KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Friday, May 14, 2010

TENGA: RAGE NI MPIGANAJI

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), limempongeza Mwenyekiti mpya wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage kwa kumuelezea kuwa ni mpiganaji halisi katika masuala yanayohusu michezo.

Rais wa TFF, Leodegar Tenga aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, Rage ni mmoja wa wadau, ambaye amepigana kwa hali na mali kulinda na kutetea katiba ya Simba, TFF na Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA).

“Kwa kweli nawapongeza wadau wa klabu ya Simba na hasa Rage, aliyechaguliwa kuwa mwenyekiti,”alisema Tenga.

Alisema kimsingi katiba zote zinapinga kitendo cha mgombea kupeleka suala la michezo kwenye mahakama za kawaida na kusisitiza kuwa, kufanya hivyo ni kosa kikatiba.

Tenga alisema inapotokea migogoro ya aina hiyo, muhusika anapaswa kufuata taratibu zilizowekwa kikatiba katika kutafuta haki yake badala ya kukimbilia mahakamani.

"Tayari soka yetu imekuwa ikikua kila kukicha na tulishaanza kusahau masuala ya watu kwenda mahakamani, lakini nashakuru kwa wadau ambao wameongozwa na Rage kuhakikisha wamesimamia matakwa ya katiba na uchaguzi umefanyika kama ilivyopangwa," alisema.

Rais huyo wa TFF alisema kitendo cha baadhi ya wanachama wa Simba kwenda mahakamani kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo, kungeiweka Simba kwenye hatari ya kufungiwa na FIFA.

Alisema kufanyika kwa uchaguzi wa Simba, siyo mafanikio pekee ya klabu hiyo bali soka ya Tanzania kwa ujumla.

"Maamuzi ya kufanyika kwa uchahuzi wa Simba yalitolewa usiku wa Ijumaa iliyopita, binafsi sikutarajia wanachama 1,500 wangejitokeza kwenda kupiga kura," alisema.

Ametoa wito kwa wanachama wa klabu zingine, kuiga mfano wa Simba na kuchagua viongozi wenye uwezo mkubwa wa kutafsiri na kutekeleza katiba zao kama alivyofanya Rage.

Katika uchaguzi huo uliofanyika Jumapili iliyopita, Rage alichaguliwa kuwa mwenyekiti baada ya kumshinda Hassan Othman Hassanoo. Uchaguzi huo ulifanyika kwenye ukumbi wa Bwalo la Maofisa wa Polisi Oysterbay, Dar es Salaam.

Papic: Ngasa APR si saizi yako

KOCHA Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amesema timu ya APR ya Rwanda haimfai Mrisho Ngasa kwa sababu kiwango chake hakina tofauti na timu za Tanzania.

Papic alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, Ngasa anapaswa kwenda kucheza soka ya kulipwa katika klabu zenye kiwango cha juu zaidi.

Kocha huyo alitoa kauli hiyo baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Ngasa amekwenda Rwanda kufanya majaribio ya kuichezea APR.

Kuna habari kuwa, APR ilitaka kumsajili Ngasa kwa kitita cha sh. milioni 20, lakini mchezaji huyo aligoma na kutaka alipwe sh. milioni 35.

Papic alisema kama Ngasa ana kiu ya kwenda nje kucheza soka ya kulipwa, ni vyema aende katika klabu kubwa kama za Afrika Kusini na za Ulaya.

"Pale Rwanda sifahamu vizuri soka yao, lakini kwa ushauri wangu, naona ni vyema mchezaji huyo angefanya mipango ya kwenda Afrika Kusini au Ulaya,"alisema kocha huyo, ambaye ni raia wa Serbia.

Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu ya Azam umesema kuwa, hauna mpango wa kumsajili mshambuliaji Mrisho Ngasa kutoka Yanga.

Mmoja wa viongozi wa Azam, Mohamed King alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, watasajili washambuliaji wapya kutoka klabu zingine na siyo Yanga.

King alisema hawajawahi kufanya mazungumzo na Ngasa kwa ajili ya kumsajili msimu ujao na kuongeza kuwa, taarifa hizo wamekuwa wakizisoma kupitia kwenye vyombo vya habari.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa Azam alikiri kuwa, wamefanya mazungumzo ya awali na beki Nadir Haroub ‘Canavaro’ wa Yanga kwa ajili ya kumsajili msimu ujao.

"Ninachoweza kukuhakikishia ni kwamba, ni kweli tumefanya mazungumzo na Canavaro, lakini kwa upande wa Ngasa, hilo jambo halipo,"alisema King.

Tayari uongozi wa Yanga umekaririwa ukisema kuwa, milango ipo wazi kwa Canavaro kujiunga na Azam, lakini anapaswa kufuata taratibu za usajili.

Rooney atoa changamoto kwa Ferguson



LONDON, England

MSHAMBULIAJI Wayne Rooney wa Manchester United amesema anaamini, klabu hiyo inahitaji wachezaji wawili zaidi wa kiwango cha juu katika ligi ya msimu ujao.

Rooney alisema mjini hapa juzi kuwa, mmoja wa wachezaji hao anapaswa kuwa mshambuliaji, ili kukiongezea nguvu kikosi hicho baada ya kupokonywa taji la ligi kuu ya England msimu huu na Chelsea.

Mshambuliaji huyo ameonyesha kiwango cha juu msimu huu, ambapo ameifungia Manchester United mabao 34.

Hata hivyo, Rooney alipatwa na mkosi mwishoni mwa ligi hiyo baada ya kuumia kifundo cha mguu na kukaa benchi kwenye mechi kadhaa.

Rooney ndiye aliyekuwa tegemeo kubwa la Manchester United katika ufungaji magoli msimu huu, kufuatia kuondoka kwa Cristiano Ronaldo na Carlos Tevez msimu uliopita.

Licha ya Manchester United kushika nafasi ya pili msimu huu, nyuma ya Chelsea kwa tofauti ya pointi moja, Rooney alisema bado kuna umuhimu wa Kocha Sir Alex Ferguson kuongeza nyota wawili msimu ujao.

“Kama tutaweza kuongeza wachezaji wawili wenye majina makubwa, itatupa nafasi kubwa ya kurejesha taji la ligi kuu,”alisema Rooney.

“Kama utatazama timu ya mwaka 1999 iliyoshinda mataji matatu, tulikuwa na washambuliaji wanne na wote walikuwa na uwezo wa kufunga mabao,”aliongeza.

