KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Sunday, July 14, 2013

TAIFA STARS YAKERA MASHABIKI

Taifa Stars imeshindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani baada ya leo (Julai 13 mwaka huu) kufungwa bao 1-0 na Uganda (The Cranes) katika mechi ya kwanza ya mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.


Denis Iguma ndiye aliyefunga bao hilo pekee kwa Uganda dakika moja baada ya mwamuzi Thierry Nkurunziza kutoka Burundi kupuliza filimbi kuanzisha kipindi cha pili cha mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumzia matokeo hayo, Kocha wa Stars, Kim Poulsen amesema mpira wa miguu ni mchezo wa kufunga mabao ambapo timu ilipata nafasi nzuri katika dakika ya kwanza tu lakini ilishindwa kuibadili kuwa bao.

“Uganda walitengeneza nafasi moja tu katika kipindi cha kwanza wakati sisi tulikuwa nazo kadhaa. Kipindi cha pili tuliwapa nafasi wakafunga bao lao. Lakini kwa kifupi kama wao wameweza kufunga hapa (Dar es Salaam), hata sisi tunaweza kufunga Kampala,” amesema Kim akizungumzia nafasi ya timu yake kusonga mbele.

Timu hizo zitarudiana jijini Kampala kati ya Julai 26 na 27 mwaka huu ambapo mshindi ndiye atakayepata tiketi ya kwenda kwenye fainali za tatu za CHAN zitakazofanyika Afrika Kusini. Stars ilicheza fainali za kwanza za CHAN zilizofanyika mwaka 2009 nchini Ivory Coast.

MAFTAH: BADO SIJAAMUA WAPI PA KWENDA

BEKI wa zamani wa klabu ya Simba, Amir Maftah amesema bado hajafanya mazungumzo na timu yoyote kwa ajili ya kuichezea katika msimu ujao wa ligi kuu.

Akizungumza na Burudani kwa njia ya simu juzi, Maftah alisema kwa sasa anakabiliwa na majukumu mengi ya kifamilia hivyo hawezi kuzungumzia masuala ya usajili.

Hata hivyo, Maftah alisema anatarajia kujua wapi pa kwenda baada ya siku chache zijazo. Ligi kuu ya Bara imepangwa kuanza Agosti 24 mwaka huu.

Maftah alisema tangu alipotofautiana na uongozi wa Simba na kusimamishwa kuichezea timu hiyo, amekuwa akifanya mazoezi kwa kujitegemea kwa lengo la kujiweka fiti.

"Nilikuwa nyumbani Mwanza kushughulikia matatizo ya kifamilia, nimerudi Dar es Salaam siku chache zilizopita. Natarajia kuanza mazungumzo na klabu mbalimbali siku chache zijazo,"alisema.

Beki huyo wa zamani wa Taifa Stars alisema tayari klabu kadhaa za ligi kuu zimeonyesha nia ya kutaka kumsajili, lakini bado hajaamua wapi pa kwenda.

Maftah, ambaye amewahi kung'ara katika klabu za Mtibwa Sugar, Yanga na Simba, alisimamishwa pamoja na wachezaji wenzake watano kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Kauli ya beki huyo imekuja siku chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti wiki iliyopita kuwa, anatarajia kujiunga na Coastal Union ya Tanga kwa ajili ya msimu ujao.

Hata hivyo, mmoja wa wakurugenzi wa Coastal Union, Bin Slum alikanusha taarifa hizo na kusema hawana mpango wa kusajili mchezaji mwingine kutoka Simba. Tayari Coastal Union imeshawasajili Haruna Moshi 'Boban' na Juma Nyosso.

KASEJA:SIWEZI KUKOSA TIMU YA KUCHEZA

KIPA namba moja wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars , Juma Kaseja amewatoa hofu mashabiki wake kwa kuwaambia, hawezi kukosa timu ya kuchezea msimu ujao wa ligi kuu ya Tanzania Bara.

Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Kaseja alisema atatangaza jina la timu atakayojiunga nayo msimu ujao baada ya pambano la michuano ya Kombe la CHAN kati ya Taifa Stars na Uganda.

Taifa Stars inatarajiwa kushuka dimbani keshokutwa kumenyana na Uganda kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya timu hizo kurudiana kati ya Julai 25 na 26 mwaka huu mjini Kampala.

Kaseja alisema kwa sasa ameelekeza nguvu na akili zake katika pambano hilo ili kuhakikisha anaisaidia Taifa Stars kupata ushindi na kujisafishia njia ya kufuzu kucheza fainali za michuano hiyo.

Kipa huyo wa zamani wa Simba alisema, anamshukuru Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen kwa kumuamini na kumwita tena kwenye kikosi chake na kuongeza kuwa, jukumu lake ni kudhihirisha kwamba bado yupo juu kisoka.

"Ninachoweza kuwaambia mashabiki wangu ni kwamba siwezi kukosa timu ya kuchezea msimu ujao. Lakini kwa sasa siwezi kuitaja kwa sababu akili yangu iko kwenye pambano letu na Uganda. Nitaitaja baada ya mchezo huo,"alisema kipa huyo, ambaye pia aliwahi kuzidakia Moro United na Yanga.

Kaseja amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi ili kuwapa nguvu na kuwaongezea ari wachezaji na kushinda pambano hilo.

Simba ilitangaza kumtema kipa huyo wiki mbili zilizopita baada ya kutokea mvutano miongoni mwa viongozi wa klabu hiyo, ambapo baadhi walitaka aongezwe mkataba mpya na wengine wakitaka aachwe.

Uchunguzi uliofanywa na Burudani umebaini kuwa, huenda kipa huyo akajiunga na klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro au Coastal Union ya Tanga, japokuwa viongozi wa klabu hizo mbili wamekanusha kuwepo kwa mipango hiyo.

Thursday, July 11, 2013

NYOTA MPYA SIMBA KAMA OKWI



KLABU ya Simba imetamba kuwa, kusajiliwa kwa mshambuliaji mpya Amissi Tambwe kutoka Vital'O ya Burundi kutamaliza tatizo la ufungaji mabao katika timu hiyo msimu ujao wa ligi.

Tambwe ni mmoja wa washambuliaji nyota wa Vital'O, ambayo ilitwaa ubingwa wa michuano ya Kombe la Kagame iliyomalizika hivi karibuni katika jimbo la Darfur nchini Sudan. Katika michuano hiyo, Tambwe aliibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao sita.

Uwezo wa mshambuliaji huyo katika kuwatoka mabeki wa timu pinzani na kufunga mabao, umefananishwa na ule aliokuwa nao mshambuliaji wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi, ambaye aliuzwa kwa klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema kwa njia ya simu jana akiwa nje ya nchi kuwa, Tambwe ameshawasili nchini kwa ajili ya kufanya mazungumzo na uongozi wa Simba.

"Kwa sasa nipo nje ya nchi kikazi, natarajia kurudi Tanzania leo au kesho, lakini tayari nimeshafanya mazungumzo ya awali na Tambwe na kimsingi tumekubaliana mambo mbalimbali. Kinachosubiriwa ni kumfanyia majaribio mchezaji huyo,"alisema Hanspope.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya usajili ya Simba alisema, kwa mujibu wa utaratibu waliouanzisha, hakuna mchezaji atakayesajiliwa bila kufanyiwa majaribio na benchi la ufundi, linaloongozwa na Kocha Abdalla Kibadeni.

"Iwapo benchi la ufundi litampitisha, uongozi utampatia mkataba wa miaka miwili wa kuichezea Simba kuanzia msimu ujao. Hatutaki kununua Mbuzi kwenye gunia na pia tupo makini kumlinda kwa sababu tumesikia wenzetu wameshaanza kumvizia,"alisema.

Tambwe alitua nchini juzi na anamsubiri Hanspope ili wamalize mazungumzo yao kabla ya kufanyiwa majaribio na kumwaga wino Simba. Ligi Kuu ya Tanzania Bara imepangwa kuanza Agosti 24 mwaka huu.

Wachezaji wengine wapya kutoka nje, ambao wamekuwa wakifanyiwa majaribio na Simba ni Assumani Kayinzi, aliyekuwa akicheza soka ya kulipwa Vietnam na Kon James kutoka Al Nasri Juba ya Sudan Kusini.

Wachezaji pekee wa kigeni waliosajiliwa Simba hadi sasa ni kipa Abel Dhaira, beki Mussa Mudde na Samuel Ssenkoom, ambaye msimu ujao utakuwa wa kwanza kwake kuichezea Simba. Dhaira na Mudde wapo Simba tangu msimu uliopita.

Kwa mujibu wa kanuni za usajili, kila klabu inayoshiriki michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara inatakiwa kusajili wachezaji watano wa kigeni.

M2 THE P KUCHORA SURA YA MANGWEA MGONGONI KWAKE


MSANII  wa muziki wa kizazi kipya, M2 The P amesema atachora tattoo kubwa yenye sura ya marehemu Albert Mangweha kwenye mgongo wake.
M2 The P alisema wiki hii mjini Dar es Salaam kuwa, amefikia uamuzi huo kwa lengo la kumkumbuka na kumuenzi rafiki yake huyo, aliyefariki dunia hivi karibuni nchini Afrika Kusini na kuzikwa Morogoro.
Msanii huyo alikuwa pamoja na Mangweha nchini Afrika Kusini kabla na siku ya kifo chake.
Alisema kabla ya kifo cha Mangweha, alimwelezea kuhusu sababu zilizomfanya achore tattoo ya chozi na ya muziki kwenye mikono yake yote miwili.
Akifafanua, alisema tattoo ya chozi ililenga kumuenzi mama yake mzazi na ile ya muziki inaonyesha jinsi fani hiyo ilivyo kwenye damu yake.
"Sasa nataka kuchora tattoo kubwa mgongoni yenye picha yake. Nadhani ndio itakuwa kumbukumbu yangu kubwa kwake. Nitakichora kichwa cha Albert Mangweha,"alisema.
M2 The P alisema anamshukuru Mungu kwamba kwa sasa anarejea katika hali yake ya kawaida baada ya kuondokewa na kipenzi chake huyo, waliyesafiri pamoja kwenda Afrika Kusini.

