi, kuwalipia ada ya Dola 2,000 kwa kila mchezaji kabla ya ligi kuanza,” alisema.
Aliongeza kuwa klabu itakayolipia idadi ndogo ya wachezaji au wote saba, ndio itakaowatumia kwa  msimu huu na si vinginevyo.
Ofisa huyo alisema wanatarajia kutoa majina ya timu na orodha ya wachezaji waliolipiwa ada baada ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Bara, Jumamosi wiki hii.

LIGI KUU TANZANIA BARA KUANZA JUMAMOSI, MKUTANO MKUU TFF DESEMBA 19


Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2015/2016 inatazamiwa kuanza kutimua vumbi jumamosi Septemba 12, 2015 kwa michezo saba kuchezwa katika viwanja tofauti nchini.

Ndanda FC ya Mtwara watakua wenyeji wa Mgambo Shooting katika uwanja wa Nagwanda Sijaona mjini Mtwara, Wana kimanumanu African Sports watawakaribisha Simba SC katika uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Wana Lizombe Majimaji wakiwa wenyeji wa maafande wa JKT Ruvu katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.

Azam FC watakua wenyeji wa Tanzania Prisons kaika uwanja wa Chamazi Complex, Stand United FC chama la wana watawakaribisha Mtibwa Sugar katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, Toto Africans watawakaribisha Mwadui FC uwanja wa CCM Kirumba na Mbeya City watacheza na Kagera Sugar katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Jumapili Ligi Kuu itaendelea kwa mchezo mmoja tu utakaochezwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam ambapo mabingwa watetezi wa kombe hilo Yanga SC watawakribisha wagosi wa kaya Coastal Union.

Katika hatua nyingine klabu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera itatumia  Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora kwa mechi zake za nyumbani dhidi ya Toto Africans (Sept 26), JKT Ruvu (Sept 30), Tanzania Prisons (Oct 4) na Yanga (Oct 31).

Mabadiliko hayo yamefanyika kupisha shughuli ya uwekaji nyasi bandia inayoendelea kwenye uwanja wao wa Kaitaba mjini Bukoba unaofanywa na wataalamu kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Kikao cha Kamati ya Utendaji cha Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) kilichokaa tarehe 06/09/2015 kilipanga tarehe ya Mkutano Mkuu wa TFF kuwa ni Disemba 19-20, 2015.

Ajenda za Mkutano zitakuwa ni kwa mujibu wa katiba ya TFF.

Sunday, September 6, 2015

TAIFA STARS YATOKA SULUHU NA NIGERIA




Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imeshindwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani baada ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana na timu ya Taifa ya Nigeria ‘Super Eagles’.
Stars itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka na ushindi katika mchezo huo uliopigwa kwenye dimba la Taifa kwani ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga ukilinganisha na wapinzani wao.
Thomas Ulimwengu, Mrisho Ngassa na Mbwana Samatta walipoteza nafasi za wazi za kuweka mpira wavuni huku kipa wa Nigeria akiibuka nyota wa mchezo kutokana na kuzuia mashambulizi mengi yaliyokuwa yakifanywa na wachezaji wa Stars.
Shukrani za pekee zimuendee Charles Boniface Mkwassa na benchi lake la ufundi kutokana na kuboresha kiwango cha Stars kwani licha ya kutopata ushindi leo, timu imeonekana ikicheza kwa kuelewana.
Nigeria imefikisha pointi nne kutoka michezo miwili baada ya matokeo ya leo, iko kileleni wakati Taifa Stars ina pointi moja.
Misri itakwaana na Chadi kesho katika mchezo mwingine wa kundi la Stars

Friday, September 4, 2015

MKWASA ATAMBA TAIFA STARS IPO TAYARI KUIKABILI NIGERIA




Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro, Charles Mkwasa amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa kesho dhidi ya Nigeria kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2017.

Akiongea na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa TFF uliopo Karume, Mkwasa amesema vijana wake wapo katika hali nzuri kuelekea kwenye mchezo huo wa kesho ambao ni muhimu kwa Taifa Stars.

