KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, November 15, 2012

OMOTOLA AZIDI KUPAA



LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu mwenye mvuto nchini Nigeria, Omotola Jalade amezidi kupaa kwa umaarufu, kufuatia filamu yake mpya ya Last Flight To Abuja kufanya vizuri kimataifa.
Omotola amecheza filamu hiyo kwa kushirikiana na waigizaji wengine maarufu wa Nigeria kama vile Jim Iyke, Jide Kosoko, Hakeem Kae Kazeem na wengineo.
Kufanya vizuri kwa filamu hiyo sokoni, kumeufanya mwaka 2012 uwe wa mafanikio makubwa kwa Omotola. Nakala zaidi ya milioni nane za filamu hiyo ziliuzwa katika wiki ya kwanza.
Kwa sasa, Omotola ndiye mwigizaji tajiri wa kike nchini Nigeria na pia amekuwa bize kucheza filamu nyingi zenye bajeti kubwa ya pesa.
Imeelezwa kuwa, ratiba ya Omotola kwa mwaka huu imejaa kutokana na kutakiwa kucheza filamu nyingi. Omotola ndiye mwigizaji pekee wa kike aliyecheza filamu nyingi mwaka huu.
Hivi karibuni, Omotola alifanya uzinduzi wa filamu yake mpya, inayojulikana kwa jina la Amina, uliofanyika mjini London, Uingereza na kuhudhuriwa na watu wengi maarufu.
Filamu hiyo imeandaliwa na kuongozwa na Christian Ashaiku na ameicheza kwa kushirikiana na Wil Johnson na Vincent Regan wa Uingereza.
Omotola pia ameshiriki kucheza filamu ya 'Ties That Bind' akiwa na baadhi ya wacheza filamu maarufu wa kike duniani kama vile Kimberley Elise, Kofi Adjorlolo, Ama K na Khareemar Aguiar.
Mama huyo wa watoto wanne, ambaye pia ni mwanamuziki amecheza filamu nyingine ya bei mbaya, inayojulikana kwa jina la Up Creek, ambayo ipo katika hatua za mwisho za matayarisho kabla ya kuingia sokoni. Pia ameitwa kucheza filamu mpya ya Teco Benson, inayojulikana kwa jina la Blood on the Lagoon.

UKWA: BADO NIPO NIPO KWANZA



LAGOS, Nigeria
MWIGIZAJI machachari wa Nigeria, Osita Iheme amesema bado hajajua ni lini atafunga ndoa na atamuoa nani.
Osita ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Ukwa au Pawpaw alisema juzi mjini hapa kuwa, atafunga ndoa wakati utakapofika.
Ukwa (32) ameelezea msimamo wake huo, kufutia ndugu, jamaa na marafiki kumuhoji mara kwa mara wakitaka kujua ni lini atafunga ndoa.
Licha ya umaarufu alionao katika fani ya uigizaji filamu na pia kuwa mmoja wa waigizaji wanaolipwa vizuri nchini Nigeria, Ukwa hajaoa.
Kaka na swahiba mkubwa wa mwigizaji huyo, Chinedu Ikedieze, maarufu kwa jina la Aki alifunga ndoa mwaka jana na imeripotiwa kuwa, tayari mkewe ni mja mzito.
Ukwa alikiri kuwa anajisikia vibaya kuona kuwa, swahiba wake huyo amefunga ndoa huku yeye akiwa bado anamsaka mchumba wa kumuoa.
"Sielewi lini nitafunga ndoa, lakini naelewa kwamba wakati utakapofika, kila mmoja atafahamu. Siwezi kueleza ni lini nitafanya hivyo," alisema Ukwa.
Aliongeza: "Mungu ananitayarishia njia kwa ajili yangu nami naelekea katika njia hiyo. Nitakapofika, kila mmoja atafahamu."
"Siwezi kusema kama tayari ninaye mchumba ninayetarajia kufunga naye ndoa. Wapo wanawake wengi sehemu mbali mbali duniani. Ni jukumu langu kumsikiliza Mungu atakapozungumza nami na kunionyesha mwanamke sahihi. Wakati utakapofika, nitachagua mwanamke huyo,"alisema Ukwa.
Katika hatua nyingine, Aki na Ukwa wameamua kuanzisha kampuni yao ya kutengeneza filamu, inayojulikana kwa jina la Aki and Pawpaw Entertainment Nigeria (APEN).
Maswahiba hao wamefikia uamuzi huo kwa lengo la kuanza kutengeneza filamu zao wenyewe na kuacha kucheza filamu za watu wengine.

GENEVIEVE ANG'ARA



LAGOS, Nigeria
MCHEZA filamu nyota wa kike wa Nigeria, Genevieve Nnaji ametajwa kuwa miongoni mwa wanawake 100 wapambanaji na wenye mvuto duniani kutokana na shughuli zao.
Jarida la Arise limemworodhesha Genevieve katika nafasi ya nane miongoni mwa wanawake wenye mvuto duniani katika masuala ya utamaduni, habari na michezo.
Mwandishi wa habari na mwanaharakati, Ahdaf Soueif wa Misri anashika nafasi ya kwanza katika orodha hiyo, akifuatiwa na mwanamuziki Angelique Kidjo wa Benin na mcheza filamu Angelina Jolie mwenye maskani yake nchini Marekani.
Mwanamuziki Buika wa Equatoria Guinea ameshika nafasi ya nne, mwandishi wa habari Charlayne Hunter-Gault wa Marekani ameshika nafasi ya tano, mwigizaji Charlize Theron wa Afrika Kusini ameshika nafasi ya sita wakati mtunzi wa vitabu Chimamanda Ngozi wa Nigeria ameshika nafasi ya saba.
Kwa upande wa siasa na harakati, Katibu Mkuu Msaidizi wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro wa Tanzania ameshika nafasi ya pili, nyuma ya Mkenya, Aicha Bah Diallo, ambaye ni mwanaharakati wa masuala ya elimu.
Katika orodha hiyo, pia yumo Mtanzania, Elsie Kanza, ambaye ni Mkurugenzi wa World Economic Forum, ambaye ameshika nafasi ya nane.
Kwa upande wa biashara na sheria, Mtanzania Genevieve Sangudi ameshika nafasi ya nane. Sangudi ni Mkurugenzi Mtendaji wa Carlyle Group Africa.
Jarida la Arise linachapishwa nchini Uingereza na kuuzwa katika sehemu mbali mbali duniani.