WABOGOJO SASA ANAPIGA SHOO ZA KIMATAIFA MACAU



Je, unamkumbuka msanii Athumani Ford, aliyekuwa maarufu kwa jina la Wabogojo? Yule aliyekuwa akipamba video za nyimbo za msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya, Lucas Nkenda 'Mr Nice'?
Sifa moja kubwa aliyokuwa nayo Wabogojo wakati huo hapa nchini ni kuvichezesha viungo vya mwili wake anavyotaka. Vitendo vyake, ambavyo havikuwa na tofauti na mchezo wa sarakasi, vilimfanya aonekane mtu wa ajabu.
Watanzania wengi walianza kumuona na kumfahamu Wabogojo wakati aliposhiriki kuipamba video ya wimbo wa Kikulacho ya Mr. Nice. Alikuwa anafurahisha kutokana na vitendo vyake.
Ni baada ya kuonekana kwenye video hiyo, Wabogojo akaanza kujulikana ndani na nje ya nchi. Wajanja wakabaini kwamba, mchezo anaoucheza ni 'dili'. Wakampa shavu.
Hivi sasa Wabogojo yupo kwenye kisiwa cha Macau kilichopo China, akifanya maonyesho kwenye kumbi mbalimbali za burudani. Inaaminika kuwa, kisiwa hiki kinakaliwa na watu wenye uwezo mkubwa kipesa.
Wabogojo ameandika kupitia kwenye mtandao wake hivi karibuni kuwa, alipata ulaji huo baada ya kufanya ziara ndefu barani Ulaya akiwa na kundi la Mother Africa.
"Kwa ufupi, baada ya ziara ya Ulaya tukiwa na kundi la Mama Africa, ambako tulipelekwa na Winston Ruddle, tukafanikiwa kupata kazi nyingine na ndio hii ya sasa,"alisema msanii huyo.
Wabogojo alisema mazoezi ya maonyesho wanayoyafanya sasa huko Macau, waliyafanya kuanzia Februari 2009 hadi Machi 2012 katika kituo cha michezo cha Antwerpen kilichopo Ubelgiji.
"Baada ya mazoezi hayo, tukaja Macau na kuandaa maonyesho. Tulianza maonyesho yetu kuanzia Septemba 17, 2012 na mkataba ni mzuri. Tumalipwa pesa nzuri kwa mwezi hadi raha!!" Ameeleza msanii huyo.
Kwa mujibu wa Wabogojo, wataendelea kuwepo Macau hadi Septemba 2014. Alisema uwepo wao zaidi kwenye kisiwa hicho utategemea mkataba mpya.
Hata hivyo, Wabogojo alisema msanii yupo huru kukatisha mkataba wake iwapo ataona amechoshwa na kazi hiyo.
Katika kikundi chao, Wabogojo alisema wapo wasanii 12 kutoka Tanzania. Alisema wengine wanatoka katika nchi za Brazil, Uingereza na Marekani.
Akifafanua kuhusu kisiwa cha Macau, Wabogojo alisema watu wenye uwezo wa kifedha kutoka sehemu mbalimbali duniani, hupenda kwenda kufanya matanuzi huko.
"Ni kisiwa chenye makasino mengi. Watu huja kutumia pesa zao tuu. Ni kama kulivyo Las Vegas kule Marekani,"alisema.
Alisema maonyesho ya kundi lao yanayojulikana kwa jina la The House of Dancing Water, yanafanyika kwenye kasino kubwa zaidi inayojulikana kwa jina la City of Dream.
" Tumejifunza mambo mengi tangu tulipofika huku. Tumejifunza kuogelea na kupiga mbizi baharini na kwenye mabwawa ya kuogelea. Kama hujui kuogelea, maonyesho haya hayakufai,"alisema.
Wabogojo alisema anamshukuru Mr. Nice kwa kumtambulisha kwenye ulimwengu wa sanaa, japokuwa hakuwa akimlipa vizuri kutokana na kazi yake hiyo. Anasema alichokipata ni zaidi ya pesa.
"Mungu yu mwema," alimalizia maelezo yake kupitia kwenye mtandao huo.
Wabogojo ni kama yake prodyuza maarufu wa muziki wa kizazi kipya nchini, Razakl Ford wa Kampuni ya 4D Videos, aliyetengeneza video ya wimbo wa Recho, unaojulikana kwa jina la Upepo. Pia ni kaka wa mwigizaji nyota wa filamu za kibongo, Shamsa Ford.