“Kwa sasa nipo mimi, Berbatov na Owen. Yupo pia Macheda, lakini kama tunaweza kumpata mwingine zaidi, itatuongezea nguvu zaidi,”alisema.

Mbali na Rooney, wachezaji wengine wanaounda safu ya ushambuliaji ya Manchester United kwa sasa ni Dimitar Berbatov, Michael Owen na chipukizi Federico Macheda na Mame Biram Diouf.

Mourinho aikana Real Madrid



MILAN, Italia

KOCHA Mkuu wa Inter Milan ya Italia, Jose Mourinho amekanusha madai kuwa, amekuwa akifanya mazungumzo kwa ajili ya kuwa kocha mkuu wa Real Madrid ya Hispania msimu ujao.

Mourinho alisema mjini hapa juzi kuwa, kwa sasa hana mpango huo na kusisitiza kuwa, ameelekeza nguvu zake katika kukabiliana na changamoto zote zinazoikabili Inter Milan.

Inter Milan inachuana vikali na AS Roma katika kuwania taji la ligi ya Serie A ya Italia na inatarajiwa kuteremka dimbani keshokutwa kumenyana na Siena. Mechi hiyo ndiyo itakayoamua bingwa wa ligi hiyo.

Mbali na kibarua hicho, Inter Milan pia inakabiliwa na mtihani mwingine mgumu wa kupambana na Bayern Munich ya Ujerumani katika mechi ya fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya, itakayocheza Mei 22 mwaka huu.

“Sijafanya mazungumzo na klabu nyingine yoyote, na kama ilivyo kwa mashabiki wote wa Inter Milan, nafikiria mechi zetu mbili muhimu dhidi ya Siena na Bayern Munich,”alisema kocha huyo, ambaye amebatizwa jina la ‘Special One’.

“Hizi ni siku za ajabu, tumeelekeza akili na nguvu zetu katika mechi hizi mbili na hakuna yeyote ndani ya Inter Milan, anayefikiria kuhusu nini watakachokifanya baada ya mechi ya fainali ya ligi ya mabingwa. Huo ndio ukweli wenyewe,”aliongeza.

Mourinho alisema ameshamweleza wakala wake, Jorge Mendez kwamba hatajadili suala hilo hadi Mei 23 baada ya mechi ya fainali ya ligi ya mabingwa.

Hata hivyo, Mourinho alikiri kwamba bado ana mambo muhimu ya kufanya katika soka na kuongeza kuwa, moja ya mipango yake ya baadaye ni kufundisha kabumbu nchini Hispania ama kuwa kocha wa timu ya taifa ya Ureno.

“Lakini hayo nitaweza kuyafanya nitakapokuwa mtu mzima zaidi, inawezekana katika miaka 15 ama 20 ijayo,”alisema.

Alipoulizwa iwapo siku moja angependa kuwa kocha wa mshambuliaji Cristiano Ronaldo wa Real Madrid, kocha huyo alisema: “Vema, Nimesema nataka kuwa kocha wa Ureno katika kipindi cha miaka 15 au 20 ijayo.”

Mapema wiki hii, Rais wa Inter Milan, Massimo Moratti alitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikikanusha madai kuwa, anamsaka mrithi wa Mourinho.

Drogba amtamani Torres


Drogba

LONDON, England

MSHAMBULIAJI Didier Drogba wa Chelsea amesema anamkaribisha kwa mikono miwili Fernando Torres wa Liverpool iwapo atasajiliwa na klabu yake.

Kauli hiyo ya Drogba imekuja siku chache baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Chelsea imetenga pauni milioni 70 za Uingereza (sh. bilioni 140) kwa ajili ya kumsajili Torres.

Gazeti la Daily Mail la Uingereza liliripoti wiki iliyopita kuwa, mmiliki wa Chelsea, Roman Abramovich amepania kuvunja rekodi ya uhamisho wa wachezaji katika ligi kuu ya England kwa kusajili kifaa kipya kwa bei kali.

Kwa sasa, rekodi hiyo inashikiliwa na beki Rio Ferdinand, aliyesajiliwa na Manchester United kwa uhamisho wa pauni milioni 29.1 kutoka klabu ya Leeds miaka minane iliyopita.

Mtendaji Mkuu wa Chelsea, Ron Gourlay alithibitisha mapema wiki hii kuwa, Kocha Carlo Ancelotti atapatiwa fedha anazotaka ili kusajili mchezaji mmoja au wawili na kwamba lengo lao kubwa ni kumnasa Torres.

Akizungumza mjini hapa juzi usiku, Drogba alisema atakuwa na furaha kubwa iwapo Torres ataungana naye katika safu ya ushambuliaji ya Chelsea.

Alisema kujiunga kwa Torres kutaifanya safu ya ushambuliaji ya Chelsea iwe tishio kwa mabeki wa klabu za timu pinzani kokote duniani.

“Bila shaka nitamkaribisha Torres kwa mikono miwili,”alisema Drogba, ambaye ameibuka kuwa mfungaji bora wa ligi kuu ya England baada ya kupachika wavuni mabao 36 msimu huu.

“Kila wakati mchezaji mpya anakuja hapa, hilo linaifanya klabu iwe kubwa zaidi na kutuongezea nguvu,” alisema Drogba.

“Kama kuna nafasi ya yeye kuja hapa, anakaribishwa kwa sababu msaada wowote unahitajika,”aliongeza.

Mbali na Chelsea, klabu nyingine iliyoonyesha dhamira ya kumsajili Torres ni Manchester City, ambayo ipo tayari kutoa dau lolote ili kumnasa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Hispania.

Torres (26) ameonyesha nia ya kutaka kuihama Liverpool baada ya kushindwa kutwaa taji lolote tangu alipojiunga na klabu hiyo miaka mitatu iliyopita.

Sunday, May 9, 2010

RAGE BOSI MPYA SIMBA



ALIYEKUWA Makamu wa Pili wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ismail Rage amechaguliwa kuwa mwenyekiti mpya wa klabu ya Simba.

Rage alichaguliwa kushika wadhifa huo juzi baada ya kumbwaga Hassan Othman 'Hassanoo' katika uchaguzi uliofanyika kwenye ukumbi wa bwalo la maofisa wa Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Katika uchaguzi huo, Rage alipata kura 785 wakati Hassanoo alipata kura 435. Idadi ya kura zilizopigwa ni 1, 437 wakati kura 127 ziliharibika.

Nafasi ya makamu mwenyekiti ilichukuliwa na Godfrey Nyange 'Kaburu, ambaye hakuwa na mpinzani. Alipata kura 1,359 sawa na asilimia 80.5.