DIAMOND AMFAGILIA WALTER WA EBSS


MSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' amemfagilia mshindi wa shindano la Epiq Bongo Star Search (EBSS), Walter Chilambo kwamba alikuwa na kila sababu ya kushinda taji hilo.
Diamond amesema Walter ni msanii mwenye kipaji na uwezo mkubwa wa kufika mbali kimuziki iwapo atapata timu nzuri ya kumsaidia na pia promota wa uhakika.
Kauli hiyo ya Diamond imekuja siku chache baada ya Walter kuibuka mshindi wa taji hilo katika fainali ya kusisimua iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.
Walter, ambaye amerithi taji hilo kutoka kwa Haji Ramadhan, aliibuka mshindi baada ya kuwabwaga Salma Abushiri wa Zanzibar na Wababa Mtuka wa Dar es Salaam katika hatua ya fainali.
Ushindi huo ulimwezesha Walter kuzawadiwa kitita cha sh. milioni 50 kutoka kwa wadhamini wa mashindano hayo, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Zanter. Shindano hilo liliandaliwa na Kampuni ya Benchmark.
"Kiukweli muda wangu huwa ni mchache sana kukaa kwenye televisheni, lakini siku ambayo Walter aliimba wimbo wa Mawazo, nilikuwa nyumbani, nikamsikiliza kwa umakini sana,"ameeleza Diamond kupitia kwenye tovuti yake wiki hii.
"Nilichogundua ni kwamba (Walter) ana kitu ndani yake. Namaanisha kwamba ana uwezo wa ziada na nafasi nzuri katika muziki wa Tanzania,"alisema Diamond.
Aliongeza: "Suala la kufika kwenye ngazi ya kimataifa hilo ni letu sisi Watanzania kumwezesha pamoja na yeye binafsi kuwa chini ya utawala makini, hasa kipindi hiki anachoanza kuingia katika fani hii ya muziki."
Diamond alifichua kuwa, binafsi alimpigia kura Walter akiwa na imani kubwa kwamba ndiye mshindi wake na kweli hakumuangusha.
"Nimefurahi sana. Namtakia kila la heri,"ameeleza Diamond kupitia tovuti yake, ambayo ni miongoni mwa mitandao yenye wasomaji wengi ndani na nje ya nchi.
Dalili za ushindi kwa Walter zilianza kuonekana mapema kutokana na kuimba nyimbo zenye mvuto na alizozimudu vyema.
Katika hatua ya fainali, washiriki walitakiwa kuchagua wasanii maarufu kwa ajili ya kuimba nao wimbo mmoja. Walter alimchagua Ditto. Katika hatua hiyo, Walter aliimba kibao cha One Love cha Steve na Nikikupata cha Ben Pol.
Akizungumza baada ya kutwaa taji hilo, Walter alisema anamshukuru Mungu kwa sababu hakuamini iwapo angeweza kuibuka mshindi.
Walter alisema kulikuwepo na changamoto nyingi wakati wote wa shindano hilo na kwamba ushindani ulikuwa mkali kwa vile kila mshiriki alipania kuibuka mshindi.
Alisema hakuna mshiriki aliyekuwa akimuhofia kwa sababu alijiamini na kufuata vyema mafunzo ya walimu wake ndio sababu ilikuwa rahisi kwake kuibuka mshindi.
Walter alisema wakati alipoingia kwenye shindano hilo, hakuwa akiufahamu vyema muziki zaidi ya kuwa na uwezo wa kuimba na kuiga nyimbo za wasanii mbalimbali maarufu, lakini kwa sasa amekomaa.
Mshindi huyo wa EBSS 2012 hakuwa tayari kueleza atazitumiaje fedha alizopata kwa kushinda taji hilo. Alisema atajiepusha na matumizi yasiyo na lazima na kuhakikisha kuwa, fedha hizo zinazalisha fedha zingine zaidi.

SIJAWAHI KUPOKEA RUSHWA-DIDA



KLABU ya Azam hivi karibuni ilitangaza kuwasimamisha wachezaji wake watatu nyota, akiwemo kipa Deogratius Boniventura Mushi, maarufu kwa jina la Dida kwa tuhuma za kupokea rushwa kutoka kwa timu pinzani wakati wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na Mwandishi Wetu ATHANAS KAZIGE, Dida anazungumzia kuhusu tuhuma hizo na mikakati yake katika soka.