RAZAK YUSUF , MWANASOKA MKONGWE ALIYEFANANISHWA NA CARECA WA BRAZIL



JINA lake halisi ni Razak Yusuf. Lakini alikuwa maarufu zaidi kwa jina la Careca, alilobatizwa na mashabiki wa soka wa mkoani Tanga kutokana na uwezo wake wa kucheza soka, uliofanana na mwanasoka huyo wa Brazil.
Hata hivyo, Razak hakuwa akilifurahia jina hilo. Alitaka Careca ndiye aitwe Razak kwa kile anachoamini kwamba, uwezo wake kisoka ulikuwa mkubwa zaidi kuliko aliokuwa nao mwanasoka huyo wa zamani wa Brazil, aliyestaafu soka akiwa na umri wa miaka 40.
Jina halisi la Careca lilikuwa Antônio de Oliveira Filho. Alikuwa mmoja wa wanasoka nyota wa Brazil waliocheza kwa mafanikio makubwa miaka ya 1980. Alikuwa na kipaji cha aina yake katika kufunga mabao. Baadhi ya klabu alizochezea ni pamoja na Sao Paulo ya Brazil na Napoli ya Italia.
Nyota ya Razak kisoka ilianza kung'ara 1985 alipojiunga na Coastal Union akitokea African Sports. Aliichezea Coastal Union hadi 1991 alipojiunga na klabu ya Simba. Alikuwa mmoja wa wachezaji walioiwezesha Simba kucheza fainali ya Kombe la CAF 1993.
Razak pia ni miongoni mwa wachezaji walioiwezesha Coastal Union kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara 1988 na kupata nafasi ya kucheza michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati na Kombe la Washindi.
Baadhi ya wachezaji aliokuwa nao katika kikosi hicho ni Mohamed Mwameja, Hamisi Makene, Saidi Korongo, Douglas Muhani, Yassin Napili, Idrisa Ngulungu, Ally Maumba, Kassim Mwajeki, Mohamed Kampira, Kasa Mussa, Juma Mgunda, Hussein Makwuruzo, Aggrey Chambo na Riffat Saidi.
Kikosi hicho cha Coastal Union kilichokuwa chini ya makocha Zakaria Kinanda (sasa marehemu) na Joel Bendera, kilifuzu kucheza fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati na kufungwa na Breweries ya Kenya mabao 3-0. Michuano hiyo ilifanyika mjini Nairobi, Kenya.
Kufungwa kwa Coastal Union katika mechi hiyo ya fainali kulitawaliwa na mizengwe mingi. Kwanza walichezeshwa mechi ya nusu fainali dhidi ya AFC Leopards nyakati za usiku, ikiwa ni siku moja kabla ya fainali. Katika mechi hiyo, waliibuka na ushindi kwa njia ya matuta baada ya timu hizo kumaliza dakika 120 zikiwa sare ya bao 1-1.
Wachezaji wa Coastal Union walilazimika kutolewa uwanjani saa saba usiku ili kuwaepusha na vurugu za mashabiki wa AFC Leopards. Walipofika kwenye hoteli waliyofikia, ilikuwa Ijumaa saa tisa usiku. Walipumzika kwa saa chache kabla ya kurudi uwanjani kucheza na Breweries katika mechi ya fainali.
Razak pia alikuwemo kwenye kikosi cha Coastal Union kilichocheza na Costa do Sol ya Msumbiji katika michuano ya Kombe la Washindi 1989. Katika mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Coastal Union ilichezea kichapo cha mabao 3-2 kabla ya kupata kipigo kingine cha mabao 2-1 mjini Maputo.
Mwanasoka huyo mkongwe pia alikuwemo kwenye kikosi cha pili cha timu ya Tanzania Bara 'Kakakuona' kilichocheza michuano ya Kombe la Chalenji 1991 na kutinga fainali, ambapo kilichapwa bao 1-0 na Uganda.
Katika michuano hiyo iliyochezwa katika miji ya Mwanza na Arusha, Kakakuona ilyokuwa ikiundwa na wachezaji wengi chipukizi, ilijipatia umaarufu mkubwa kutokana na kuonyesha uwezo mkubwa wa kucheza soka. Katika mechi za awali, ilitoka sare ya bao 1-1 na Uganda kabla ya kuichapa Shelisheli mabao 2-0.
Razak pia alikuwemo kwenye kikosi cha Simba kilichotinga fainali ya Kombe la CAF 1993 na kufungwa mabao 2-0 na Stella Abidjan ya Ivory Coast kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya timu hizo kutoka suluhu katika mechi ya awali iliyopigwa mjini Abidjan.
Hata hivyo, Razak alicheza mechi chache za hatua ya awali ya michuano hiyo na kuumia. Alikuwa mmoja wa wachezaji walionyimwa zawadi ya magari waliyoahidiwa na mfadhili wao, Azim Dewji, kwa kile ambacho hadi sasa anashindwa kukielewa.
Akizungumza na Burudani kwenye uwanja wa Popatlal mjini Tanga hivi karibuni, Razak alisema alilazimika kustaafu soka 1993 kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
"Wakati ule hakukuwa na utaalamu wa tiba ya ugonjwa huo. Nililazimika kuacha soka bila kupenda nikiwa bado nina uwezo mkubwa,"alisema Razak, ambaye kwa sasa ni mfanyabiashara na pia mmoja wa maofisa wa benchi la ufundi la Coastal Union.
Miongoni mwa mechi, ambazo Razak hawezi kuzisahau katika maisha yake ni ile iliyozikutanisha Coastal Union na AFC Leopards katika nusu fainali ya michuano ya klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati 1988 nchini Kenya.
"Ilikuwa mechi ngumu, nzuri na kali. Mimi ndiye niliyefunga bao la Coastal Union. Nilifunga bao hilo kwa shuti kali la mbali. Lilikuwa bao zuri sana,"alisema.
Kinachomfanya Razak aendelee kuikumbuka mechi hiyo ni ukali wa AFC Leopards wakati huo, hasa baada ya kuzifunga Simba na Yanga katika mechi za kirafiki zilizochezwa mjini Dar es Salaam, lakini baadaye ikakubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Coastal Union mjini Tanga.
"Kocha wao, ambaye alikuwa raia wa Ghana, alitutabiria mapema kwamba tungetwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati na kweli tulifika mbali, lakini tulifungwa na Breweries katika fainali,"alisema mkongwe huyo.
Akizungumzia kiwango cha soka nchini hivi sasa, Razak alisema hakiridhishi kwa sababu mpira umegeuzwa zaidi kuwa mchezo wa kibiashara kwa wachezaji na viongozi. Alisema wachezaji wa sasa hawana ari na hawachezi kwa kujituma kama ilivyokuwa enzi zao.
"Zamani hakukuwa na pesa, lakini wachezaji walicheza kwa ari na kujituma. Lakini kikubwa zaidi ni kwamba walikuwa na vipaji vya kucheza soka, tofauti na ilivyo sasa,"alisema.
Razak pia amelalamikia maumbile ya sasa ya wanasoka wa Tanzania kwamba hayapo kisoka. Alisema wachezaji wengi wana maumbile madogo na hivyo kushindwa kuhimili ushindani wa timu pinzani, hasa kutoka nchi za Magharibi na Kaskazini mwa Afrika.
"Hebu tazama Taifa Stars ya 1981 iliyocheza fainali za Afrika kule Nigeria. Karibu wachezaji wote walikuwa na maumbile makubwa. Tazama walivyokuwa akina Jella Mtagwa, Peter Tino, Juma Pondamali na Mohamed Salim. Maumbo ya aina ile ni nadra kuyaona uwanjani hivi sasa,"alisema.
Mwanasoka huyo mkongwe alisema ujio wa Kocha Marcio Maximo kutoka Brazil ulisaidia kwa kiasi kikubwa kuinua kiwango cha soka cha Taifa Stars, ambayo tangu wakati huo, wachezaji wake wamekuwa hawahofii kupambana na timu kama Zambia, Senegal, Morocco, Cameroon na Ivory Coast.
Alisema miaka michache ya nyuma, ilikuwa kitu adimu kwa Taifa Stars kuifunga timu kama Morocco kwa idadi kubwa ya mabao, lakini hilo kwa sasa linawezekana na kwamba kikosi cha timu bora hakiwezi kujengwa kwa siku moja.
"Iwapo Maximo angekuwepo kwa miaka mingi zaidi, hivi sasa tungekuwa mbali sana kisoka kwa sababu alikuwa kocha muhamasishaji,"alisema Razak.
Hata hivyo, mkongwe huyo alieleza pia kuridhishwa kwake na uwezo wa kocha wa sasa wa timu hiyo, Kim Poulsen kutoka Denmark, ambaye amemwelezea kuwa amesaidia kuendeleza kiwango cha timu hiyo kutoka pale alipoishia Maximo.
Kwa mujibu wa Razak, Ivory Coast ilifanikiwa kuifunga Taifa Stars katika michuano ya awali ya Kombe la Dunia kwa sababu ya ujanja na mbinu za kisoka za wachezaji wake. Alisema hata mabao ya Ivory Coast katika mechi hiyo yalikuwa ya kiujanja zaidi kuliko mbinu za kisoka kama ilivyokuwa kwa mabao ya Taifa Stars.
Razak ametoa mwito kwa klabu za soka nchini kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika kukuza na kuendeleza soka ya vijana. Alisema wapo vijana wengi nchini wenye vipaji vya kucheza soka, lakini wanakosa watu wa kuwafuatilia na kuwaendeleza.
Alisema mchezo wa soka hauna mwenyewe duniani na kwamba, timu inayowekeza kwa vijana, inajitengenezea mazingira mazuri ya kutamba miaka ijayo kama zinavyofanya Hispania na Ujerumani.
"Tunapaswa kuwatengeneza vijana wengi zaidi na kuwauza nje ya nchi. Angalia jinsi Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka ya kulipwa DRC walivyoleta mabadiliko makubwa kwa Taifa Stars. Tukiwa na akina Samatta watano, tutakuwa mbali sana kisoka,"alisema.
Aliupongeza uamuzi wa TFF kuzitaka klabu zote za ligi kuu kuwa na timu za vijana wa chini ya miaka 20 na pia kuwepo kwa mashindano ya Copa Coca Cola na Kombe la Uhai, ambayo alisema yamesaidia kuongeza ari ya vijana kushiriki katika mchezo huo.
Razak pia alieleza kufurahishwa kwake kutokana na kampuni nyingi kujitokeza kudhamini mchezo wa soka. Hata hivyo, alisema udhamini huo unapaswa kulenga zaidi timu za vijana kuliko kuwa wa kibiashara zaidi.
Mkongwe huyo alieleza kusikitishwa kwake na vurugu za uongozi zinazotokea mara kwa mara katika vyama vya soka vya mikoa na katika ngazi za klabu. Alisema vurugu hizo zinatokana na kuwepo kwa utitiri wa wafanyabiashara wanaojitosa kwenye uongozi wa mchezo huo kwa lengo la kujineemesha.

Wednesday, July 10, 2013

CAF YABADILI MWAMUZI MECHI YA STARS



Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanya mabadiliko ya mwamuzi wa mechi ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwamuzi aliyeondolewa kutokana na sababu za kiufundi ni Jean Claude Birumushahu aliyekuwa mwamuzi msaidizi namba moja. Nafasi yake sasa inachukuliwa na Herve Kakunze pia kutoka Burundi.

CAF imemuondoa mwamuzi huyo baada ya kufeli katika mtihani wa waamuzi (Cooper Test) kwa waamuzi wa Burundi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika nchini humo siku tatu zilizopita.

Waamuzi hao na Kamishna wa mechi hiyo Gebreyesus Tesfaye kutoka Eritrea wanatarajiwa kuwasili nchini kesho (Julai 11 mwaka huu) kwa ndege za Kenya Airways na EgyptAir kwa muda tofauti.

Nayo Uganda Cranes inatarajiwa kuwasili nchini kesho (Julai 11 mwaka huu) na itafikia hoteli ya Sapphire. Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) bado halijatuma taarifa rasmi juu ya ujio wa timu hiyo.

Wakati huo huo, makocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen na wa Uganda, Milutin Micho pamoja na manahodha wao watakuwa na mkutano na Waandishi wa Habari utakaofanyika keshokutwa (Julai 12 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za TFF kuzungumzia mechi ya Jumamosi.

FRIENDS, POLISI KUCHEZA MECHI YA RCL JUMAPILI
Mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na Polisi Jamii ya Mara iliyokuwa ichezwe Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) imesogezwa mbele kwa siku moja.
Timu hizo sasa zitacheza Jumapili (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi. Polisi Jamii ilishinda bao 1-0 mechi ya kwanza iliyochezwa Julai 6 mwaka huu Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Refa Hans Mabena kutoka Tanga ndiye atakayechezesha mechi akisaidiwa na E. Mkumbukwa na Hajj Mwalukuta wote kutoka Tanga. Mwamuzi wa akiba (fourth official) ni Kessy Ngao wa Dar es Salaam.

Mechi kati ya Stand United FC ya Shinyanga na Kimondo SC ya Mbeya itachezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga. Mwamuzi atakuwa Daniel Warioba kutoka Mwanza. Kimondo SC ilishinda mechi ya kwanza bao 1-0.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

HAKUNA HILA KWENYE MAREKEBISHO YA KATIBA-TENGA



Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga amesema hakuna hila yoyote katika marekebisho ya Katiba kwa vile yametokana na maagizo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

Akizungumza na Wahariri wa Michezo kwenye ofisi za TFF, Dar es Salaam leo (Julai 9 mwaka huu), Rais Tenga amewahakikishia wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Dharura kuwa dhamira ya marekebisho hayo ni nzuri, kwani lengo ni kila mtu apate haki yake.

Amesema Mkutano huo utakaofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) utakuwa na ajenda moja tu ya kuingiza Kamati ya Maadili, na Kamati ya Rufani ya Maadili katika Katiba ya TFF kama ilivyoelekezwa na FIFA ili baadaye uanze mchakato wa uchaguzi.