“Tumefanya mazoezi kwa takribani siku kumi, vijana wako katika hali nzuri ya mchezo, uwezo waanaouonyesha mazoezini ni wa hali ya juu na unatupa matumaini ya kufanya vizuri” Alisema Mkwasa.

Aidha Mkwasa amesema katika mpira hakuna kinachoshindakana, anatambua Nigeria ni timu kubwa Afrika, wameshatwaa ubingwa wa Afrika mara tatu, lakini mpira wa sasa lolote linaweza kutokea, hivyo sisi tumejiandaa vilivyo kufanya vizuri katika mchezo huo.

Mwisho Mkwasa amesema wamejindaa vizuri kwa mchezo huo wa kesho, na kuwaomba watanzania kuja kuwapa sapoti wachezaji uwanjani kwa kuwashangilia muda wote wa mchezo, na kusema kikosi chake hakina mchezaji majeruhi hata mmoja kuelekea kwa mechi hiyo.

Mechi hiyo ya kesho jumamosi itachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Rwanda ambao ni Louis Hakizimana (mwamuzi wa kati) Honore Simba (mwamuzi msaidizi), Jean Bosco Niyitegeka (mwamuzi msaidizi), Abdoul Karim Twagiramukiza (mwamuzi wa akiba) na kamisaaa wa mchezo ni Charles Kasembe kutoka nchini Uganda ambao wote tayari wameshawaili jijini Dar es salaam tangu jana jioni.

Tiketi za mchezo huo tayari zimeshaanza kuuzwa leo saa 4 kamili asubuhi katika vituo vya (i) Ofisi za TFF - Karume , (iii) Mbagala – Dar live, (iv) Ubungo – Oilcom, (v) Makumbusho – Stendi, (vi) Uwanja wa Taifa, (vii) Mwenge – Stendi, (viii) Kivukoni-  Feri, (ix) Posta – Luther House, (x) Big Bon – Msimbazi Kariakooo

Viingilio vya mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON Qaulifier 2017) kundi G itakua ni VIP A Tsh 40,000, VIP B Tsh 30,000, VIP C Tsh15,000, Rangi ya Machungwa (Orange) Tsh 10,000, na viti vya rangi ya Bluu na Kijani Tsh 7,000.

TFF inawaomba watanzania, wapenzi na wadau wa mpira wa miguu kununua tiketi za mchezo huo katika magari yaliyopo kwenye vituo vilivyotajwa ili kuondokana na tatizo la kuuziwa tiketi zisizokuwa halali.

Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na idara nyingine za kiusalama wameandaa usalama wa kutosha katika kuelekea kwenye mchezo na kuhakikisha kila mpenzi wa mpira wa miguu anaingia kushuhudia mchezo huo salama na kuondoka salama.

Mchezo huo utaanza saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Rwanda ambao wanatarajiwa kuwasili leo jioni pamoja na kamisaa wa mchezo huo.

Wakati huo huo Kikosi cha wachezaji 23 cha timu ya Taifa ya Nigeria (Super Eagles) kimewasili nchini jana usiku na kufikia katika hoteli ya Kempsink iliyopo eneo la Posta ambapo leo jioni watafanya mazoezi katika uwanja wa Taifa uliopo jijini Dar es salaam.

Kikosi hicho cha Nigeria kinachoongozwa na kocha Sunday Oliseh kinawajumuisha makipa Ikeme Onoro, Ezenwa Ikechukwu, walinzi Thomas Olufemi, Balogun Aderemi, kwambe Solomon, Omeruo Keneth, Ekong William, Oboroakpo Austin, Akasi Chima, na Madu Kingsley.

Wengine ni viungo Ibrahim Rabiu, Muhamed Usman, Uzochukwu Izunna, Haruna Lukman, Nwankwo Obiora, Igboun Emeka, washambuliaji Simon Daddy, Ujah Anthony, Emenike Chinenye, Musa Ahmed, Aggreh Obus na Eduok Samuel.