SWALI: Wiki iliyopita ilitolewa taarifa na klabu ya Azam ikikuhusisha wewe na wachezaji wenzako wawili, Erasto Nyoni, Said Morad na Aggrey Morris mkituhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa timu pinzani wakati wa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Nini ukweli kuhusu tuhuma hizo?
JIBU:Kwa kweli nimejisikia vibaya sana kutokana na kuhusishwa na jambo hilo. Mimi ni Mkristo tena Mromani, sijawahi kufanya jambo hilo hata siku moja katika maisha yangu na kwa kweli taarifa hizi zimeniumiza sana.
Nadhani viongozi wa Azam hawakututendea haki, hasa mimi binafsi. Ni kweli kila kukicha tuhuma hizi zimekuwa zikitawala katika soka ya Tanzania, lakini si jambo zuri kumuhusisha mchezaji bila ya kuwa na ushahidi.
Kwa vile uongozi wa Azam umesema umewasilisha tuhuma hizo TAKUKURU (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa), nina hamu kubwa ya kusikia matokeo ya uchunguzi wao ili haki itendeke na kwa wale waliojihusisha kweli na vitendo hivyo, sheria ichukue mkondo wake.
Hivyo ndivyo ninavyoweza kuzungumza kwa sasa. Lakini napenda kuweka wazi kuwa, sijawahi kujihusisha na vitendo hivyo hata siku moja katika maisha yangu na kama nimefanya hivyo, Mungu atanihukumu. Namuachia yeye kwa sababu ndiye muweza wa yote.
SWALI: Familia yako ilizipokea vipi hizi taarifa?
JIBU: Naweza kusema kwa mara ya kwanza nimepata aibu kubwa katika maisha yangu. Lakini kwa sababu familia yangu, hasa wazazi, ndugu na marafiki wananifahamu vyema, wameshangazwa na tuhuma hizo na hakuna anayeamini kwamba ninaweza kufanya vitendo hivyo.
Kushangaa kwao kumetokana na ukweli kwamba, mbali na kujihusisha na soka, mimi ni mfanyabiashara hivyo ninakuwa na shughuli nyingi za kufanya na kujishughulisha nazo. Kwa kweli imeniuma sana.
Mbali na kufanya biashara, nilikuwa nikilipwa mshahara mzuri na Azam, hivyo sikuwa na sababu ya kujihusisha na vitendo vichafu kama vile kupokea rushwa. Hakuna timu inayowalipa vizuri wachezaji wake kama Azam. Sidhani kama kuna mchezaji anayeweza kukubali apewe rushwa ili aihujumu timu inayomsaidia kuendesha maisha yake.
Napenda kutumia nafasi hii kuuhakikishia uongozi wa Azam na wapenzi wa soka nchini kwamba, sijawahi kupokea rushwa ili niihujumu Azam na hizi tuhuma kwangu ni za uongo na kupandikiza kwa lengo la kuchafua jina langu.
SWALI: Unadhani tuhuma hizi zinaweza kuwa zimepandikizwa kwa lengo la kukuchafua?
JIBU: Hiyo ni kweli kabisa. Kuna baadhi ya watu, ambao wamekuwa wakipeleka taarifa potofu kwa uongozi kwa lengo la kutuchafua baadhi yetu. Na inasikitisha kuona kuwa, uongozi umekuwa ukizipokea taarifa hizi na kuchukua hatua bila ya kufanya uchunguzi.
Kwa mchezaji yeyote mwenye akili timamu hawezi kufanya kitu kama hicho kwa sababu soka ndiyo ajira yake. Akicheza vizuri, ulaji ndipo unaongezeka. Kwa mtu kama mimi, nikifanya kitu kama hicho ni sawa na kujiua kisoka.
Ukifuatilia kwa makini, katika mechi zetu dhidi ya Simba na Yanga, mimi sikukaa langoni. Mechi zote mbili alicheza Mwadin Ally, sasa iweje niambiwe kwamba nilipewa rushwa wakati sikucheza? Kama huku si kuharibiana, ni nini? Ninawezaje kuhujumu timu wakati sikucheza?
SWALI: Baada ya vipigo hivyo, bodi ya wakurugenzi ya Azam ilifanya mabadiliko kwenye benchi la ufundi kwa kumuondoa Kocha Boris Bunjak wa Serbia na kumrejesha Stewart Hall, ambaye alitimuliwa mwishoni mwa msimu uliopita. Nini maoni yako kuhusu mabadiliko haya?
JIBU: Kwa hilo siwezi kusema lolote kwa sababu mimi siye mwajiri. Inawezekana uongozi ulimuona Bunjak uwezo wake ni wa chini. Kazi yangu ni kucheza soka, hivyo jukumu langu ni kufuata maelekezo ya kocha yoyote.
SWALI: Baada ya kusimamishwa na uongozi kwa tuhuma za rushwa, unafikiri wachezaji wenzenu watakuwa katika morari?
JIBU: Ni wazi kwamba uamuzi huu umewashtua sana wachezaji wenzetu na nina hakika wapo baadhi ambao wataanza kucheza kwa woga kwa vile watakuwa hawajui hatma yao. Hili ni jambo la hatari sana kwa timu kubwa kama Azam.
SWALI: Baada ya sakata hili, kumekuwepo na uvumi kwamba unataka kurejea katika klabu yako ya zamani ya Simba. Je, kuna ukweli wowote kuhusu taarifa hizi?
JIBU: Taarifa hizo hazina ukweli wowote. Mimi bado ni mchezaji wa Azam kwa vile nina mkataba nayo, labda litokee jambo jingine. Lakini kwa sasa bado mimi ni mchezaji wa Azam.
SWALI: Una maoni gani kuhusu maendeleo ya soka nchini?
JIBU: Napenda kuwashauri viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), kufuatilia kwa makini mambo yanavyokwenda ndani ya klabu za ligi kuu kwa vile wachezaji wengi wanakosa haki zao za msingi.
Kwa mfano hivi karibuni, mwenzetu Nsa Job aliumia katika mechi ya ligi kuu na kibaya zaidi hakuwa na bima, ingawa sheria zinataka timu zote za ligi kuu ziwakatie bima wachezaji wake.
Sio jambo zuri kuwaacha wachezaji wanaumia na kupata ulemavu kutokana na mechi za ligi huku viongozi wakinufaika kwa mapato ya milangoni. Ni vyema viongozi wa TFF wafuatilie kwa makini suala hili.

Friday, November 9, 2012

10 WATEULIWA KUISAIDIA SERENGETI BOYS



SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania limeteua wadau 10 kwa ajili ya kusaidia timu ya taifa ya vijana walio na umri chini ya miaka 17, Serengeti Boys itakayopambana na Congo (Brazaville) katika mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya awali ya Mataifa ya Afrika.
Uteuzi huo umefanywa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga baada ya Kamati ya Vijana ya TFF kufanya kikao chake kujadili kwa umakini ushiriki wa timu hiyo na kupeleka mapendekezo yake kwa rais huyo wa shirikisho.
Kutokana na umuhimu wa mechi hiyo itakayoamua timu itakayofuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika, TFF imeona umuhimu wa kuwa na kamati ambayo itakuwa na majukumu mawili makubwa ambayo ni:
1. Kuhamasisha vijana waone umuhimu na kuwa na ari ya kushinda mechi hiyo
2. Kuhamasisha umma uone umuhimu wa mechi hiyo na hivyo kuisaidia iweze kufuzu.
Walioteuliwa kuunda kamati hiyo ni:
1. Ridhiwani Kikwete Mwenyekiti
2. Ahmed Seif (Magari) Mjumbe
3. Nassoro Bin Slum Mjumbe
4. Henry Tandau Katibu
5. Ahmed Mgoyi Mjumbe
6. Aboubakar Bakhresa Mjumbe
7. Angetile Osiah Mjumbe
8. Kassim Dewji Mjumbe
9. Abdallah Bin Kleb Mjumbe
10. Salim Said Mjumbe

Baada ya kuvuka raundi mbili za kwanza bila ya kucheza mechi kutokana na wapinzani wake kujitoa, timu ya Serengeti Boys inahitaji kufanya kila iwezalo kuweza kuiondoa Congo kwenye mashindano hayo na kuweka rekodi ya kufuzu kucheza fainali hizo za Afrika ambazo pia zitatoa wawakilishi wa Afrika kwenye mashindano ya Kombe la Dunia. Mechi za kwanza za raundi ya tatu zitachezwa kati ya Novemba 16 na 18, 2012 na mechi za marudiano zitachezwa kuanzia Novemba 30, 2012 hadi Desemba 2, 2012

UCHAGUZI TARFA, TAFCA SASA DES 22




Uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tabora (TAREFA) na Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) sasa utafanyika Desemba 22 mwaka huu.
Kwa mujibu wa ratiba za uchaguzi za vyama hivyo, Kamati zao za uchaguzi zitatangaza kuanza mchakato wa uchaguzi Novemba 10 mwaka huu wakati fomu kwa wanaotaka kugombea uongozi zitaanza kutolewa Novemba 12 mwaka huu. Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni Novemba 16 mwaka huu.
Kamati ya Uchaguzi ya Shirkisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imetoa mwongozo huo kwa Kamati ya Uchaguzi ya TAFCA baada ya kuomba hivyo kutokana na wagombea sita tu kujitokeza kuomba nafasi tatu za uongozi katika mchakato wa awali.
Kwa waombaji ambao awali walichukua na kulipia ada ya fomu za kugombea uongozi TAFCA na TAREFA, hawatatakiwa kulipia tena ada kwa nafasi zile zile walizoomba, isipokuwa watatakiwa kujaza fomu upya.
PONGEZI KWA UONGOZI MPYA FA MWANZA
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika Novemba 8 mwaka huu.
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa MZFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo katika Mkoa wa Mwanza.
TFF inaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Kamati za Utendaji ya MZFA iliyochaguliwa chini ya uenyekiti wa Patrick Songora aliyechaguliwa kwa kipindi cha pili mfululizo.
Uongozi huo mpya wa MZFA una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu kwa kuzingatia katiba ya chama chao pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yao.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa kuongoza MZFA ni Patrick Songora (Mwenyekiti), Nassoro Mabrouk (Katibu) na Richard Kadutu (Mwakilishi wa Klabu TFF).