“Katika kuunda Kamati ya Maadili tumeangalia ile ile ya FIFA, tusitengeneze kitu kipya, yaondolewe yale yanayotakiwa kuondolewa, na yaongezwe yale yanayotakiwa kuongozwa. Kwa sababu tumeangalia mazingira kwa Tanzania ni tofauti na Ujerumani au nchi za sehemu zingine,” amesema.

Rais Tenga amewataka wajumbe wafike kwenye Mkutano wakiwa na mtazamo wa kujenga, kwani kuna maagizo ya FIFA ambayo wanatakiwa kuyatekeleza ili wasonge mbele.

“Tutawaeleza kwanini hili limewekwa na lile limeondolewa. Mpira unataka unit (kitu kimoja), ni mchezo wa kila mtu. Baada ya hapa tunaanzisha mchakato wa uchaguzi. Watu wanaingia wakiwa wamoja, wanatoa hoja wanasikilizwa. Wanahukumiwa kwa hoja,” amesema na kuongeza utatolewa muda wa kutosha wajumbe ili wayaone na kuelewa marekebisho hayo.

Rais Tenga pia alizungumzia kipindi hiki cha usajili na kutaka klabu ziwaachie wataalamu wa mpira wa miguu kwani ndiyo wanaojua upungufu wa timu, hivyo wanaweza kusajili wachezaji sahihi.
Amesema tatizo kubwa la klabu za Tanzania ni kuwa timu zao hazina uwezo wa kuhimili dakika 90, hivyo watu wanapaswa pia kuzungumzia aina ya mazoezi ambayo timu zao zinafanya badala ya kubakia kutaja tu majina ya wachezaji wanaotaka kusajiliwa.

KIINGILIO MECHI YA STARS, UGANDA 5,000/-
Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.

Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 kiingilio ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.

Viingilio vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.

Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika itachezeshwa na mwamuzi Thierry Nkurunziza kutoka Burundi. Mechi ya marudiano itachezwa jijini Kampala kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu.

Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo (Ijumaa) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Barbershop iliyoko Sinza Madukani.

Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi.

Tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.

MIKOA YATAKIWA KUWASILISHA RATIBA COPA COCA-COLA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), linavitaka vyama vya mpira wa miguu vya mikoa kuwasilisha ratiba zao za michuano ya U15 Copa Coca-Cola kabla ya Julai 15 mwaka huu.

Ni vyama vya mpira wa miguu vya mikoa 16 pekee ambavyo ndivyo vimewasilisha TFF ratiba hizo mpaka sasa. Jumla ya mikoa 32 ya Tanzania Bara na Zanzibar inashiriki katika michuano hiyo ya umri chini ya miaka 15 kuanzia ngazi ya wilaya ambapo ngazi ya mikoa inatakiwa kuanza Julai 15 mwaka huu.

Mikoa ambayo tayari imewasilisha ratiba zao ni Arusha, Ilala, Kagera, Kaskazini Pemba, Kaskazini Unguja, Kigoma, Kinondoni, Kusini Pemba, Kusini Unguja, Manyara, Mara, Mjini Magharibi, Morogoro, Singida, Tanga na Temeke.

WASH UNITED YAKABIDHI FULANI 200 KWA KLINIKI YA TFF
Taasisi ya Wash United inayojishughulisha na usaji na utunzaji mazingira imeikabidhi fulana 200 na dola 1,000 za Marekani kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano kati yake na TFF yaliyosainiwa Novemba mwaka jana.

Fulana hizo kwa ajili ya kliniki za kila wikiendi (Jumamosi na Jumapili) zinazoendeshwa na TFF katika vituo 20 nchini kikiwemo cha Karume ikiwa ni sehemu ya mpango wa grassroots unaoshirikisha watoto wa umri kati ya 6 na 17 zimekabidhiwa na Mratibu wa Wash United, Femin Mabachi.

Hafla ya kukabidhi msaada huo imefanyika leo (Julai 9 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF ambapo kwa upande wake ulipokelewa na Ofisa Maendeleo wake Salum Madadi.

Wash United inafadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika lake la maendeleo la GIZ, na hapa nchini moja ya eneo wanalotumia katika kampeni hiyo ili kupambana na magonjwa kama kuhara yanayosababishwa na uchafu ikiwemo kutonawa mikono vizuri, hivyo kusababisha vifo kwa Watanzania ni mpira wa miguu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF

Sunday, July 7, 2013

MKUTANO MKUU SIMBA JULAI 20



KLABU ya Simba imepanga kufanya mkutano wake mkuu wa mwaka wa wanachama Julai 20 mwaka huu.

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are alisema jana kuwa, mkutano huo utafanyika kwenye Bwalo la Maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Itang'are, maarufu kwa jina la Kinesi alisema, uamuzi wa kuitisha mkutano huo taehe hiyo, ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji kilichofanyika juzi na jana mjini Dar es Salaam.

Alizitaja ajenda zitakazojadiliwa katika mkutano huo kuwa ni pamoja na kupokea taarifa mbalimbali za msingi za klabu kwa mwaka mzima, ikiwemo ripoti ya mapato na matumizi kwa mwaka mzima.

Ajenda zingine ni ushiriki wa Simba katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara msimu uliopita pamoja na ombi la kujiuzulu kwa aliyekuwa makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu'.

Kinesi alisema tayari maandalizi kwa ajili ya mkutano huo yameshaanza na amewataka wanachama kujitokeza kwa wingi kuhudhuria ili waweza kujadili mambo mbalimbali yanayoihusu klabu yao.

Kuitishwa kwa mkutano huo kumekuja siku chache baada ya baadhi ya wanachama kuushinikiza uongozi chini ya Mwenyekiti, Ismail Aden Rage uitishe mkutano kwa ajili ya kujadili kuvurunda kwa Simba katika ligi.

Wakati huo huo, kamati ya utendaji ya Simba imeridhia kuongezwa mikataba kwa Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelo 'Julio' na Ofisa Habari wa klabu, Ezekiel Kamwaga.

Katika kikao hicho, wajumbe pia waliridhia kiungo wa timu hiyo, Kigi Makasi apelekwe India kwa ajili ya kupatiwa matibabu ya goti baada ya kuumia wakati wa mechi ya kirafiki kati ya Simba na CDA iliyochezwa mjini Dodoma.

Katika hatua nyingine, klabu ya Simba inatarajia kufanya ziara katika vituo mbalimbali vya watoto yatima na kutembelea wagonjwa kuanzia Agosti 5 hadi 11 mwaka huu.

Ziara hiyo ni miongoni mwa shughuli mbalimbali za kijamii, ambazo Simba itazifanya katika wiki ya kuelekea Tamasha la Simba, maarufu kwa jina la 'Simba Dar'.

Katika wiki hiyo, wachezaji na viongozi wa Simba pia watahudhuria kozi maalumu, itakayoandaliwa na wadhamini wa klabu hiyo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) na kutembelea shule za msingi kwa lengo la kuwahamasisha watoto wapende mchezo wa soka.

Shughuli zingine zitakazofanywa na Simba katika wiki hiyo ni pamoja na kutembelea vyombo vya habari na kusoma hitma kwa ajili ya kuwarehemu wachezaji, viongozi na wanachama wa klabu hiyo waliotangulia mbele ya haki.

WARUNDI KUCHEZESHA MECHI YA STARS NA UGANDA


Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya kwanza ya mchujo ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayofanyika Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Waamuzi hao ni Thierry Nkurunziza atakayepuliza filimbi wakati wasaidizi wake watakuwa Jean Claude Birumushahu na Pascal Ndimunzigo. Mwamuzi wa akiba (fourth official) ni pacifique Ndabihawenimana.

Kamishna wa mechi hiyo Gebreyesus Tesfaye kutoka Eritrea. Tesfaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Eritrea na mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mashindano ya CHAN.

FAINALI AIR RISING STARS ‘LIVE’ SUPERPORT
Fainali za michuano ya Airtel Rising Stars kwa wavulana na wasichana zinazochezwa kesho (Julai 6 mwaka huu) Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam zitaoneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport.

Mechi za fainali ambazo mgeni rasmi atakuwa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala zitachezwa kuanzia saa 7.30 mchana kwa wasichana wakati ile ya wavulana itaanza saa 9.30 alasiri.

Nusu fainali za mashindano hayo ambazo pia zinaonekana moja kwa moja SuperSport zinachezwa leo (Julai 5 mwaka huu). Kwa upande wa wasichana ni kati ya timu za Kinondoni na Kigoma wakati Ilala inaumana na Temeke.

Kwa upande wa wavulana nusu fainali ya kwanza ni kati ya Mwanza na Ilala ambapo baadaye itafuatiwa na nyingine kati ya Morogoro na Kinondoni. Mechi za kutafuta mshindi wa tatu zitachezwa kesho asubuhi (Julai 6 mwaka huu).

28 KUSHIRIKI KOZI YA FIFA 11 FOR HEALTH
Jumla ya makocha wa mpira wa miguu na walimu 28 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na shule za msingi na sekondari wameteuliwa kuhudhuria kozi ya FIFA 11 For Health inayoanza keshokutwa (Julai 7 mwaka huu) Homboro mkoani Dodoma.

Kozi hiyo itakayomalizika Julai 20 mwaka huu itakuwa chini ya ukufunzi wa Rogasian Kaijage ambaye pia ni Kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars).