Waliochaguliwa kuunda safu ya wajumbe wa kamati ya utendaji, idadi ya kura zikiwa kwenye mabano ni Joseph Kinesi (991), Mkwabi Sued (823), Damian Manembe (725), Saidi Pamba (793), Francis Waya (695) na Ibrahim Masoud (638).

Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Rage alisema huu ni wakati mwafaka kwa wana-Simba kuendeleza amani na utulivu uliopo klabuni. Pia aliwataka wanachama kuungana na kuijenga upya Simba.

Rage alisema jukumu lililo mbele yake ni zito kwa sababu anapaswa kuhakikisha Simba inapata maendeleo makubwa zaidi kuanzia klabu hadi kwenye timu, lengo likiwa ni kuweka historia mpya.

Alisema kutokana na ukongwe wake, Simba inapaswa kuwa klabu ya kupigiwa mfano katika mashindano ya kimataifa na kurejesha rekodi yake iliyopotea muda mrefu.

Rage alisema kinachotakiwa kwa sasa ni viongozi na wanachama kushirikiana, kuheshimiana na kutambua mipaka ya kazi, jambo ambalo litaifanya klabu hiyo kuwa na taratibu nzuri za uongozi.

Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Hassan Dalali alisema anajivunia kwamba anaondoka Simba akiwa ameiacha klabu ikiwa na amani na utulivu. Alisema angependa kuona mambo hayo yanaendelezwa katika kipindi cha uongozi mpya.

Saturday, May 8, 2010

SIMBA YANG'ARA TUZO ZA VODACOM

Na Sophia Ashery

KLABU ya Simba imeng'ara katika tuzo za ligi kuu ya soka ya Vodacom msimu huu baada ya kocha wake, Patrick Phiri na wachezaji Juma Kaseja na Mussa Hassan 'Mgosi' kushinda tuzo mbalimbali.

Phiri, raia kutoka Zambia ameibuka kuwa kocha bora wa ligi hiyo baada ya kuiwezesha Simba kutwaa ubingwa kabla ya ligi kumalizika wakati Kaseja na Mgosi walitwaa tuzo za kipa na mfungaji bora.

Kufuatia kunyakua tuzo hizo, Phiri amezawadiwa kitita cha sh. milioni 2.8 wakati Kaseja na Mgosi wamezawadiwa sh. milion mbili kila mmoja.

Mbali ya zawadi hizo, Simba pia imezawadiwa sh. milioni 38 kwa kuibuka mabingwa wapya wa ligi hiyo wakati watani wao wa jadi Yanga wamezawadiwa sh. milioni 15 kwa kushika nafasi ya pili. Azam FC imezawadiwa sh. milioni 10 kwa kushika nafasi ya tatu.

Mshambuliaji Mrisho Ngassa wa Yanga amezawadiwa sh. milioni 2.5 kwa kuibuka kuwa mchezaji bora wa michuano hiyo wakati tuzo ya mwamuzi bora imenyakuliwa na Oden Mbaga kutoka Dar es Salaam, aliyezawadiwa sh. milioni 2.5. African Lyon imezawadiwa sh. milioni 5.5 kwa kuibuka kuwa timu yenye nidhamu.

Akikabidhi zawadi hizo kwa viongozi wa klabu hizo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera alisema Phiri anapaswa kuwa mfano wa kuigwa na makocha wengine kutokana na kuiongoza vyema Simba kutwaa ubingwa.

KESI YA WAMBURA YATINGA MAHAKAMA KUU

Na Furaha Omary

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imeitisha mafaili ya kesi mbili za kupinga uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba, zilizofunguliwa na wanachama Michael Wambura na Juma Mtemi.

Licha ya kuitishwa mafaili hayo kwa ajili ya kupitiwa upya, uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kisutu wa kusitisha kwa muda uchaguzi wa klabu hiyo, uliopangwa kufanyika Mei 9, unabaki palepale.

Msajili wa Mahakama hiyo, Kanda ya Dar es Salaam, Lameck Mlacha alisema jana kuwa, kuitishwa kwa mafaili hayo, kumefanyika kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa na wagombea wa nafasi ya mwenyekiti, Ismail Aden Rage na Hassan Othman 'Hassanoo'.

Alisema Mahakama Kuu iliamua kuitisha faili la kesi namba 100 ya mwaka 2010 iliyofuguliwa na Wambura dhidi ya Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali ili kupitiwa upya.

Mlacha alisema wamepata pia taarifa kwamba kuna kesi nyingine kama hiyo imefunguliwa mahakama ya Ilala na Mtemi dhidi ya kamati ya utendaji ya Simba, hivyo wameamua kuziunganisha.

Msajili alisema baada ya kuitishwa kwa mafaili hayo, Kaimu Jaji Mfawidhi wa kanda hiyo, Njengafibili Mwaikugile alielekeza wanaolalamika wapeleke malalamiko rasmi ya kisheria ili yasikilizwe na baada ya kuitwa pande zote mbili, ndipo Mahakama Kuu itoe maelekezo.

"Nilipompelekea Jaji Mfawidhi, ameipanga kwa Jaji Augustine Mwarija na kwa sababu muda wa saa kazi umekwisha, imeshindwa kusikilizwa, hivyo imepangwa Jumatatu,"alisema Mlacha.

Alisema jalada hilo litakapofika kwa Jaji Mwirija, ndipo atapanga muda wa wahusika kufika mahakamani na wa kusikilizwa.

Mapema wiki hii, Mahakama ya Kisuti ilisitisha kwa muda uchaguzi huo baada ya kukubali ombi lililowasilishwa na Wambura la kutaka kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo mpaka kesi yake ya msingi itakaposikilizwa.

Uamuzi huo ulitolewa na Hakimu Mkazi Rita Tarimo baada ya upande wa mlalamikiwa, Hassan Dalali kutokuwa na pingamizi kuhusu ombi hilo.

Wakati huo huo, Rage amesema wamewasilisha malalamiko hayo Mahakama Kuu kuomba kupitiwa mafaili hayo kwa madai kuwa, utaratibu haukufuatwa wa kufunguliwa kwa kesi hizo.