NYOTA WA AIRTEL RISING STARS KUJIUNGA NA SERENGETI BOYS

Hivi karibuni timu ya taifa ya Tanzania Chini ya miaka 17 ilimchangua kujiunga na kikosi hicho mchezaji nyota wa Airtel Rising Stars Abdul Suleiman ambaye alichaguliwa kati ya mmoja wa wachezaji bora wakati wa kliniki ya soka Afrika iliofanyika Septemba 2012 mjini Nairobi.
Abdul Suleimani ambaye anacheza kama kiungo ubunifu, ameendelea kuwa kivutio kikubwa na kuvuta hisia za makocha wa soka wakati wa michuano ya Airtel Rising Stars katika ngazi zote kuanzia kikanda, kitaifa na kimataifa.
Kuchaguliwa kwake timu ya taifa kumeenda sambamba na hisia chanya za makocha watatu wa shule ya soka wa Manchester United walizoona juu ya mchezaji huyo ambazo ni nidhamu yake, kudhibiti mpira na ujuzi wake wa kutoa pasi, kumekuwa sababu Abdul alichaguliwa kama mmoja wawachezaji nyota ya juu kati ya watatu( 3) baada ya kliniki. Kliniki ya soka iliendeshwa na Makocha kutoka Manchester united kwa kushirikiana na Airtel Afrika yenye lengo la kuwapatia vijana wachezaji wa soka Afrika uzoefu na mbinu za kuwa mchezaji bora na wa kitaalamu
Abdul Suleiman ni mtoto wa mwisho na wakiume pekee katika familia ya watoto wa Nne ya mzee Suleiman Mshilu. Alionyesha uwezo wake wa soka wakati wa michuano ya Airtel Rising stars 2012 akitokea katika shule ya sekondari Tiravi akishiriki kutoka katika mkoa wa kisoka wa Temeke, Abdul aliibuka kuwa mchezaji bora wakati wa michauano ya Airtel Rising Stars kitaifa na kuchaguliwa kuiwakilisha Tanzania katika michuani ya Airtel Rising Stars Tanzania.
Ingawa Timu ya Tanzania haikufika katika hatu ya finali katika michuano ya Afrika uwezo wakucheza mpira wa mchezaji wa Abdul haukufichika kwani aliweza kutoa pasi zilizowawezesha timu yake kufunga mabao mawili wakati wa michuano hiyo
Akiongea kuhusu Mchezaji huyo Kocha John "Del Piero" William amesema Abdul Sulemani ni mchezaji kiungo anayecheza namba 7 na amekuwa mchezaji bora na kuwezesha timu yake ya temeke kuibuka mabingwa kwa kutoa pasi nzuri kwa wafungaji wake na kumwezesha mshambuliaji wa timu yake, Paulo Balama, kuibuka kuwa Mfungaji Bora wakati wa michuano ya taifa ya ARS 2012
Abdul tayari amejiunga na timu ya taifa kwaajili ya kujiandaa na mechi dhidi ya Msumbiji na Kongo. Hii ni ndoto aliyokuwa nayo na sasa imeanza kutimia, "Nafasi Hii itaniwezesha kuonyesha vipaji yangu kwa wadau wa soka dunia nzima na hatimaye kufikia dhamira na lengo langu la kuwa mchezaji wa kimataifa, naamini kwa kuchaguliwa Kucheza timu ya Taifa ni dhahiri kutafungua milango yangu.” alisema mchezaji huyo nyota. Ndoto yangu ni kucheza katika Ligi ya Kiingereza au Kihispania
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania Sam Elengahoor, alisema: "Tunasikia fahari kwamba shirikisho la mpira Tanzania tayari limeaona mchango wa mpango wa Airtel Rising stars katika kuvumbua na kuinua vipaji vya vijana kwa ajili ya kujiunga na kucheza katika klabu na timu za taifa. Huu ni ushirikiano sawia kwa wachezaji na mpango huu kambambe wa kuinua vipaji. Wachezaji wengine walioshiriki Airtel Rising Stars mwaka huu wanacheza katika vilabu mbalimbali na mashule ikiwemo Paulo Balama na Denis Richard ambao wanacheza katika klabu ya Simba B. Mwaka jana, Airtel Rising Star ilifungua milango kwa Suleiman Bofu kujiunga timu ya Taifa chini ya miaka 17 ambapo Bofu bado ni mchezaji katika kikosi cha timu ya taifa hadi sasa.
Airtel Rising Stars ni mpango maalumu ulioanzishwa na Airtel mwaka 2011 kwa lengo la kuinua, kugundua na kuendeleza wachezaji wenye vipaji chini ya umri wa miaka 17 'katika makundi yote mawili ya kiume na kike. Mpango huu unaendesha katika nchi 15 barani Afrika ambapo Airtel inaendesha shughuli za kibiashara na mikakati iliyopo ni kupanua na kuongeza nchini nyingi zaidi ambazo Airtel inafanya biashara katika msimu ujao.
Wachezaji wengine wengi wenye vipaji katika bara la Afrika wamepokea wito wa kujiunga na timu za Taifa chini ya miaka 17. Airtel Ghana hivi karibuni imesherehekea mchezaji nyota - Priscilla Okyere ambaye alikuwa nahodha na alifunga bao na kuwawezesha timu ya Ghana wanawake chini ya miaka 17 kutwaa medali ya shaba katika Michuano ya FIFA ya mashinda ya kombe la wanawake chini ya miaka 17 ya duani yaliyohitimisha na kufanyika katika Jamhuri ya Azerbaijan.