Washiriki ni Abdul Mikoroti (Shule ya Msingi Nzasa), Baltazar Kagimbo (Shule ya Msingi Tabata Jica), Baraka Baltazar (Shule ya Msingi Muhimbili), David Kivinge (Shule ya Msingi Temeke), Dismas Haonga (Tambaza Sekondari), Exuperus Kisaka (Shule ya Msingi Mavurunza) na Hadija Kambi (Shule ya Msingi Karume).

Hamis Chimgege (Shule ya Msingi Tusiime), Hobokela Kajigili (Shule ya Msingi Buguruni), Issack Mhanza (Shule ya Msingi Airwing), Job Ndugusa (Shule ya Msingi Upanga), John Sebabili (TFF), Lutta Rucharaba (Shule ya Msingi Montfort), Maua Rahidi (Shule ya Msingi Uhuru Wasichana), Michael Bundala (TFF) na Mussa Kapama (Shule ya Msingi Bunju ‘A’).

Priscus Silayo (Shule ya Msingi J.K. Nyerere), Peter Manyika (TFF), Rajabu Asserd (Shule ya Msingi Mtoni Kijichi), Raphael Matola (TFF), Raymond Rupia (St. Anne Maria Academy), Renatus Magolanga (Ulongoni Sekondari), Ruth Mahenge (Shule ya Msingi Chang’ombe), Said Pambaleo (TFF), Sebastian Nkoma (TFF), Titus Michael (TFF), Wane Mkisi (Jangwani Sekondari),

LIUNDA KUSIMAMIA MECHI YA CHAN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa Kamishna wa mechi kati ya Burundi na Sudan itakayochezwa jijini Bujumbura.

Mechi hiyo ya kwanza ya mchujo ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) itafanyika keshokutwa (Julai 7 mwaka huu). Liunda anatarajia kuondoka leo usiku (Julai 5 mwaka huu) kwenda Bujumbura..

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Friday, July 5, 2013

KIGOMA HOI KWA KINONDONI



Mchezaji wa timu ya soka ya wanawake ya Ilala, Zuena Azizi (kushoto) na Neema Paul wa Temeke wakigombea mpira wakati timu hizo zilipomenyana katika mechi ya michuano ya Kombe la Airtel Rising Star iliyochezwa jana kwenye uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam.  Ilala ilishinda kwa penalti 2-0. (Picha na Abubakari Habibu wa A3 Institute of Professional Studies).

NA MKUNDAPAI ABDALLAH
TIMU ya soka ya wanawake ya vijana wa chini ya miaka 17 ya Kigoma jana ilipata kichapo cha mabao 7-0 kutoka kwa Kinondoni katika mechi ya michuano ya Kombe la Airtel Rising Star iliyochezwa kwenye Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam.

Katika mechi hiyo ya nusu fainali,  mshambuliaji Sherida Boniface ndiye aliyeibeba Kinondoni baada ya kuifungia mabao manne kati ya saba. Alifunga mabao hayo dakika za 10, 14, 26 na 38.

Mabao mengine ya Kinondoni yalifungwa na Tatu Iddi dakika ya sita, Shamimu Hamisi dakika ya 23 na Cristina Daudi dakika ya 40.

Kutokana na ushindi huo, Kinondoni sasa itakutana na Ilala katika mechi ya fainali. Ilala ilifuzu kucheza hatua hiyo baada ya kuichapa Temeke mabao 2-0. Temeke na Kigoma zitakutana katika mechi ya kutafuta mshindi wa tatu.

Pambano kati ya Ilala na Temeke lilikuwa na ushindani mkali na ilibidi mshindi apatikane kwa njia ya matuta baada ya timu hizo kumaliza dakika 90 zikiwa sare ya bao 1-1.

Temeke ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 32 kupitia kwa Neema Paul kabla ya Ilala kusawazisha dakika ya 50 kupitia kwa Donisia Daniel.

Katika kupigiana penalti tano tano, Ilala ilipata penalti mbili wakati Temeke ilipoteza tatu.


MARIAMU AWA KINYOZI BORA ARUSHA



NA SHAABAN MDOE, ARUSHA.
MSICHANA Mariamu Miraji (25), mkazi wa Arusha, ameibuka mshindi baada ya kuwabwaga wanaume 33 katika shindano la kumsaka kinyozi bora lililofanyika jana mjini hapa.
Shindano hilo liliwashirikisha vinyozi 35 kutoka saluni mbalimbali za mjini Arusha, akiwemo msichana mwingine, Janeth Kimaro.

Jaji mkuu wa shindano hilo, Koroli Mbise alisema Mariamu aliibuka mshindi kutokana na kufuzu vigezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujieleza bila kusita katika kujibu maswali aliyoulizwa na jopo la majaji.

Alizitaja sifa zingine zilizomwezesha Mariamu kushinda shindano hilo kuwa ni kunyoa kwa wakati uliopangwa na ubora wa kazi yake kupitia mtindo wa 'Low cut' aliotakiwa kuutumia.

Kufuatia ushindi huo, Mariamu alizawadiwa televisheni ya ukubwa wa inchi 42 aina ya LG yenye thamani ya shilingi 1,600,000, mashine moja ya kunyolea pamoja na cheti cha kumtambulisha.

Mshindi wa pili wa shindano hilo alikuwa Abdul Razak, aliyejipatia zawadi ya simu ya mkononi aina ya Sony Ericson yenye thamani ya shilingi 100,000,mashine moja ya kunyolea pamoja na cheti.

Nafasi ya tatu ilinyakuliwa na Andrew Modest aliyezawadiwa simu ya mkononi aina ya Sony Ericson yenye thamani ya shilingi 80,000,mashine moja ya kunyolea pamoja na cheti. Washiriki wengine wa shindano hilo walizawadia vyeti vya ushiriki.

Akizungumza baada ya kutangazwa kwa washindi hao, Diwani wa Kata ya Kati, Abdul Tojo aliahidi kuwa, Jiji la Arusha pamoja na uongozi mzima wa serikali utayaendeleza mashindano hayo ili yatambulike kitaifa.

Abdul, ambaye alimwakilisha Meya wa Jiji la Arusha, alisema watamtangaza mshindi huyo mwanamke ili aweze kupata kazi nyingi za kimkoa kwa lengo la kuwapa ari wanawake wengine kujitokeza kufanya kazi hiyo badala ya kuiona kuwa ni ya wanaume pekee.

Mkurugenzi wa saluni ya Mnyampaa Baber Shop, iliyomtoa mshindi huyo, Charles Kisuke alisema, lengo lake ni kumtumia Mariamu katika kuitangaza kazi hiyo ya kunyoa kama kazi nyingine na kwa watu wote wakiwemo wanawake.

Charles alisema kwa sasa anajipanga zaidi kusambaza huduma zake hizo katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha na mikoani ili kuhakikisha huduma za kinyozi zinapatikana kwa watu wote, hasa wageni wanaofika katika mkoa wa Arusha kwa shughuli mbalimbali.

Mratibu wa shindano hilo, Zuberi Mwinyi aliahidi kuliendeleza kwa kuliendesha kila mwaka kama njia ya kuitangaza kazi hiyo kitaifa na kuondoa dhana kwamba kazi hiyo ni kwa ajili ya watu wasio na kazi maalumu.

Alisema kwa mwaka ujao wa 2014, anatarajia kuboresha zaidi shindano hilo ikiwa ni pamoja na kuongeza zawadi na wigo wa washiriki

SJMC, TASWA KUENDESHA MAFUNZO KWA WAANDISHI WA HABARI ZA MICHEZO



SHULE Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), wataendesha mafunzo ya siku tano kwa waandishi wa habari za michezo nchini.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Makamu Mkuu wa SJMC, Dk. Michael Andindilile alisema mafunzo hayo yatafanyika Agosti mwaka huu na yataendeshwa na wahadhiri kutoka chuoni hapo, waandishi wa siku nyingi na wataalamu wa michezo mbalimbali.

“Tunao wahadhiri waliobobea katika tasnia ya habari, lakini pia wapo waandishi wa habari wakongwe ambao ni waalimu kitaaluma, pia tutachukua wataalamu wa michezo mbalimbali kuja kufundisha kwa siku hizo tano,” alisema Dk. Andindilile.

Makamu Mkuu huyo wa SJMC, aliupongeza uongozi wa TASWA kwa wazo lao la kushirikiana na SJMC na kuongeza kuwa, mafunzo hayo yatachukua siku tano na yatafanyika Dar es Salaam yakihusisha washiriki 45 kutoka vyombo mbalimbali vya habari katika tarehe itakayotangazwa.

Alisema wataalamu wa michezo mbalimbali kama vile soka, riadha, netiboli, gofu, kikapu, wavu na mikono watapata fursa ya kutoa mada kuhusiana na michezo yao na kwamba TASWA na SJMC wanashirikiana katika kuomba wadhamini wasaidie mafunzo hayo.

“Hii ni awamu ya kwanza kwa waandishi wachanga na baadhi ya wa kada ya kati, baada ya hapo tutaendesha mafunzo ya namna hii kwa waandishi wa siku nyingi wa habari za michezo na wahariri wa habari za michezo, tunaamini baada ya hapo kutakuwa na mabadiliko upande wa uandishi wa habari za michezo,” alisema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto aliishukuru SJMC kwa kukubali kushirikiana na TASWA na kwamba siku zote chama chake kimekuwa kikipigania kuandaa mafunzo kwa wanahabari wa michezo kama sehemu mojawapo ya kukuza weledi.