Thursday, September 3, 2015

NGASSA, SAMATTA, ULIMWENGU WAJA KUIONGEZEA NGUVU STARS


Wachezaji watatu wa kimataifa wa Tanzania wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi, Mrisho Ngasa (Free State – Afrika Kusini) Thomas Ulimwengu na Mbwana Samatta (TP Mazembe – Congo DRC) wamejiunga na kambi ya Taifa Stars iliyopo katika hoteli ya Urban Rose – Kisutu jana jijini Dar es salaam.

Kocha Mkuu wa Taifa Stars Charels Mkwasa amewapokea wachezaji hao na jana kufanya mazoezi pamoja na wachezaji waliokuwa kambini nchini Uturuki saa 10 jioni katika uwanja Taifa jijini Dar salaam.

Kwa mujibu wa ratiba ya kocha Mkwasa Stars leo alhamis itaendelea na mazoezi jioni saa 10 katika uwanja wa Taifa kabla ya kufanya mazoezi mepesi ya mwisho kesho ijumaa asubuhi.

Wachezaji waliopo kambini ni magolikipa Ally Mustafa, Said Mohamed, walinzi Juma Abdul, Shomari Kapombe, Haji Mwinyi, Mohamed Hussein, Kelvin Yondani, Hassan Isihaka na nahodha Nadri Haroub “Cannavaro”.

Viungo ni Himid Mao, Frank Domayo, Mudathir Yahya, Said Ndemla, Salum Telela, Deus Kaseke, Saimon Msuva na Farid Musa, huku safu ya ushambuliaji ikiwa na John Bocco, Rashid Mandawa, Ibrahim Ajib, Thomas Ulimwengu, Mrisho Ngasa na Mbwana Samatta.



Maandalizi ya mchezo kati ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Nigeria (Super Eagles) yamekamilika, ambapo leo Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo huo wa jumamosi kati huku kiingilio cha chini kabisa kikiwa shilingi elfu saba tu.

Viingilio vya mchezo huo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON Qaulifier 2017) kundi G itakua ni VIP A Tsh 40,000, VIP B Tsh 30,000, VIP C Tsh15,000, Rangi ya Machungwa (Orange) Tsh 10,000, na viti vya rangi ya Bluu na Kijani Tsh 7,000.

Tiketi za mchezo huo zinatarajiwa kuanza kuuzwa kesho siku ya ijumaa saa 4 kamili asubuhi katika vituo kumi vifuatavyo:
(i) Ofisi za TFF - Karume

(ii) Buguruni – Oilcom

(iii) Mbagala – Dar live

(iv) Ubungo – Oilcom

(v) Makumbusho – Stendi

(vi) Uwanja wa Taifa

(vii) Mwenge – Stendi

(viii) Kivukoni-  Feri

(ix) Posta – Luther House

(x) Big Bon – Msimbazi Kariakooo

TFF inawaomba watanzania, wapenzi na wadau wa mpira wa miguu kununua tiketi za mchezo huo katika magari yaliyopo kwenye vituo vilivyotajwa ili kuondokana na tatizo la kuuziwa tiketi zisizokuwa halali.

Jeshi la Polisi nchini kwa kushirikiana na idara nyingine za kiusalama wameandaa usalama wa kutosha katika kuelekea kwenye mchezo na kuhakikisha kila mpenzi wa mpira wa miguu anaingia kushuhudia mchezo huo salama na kuondoka salama.

Mchezo huo utaanza saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki utachezeshwa na waamuzi kutoka nchini Rwanda ambao wanatarajiwa kuwasili leo jioni pamoja na kamisaa wa mchezo huo.