TASWA YAISHTAKI TFF KWA MOAT



CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kimeamua kulipeleka kwa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), suala la kuzuia televisheni na redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na wapiga picha za televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari.
Hatua hiyo ya TASWA ina lengo la kuomba mwongozo kwa chama hicho ambacho ndio kinachomiliki vyombo vya habari kuhusiana na suala hili ambalo limekuwa likilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na wanachama wetu.
Tayari TASWA imefanya mazungumzo ya awali na MOAT, ambayo imeridhia iandikiwe barua rasmi ili jambo hilo lijadiliwe kwenye vikao vyake na baada ya hapo TASWA itapewa mwongozo ambao itautoa kwa waandishi wa habari za michezo.
Kwa kuwa Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto pia ni mjumbe wa MOAT, basi suala hilo tunaamini litafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo, hivyo tunawaomba waandishi wa habari za michezo waendelee kuwa watulivu na wavumilivu kipindi hiki na wafanye majukumu yao kama kawaida.
Siku zote chama chetu kimekuwa na uhusiano mzuri na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na wadau wengine wote na TASWA haitaki ifike mahali iwe na mgogoro na chama chochote cha michezo, lakini pia haitakuwa tayari kuona wanachama wake wakishindwa kutekeleza majukumu yao.
Kama mnavyojua wiki iliyopita kulifanyika kikao cha Kamati ya Ligi na baadhi ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo kuhusiana na tukio la kuzuia televisheni na redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na wapiga picha za televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari.
Katika kikao hicho ambacho Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alihudhuria kulitoka maelezo mbalimbali ambayo baadhi ya wanahabari hawakubaliani nayo na wamekuwa wakitaka TASWA ichukue hatua uamuzi mgumu.
Sekreterieti ya TASWA imeona si vizuri kukurupuka kuchukua uamuzi wowote ule kwa sasa kwani yenyewe haina chombo cha habari, lakini wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari ndiyo wanachama wake. Itawasilisha MOAT maazimio ya kikao cha Kamati ya Ligi kuhusiana na jambo hili, tuna hakika tutalimaliza.
B.MKUTANO MKUU
Jumatano Novemba 16, 2012 Kamati ya Utendaji ya TASWA itakutana Dar es Salaam kupitia ajenda za Mkutano Mkuu wa chama chetu, kisha Jumatatu Novemba 18 Mwenyekiti wa TASWA atafanya mkutano na wanahabari kutangaza mdhamini wa mkutano huo pamoja na tarehe rasmi na mahali utakapofanyika.
Kutokana na kuandaliwa kwa ajenda mpya ya kuboresha chama na maslahi ya wanachama wake, TASWA inaendelea kutafuta wadhamini zaidi ili kuufanya mkutano huo uwe wa siku mbili.

MECHI TANO ZA LIGI KUU ZAIPISHATAIFA STARS




Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imefanya mabadiliko madogo ya ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom ili kupitisha mechi ya kirafiki ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kati ya Taifa Stars na Kenya (Harambe Stars) itakayochezwa Novemba 14 mwaka huu jijini Mwanza.
Mechi tano za ligi hiyo zilizokuwa zichezwe Novemba 11 mwaka huu, zimerejeshwa nyuma kwa siku moja ambapo sasa zitafanyika Novemba 10 mwaka huu. Mechi hizo ni Simba vs Toto Africans (Uwanja wa Taifa), Kagera Sugar vs Polisi Morogoro (Uwanja wa Kaitaba) na Oljoro JKT vs Ruvu Shooting (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid).
Nyingine ni Tanzania Prisons vs JKT Ruvu (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine) na African Lyon vs Mtibwa Sugar (Azam Complex). Mechi ya Mgambo Shooting vs Azam (Azam Complex) yenyewe itachezwa Novemba 10 mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa.
Nayo mechi ya Coastal Union vs Yanga (Uwanja wa Mkwakwani) itabaki Novemba 11 mwaka huu kwa vile Novemba 10 mwaka huu uwanja huo utakuwa na mechi nyingine. TFF imepanga utaratibu wa kuwapata kwa wakati wachezaji wa Yanga walioitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Mabadiliko mengine ni ya Ligi Daraja la Kwanza (FDL) ambapo mechi ya Villa Squad vs Transit Camp iliyokuwa ichezwe Novemba 8 mwaka huu sasa inachezwa Novemba 9 mwaka huu, na ile ya Novemba 7 mwaka huu kati ya Burkina Faso na Small Kids inachezwa Novemba 9 mwaka huu. Viwanja ni vilevile.
Kamati ya Ligi imelazimika kufanya mabadiliko hayo kutokana na viwanja husika kuwa na mechi nyingine, na vilevile Small Kids kupata matatizo ya usafiri kutoka mkoani Rukwa kwenda Morogoro.

Tuesday, November 6, 2012

ABEDI PELE AWAPA MOYO CHIPUKIZI WA BONGO




Na Angetile Osiah NYOTA wa zamani wa Ghana na klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa, Abedi Ayew Pele, amewaambia wachezaji chipukizi wa Tanzania kwamba, hakuna njia ya mkato katika kutafuta mafanikio na kuwataka kufanya jitihada ili watimize ndoto zao, ikiwa ni pamoja na Serengeti Boys kuhakikisha inafuzu kucheza fainali za Afrika mwakani. Pele, ambaye aliiongoza Marseille kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992 akifunga moja ya mabao dhidi ya AC Milan ya Italia, alisema hayo Jana asubuhi wakati alipotembelea Kiti cha ufundi cha Karume kushuhudia programu ya mazoezi ya vijana wadogo inayofanyika kila misho wa wiki kwenye Uwanja wa Karume ambako watoto wa kuanzia umri wa miaka sita hadi 17 hufundishwa mbinu za kusakata soka. "Katika kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato," alisema Pele ambaye ameletwa nchini na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) kuangalia shughuli mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu nchini. "Tunaona wachezaji wenye vipaji vikubwa duniani wakifanya jitihada kubwa ili waweze kucheza kwa kiwango cha juu. Bila ya kufanya juhudi, kujituma na kudhamiria huwezi kufanikiwa. "Wale wenye vipaji vikubwa, lakini hawafanyi jitihada watabakia I. Wale wasiojaliwa kuwa na vipaji, lakini wanafanya jitihada, watakwenda mbele na kupata mafanikio," alisema nyota huyo ww Ghana ambaye alijijengea jina kwa kufunga mabao safi na muhimu kwa nchi yake na klabu ya Olympique Marseille wakati ikitamba katika soka barani Ulaya. "Soka barani Afrika Lina mazingira yanayofanana. Hakuna motto wa waziri anayecheza soka. Wala hakuna mtoto wa mwanasheria au mfanyakazi ww benki ambaye anacheza soka. Soka inachezwa na watu wanaotoka kwenye familia ambazo hazina maisha mazuri na hivyo man nafasi sawa na wengine wote. Mnachotakiwa kufanya ni kujituma, kudhamiria na kufanya jitihada ili mfungue mlango wa mafanikio. Pele, ambaye jina lake halisi ni Abedi Ayew na ambaye watoto wake wainaichezea Marseille, pia aliwataka wacheaji aw timu ya Taifa ya Vijana walio na umri china ya miaka 17 kufanya kila wawezalo ili wafuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Algeria mapema mwakani. "Mkifuzu mtakuwa mmefungua milango ya mafanikio ya maisha yenu," alisema gwiji huyo ambaye anaiwakilisha FIFA katika kufuatilia programu mbalimbali za maendeleo. "Nikiwaangalia naona mna man uwezo wa kuwaondoa wapinzani wenu na nitafuatilia mechi yenu. Mkifuzu tutakuwa wote na nitawaunga mkono. Pele, ambaye kwa sasa anamiliki shule ya mpira wa miguu ambayo imeshanikiwa kutwaa Kombe la FA mara moja, ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo wa FIFA kwa nchini za Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi na mmoja wa viongozi wa Idara ya Mawasiano ya FIFA, Emmanuel, atakuwa nchini kwa siku tatu ambazo atazitumia kupata taarifa za shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwemo za soka la watoto (grassroots), soka la vijana, soka la wanawake na miradi mingine ya maendeleo. (Angetile Osiah ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, TFF)

TFF YAIPONGEZA TRFA



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa uongozi mpya wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Tanga (TRFA) uliochaguliwa katika uchaguzi uliofanyika jana (Novemba 3 mwaka huu).
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TRFA walivyo na imani kubwa kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Tanga.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya Utendaji ya TRFA ambayo imechaguliwa chini ya uenyekiti wa Said Soud.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu Tanga kwa kuzingatia katiba ya TRFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya TRFA na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa ni Said Soud (Mwenyekiti), Beatrice Mgaya (Katibu), Khalid Mohamed (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF) na Juma Mgunda (Mwakilishi wa Klabu TFF).