SERIKALI YAMSHANGAA WAMBURA

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imeeleza kushangazwa na kitendo cha aliyekuwa mgombea uongozi katika uchaguzi mkuu wa Simba, Michael Wambura kufungua kesi mahakamani kupinga uchaguzi huo.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Joel Bendera amesema kitendo hicho cha Wambura kimedhihirisha wazi kwamba si mwanamichezo kwa sababu masuala yanayohusu soka hayapaswi kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Bendera alisema inasikitisha kuona kuwa, wapo watu wanaofikisha masuala ya michezo mahakamani wakati zipo taratibu na vyombo maalumu vilivyowekwa kikatiba, vinavyopaswa kushughulikia mambo hayo.

Alisema katiba ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) zinaeleza wazi kuwa, migogoro inayohusu soka haipaswi kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Naibu Waziri alisema migogoro ya michezo inapaswa kushughulikiwa na vyombo husika vilivyowekwa kikatiba na kila mwanamichezo anapaswa kuheshimu katiba ya chama ama klabu aliyomo.

Kauli hiyo ya Bendera imekuja siku chache baada ya Wambura kufungua kesi mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam, akipinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Simba, uliopangwa kufanyika Jumapili ya Mei 9, 2010.

Kufuatia malalamiko hayo yaliyofunguliwa na Wambura, mahakama ya Kisutu imetoa amri ya kusimamisha uchaguzi huo hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa.

Mbali na Wambura, mwanachama Juma Mtemi wa Simba naye amefungua kesi ya kupinga uchaguzi huo kwenye mahakama ya Ilala, ambayo juzi ilishindwa kutoa uamuzi kuhusu maombi yake kutokana na kufunguliwa kwa kesi nyingine kama hiyo kwenye mahakama ya Kisutu.

Friday, May 7, 2010

BREAKING NEWS!!! Mahakama yasimamisha uchaguzi Simba

Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam imesimamisha kwa muda uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba uliopangwa kufanyika Jumapili ya Mei 9, 2010.

Uamuzi huo wa mahakama umekuja, kufuatia malalamiko yaliyowasilishwa na Michael Wambura, ambaye amefungua kesi ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi huo.

Katika madai yake, Wambura anataka haki itendeke baada ya kuenguliwa kuwania uongozi na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Katika kuomba haki, Wambura pia ameitaka mahakama imlinde asije kuchukuliwa hatua zozote za kufikishwa mahakamani hadi shauri lake kuu litakapoamuliwa.

Kwa mujibu wa katiba ya Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), ni marufuku kwa masuala yanayohusu soka kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria.

Hati ya kusimamisha uchaguzi huo, imetolewa na Hakimu Tarimo wa Kisutu. Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa Mei 31 mwaka huu.

SOKA LIBERIA IMEKUFA

MONROVIA, Liberia
CHAMA cha Soka cha Liberia (LFA), kimekiri kuwa mchezo wa soka nchini humo umekufa.
Rais wa LFA, Musa Hassan Bility aliieleza BBC wiki hii kuwa, jitihada zinahitajika ili kuunusuru mchezo huo.
Musa ameliomba Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA) na lile la Afrika (CAF), kuisaidia nchi hiyo katika jitihada zake za kuinua soka.
Rais huyo mpya wa LFA alitarajia kukutana na Rais wa FIFA, Sepp Blatter wiki hii kujadili tatizo hilo, ambalo limeifanya timu ya taifa ya nchi hiyo na za klabu kupoteza umaarufu.
“Soka imekufa Liberia na tunatafuta njia za kuifufua,”alisema Musa, aliyeukwaa wadhifa huo baada ya kushinda uchaguzi mkuu.
“Hapa ndipo nchi pekee ya Afrika iliyotoa mwanasoka bora wa dunia (George Weah), kunapaswa kuwepo na kitu fulani kizuri kuhusu nchi hii,”aliongeza.
“Bahati mbaya ni kwamba, Liberia ni moja ya nchi zenye kiwango cha chini kisoka miongoni mwa nchi za Afrika,”alisema.
Timu ya taifa ya Liberia, Lone Star inashika nafasi ya 152 kwa ubora wa viwango vya soka duniani, miongoni mwa nchi 202 zilizo wanachama wa FIFA. Mwaka 2001, nch hiyo ilikuwa ikishika nafasi ya 66.
“Tunaamini FIFA na CAF zinaweza kutusikiliza na kutusaidia kuinua tena kiwango cha soka,”alisema Musa.
Musa alisema wanahitaji msaada wa kifedha na kiufundi na kuongeza kuwa, ataomba wapatiwe programu ya miaka miwili kwa ajili ya kufufua mchezo huo.
Alisema kwa sasa, chama chake kinatafuta makocha wa kigeni kwa ajili ya kuinoa Lone Star, lakini pia watajaribu kuwaendeleza makocha wazalendo.
“Lengo letu kwanza ni kuiweka nyumba yetu kuwa katika hali nzuri na kuiwezesha nchi kufuzu kucheza fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika,”alisema.

Posho wa Maisha Plus aja na mduara


Na Badru Kimwaga
MSHINDI wa nne wa Shindano la Maisha Plus 2010, Leonard Erasmos Komba 'Ponyo', yupo mbioni kuachia kibao kipya cha muziki kiitwacho Pwani, kitakachokuwa katika miondoko ya mduara.
Ponyo, maarufu pia kama Man, aliyewahi kuliimbia kundi la Migo Massive, alisema baada ya ukimya wa muda mrefu katika fani ya muziki, ameamua kutoka na kibao hicho kwa nia ya kutambulisha ujio wa albamu yake na kuthibitisha kuwa bado wamo kwenye 'gemu' hiyo.
Msanii huyo anayeigiza pia filamu na kuchonga vinyago, alisema kibao hicho cha Pwani anachotarajiwa kukiingiza studio hivi karibuni atakiimba na msanii nyota wa kundi la Tip Top Connection, Tundaman.
Alisema kibao hicho ni kati ya vibao nane vitakavyokuwa katika albamu yake mpya na ya kwanza itakayokuwa na miondoko tofauti kuanzia reggae, mduara, R&B na Zouk.
"Baada ya ukimya mrefu kutokana na kujitumbukiza kwenye filamu, nimepanga kurejea tena na safari hii najiandaa kuachia Mduara utakaoenda kwa jina la Pwani utakaotambulisha albamu yangu ijayo," alisema Ponyo.
Ponyo, aliyetamba kwenye Maisha Plus na kibuyu chake cha ajabu, alisema albamu hiyo ijayo na ya kwanza kwake itakuwa na nyimbo nane, baadhi ikiwa ni Pwani, Mzuka, Tobi na Nini Unataka.
Aliongeza kwa sasa anahaha kusaka watu wa kumpiga tafu kuweza kufanikisha mipango ya kuachia albamu hiyo mapema kabla ya kufika mwezi Agosti.
"Tatizo linalonikwamisha kwa sasa ni mshiko wa kukamilisha kazi hii, hivyo kama kutakuwa na wenye uwezo wajitokeza kunisaidia," alisema Ponyo.
Akiwa na Migo Massive lililokuwa likiundwa na wasanii wengine kama Luga Chriss na Bob Lee, Ponyo na wenzake walitamba na vibao kama Sitaki Demu na Summer Party kilichowafanya washiriki tamasha la Fiesta la mwanzoni mwa 2000.