Waamuzi wa mchezo huo ni Louis Hakizimana (mwamuzi wa kati) Honore Simba (mwamuzi

msaidizi), Jean Bosco Niyitegeka (mwamuzi msaidizi), Abdoul Karim Twagiramukiza (mwamuzi wa akiba) wote kutoka Rwanda na kamisaaa ni Charles Kasembe kutoka nchini Uganda

Wednesday, September 2, 2015

NIGERIA KUTUA DAR KESHO


Timu ya Taifa ya Nigeria (Super Eagles) inatarajiwa kuwasili kesho AlhamisI saa nne usiku kwenye uwanja wa JK Nyerere jijini Dar es salaam kwa usafiri wa ndege binafsi tayari kwa mchezo dhidi ya Tanzania siku ya jumamosi uwanja wa Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano cha Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Nigeria (NFF), kupitia kwa Toyin Ibitoye msafara huo unatarajiwa kuwa na wachezaji 23 pamoja na viongozi wa benchi la ufundi linaloongozwa na kocha mkuu Sunday Oliseh pamoja na viongozi wengine waandamizi wa shirikisho hilo.

Nigeria inatarajiwa kufanya mazoezi siku ya ijumaa saa 10 jioni katika uwanja wa Taifa, ikiwa ni mazoezi mepesi ya kuelekea kwenye mchezo huo.

KOZI YA UKOCHA LESENI B YAFUTWA Z'BAR
 Kozi ya makocha wa CAF ya Leseni B iliyokua ifanyike kwa muda wa wiki tatu mwezi Septemba mwaka huu kisiwani Zanzibar sasa imefutwa kufuatia kupeleka mpira mahakamani.

Sasa kozi hiyo itafanyika tena pindi kesi ya mpira itakapoondelewa mahakamani. Kumekua na hali ya kutokuelewana kwa uongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu kisiwani Zanzibar (ZFA) hali iliyopelekea uongozi wa ZFA kupelekwa mahakamani.

Kwa mujibu wa kanuni za FIFA, masuala ya mpira wa miguu hayapaswi kupelekwa mahakamani



VODACOM YAKABIDHI VIFAA VYA MICHEZO KWA TIMU ZA LIGI KUU




Kampuni ya mawasiliano ya Vodacom Tanzania, ambayo ni mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya mpira wa miguu Tanzania bara leo imekabbidhi vifaa kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo yenye thamani ya shilingi milioni 490,00,000.

Akikabidhi vifaa hivyo leo jijini Dar es salaam, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom Kelvin Twisa alsiema kuwa kwa mara nyingine tena katika kuhakikisha ligi ya soka nchini inaenda vizuri Vodacom inakidhi vifaa mbalimbali vy a ligi ambavyo ni jezi za kawaida, jezi za mechi, viatu na vifaa vingine vinayohitajika.

“Tunajisikia furaha kukabidhi vifaa hivi siku ya leo tukiwaa tunatekeleza matakwa ya mkataba wa udhamini, ni imani yetu kwamba timu zitakazoshiriki lii zimejiandaa vya kutosha  kwa msimu mpya 2015/2016” Alisema Twissa.

Twissa alisema Vodacom inaendelea kudhamini ligi kuu kwa sababu soka ni mchezo unaopendwa sana hapa nyumbani ukiwa na washabiki wengi hivyo inapenda kuona wananchi ambao baadhi yao ni wateja wake wanapata buruddaniya mchezo waupendao pia siku zote inaamini kuwa michezo ni ajira kubwa duniani kote, ikiendelezwa inaweza kubadilisha maisha ya watu wengi na taifa kunufaika kwa mapato makubwa ya kodi kutoka sekta hii.

 Aliwataka wadhamini wengine kujitokeza ili kuboresha zaidi ligi ya Tanzania na kuongeza maslahi kwa wachezaji wanaoshiri katika ligi “Tukiunganisha nguvu timu zetu zinaweza kuwa na wachezaji wa kimataifa pia ni muhimu kwa wadau mbalimbali kuanza kuwekeza katika timu za vijana chipukizi kwa kuwa vipaji vinaanza ngazi ya chini ambako vinapaswa kuibuliwa na kuendelezwa” Alisema Twissa.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura aliishukuru Kampuni ya Vodacom na kuvitaka vilabu vinavyoshiriki ligi kuu ya Vodacom kuheshimu chapa ya mdhamini wakati wote wa ligi.