TFF YAREKEBISHA RATIBA YA LIGI



Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limefanya mabadiliko ya mechi hizo baada ya kutokea dharura, hivyo kushindwa kufanyika kwa mujibu wa kanuni.
Sababu za mabadiliko hayo ni timu ya Tanzania Prisons kupata ajali wakati ikienda Tanga kwa ajili ya mechi dhidi ya Mgambo Shooting. Pia mvua kubwa iliyonyesha jijini Mwanza ilisababisha kutofanyika kwa mechi ya Oktoba 31 mwaka huu kati ya Toto Africans na Kagera Sugar.
Mechi hizo sasa zitafanyika kama ifuatavyo; Mgambo Shooting vs Tanzania Prisons (14/11/2012- Mkwakwani, Tanga), Ruvu Shooting vs Tanzania Prisons (18/11/2012- Mabatini, Pwani), Mtibwa Sugar vs JKT Ruvu (7/11/2012- Manungu, Morogoro), Kagera Sugar vs Tanzania Prisons (4/11/2012- Kaitaba, Bukoba), na Ruvu Shooting vs Toto Africans (4/11/2012- Mabatini, Pwani).
Mechi mbili za Ligi Daraja la Kwanza zimefanyiwa mabadiliko. Mechi kati ya Tessema vs Ndanda iliyokuwa ichezwe tarehe 4/11/2012 Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani sasa itafanyika tarehe 5/11/2012 katika uwanja huo huo. Mabadiliko hayo yanapisha mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Ruvu Shooting vs Toto Africans ambayo itachezwa 4/11/2012 kwenye uwanja huo huo.
Ashanti United vs Tessema zilizokuwa zicheze Uwanja wa Mabatini 7/11/2012 sasa zitacheza siku inayofuata (8/11/2012). Mabadiliko hayo ni kutoa fursa ya kupumzika kwa Tessema ambayo 5/11/2012 itacheza na Ndanda.

YANGA SPIDI 120



BAADA ya kuichapa Azam mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara jana iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga imetwaa uongozi wa ligi kuu na huenda isikamatike tena.
Ushindi wa Yanga umeiwezesha kutwaa uongozi wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 26 baada ya kucheza mechi 12, ikifuatiwa na Simba yenye pointi 23 na Azam yenye pointi 21.
Yanga sasa itamaliza mechi zake za mzunguko wa kwanza kwa kumenyana na Coastal Union kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga wakati Simba itahitimisha ligi hiyo kwa kumenyana na Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Mabao ya Yanga yalifungwa na Didier Kavumbagu na Hamisi Kiiza, moja katika kila kipindi. Mechi hiyo ilishuhudiwa na mjumbe maalumu wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), Abedi Pele.
Mara baada ya mechi hiyo, uongozi wa Yanga uliamua kuwazawadia wachezaji wake sh. milioni 15 kwa kuifunga Azam.
Hiyo ilikuwa mara ya pili kwa Yanga kuitambia Azam msimu huu. Katika mechi ya fainali ya Kombe la Kagame, Yanga iliichapa Azam mabao 2-0.

MGOMO WA WACHEZAJI WAIPONZA SIMBA



MGOMO baridi unaofanywa na wachezaji wazalendo umeelezwa kuwa ndio chanzo cha timu hiyo kuvurunda katika mechi zake za hivi karibuni za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Uchunguzi uliofanywa na Liwazozito umebaini kuwa, baadhi ya wanasoka wazalendo hawaafiki wenzao wa kigeni kulipwa mishahara mikubwa wakati mchango wao ni mdogo katika timu.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, hali hiyo imewafanya wachezaji hao wazalendo wacheze chini ya kiwango kwa lengo la kuushinikiza uongozi uwepo uwiano mzuri wa malipo ya mishahara.
Mmoja wa wachezaji waandamizi wa timu hiyo, aliieleza Liwazozito kwamba, wachezaji kama Komabil Keita na Paschal Ochieng wanalipwa mshahara wa sh. milioni 1.5 kwa mwezi, lakini wamecheza idadi ndogo ya mechi hadi sasa.
Mchezaji huyo alidokeza kuwa, viwango vya mishahara kwa wachezaji wazalendo ni kati ya sh. 500,000 na milioni moja wakati kiwango cha juu cha wanasoka wageni ni sh. milioni tatu.
Felix Sunzu ndiye mchezaji ghali kuliko wote Simba akiwa analipwa mshahara wa sh. milioni tatu wakati Emmanuel Okwi naye amekuwa akishinikiza kuongezwa mshahara katika mkataba wake mpya. Kwa sasa, Okwi analipwa sh. milioni 1.5.
Wachezaji, ambao wamekuwa wakitajwa kulipwa kiwango kidogo cha mshahara wakati mchango wao ni mkubwa katika timu ni pamoja na Shomari Kapombe, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto na Masoud Nassoro 'Cholo'.
Mrisho Ngasa, ambaye amesajiliwa na Simba akitokea Azam, analipwa mshahara wa sh. milioni mbili wakati Kapombe analipwa sh. 700,000 baada ya kupandishiwa hivi karibuni kutoka sh. 500,000.
Kwa mujibu wa mchezaji huyo, mgomo huo ndio uliosababisha Simba ilazimishwe kutoka sare ya bao 1-1 na Polisi Morogoro kabla ya kuchapwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar jana kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Mmoja wa viongozi wa Simba amekiri kutambua kuwepo kwa mgomo huo na kuongeza kuwa, wanatarajia kukutana hivi karibuni kujadili hatua za kuwachukulia wachezaji wanaowashawishi wenzao kucheza chini ya kiwango.
Katika mechi ya jana, Mtibwa Sugar ilijipatia mabao yake kupitia kwa Mohamed Mkopi na Hussein Javu, kufuatia uzembe wa kipa Juma Kaseja wa Simba, ambaye mashabiki wameanza kumshutumu kwamba kiwango chake kimeporomoka na anahitaji kupumzika.