“Fursa hii ni moja ya jitihada za TASWA kuhakikisha waandishi wa habari za michezo wanapata nafasi ya kujifunza zaidi kuhusu namna bora ya kuripoti habari za michezo kwa ujumla wake, hivyo nafasi hii si tu itasaidia wanachama wa TASWA bali pia na vyombo vya habari na washiriki hawatalipia chochote.

“Tunaamini waandishi wanapoboresha uandishi wao, inachangia kwa kiasi kikubwa kukuza heshima ya vombo vya habari, hivyo tunaomba wadau mbalimbali washirikiane nasi kudhamini mafunzo haya,” alisema Pinto na kuongeza kuwa kwa kushirikiana na SJMC wanaamini siku za usoni wanaweza kuandaaa mafunzo ya muda mrefu.

Thursday, July 4, 2013

KHADIJA MNOGA, PAULYNE ZONGO WAUNGANA



WANAMUZIKI nyota watatu wa kike nchini wameanzisha kundi jipya la muziki litakalojulikana kwa jina la Ndege Watatu.

Nyota hao watatu wanaongozwa na Khadija Mnoga, ambaye ni mwimbaji wa bendi ya Extra Bongo, Paulyne Zongo na Joan Matovolwa, ambao ni wanamuziki huru.

Khadija alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, tayari kundi hilo limesharekodi kibao kimoja kinachokwenda kwa jina la Misukosuko ya Mapenzi.

Kwa mujibu wa Khadija, tayari kibao hicho kimeshaanza kurushwa katika vituo mbalimbali vya redio nchini na kupokewa vizuri na mashabiki.

Alisema kibao hicho kimetungwa kwa pamoja na wanamuziki hao watatu kwa kiwango cha juu kwa lengo la kuonyesha umahiri wao katika muziki.

Khadija alisema kundi hilo linaundwa na wanamuziki mchanganyiko wa miondoko ya dansi na kizazi kipya na limedhamiria kuleta ladha na changamoto mpya katika muziki.

Wednesday, July 3, 2013

SHAMBA LA BIBI KUKAMILIKA NOVEMBA

WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara amesema ukarabati unaoendelea kufanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam utakamilika kabla ya Novemba mwaka huu.

Fenella alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Alisema baada ya kukamilika kwa ukarabati, uwanja huo utaanza kutumika kwa ajili ya michuano mbalimbali.

Waziri Fenella alisema ukarabati wa uwanja huo umekuwa ukifanywa na kampuni moja ya China na kuongeza kuwa, kwa sasa upo kwenye hatua nzuri kabla ya kukamilika.

Katika hatua nyingine, Waziri Fenella amesema serikali inaendelea kutafuta mdhamini kwa ajili ya kuendesha Uwanja wa Taifa wa Dar es Salaam.

Waziri Fenella amesema lengo la kusaka mdhamini wa kuwekeza kwenye uwanja huo ni kuuongezea mapato na pia kutangaza vivutio vya kitalii nje ya nchi.

Dk. Fenella alisema hayo jana wakati alipokabidhiwa rasmi uwanja huo na Balozi wa China hapa nchini, Luyon Ring katika hafla iliyofanyika kwenye uwanja huo.

Alisema vivutio vya kitalii wanavyotarajia kuvitangaza kupitia uwanja huo ni pamoja na Mlima Kilimanjaro, mbuga za wanyama na madini.

Kwa kuanzia, Dk. Fenella alisema tayari wameshaanza kuutangaza uwanja huo kupitia matangazo mbalimbali ya moja kwa moja yanayoonyeshwa na kituo cha televisheni cha Superspot.

Alisema hawawezi kuendelea kutegemea mapato ya milangoni kwa ajili ya kuendesha uwanja huo kwa vile ni madogo na hayakidhi gharama za uendeshaji.

Alitoa mwito kwa mashabiki wa soka wanaofika kwenye uwanja huo kwa ajili ya kushuhudia mechi mbalimbali kuutunza na kuacha tabia ya kubomoa vitu na vifaa vingine muhimu.

Kwa upande wake, Balozi Luyon alisema anaamini watanzania watautunza uwanja huo ili kuenzi uhusiano mzuri uliopo kati ya serikali ya China na Tanzania.

Mhandisi wa kampuni ya Beijing, Nang alisema uwanja huo ni bora kati ya viwanja vilivyopo sasa barani Afrika kutokana na kuwa na kumbi nyingi za mikutano na ofisi.

Uwanja wa Taifa umejengwa na Kampuni ya Beijing Construction Engineering Group (T) Ltd (BCEG) ya China kwa gharama za dola milioni 56.4 za Marekani (sawa na sh. bilioni 80). Uwanja huo una uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000.

SIMBA YAMNASA NYOTA WA SUDAN

BENCHI la ufundi la klabu ya Simba jana lilitarajiwa kuwafanyia majaribio wachezaji wapya wawili kutoka Uganda na Sudan Kusini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope aliwataja wachezaji hao kuwa ni Assumani Kayinzi, aliyekuwa akicheza soka ya kulipwa Vietnam na Kon James kutoka Al Nasri Juba ya Sudan Kusini.

Kayinzi alikuwa akicheza timu moja na mshambuliaji wa zamani wa Simba, Danny Mrwanda na beki Moses Oloya wa Uganda, ambaye alikuwa akiwindwa pia na klabu hiyo ya Msimbazi.

Kon ni mmoja wa wachezaji waliong'ara wakati Al Nasri ilipomenyana na Azam katika mechi ya michuano ya Kombe la Shirikisho na kutolewa kwa jumla ya mabao 8-1.

Hanspope alisema wachezaji hao wanakuja nchini kwa ajili ya majaribio na iwapo watamvutia Kocha Abdalla Kibadeni, watasajiliwa.

Mwenyekiti huyo wa kamati ya usajili ya Simba alimwelezea Kayinzi kuwa ni mchezaji mwenye uzoefu mkubwa na ambaye wana matumaini atakidhi vigezo vya Kibadeni.

Tayari Simba inao wachezaji watatu wa Uganda katika kikosi chake, kipa Abbel Dhaira, beki Samuel Ssenkoom na kiungo Mussa Mudde. Dhaira na Mudde wanaingia katika msimu wa pili Msimbazi wakati Ssenkoom utakuwa msimu wake wa kwanza.

Wakati huo huo, beki Shomari Kapombe wa Simba amechelewa kwenda Uholanzi kufanyiwa majaribio ya kucheza soka ya kulipwa kutokana na kukabiliwa na majukumu ya kuichezea Taifa Stars.

Kapombe alitakiwa kwenda Uholanzi tangu Juni 28 mwaka huu, lakini alishindwa kutokana na Taifa Stars kukabiliwa na mechi muhimu ya michuano ya awali ya Kombe la Dunia dhidi ya Ivory Coast.

Wakala wa mchezaji huyo, Denis Kadito alisema jana kuwa, kuchelewa kwa Kapombe kwenda kufanya majaribio hayo katika klabu ya FC Twente huenda kukavuruga mipango hiyo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema jana kuwa, Kapombe anatarajiwa kwenda Uholanzi baada ya Taifa Stars kumenyana na Uganda katika mechi ya michuano ya Kombe la CHAN.

NGASA AWEKA MAMBO HADHARANI

MSHAMBULIAJI Mrisho Ngasa wa klabu ya Yanga ameahidi makubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo wakati atakapoanza kuichezea katika msimu ujao wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Ngasa amesema atahakikisha anawarejeshea fadhila mashabiki wa klabu hiyo kutokana na kumuunga mkono alipokuwa akizichezea timu za Simba na Azam.


Mshambuliaji huyo nyota wa timu ya Taifa, Taifa Stars alisema hayo juzi aliporipoti kwa mara ya kwanza katika mazoezi ya Yanga yaliyofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi ya Loyola, Dar es Salaam.

"Ninawahakikishia mashabiki wa Yanga kwamba mimi ni mchezaji halali wa timu yao na sina deni lolote na Simba kwa vile nilishamaliza mkataba wangu,"alisema mshambuliaji huyo, ambaye alikuwa wa kwanza kuripoti mazoezini.

Ngasa aliihama Yanga miaka mitatu iliyopita na kujiunga na Azam kwa uhamisho uliogharimu sh. milioni 50 kabla ya kuuzwa kwa mkopo kwa klabu ya Simba.

"Naipenda sana Yanga. Nilikwenda Azam na Simba kwa ajili ya kutafuta maisha. Nitawadhihirishia mashabiki wa Yanga kwamba kiwango changu bado kipo juu,"alisema mshambuliaji huyo.

Ngasa alisema atakapoanza kuichezea Yanga katika michuano ya ligi na kimataifa, atahakikisha anakuwa mpishi mzuri wa mabao na pia mfungaji.

Aliwasifu washambuliaji Didier Kavumbagu na Saidi Bahanuzi kwamba ni washambuliaji wazuri na kusisitiza kuwa, uwepo wake utawafanya wazidi kung'ara.

"Inawezekana Kavumbagu na Bahanuzi walikosa mpishi mzuri wa mabao, lakini sasa wamempata, washindwe wenyewe. Hakutakuwa na sababu ya kutafuta mchawi,"alisema.

Ngasa alisifu usajili uliofanywa na benchi la ufundi la Yanga kwa ajili ya msimu ujao wa ligi na kuongeza kuwa, ana hakika wanaweza kutwaa ubingwa mapema zaidi kuliko msimu uliopita.

Amewaomba mashabiki wa Yanga wampokee kwa mikono miwili na kumuunga mkono ili wamuongezee ari ya kuitumikia vizuri klabu hiyo kongwe nchini.