“Ninatoa mwito kwa vilabu vyote kutumia jezi zenye nembo ya mdhamini katika kuhakikisha ligi inafanikiwa kama inavyotakiwa” alisema.

Aliongeza kuwa TFF isingependa kutumia kanuni na sharia kuadhibu klabu inayokwenda kinyume, bali kila klabu izingatie masharti ya madhamini kama ambavyo anavyotimiza haki yake ya kuwapatia vifaa.

 Alisema ligi ya mwaka huu itakuwa bora kutokana na maandalizi yote kukamilika mapema pia timu zitakazoshiriki zimejiandaa vya kutosha kuhakikisha ligi inakuwa na msisimko na ushindani mkubwa.

Tuesday, September 1, 2015

TAIFA STARS YAMALIZA KAMBI UTURUKI


Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro chini ya Kocha wake Mkuu Charles Boniface Mkwasa imefanya mazoezi yake ya mwisho leo asubuhi katika viwanja vya hoteli ya Green Park Kartepe – Kocaeli nchini Uturuki.

Taifa Stars ambayo imeweka kambi nchini Uturuki kwa takribani wiki moja, inajiwinda na mchezo wake dhidi ya Nigeria siku ya Jumamosi Septemba 5, 2015 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa Afrika mwaka 2017.

Kocha Mkuu wa Stars Charles Mkwasa akiongea na tovuti rasmi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) www.tff.or.tz amesema anashukuru kambi imekua na mafanikio makubwa kwani vijana wanaonyesha mabadiliko makubwa sana.

“Ukiondoa mchezaji moja tu ambaye ni majeruhi Abdi Banda, Mkwasa amesema wachezaji wengine wote wapo fit na kila mmoja atakayepata nafasi katika mchezo wa sikuya jumamosi atafanya vizuri” amesema Mkwasa.

Mkwasa amesema mazingira ya kambi yamekua mazuri, na katika mechi ya maozezi dhidi ya Libya iliyochezwa siku ya ijumaa, vijana wake walicheza vizuri kwa nguvu na kufuata maelekezo yake, makosa machache yaliyojitokeza katika mchezo huo wameyafanyia kazi na sasa anaamini wako tayari kuwakabili Nigeria.

Mwisho Mkwasa amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi uwanja wa Taifa siku ya jumamosi  kuishangilia timu ya Taifa, kwani uwepo wa washabiki wengi uwanjani utawaongeza morali zaidi wachezaji na kujiona wapo nyumbani wanapambana kwa ajili ya Taifa lao.

Naye nahodha wa Taifa Stars, Nadir Haroub “Cannavaro” amesema maandalizi waliyopata ni mazuri na yamewajenga vilivyo kuelekea kwenye mchezo dhidi ya Nigeria siku ya jumamosi na kuwaomba watanzania kuja kwa wingi kuwasapoti.

Nadir amesema wao kama wachezaji kila mmoja yupo fit na anahitaji  kucheza mechi hiyo, hivyo yeyote atakayepata nafasi ya kucheza ana imani atafanya vizuri katika kuipeperusha bendera ya Tanzania.

Stars ambayo iliweka kambi ya takribani siku nane katika milima ya Katrepe - Kocaeli, inatarajiwa kuodoka kesho jumanne saa 1 jioni nchini Uturuki kurejea nyumbani kwa usafiri wa shirika la Ndege la Uturuki (Turkish Airlines) na kuwasili uwanja wa JK Nyerere majira ya saa 9 kasoro usiku.

Mara baada ya kuwasili Dar es salaam timu itaendelea na kambi kwa kufanya mazoezi mepesi siku ya jumatano pamoja wa wachezaji wa kimataifa Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Mrisho Ngasa katika uwanja wa Taifa kujiandaa na mchezo wa siku ya jumamosi dhidi ya Nigeria.