VUMBI AFYATUA NNE MPYA



Na Badru Kimwaga
MWANAMUZIKI mahiri, aliyewahi kuipigia bendi ya Marquiz Original, Alain Dekula 'Vumbi', amefyatua nyimbo mpya nne ikiwa ni maandalizi ya kupakua albamu yake ya tatu mpya.

Akizungumza na mtandao huu juzi jijini akiwa kwenye mapumziko, Vumbi alisema nyimbo hizo nne zimerekodiwa nchini Sweden anapofanyia shughuli zake za muziki na kwamba ni mbio zake za kutoa albamu yake ya tatu nje ya bendi yake ya Makonde.

Vumbi alisema nyingine nne zitakazokamilisha jumla ya nyimbo nane za albamu hiyo mpya, tayari zimeshatungwa mashairi yake, lakini hazijapewa jina hadi atakapoingia studio kuzirekodi.

"Baada ya kutamba na albamu za Sultan Qaboos na Rumaliza ambayo bado ipo kwenye chati na
nimeleta video yake ili Watanzania nao mpate uhondo, nimeanza maandalizi ya albamu ya tatu,
ambayo itakuwa na jumla ya nyimbo nane," alisema Vumbi.

Mkali huyo wa kucharaza gita la solo, alizitaja nyimbo zilizokamilika ni Mawele, Tenda Wema, Coco na Dar Night maarufu kama No Stop.

Vumbi aliyeondoka nchini mwaka 1991 baada ya kukaa na Marquiz kwa karibu miaka nane, alisema nyimbo hizo za awali anatarajia kuanza kuzisambaza kenye blog yake pamoja na kwenye vituo vya redio vya nchi mbalimbali kwa lengo la kuzitangaza.

Aliongeza kuwa kama albamu zake za awali, hata hiyo ya tatu atafyatua kwa kushirikiana na baadhi ya wanamuziki wa bendi yake ya Makonde, akiwemo Mganda Sammy Kasule, Bobo Sukari aliyewahi kutamba Marquiz kabla ya kuondoka nae kwenda Sweden.

Hata hivyo Vumbi alisema Bobo Sukari kwa sasa amejiondoa kwenye bendi yao yenye wasanii nane wakiwemo wanne wazungu kutokana na kile alichokataa kukieleza."

Kwa sasa Bobo hayupo nasi, ila siwezi kusema ni kwa ajili ya nini, lakini tunaendelea kuwasiliana na atashiriki pia katika albamu hii ya tatu," alisema Vumbi.

MERCY KUSUJUDU VIDEON

Na Badru Kimwaga
MSANII anayekuja juu katika muziki wa Injili nchini, Mercy Margareth Mbilu ameanza kurekodi video ya nyimbo za albamu yake ya kwanza iitwayo Ukinisujudia.
Kazi ya 'kushuti' video hiyo ilianza mapema wiki hii, ingawa imesimama kupisha hali ya mvua inayoendelea jijini Dar es Salaam na Mercy alisema itaendelea tena mvua zikitulia na huenda kabla ya kumalizika kwa mwezi huu wa Mei, video hiyo ikawa mitaani.
Mercy aliuambia mtandao huu kuwa, ameamua kufyatua video ya albamu hiyo ili kuweza kuiingiza sokoni sambamba na albamu kamili kutoa fursa kwa wapenzi na mashabiki wa muziki wa injili kuzipata zote kwa pamoja.
"Nimeanza kushuti, vieo ya albamu yangu ya Ukinisujudia kwa lengo la kutaka kuziingiza sokoni pamoja na audio, ili kila mpenzi apate kile roho inapenda na mipango huenda ikakamilika katikati ya mwezi Mei," alisema Mercy.
Alizitaja nyimbo zilizoanza kurekodiwa video kuwa ni Ukinisujudia, Utafuteni Upendo na Nitakusifu Mungu wa Rehema.
"Hizo ndizo nilizoanza nazo na mvua zikiacha kunyesha na hali ya hewa kuwa nzuri nitamalizia nyimbo tano zilizosalia ambazo ni Zakayo, Na Hili Bwana Nishindie, Nitakukimbilia, Bwana Yesu Atasimama na Unirehemu Ewe Yesu.
Mercy alisema amepanga video yake irekodiwa katika ubora na kiwango cha hali ya juu ili kuweza kuteka soko la muziki huo ambalo kwa sasa lina ushindani mkubwa.
Kampuni inayomfanyia kazi hiyo ya kurekodi video hiyo ni moja ya kampuni maarufu za kazi hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam ambayo imewarekodia wasanii mbalimbali nyota wa muziki huo wa Injili na ule wa kizazi kipya.