Ngasa alisema uamuzi wake wa kurejea Yanga umetokana na mapenzi yake mwenyewe na kusisitiza kuwa, ataendelea kuziheshimu Simba na Azam kwa sababu zimemsaidia kisoka na kimaisha.

AFANDE SELE ATEMA CHECHE

MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Selemani Msindi 'Afande Sele' amesema, uamuzi wa serikali kutoza kodi kazi za wasanii ni mzuri, lakini hautakuwa na maana iwapo itashindwa kulinda kazi zao.

Akizungumza na Burudani mjini Morogoro wiki hii, Afande Sele alisema serikali inapaswa kutengeneza mazingira mazuri ya kulinda kazi za wasanii, ambazo bado zinaendelea kuuzwa holela nchini.

Afande Sele alisema kabla ya serikali kupitisha uamuzi huo, ilipaswa kukomesha kwanza wizi wa kazi za wasanii ili iweze kupata fedha nyingi za kodi na pia kuwakomboa wasanii kimapato.

Alisema ilivyo sasa ni sawa na mtu kupanga kulima shamba na kutarajia kupata mavuno mengi bila ya kuweka mazingira mazuri ya kuhakikisha kuwa, shamba lake linalindwa.

"Ni kweli serikali imeweka utaratibu huo kwa nia nzuri, lakini bado haijaweka mazingira mazuri ya kulinda kazi za wasanii,"alisema.

"Hadi leo hii CD za nyimbo za wasanii zinaendelea kutengenezwa na kuuzwa holela mitaani, nyimbo za wasanii zinatumika kama miito ya simu bila wenyewe kunufaika kwa lolote huku kazi zao zikiwa haziuziki,"aliongeza msanii huyo, ambaye aliwahi kutwaa taji la Mfalme wa Mashairi.

"Lazima serikali iwalinde wasanii kwa sababu ilivyo sasa, wanaonufaika bado ni wachache, wengi hawafaidiki kwa lolote,"alisisitiza.

Afande Sele alisema sheria zilizopo sasa za kulinda kazi za wasanii hazina nguvu na zinaendelea kutoa mwanya kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu kutumia kazi za wasanii kwa manufaa yao.

Alisema licha ya kuwepo kwa Chama cha Hatimiliki nchini (COSOTA), kimeshindwa kusimamia vyema majukumu yake kutokana na kuwa na watumishi wachache.

Msanii huyo pia alilitupia lawama Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa kushindwa kuwasaidia wasanii, lakini alisema huenda ni kutokana na kutokuwa na nguvu ya kufanya hivyo.

"Leo hii ukipanda basi na kusafiri nalo kwenda mikoani, mwanzo wa safari hadi mwisho mtawekewa kanda za sinema za wasanii wa Bongo na kupigiwa nyimbo zao.

"Ukitembelea kumbi za burudani, utasikia nyimbo za wasanii wa Tanzania zikipigwa mwanzo wa onyesho hadi mwisho. Ukipita mitaani, kuna vibanda vinaonyesha filamu za Kitanzania na kutoza viingilio.

"Huwezi kuwalaumu wananchi hawa kwa sababu sio kosa lao. Ni kwa sababu hawajui sheria. Wahusika wanaosimamia sheria za hatimiliki wapo na wanaona, lakini wanashindwa kuchukua hatua. Kwa staili hii, hatuwezi kufanikiwa,"alisema msanii huyo mwenye kipaji cha kutunga nyimbo zenye mashairi yenye mvuto.

Afande Sele aliishauri serikali izifanyie marekebisho sheria mbovu na zilizopitwa na wakati zinazohusu wizi wa kazi za sanaa ili iweze kutekeleza vyema mpango wake wa kutoza kodi kazi za wasanii.

HILAL HEMED, MTANZANIA ALIYECHEZA SOKA YA KULIPWA ARABUNI KWA MIAKA 18

 
 
 
KUMPATA Hilal Hemed mjini Tanga si kazi ngumu kwa sababu mara nyingi huonekana mara kwa mara akiwa na timu yake ya vijana, inayoshiriki michuano ya ligi daraja la tatu mkoa wa Tanga, inayojulikana kwa jina la Bomboka. Timu hii ndiyo aliyokuwa akiichezea alipokuwa mdogo na sasa ameamua kuifadhili.


Hilal pia ndiye kocha mkuu wa timu hiyo, ambayo imefanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi daraja tatu na pia kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe la Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) iliyomalizika wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga baada ya kuishinda Makorola kwa penalti 5-4.

Kazi kubwa ilikuwa ni kumshawishi Hilal kuzungumza naye masuala mbalimbali yanayohusu maisha yake soka. Ni kwa sababu huwa hapendi kuzungumza na vyombo vya habari. Hapendi kuhojiwa jambo lolote kuhusu maisha yake kisoka.

"Hata nilipokuwa Oman, kila waandishi wa habari walipokuwa wakinifuata, nilikuwa nikiwaambia andikeni mlichokiona uwanjani. Huwa sipendi kabisa kuzungumza na vyombo vya habari,"alisema Hilal nilipokutana naye wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.

"Naweza kusema wewe una bahati kwa sababu ulianza kunipigia simu mapema na umefunga safari kutoka Dar es Salaam hadi Tanga. Nimeona kukukatalia, lisingekuwa jambo la kistaarabu," aliongeza nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania.

Jina la Hilal si geni kwa mashabiki wa soka nchini, hasa wa miaka ya 1980. Alikuwa mchezaji mwenye kipaji cha aina yake, akiwa na uwezo mkubwa wa kuwatoka mabeki wa timu pinzani anavyotaka na pia kufunga mabao.

Uwezo huo wa Hilal ndio uliomfanya awindwe kwa udi na uvumba na klabu za Arabuni wakati huo na hatimaye kuondoka nchini kwa siri mwaka 1984 kwa kupitia nchi jirani ya Kenya, akihofia kuzuiwa.

Mpango huo wa kwenda Arabuni pia ulimuhusisha beki nyota wa zamani wa klabu ya Yanga, Ahmed Amasha, ambaye aliondoka nchini wiki moja kabla ya Hilal. Amasha naye aliondoka nchini kwa siri kwa kupitia Kenya, akihofia kuzuiwa na viongozi wa klabu ya Yanga.

Hilal aliondoka nchini miaka miwili baada ya kuichezea Coastal Union ya Tanga kwa mafanikio makubwa msimu wa 1983 na 1984. Pia alikuwa mmoja wa wachezaji wa timu ya Tanzania Bara, iliyoshiriki michuano ya Kombe la Chalenji 1984 ilipofanyika nchini Uganda.

Katika michuano hiyo, mshambuliaji huyo aliyekuwa na kipaji cha kuzifumania nyavu, ndiye aliyeifungia Tanzania Bara bao la kusawazisha ilipotoka sare na Uganda kwenye uwanja wa Nakivubo. Pia ndiye aliyeifungia bao Tanzania Bara ilipofungwa mabao 2-1 na Zambia.

Nyota ya Hilal kisoka ilianza kung'ara 1982 alipojiunga na Coastal Union akitokea timu ya vijana ya African Sports. Hakuweza kuichezea timu hiyo katika msimu wa kwanza baada ya kufungiwa na Chama cha Soka cha Tanga kwa tuhuma za kusajiliwa na timu mbili, ikiwemo Mchakamchaka.

Aliichezea timu hiyo msimu wa 1983 na 1984 akiwa na baadhi ya wanasoka nyota wa zamani kama vile Saidi Jacky, Bakari Jacky, Hemed Morocco, Duglas Muhani, Abdalla Shamimu, Salim Omar, Titus Bandawe na Elisha John.

Kung'ara kwake katika michuano ya ligi daraja la kwanza Tanzania Bara wakati huo, ndiko kulikomfanya aitwe kwenye kikosi cha Tanzania Bara na hatimaye kuichezea katika michuano ya Kombe la Chalenji iliyofanyika Uganda.

"Naikumbuka sana mechi yetu dhidi ya Uganda kwa sababu ilikuwa ya kwanza kwangu kubwa na ilikuwa ngumu. Uwanja ulikuwa umefurika mashabiki ile mbaya. Baada ya waganda kutufunga, nilifanikiwa kufunga bao la kusawazisha," alisema Hilal.

Mtanzania aliyekuwa akifahamika kwa jina la Swalehe, aliyekuwa akiishi Oman wakati huo, ndiye aliyemfungulia Hilal milango ya heri ya kwenda kucheza soka ya kulipwa Arabuni baada ya kumuona na kuvutiwa na kiwango chake kisoka alipokuwa akiichezea Taifa Stars mjini Mwanza.

"Huyu mzee ni Mtanzania aliyekuwa akiishi Oman. Alinifuata siku moja nikiwa na Amasha na kunieleza kwamba habari zangu zote zimeshafika Oman na ningeletewa viza wakati wowote kwa ajili ya kwenda huko," alisema Hilal.

Baada ya kufika Arabuni, Hilal alijiunga na klabu ya Fanja ambayo aliichezea kwa misimu tisa akiwa na baadhi ya wanasoka wenzake nyota kutoka Tanzania, kama vile marehemu Ramadhani Lenny, Twalib Hilal, Amasha, Madaraka Selemani, Zahor Salum na Abdul Wakati Juma.

Akiwa Fanja, Hilal aliweka rekodi ya kutwaa nayo taji la kwanza la ubingwa wa ligi ya Oman 1989 kabla ya kutwaa nayo mataji mengine matatu. Pia aliweka rekodi ya kutwaa nayo Kombe la Mfalme wa Oman mara tatu.