Saturday, November 3, 2012

BRIDGIT NDIYE MISS TANZANIA 2012




Bridgit Alfred mwenye umri wa miaka 18, ametwaa taji la Miss Tanzania 2012 katika shindano lililofanyika jana kwenye ukumbi wa Blue Pearl Hotel, uliopo ndani ya jengo la Ubungo Plaza, Dar es Salaam. Ushindi huo ulimwezesha Bridgit kutoka Kinondoni, Dar es Salaam kuzawadiwa sh. milioni nane na gari, ambalo aina yake na thamani yake vitajulikana baadaye. Euegene Fabian aliibuka kuwa mshindi wa pili na kupewa sh. milioni 6.2 wakati Eddah Sylvester aliibuka kuwa mshindi wa tatu na kupewa sh. milioni nne.

DOGO ASLAY KUWANIA TUZO YA KORA


Msanii mdogo anayekimbiza wenzake wadogo wanaokuja hapa Bongo (Aslay), ametajwa kama msanii mpya katika tuzo za Kora mwaka huu (Best Male Newcomer). Wimbo uliompeleka katika tuzo hizo unaitwa NIWE NAWE, Aslay anapambana na wasanii kutoka nchi nyingine kama Uganda, Burkina Faso, Zambia, Nigeria na Afrique Du Sud. Mbali na Dogo Aslay tunao wasanii wengine wakubwa kutoka Tanzania hapa kama Lady Jay Dee, Saida Karoli na Ali Kiba...

Thursday, November 1, 2012

YANGA YAITEKA DRFA


KLABU ya Yanga imeamua kukiteka Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) baada ya wanachama wake maarufu kuchukua fomu za kuwania uongozi wa chama hicho.
Wanachama waliochukua fomu leo katika ofisi za DRFA ni Ahmed Seif 'Magari' anayewania nafasi ya mwenyekiti na Ally Mayay, anayewania nafasi ya makamu mwenyekiti.
Uamuzi wa wanachama hao kuwania uongozi wa DRFA, umekuja siku chache baada ya kubaini kuwa, watani wao wa jadi Simba, wamejaza viongozi wengi katika baadhi ya vyama vya mikoa.
Hivi karibuni, mjumbe wa kamati ya usajili ya Simba, Othman Hassan 'Hassanoo' alifanikiwa kukitetea kiti chake cha mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Pwani (COREFA) wakati makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Geofrey Nyange 'Kaburu' alichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Simba pia imefanikiwa kuweka wanachama wake wengi katika nyadhifa mbali mbali za vyama vya mikoa, akiwemo Athumani Kambi, ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Soka mkoa wa Mtwara.
Wakati Simba na Yanga zikipigana vikumbo kuweka wanachama wake katika vyama vya mikoa, wagombea wa nafasi ya urais wa TFF katika uchaguzi mkuu wa chama hicho, nao wamekuwa wakipigana vikumbo kuweka watu wao.
Baadhi ya wagombea wanaotajwa kupachika watu wao mikoani ni pamoja na Jamal Malinzi na Athumani Nyamlani, ambao wametajwa kuwa wanataka kumrithi rais wa sasa wa TFF, Leodegar Tenga.
Kwa sasa, Nyamlani ni makamu wa kwanza wa rais wa TFF wakati Malinzi aligombea wadhifa wa uraia katika uchaguzi uliopita na kubwagwa na Tenga.
Uchaguzi mkuu wa DRFA umepangwa kufanyika Desemba 12 mwaka huu.

STEWART AREJEA AZAM KWA ZALI



Gaudence Mwaikimba na Mcha Khamisi wakipongezana baada ya Azam kupata bao la tatu katika mechi kati yake na Coastal Union leo. Azam ilishinda mabao 4-1. (Picha kwa hisani ya Bin Zubeiry).

KOCHA John Stewart Hall leo amerejea Azam kwa zali baada ya kuiongoza timu hiyo kuibugiza Coastal Union mabao 4-1 katika mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Stewart amerejeshwa Azam baada ya kutimuliwa kwa Kocha Boris Bunjak, kufuatia mwenendo mbaya wa timu hiyo katika mechi za ligi kuu ya Tanzania Bara.
Ushindi huo uliiwezesha Azam kushika nafasi ya tatu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 21 baada ya kucheza mechi 21, nyuma ya Simba na Yanga, zinazoongoza kwa kuwa na pointi 23 kila moja, lakini zikitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Mechi hiyo ilitawaliwa zaidi na Azam, ambayo hadi mapumziko ilikuwa mbele kwa mabao 3-0, yaliyofungwa na Gaudence Mwaikimba, Kipre Tchetche na Mcha Khamisi.
Bao la nne la Azam lilitokana na makosa ya beki Othman Tamimu wa Coastal Union kujifunga wakati akijaribu kuondosha hatari kwenye lango lake.
Bao la kufutia machozi la Coastal Union lilifungwa na kiungo wa kimataifa wa Kenya, Jerry Santo.

TAARIFA KUTOKA TFF LEO




Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kuzingatia Katiba ya TFF Ibara ya 49(1), Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 8(2), 10(6), 12(1) na 26(2) na (3) katika kikao chake kilichofanyika Oktoba 30, 2012 ilijadili rufani dhidi ya Kamati za Uchaguzi za MZFA na GEREFA na michakato ya uchaguzi ya vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Mwanza, Rukwa, Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake (TWFA), Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA) na Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) na kutoa uamuzi kama ifuatavyo;


1. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA)

(a) Rufani ya Ndg. Jackson Manji Songora: Kamati ilijadili rufani iliyowasilishwa na Ndg. Jackson Manji Songora dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA, iliyoomba Kamati ya Uchaguzi ya TFF kubatilisha uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya MZFA kumpitisha Ndg. Jumbe O. Magati kugombea nafasi ya Mwenyekiti wa MZFA, kwamba Kamati ya Uchaguzi ya MZFA ilikosea:

(i)Kupokea Statement of Results ya Baraza la Mitihani Tanzania yenye jina la Fredrick J. Magati wakati jina la mgombea alilojaza kwenye fomu ya maombi ya uongozi ni Jumbe O. Magati.

(ii)Kumsaili Jumbe O. Magati kwa kuwa hakuwasilisha nakala halisi ya cheti cha elimu yake.

(iii)Kumpitisha Ndg. Jumbe O. Magati kugombea uongozi na kuwa Ndg. Jumbe O. Magati hana sifa zinazokidhi matakwa ya Katiba ya MZFA Ibara ya 29(2).

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilipitia maelezo ya Mrufani na ilijiridhisha kuwa rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Songora haikutanguliwa na pingamizi mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA, hivyo ilikosa sifa ya kuwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF. Hata hivyo, kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49(1); Katiba ya MZFA Ibara ya 47 na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF Ibara ya 26(2), Kamati ya Uchaguzi ya TFF, kwa kutumia mamlaka yake ya kikatiba na kanuni za uchaguzi, ilimuhoji Ndg. Magati kuhusu elimu yake na majina yaliyo kwenye Statement of Results na fomu yake ya maombi ya uongozi.

Baada ya kupitia vielelezo na maelezo yaliyowasilishwa mbele ya Kamati kuhusu majina ya Ndg. Jumbe O. Magati, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijiridhisha kuwa Jumbe O. Magati na Fredrick J. Magati ni mtu huyo huyo. Kamati ya Uchaguzi imetupa rufani ya Ndg. Patrick Manji Songora.

2. Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Geita (GEREFA)

(a) Rufani ya Ndg. Abdallah H. Hussein: Kamati ilijadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Abdallah H. Hussein ikipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, kwa kigezo cha kutokuwa Mkazi wa Mkoa wa Geita. Kamati ilipitia vielelezo vilivyowasilishwa mbele yake na Mrufani na ilijiridhisha kuwa vielelezo hivyo vinakidhi kuthibitisha kuwa mwombaji uongozi ni Mkazi wa Mkoa wa Geita. Kamati inakubaliana na maombi ya mrufani na inamrejesha Ndg. Abdallah H. Hussein kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.

(b) Rufani ya Ndg. Aziz Mwamcholi: Kamati ilijadili rufani iliyowasilishwa mbele yake na Ndg. Aziz Mwamcholi ikipinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa GEREFA, kwa kigezo cha kushindwa kuwasilisha cheti cha elimu ya sekondari. Kamati ilipitia maelezo ya Ndg. Mwamcholi na ya Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA na ikajiridhisha kuwa Ndg. Mwamcholi hakukidhi matakwa ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, hususan Ibara ya 10(5). Kamati imekubaliana na uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA wa kutompitisha Ndg. Mwamcholi kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa GEREFA. Kamati ya Uchaguzi ya TFF imetupa rufani hiyo.

(c) Rufani ya Ndg. Kaliro Samson: Ndg. Samson aliwasilisha rufani kupinga uamuzi wa Kamati ya Uchaguzi ya GEREFA kuliondoa jina lake kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kigezo cha kutowasilisha cheti cha kuhitimu elimu ya kidato cha nne. Kamati ilipitia maelezo na vielelezo vya rufani ya Ndg. Samson nay a Mrufaniwa na kujiridhisha kuwa nakala ya cheti cha elimu ya kidato cha sita inakidhi matakwa ya Katiba ya GEREFA Ibara ya 29(2). Kamati inakubaliana na maombi ya mrufani na inamrejesha Ndg. Kaliro Samson kugombea nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF.

3. Mchakato wa Uchaguzi Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mwanza (MZFA)

Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilijadili mchakato wa uchaguzi wa MZFA ikiwa ni pamoja na mchakato wa uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Ukerewe (UDFA), baada ya uchaguzi wa awali wa UDFA kuwa umefutwa na Kamati ya Uchaguzi ya MZFA kutokana na Kamati ya Uchaguzi ya UDFA kutozingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

Baada ya maelezo ya kina ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na vielelezo vilivyowasilishwa mbele ya Kamati kuhusu mwenendo wa uchaguzi wa UDFA, Kamati ya Uchaguzi ya TFF ilibaini kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa Kanuni na taratibu za uchaguzi uliofanywa na Kamati ya Utendaji ya UDFA kwa kutozingatia kikamilifu maagizo ya Kamati ya Uchaguzi ya MZFA na hivyo kusababisha mkanganyiko katika mchakato wa Uchaguzi ambao kwa wakati mmoja ulikuwa na Kamati mbili za Uchaguzi kusimamia uchaguzi huo. Mikanganyiko inayojionyesha dhahiri na kusababisha nafasi zote sita zinazogombewa katika mchakato unaoendelea kuwa na mgombea mmoja mmoja tu katika kila nafasi, imeufanya mchakato wa uchaguzi wa UDFA kupoteza hadhi ya uchaguzi unaozingatia Kanuni za Uchaguzi na misingi ya demokrasia na uwazi kama ilivyoainishwa katika Kanuni za Uchaguzi za TFF. Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa mamlaka yake ya kikatiba Ibara ya 49(1) ya Katiba ya TFF na Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya 10(6) na 26(2) na (3) imeamua:

(i)Kuzifuta Kamati zote za Uchaguzi za UDFA zilizoteuliwa na Kamati ya Utendaji ya UDFA kabla ya baada ya mchakato wa uchaguzi wa sasa wa UDFA.

(ii) Kuufuta Uchaguzi wa UDFA uliokuwa ufanyike Novemba 5, 2012. Mchakato wa uchaguzi utaanza upya kwa tarehe zitakazopangwa na Kamati ya Uchaguzi ya MZFA baada ya kupata maelekezo ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF.

(iii) Kuiagiza Kamati ya Uchaguzi ya MZFA katika kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Ibara ya 6 ya Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF kutoiruhusu UDFA kushiriki Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa MZFA kwa kuwa UDFA imeshindwa kuzingatia matakwa ya Katiba kuhusu ukomo wa mamlaka ya Kamati ya Utendaji na kufanya uchaguzi kwa wakati muafaka unaozingatia Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF.

4. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake (TWFA)

Kwa kuzingatia changamoto za kuijenga TWFA ambayo bado ni change, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imekubali ombi la TWFA la kusogeza mbele tarehe ya uchaguzi kwa wiki mbili. Uchaguzi wa TWFA ngazi ya Taifa sasa utafanyika Novemba 18, 2012.

5. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Waamuzi wa Mpira wa Miguu Tanzania (FRAT)

Uchaguzi wa viongozi wa FRAT utafanyika Novemba 17, 2012 kama ulivyopangwa.

6. Mchakato wa Uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Rukwa (RUREFA)
TFF imesimamisha kuanza kwa mchakato wa uchaguzi wa RUREFA kutokana na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya RUREFA kuendeleza malumbano kati yao kuhusu uhalali wa uteuzi wa Kamati mpya ya Uchaguzi ya RUREFA, uteuzi ambao ulifanywa na Kamati ya Utendaji ya RUREFA, Oktoba 18, 2012. Kwa kuwa hali hii imetokea tena baada ya Kamati ya Utendaji ya RUREFA kuwa imepewa fursa ya kikatiba kuteua Kamati ya Uchaguzi na ni mwendelezo wa mgawanyiko ndani ya Kamati ya Utendaji ya RUREFA unaoathiri mchakato wa uchaguzi wa chama hicho, Kamati ya Uchaguzi ya TFF inatafakari hatua muafaka za kikatiba na kikanuni zitakazoondoa ukwamishaji wa mchakato wa Uchaguzi wa RUREFA unaosababishwa na Kamati ya Utendaji ya RUREFA. Uamuzi kuhusu mustakabali wa Uchaguzi wa RUREFA utatolewa baada ya kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Novemba 6, 2012.
7. Mchakato wa Chama cha Wanasoka Tanzania (SPUTANZA) na Chama cha Makocha (TAFCA)
Uamuzi kuhusu mustakabali wa uchaguzi wa SPUTANZA na TAFCA utatolewa baada ya vyama hivyo kuwasilisha taarifa za kina kuhusu michakato ya chaguzi za wanachama wao katika ngazi ya mikoa, katika kikao cha Kamati ya Uchaguzi ya TFF kitakachofanyika Novemba 6, 2012.
Moses Kaluwa
Mjumbe- Kamati ya Uchaguzi TFF