Thursday, May 6, 2010

ALIYEFUNGUA KESI YA KUPINGA UCHAGUZI SIMBA AKANA KUIFUTA

Na Wilson Kimaro
HATMA ya uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba bado imeendelea kuwa kitendawili baada ya mahakama ya Ilala kupokea barua kutoka kwa mwanachama Juma Mtemi akidai kuwa, ameamua kuifuta kesi aliyofungua ya kupinga uchaguzi huo.
Hilo lilibainishwa na Hakimu wa Mahakama hiyo, Janeth Kinyange wakati kesi hiyo ilipotajwa mahakamani hapo jana.
Hakimu Janeth alisema alipokea barua muda mfupi kabla ya kuingia mahakamani, ikiwa imeandikwa na Juma Mtemi ikitaka kesi hiyo ifutwe.
Alipoulizwa kupitia wakili wake, Jerome Msemwa, Mtemi alikana kuandika barua hiyo na kusema hata sahihi iliyokuwemo haikuwa yakwake bali ilighushiwa.
Wakili Jerome aliiomba nakala ya barua hiyo kwa lengo la kufungua kesi ya jinai ya kughushiwa kwa jina na saini ya mteja wake.
Kabla ya kuzuka kwa utata wa barua hiyo, Hakimu Janet aliamua kuiahirisha kesi hiyo hadi leo na kuutaka uongozi wa Simba ukubaliane juu ya nani wakili wao.
Hakimu Janeth alifikia uamuzi huo baada ya Wakili, Peter Swai kuwasilisha barua mahakamani hapo iliyotiwa saini na Makamu Mwenyekiti wa Simba, Omari Gumbo ikimtambua kuwa ndiye wakili wa utetezi.
Mbali na barua hiyo, mahakama pia ilipokea barua kutoka kwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali ikitoa taarifa kuwa Wakili Majura Magafu ndiye anayeiwakilisha klabu hiyo.
Kufuatia utata huo, Hakimu Janeth alisema mahakama ipo njia panda juu ya wakili gani anayepaswa kuiwakilisha klabu hiyo.
Aliutaka ungozi wa Simba kukutana na kujadili kwa kina kabla ya kuamua juu ya mwakilishi wao mahakamani na kusisitiza kwamba kazi ya mahakama ni kutoa uamuzi juu ya suala hilo.
Kesi hiyo ya madai ilifunguliwa na Mtemi mwanzoni mwa wiki hii akipinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Simba.
Mtemi alifungua kesi hiyo siku chache baada ya Michael Wambura kuenguliwa kugombea nafasi ya mwenyekiti na kueleza azma yake ya kufungua kesi mahakamani kupinga uamuzi huo.
Wambura alienguliwa kugombea wadhifa huo na Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kufuatia rufani iliyowasilishwa na mwanachama Daniel Kamna.

MANJI APASUA BOMU YANGA



Na Emmanuel Ndege
MFADHILI mkuu wa klabu ya Yanga, Yusuf Manji amekanusha madai kuwa, aliihujumu timu hiyo ilipocheza na Simba katika mechi ya mzunguko wa pili wa michuano ya soka ya ligi kuu ya Vodacom.
Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Manji alisema asingeweza kufanya kitu kama hicho kwa sababu ana mapenzi makubwa na Yanga na amekuwa akiifadhili kwa mamilioni ya fedha.
Katika mechi hiyo, iliyochezwa Aprili 14 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga ilipigwa mweleka wa mabao 4-3 na Simba.
Manji alisema wanachama wa Yanga waliotoa madai hayo kwenye vyombo vya habari, hawana shukurani kwa sababu haiingii akilini ni vipi anaweza kufanya hivyo kwa timu, ambayo amekuwa akitumia fedha zake nyingi kuisaidia.
“Mimi naipenda sana Yanga, siwezi na sintaweza kuihujumu kwa sababu yoyote ile,” alisema Manji.
Aliongeza kuwa, tangu alipojiunga na klabu hiyo, amefanikiwa kurejesha amani na mshikamano baada ya kumaliza tofauti zilizokuwa zimejitokeza kati ya makundi mawili yaliyokuwa yakipingana ya Yanga Asili na Yanga Kampuni na kuifanya Yanga iwe moja.
“Tazama, nimekarabati jengo la Yanga kwa fedha nyingi, nimetengeneza eneo la kuchezea soka, nimetumia fedha nyingi kusajili wachezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi, sasa iweje baadhi ya wanachama wanadai kuwa nimeichoka Yanga!”Alihoji.
“Wanaosema nimeihujumu Yanga, nawauliza nifanye hivyo ili iweje? Ili nipate nini? Nitumie mamilioni ya pesa zangu kuisaidia, halafu eti niihujumu!” Alisema mfadhili huyo huku akionyesha uso wa masikitiko.
Manji alisema chini yake, ameiwezesha Yanga kutwaa ubingwa wa ligi kuu mara mbili mfululizo pamoja na Kombe la Tusker, hivyo haoni kitu gani kinachoweza kumfanya ageuke na kuihujumu.
“Hizi ni kauli zisizo na msingi wowote. Wanachama wanaosema maneno hayo, hawana shukurani kabisa,”alisema.
Manji alisema milango ipo wazi kwa mtu yeyote anayetaka kuifadhili Yanga ajitokeze. Lakini alisisitiza kuwa, hatoweza kutokea mfadhili atakayeweza kufanya mambo aliyoyafanya ndani ya klabu hiyo.
Mfadhili huyo amewataka wanachama wa Yanga wawe makini na watulivu katika kipindi hiki, ambacho klabu hiyo inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Alionya kuwa, iwapo wanachama wataanza kutofautiana na kutoa kauli za uchochezi, upo uwezekano mkubwa wa kuibuka kwa mgogoro mwingine unaoweza kusababisha klabu irejee ilikotoka.
Akizungumzia usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa ligi, Manji alisema kazi hiyo amemkabidhi Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic kutoka Serbia.
“Masuala yote ya usajili yapo chini ya Papic kwa sababu yeye ndiye anayejua nani anahitajika na nani hahitajiki ndani ya Yanga. Mimi kazi yangu ni kutoa pesa tu,”alisema.
Alizionya klabu za ligi kuu kuepuka kugombea wachezaji wakati wa kipindi cha usajili, badala yake zifanye majadiliano iwapo klabu moja inataka mchezaji kutoka klabu nyingine.
“Kama kuna klabu yoyote itakayofanya umafia Yanga, itakiona cha moto. Nitajibu mapigo kwa nguvu zote,”alijigamba,