Hilal aliihama Fanja 1993 baada ya kununuliwa na klabu ya Dhofar yenye maskani yake katika mji wa Salala. Aliichezea klabu hiyo kwa miaka tisa na kuiwezesha kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Oman mara nne na Kombe la Mfalme mara moja.

Katika kikosi cha Dhohar, Hilal alicheza pamoja na Amasha, Gabriel Olanga, Douglas Mutua, Benard Otieno na Vitalis Oduor kutoka Kenya pamoja na Shock Gharib kutoka Misri, ambaye kwa sasa ni kocha msaidizi wa timu ya taifa ya nchi hiyo. Wachezaji wengine walikuwa wazawa.

Hilal aliamua kutundika daruga zake ukutani 2002 kwa kile alichokieleza kuwa ni kupumzika baada ya kucheza soka kwa miaka mingi. Lengo lake kubwa lilikuwa kutoa nafasi kwa wanasoka wengine chipukizi kuonyesha uwezo wao.

Mwanasoka huyo alisema alitamani sana kwenda kucheza soka ya kulipwa barani Ulaya, lakini ilikuwa vigumu kwa mchezaji anayetokea Arabuni kupata nafasi hiyo. Alisema anasikitika kwa kuikosa nafasi hiyo kwa vile ilikuwa ndoto yake kubwa kutokana na kuwa na sifa zote za kucheza soka ya kulipwa Ulaya.

Baada ya kustaafu soka, Hilal aliweza kusafiri katika nchi mbalimbali za Ulaya, ikiwa ni pamoja na Uholanzi, ambako aliishi kwa miaka kadhaa. Pia amewahi kutembelea Brazil zaidi ya mara tatu.

Hilal alisema anamshukuru Mungu kwamba mchezo wa soka umemwezesha kufanikisha mambo yake mengi, ikiwa ni pamoja na kuwa na maisha mazuri kutokana na kulipwa vizuri na klabu zote mbili alizokuwa akizichezea Arabuni.

"Wakati nilipokuwa nikicheza soka, nilihakikisha nafanyakazi kisawasawa. Sikuwa na mchezo katika kazi yangu. Nilikuwa mfungaji nyota wa mabao. Namshukuru Mungu alinijalia kipaji cha kucheka na nyavu. Hadi leo hii, nina jina kubwa Arabuni,"alisema Hilal.

Aliongeza: "Nilifanya vizuri sana nilipokuwa Fanja. Ilikuwa kila mechi, sikosi kufunga bao. Nikikukosa leo, lazima mechi inayofuata nikufunge."

Hilal alisema hakuweza kuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars baada ya kwenda Arabuni kutokana na kutokuwepo kwa utaratibu wa kufuatilia wachezaji wanaocheza nje ya nchi kama ilivyo sasa. Alisema utaratibu wa zamani wa makocha waliowahi kuifundisha Taifa Stars, ulikuwa ni kufuatilia wachezaji wanaocheza ligi za ndani.

Alisema makocha hao pamoja na viongozi wa kilichokuwa Chama cha Soka nchini (FAT) waliwadharau wachezaji waliokwenda Arabuni kwa kudhani kiwango cha soka katika nchi hizo ni duni.

"Lakini kusema ukweli, timu za Arabuni zilikuwa zikifundishwa na makocha wazuri na wenye uwezo mkubwa, kulikuwa na viwanja vizuri vya mazoezi, wachezaji walikuwa wanalipwa vizuri na timu zilikuwa zikiweka kambi katika baadhi ya nchi za Ulaya. Kwa jumla kulikuwa na kila kitu cha kumfanya mchezaji acheze soka kwa uwezo wake wote,"alisema.

Hilal anakiri kwamba, kiwango cha soka nchini miaka ya nyuma kilikuwa juu ikilinganishwa na sasa kwa vile wachezaji walicheza kwa ari kubwa na kujitolea kutokana na kuupenda mchezo huo.
Alisema ari waliyokuwa nayo wachezaji wa zamani ingekuwepo sasa, Tanzania ingekuwa imepiga hatua kubwa kimaendeleo.

Hata hivyo, Hilal alisema kiwango cha sasa kisoka kinaridhisha kutokana na kuwepo kwa mwamko kutoka kwa serikali na kampuni mbalimbali, ambazo zimeamua kuwekeza fedha zake ama kujitangaza kibiashara kupitia soka.

"Taifa Stars ya zamani haikuwa na mdhamini, ilikuwa ikisaidiwa na serikali, lakini wachezaji walicheza kwa ari kubwa. Hivi sasa kuna mabadiliko makubwa. Baadhi ya klabu zimekuwa zikiajiri makocha na wachezaji wa kigeni na hivyo kuongeza ushindani,"alisema.

Pamoja na kuwepo kwa ushindani wa klabu kusajili wachezaji wa kigeni, Hilal alisema haridhishwi na viwango vya baadhi yao kwa vile ni vya chini ikilinganishwa na wazawa. Alisema baadhi ya wachezaji wa kigeni wanapewa sifa na vyombo vya habari wakati uwezo wao ni mdogo.

Hilal alisema si rahisi kwa mchezaji kutoka Cameroon, Ghana au Nigeria kuja kucheza soka ya kulipwa Tanzania na kuongeza kuwa, wanaofanya hivyo wanafuata fedha kwa kulazimisha.

"Mimi nimeishi Uholanzi kwa miaka 10 baada ya kustaafu soka. Nimeona jinsi wachezaji wa kigeni wanavyotafutwa. Hakuna mchezaji wa kigeni anayechukuliwa akiwa na umri wa miaka zaidi ya 25,"alisema.

Hilal amelishauri Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutoa mafunzo ya utawala kwa wanasoka wa zamani ili waweze kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika ngazi za chini hadi Taifa. Alisema ni aibu kwa vyama vya michezo nchini kuongozwa na watu, ambao hawajahi kucheza soka na kufikia hatua ya kuichezea timu ya taifa ama hawana elimu yoyote kuhusu uongozi wa michezo.

"Uongozi wa soka lazima wapewe wanaojua soka na wafanyabiashara waendelee na biashara zao. Hata ukitazama katika nchi za Ulaya, wanasoka wastaafu ndio wanaopewa uongozi katika klabu na vyama vya michezo,"alisema.

Hilal alisema Tanzania haipaswi kuendelea kuwa na mizengwe iliyopo sasa katika uongozi wa soka na kwamba wachezaji wa zamani wanapaswa kupewa elimu ya uongozi wa mchezo huo ili washike madaraka.

Aliupongeza uongozi wa Coastal Union kwa kuwashirikisha wanasoka wake wa zamani kuunda benchi la ufundi. Alisema utaratibu huo utaisaidia klabu hiyo kupata mafanikio makubwa zaidi kisoka katika miaka michache ijayo.

Hilal pia alimpongeza Rais wa TFF, Leodegar Tenga kwamba ni kiongozi mzuri na aliyeleta mabadiliko makubwa katika shirikisho hilo kwa vile alicheza soka, lakini kelele zinazosikika sasa katika uongozi wake zinatokana na wasaidizi wake kushindwa kumsaidia.

Ameitaka TFF kuendelea kutoa kipaumbele kwa soka ya vijana kwa vile ndiyo msingi mzuri katika kuwaandaa wanasoka wa baadaye. Pia alizipongeza klabu za ligi kuu kwa kuwa na timu za vijana wa chini ya miaka 20.

Hata hivyo, Hilal alisema haitakuwa na maana kwa klabu hizo kuwa na timu vijana, lakini haziwathamini. Alisema timu za vijana zinapaswa kupewa hadhi sawa na za wakubwa ili kuwaongezea ari ya kufanya vizuri zaidi.

"Duniani kote, wachezaji wanaanza kuandaliwa wakiwa vijana. Wachezaji waliopo sasa katika timu ya Taifa ya Hispania walianza kuandaliwa tangu wakiwa wadogo. Ndio sababu unaona mbali na kutwaa ubingwa wa dunia, Hispania imetwaa ubingwa wa Ulaya na wa timu za vijana wa chini ya miaka 21,"alisisitiza mwanasoka huyo.

Hilal ameishauri TFF kuzipigania klabu za ligi kuu ili ziwe na ufadhili badala ya ilivyo sasa, ambapo baadhi ya timu zinashiriki ligi kwa matatizo kutokana na kukosa fedha. Alisema ni aibu kwa timu ya ligi kuu kukosa fedha za kusafiria kutoka kituo kimoja au kingine ama kukosa pesa za chakula na kuwalipa posho wachezaji wake.

"Nimecheza soka Arabuni kwa miaka 18, sijawahi kusikia timu imekwama kusafiri kwenda kituo cha ligi kwa kukosa pesa. Ni lazima tuondokane na uendeshaji soka wa aina hii. Ikiwezekana timu zisafirishwe kwa ndege na kupangiwa kwenye hoteli nzuri,"alisisitiza.

Hilal pia ameitaka TFF kurejesha utaratibu wa klabu mwenyeji katika ligi kuchukua mapato yote ili kuziwezesha kujikwamua kiuchumi. Ikiwezekana, Hilal alisema ni vyema kila klabu ikawa na uwanja wake ili ziweze kunufaika zaidi kimapato.

Hilal alizaliwa 1967 mkoani Tanga. Alisoma shule ya msingi ya Chuma kuanzia 1975 hadi 1981 alipomaliza darasa la saba. Alianza kucheza soka tangu akiwa shule ya msingi na pia alichezea timu ya mtaani ya Bomboka kabla ya kujiunga na timu ya African Sports Kids.