SIMBA VURUGU TUPU

MICHAEL Wambura


Wambura afungua kesi Kisutu

Aichongea TFF kwa FIFA

MGOMBEA uenyekiti aliyeenguliwa katika uchaguzi mkuu wa klabu ya Simba, Michael Wambura amefungua kesi kwenye mahakama ya Kisutu ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Simba.
Mbali na kesi hiyo, Wambura ameandika barua kwa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), akilifahamisha kuhusu mgogoro wa Simba uliopo mahakamani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Wambura alisema ameamua kufungua kesi ya kupinga kufanyika kwa uchaguzi wa Simba ili haki itendeke. Alifungua kesi hiyo jana.
Akifafanua kuhusu uamuzi wake huo, Wambura alisema haoni vipengele vyovyote ndani ya katiba ya Simba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) vinavyomzuia kugombea uongozi katika klabu hiyo.
Wambura alisema anataka apate ufafanuzi wa kina wa kisheria kuhusu kipengele cha ‘kukosa uaminifu’ kilichotumiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF katika kumuengua kugombea wadhifa huo.
Wambura ni miongoni mwa wagombea wawili walioenguliwa na kamati hiyo, kufuatia rufani zilizowasilishwa na wanachama Asha Kigundula na Daniel Kamna. Mgombea mwingine aliyeenguliwa ni Zacharia Hanspope.
“Lazima tuelewe kwamba binadamu anaishi kwa misingi ya sheria. Katika mpira wa miguu, tuliweka utaratibu, tukikataza masuala ya mpira kwenda mahakamani. Lakini huwezi kumzuia mtu kama hujamwambia haki yake ataipata wapi,”alisema.
“Unapotaka kumzuia mtu kwenda mahakamani, unamweleza kuna utaratibu fulani unaotakiwa kufuata, ikishindikana huko ndio uende mahakamani. Usipofanya hivyo, unakuwa umemfunga mtu mikono asipate haki yake,”aliongeza.
Wambura alisema kipengele kilichotumiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF kumuengua kugombea uongozi wa Simba ni batili na kinapaswa kutumiwa kwa vyama vilivyo chini ya shirikisho hilo, kama vile vya mikoa na si klabu.
Alisema katiba ya Simba ibara ya 55 inaeleza wazi kuwa, kutakuwepo na kamati maalumu ya kushughulikia migogoro ndani ya klabu hiyo, hivyo suala hilo halikupaswa kushughulikiwa na TFF.
Wambura alisema asingeweza kuwasilisha malalamiko yake kwa Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS) kwa sababu suala hilo linapaswa kushughulikiwa na vyombo vya chini kwanza kabla ya kufika huko.
“Katiba ya Simba inasema kwamba, wanachama wanaunganishwa kwa muundo wa chombo cha kushirikisha wanaofuata sheria za Tanzania, hivyo inatambua mamlaka za kisheria na haiwezekani kumzuia mtu kwenda mahakamani,” alisema.
“Mimi nasema kwenda mahakamani ni halali kwa mujibu wa sheria za nchi hii na huwezi kumzuia mtu kwenda kukata rufani katika vyombo ulivyovifungua wewe mwenyewe,” aliongeza.
Wambura alisema pia kuwa, ameamua kuiandikia FIFA kuieleza kuhusu kesi zilizopo mahakamani na nakala yake ameituma kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Alisema katika barua hiyo, ameeleza kwa kina sababu za yeye kuenguliwa kugombea uongozi ndani ya Simba na mchakato mzima ulivyokuwa na kuliomba shirikisho hilo liwasaidie wawaruhusiwe kugombea.
Uchaguzi wa Simba umepangwa kufanyika Jumapili, lakini kufuatia kufunguliwa kwa kesi hiyo na ile iliyofunguliwa na mwanachama Juma Mtemi kwenye mahakama ya Ilala, huenda ukasogezwa mbele.

BYE BYE BENITEZ, ZOLA MANCINI WAKALIA KUTI KAVU

RAFAEL Benitez
ROBERTO MANCINI

GIANFRANCO Zola

LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Liverpool, Rafael Benitez amedhihirisha wazi kuwa ataihama klabu hiyo mwishoni mwa msimu huu baada ya kuishutumu bodi ya wakurugenzi kwa kushindwa kutimiza ahadi walizompa.
Akizungumza mara baada ya timu hiyo kuchapwa mabao 2-0 na Chelsea mwishoni mwa wiki iliyopita, Benitez alisema ahadi nzuri alizopewa na viongozi wa Liverpool ndizo zilizomshawishi atie saini mkataba mpya mwaka jana.
Benitez alisema huenda mechi kati ya Liverpool na Chelsea itakuwa ya mwisho kwake, akiwa kocha mkuu wa timu hiyo yenye makao makuu yake Anfield.
Liverpool inatarajiwa kucheza mechi yake ya mwisho ya ligi kuu ya England Jumapili kwa kumenyana na Hull City, huku ikiwa imeshapoteza matumaini ya kushika nafasi ya nne. Kocha huyo amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na klabu ya Juventus ya Italia.
Benitez amedai kuwa, bodi ya wakurugenzi ya Liverpool imeshindwa kumhakikishia kwamba atapata fungu la kutosha kwa ajili ya kusajili wachezaji wapya, kama ilivyofanya msimu uliopita.
Kocha huyo alisema, anaelewa wazi kwamba, bodi hiyo inataka ajiuzulu ili kukwepa kumlipa fidia ya pauni milioni 16 za Uingereza kwa ajili ya fidia ya kuvunja mkataba wake.
Aliongeza kuwa, bodi hiyo pia inatumia ujanja wa kutaka ilipwe fidia iwapo itapata uthibitisho kwamba, Juventus imekiuka taratibu katika kufanya naye mazungumzo ya kumwajiri.
Hata hivyo, Benitez alisema ana hakika kwamba ataondoka klabu hiyo akiwa msafi, kutokana na kulazimishwa kufanyakazi kinyume na makubaliano kati yake na uongozi wa Liverpool.
“Niliamua kutia saini mkataba mpya kwa sababu kikosi kilikuwa kizuri na fedha za usajili zilikuwepo. Mwishoni, mambo yalibadilika. Tumekuwa na msimu mbovu na natumaini mambo yatakuwa tofauti siku zijazo, lakini kwa sasa naweza kuzungumzia hatma yangu kwa sababu sielewi nini kinachoendelea,”alisema.
“Niliamua kubaki kwa masharti fulani, ambayo yamebadilika. Niliiacha Valencia kwa sababu mazingira yalibadilika. Msimu huu haukuwa mzuri, hilo lipo wazi. Tunaelewa ni kwa nini na kipi kinapaswa kubadilika,”aliongeza.
Benitez alitia saini mkataba mpya wa kuinoa Liverpool mwaka jana. Mkataba huo wa miaka mitano una thamani ya pauni milioni 20.
Kocha huyo alisema, alikuwa na imani kwamba angepata pauni milioni 20 kwa ajili ya usajili wa wachezaji wapya kutokana na fedha za wachezaji aliowauza.
Benitez alipigania kuwa na uamuzi wa mwisho kuhusu masuala ya wachezaji na aliupata baada ya kuondoka kwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo, Rick Parry.
Lakini kuajiriwa kwa mkurugenzi mtendaji mpya, Christian Purslow mwaka jana, kulimuondolea maamuzi hayo baada ya kuishawishi bodi ya wakurugenzi iwe na sauti katika kupanga bajeti na kushiriki katika mazungumzo ya uhamisho.
Liverpool ilitumia fungu kubwa la fedha baada ya kuwaongezea mikataba mipya baadhi ya wachezaji wake nyota kama vile Steven Gerrard, Fernando Torres, Dirk Kuyt, Yossi Benayoun kocha Benitez mwenyewe.
Benitez alisema hakutarajia iwapo kuajiriwa kwa Purslow kungeweza kusababisha matatizo kiasi cha kusababisha uhusiano kati yake na mkurugenzi huyo kukaribia kuvunjika.
Hatma ya Benitez sasa ipo mikononi mwa bodi ya wakurugenzi, ambayo italazimika kuchukua uamuzi haraka baada ya pambano kati ya Liverpool na Hull City, ama isubiri kocha huyo ajiondoe mwenyewe.
Kocha Jose Mourinho wa Inter Milan ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kumrithi Benitez. Makocha wengine wanaopewa nafasi hiyo ni Martin O’Neill, Roy Hodgson na Jesus Jorge wa Benfica ya Ureno.
Juventus ilianza kumuwinda Benitez tangu Januari mwaka huu wakati kocha huyo aliposema, anaona fahari kuhitajiwa na klabu hiyo. Pia aliitaka Inter Milan nayo ifuate nyayo hizo, lakini ilimweka kando na kumuajiri Jose Mourinho.
Katika hatua nyingine, Kocha Roberto Mancini wa Manchester City ameahidi kusajili wachezaji nyota wa dunia, iwapo timu hiyo itapata nafasi ya kucheza ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu ujao.
Miongoni mwa wachezaji, ambao Mancini amepania kuwasajili kwa ajili ya kukiongezea nguvu kikosi chake ni pamoja na Fernando Torres wa Liverpool.
Manchester City ipo kwenye kibarua kigumu cha kuwania nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu ya England sanjari na Tottenham. Timu hizo zinashika nafasi ya nne na ya tano, zikiwa zinatofautiana kwa pointi moja.
Mancini anaamini kuwa, Manchester City inaweza kushika nafasi hiyo iwapo itaishinda Tottenham katika mechi iliyotarajiwa kuchezwa jana kabla ya kuishinda West Ham Jumapili.
Hata hivyo, Mancini alikiri kuwa, ataweza kumnasa Torres iwapo tu timu hiyo itafuzu kucheza ligi ya mabingwa wa Ulaya.
“Ni jambo la kawaida kwa wachezaji kufikiria jambo hilo. Wachezaji wengi wanataka kucheza ligi ya Ulaya. Ili kukiongezea nguvu kikosi, ni lazima tununue wachezaji wazuri na wachezaji watataka kuja hapa. Lakini hata kama hatutafuzu kucheza ligi ya Ulaya, lazima tununue wachezaji wazuri,”alisema.
Wakati huo huo, Kocha Slaven Bilic wa Croatia ni miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kumrithi Gianfranco Zola katika kibarua cha kuinoa West Ham msimu ujao.
Zola huenda akajiuzulu kuinoa timu hiyo baada ya kuwashutumu waziwazi wamiliki wa klabu hiyo, David Gold and David Sullivan.
Kocha huyo kutoka Italia amekerwa baada ya klabu hiyo kudaiwa kuwa, imetenga pauni milioni nne kwa ajili ya kumsajili kiungo Graham Dorrans kutoka Scotland, ambaye amedai kuwa, kamwe hakuwahi kuzungumza naye.
“Ninapaswa kuwa na sauti kwa wachezaji wanaosajiliwa ama kuuzwa. Mimi ndiye ninayewafundisha wachezaji na nahitaji kuelewa nani ninayemfundisha,”alisema.
“Si sahihi kufikiria kwamba sikutaka nihusishwe katika uhamisho wa wachezaji. Nataka kufahamu watu wanaokuja, nahitaji kuelewa nani ninayehusika naye,”alisema.
Zola (43), analipwa mshahara wa pauni milioni 1.9 kwa mwaka na mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2013.





DROGBA, ROONEY WACHUANA KUWANIA KIATU CHA DHAHABU

WAYNE Rooney

DIDIER Drogba


LONDON, England
WAKATI ligi kuu ya soka ya England ikiwa inafikia ukingoni Jumapili, washambuliaji Didier Drogba wa Chelsea na Wayne Rooney wa Manchester United wanachuana vikali kuwania tuzo ya kiatu cha dhahabu, inayotolewa kwa mfungaji bora.
Mbali na washambuliaji hao wawili, ambao timu zao zinapambana vikali kuwania ubingwa, pia wamo Darren Bent wa Sunderland na Carlos Tevez wa Manchester City.
Kabla ya mechi za jana, Drogba na Rooney walikuwa wamefungana kwa kufunga mabao 26 kila mmoja, huku timu zao zikiwa zimebakiwa na mechi moja kila moja kumaliza ligi hiyo.
Hatma juu ya mfungaji bora wa ligi hiyo atajulikana baada ya mechi za mwisho za timu hizo, ambapo mabingwa watetezi Manchester United watamenyana na Stoke City wakati Chelsea itavaana na Wigan.
Wachezaji wengine wenye nafasi ya kunyakua kiatu hicho cha dhahabu ni Bent mwenye mabao 24 na Tevez mwenye mabao 23. Wachezaji hao wawili wanaweza kutwaa tuzo hiyo, iwapo wataongeza mabao wakati Sunderland itakapomenyana na Wolves na Manchester City itakapovaana na West Ham.
Kiungo Frank Lampard wa Chelsea anashika nafasi ya tano kwa kufunga mabao 21 akifuatiwa na Jermaine Defoe wa Tottenham na Fernando Torres wa Liverpool waliofunga mabao 18 kila mmoja.
Cesc Fabregas wa Arsenal anashika nafasi ya nane kwa kufunga mabao 15, akifuatiwa na Emmanuel Adebayor wa Manchester City aliyefunga mabao 14. Louis Saha wa Everton na Gabriel Agbonlahor wa Aston Villa wamefunga mabao 13 kila mmoja.
Waliofunga mabao 12 kila mmoja ni Florent Malouda wa Chelsea na Dimitar Berbatov wa Manchester United wakati waliofunga mabao 10 kila mmoja ni Craig Bellamy wa Manchester City, John Carew wa Aston Villa, Carlton Cole wa West Ham, Cameron Jerome wa Birmingham na Hugo Rodallega wa Wigan.
Wachezaji waliofunga mabao tisa kila mmoja ni Steven Gerrard wa Liverpool, Nicolas Anelka wa Chelsea, Dirk Kuyt wa Liverpool, Andrei Arshavin wa Arsenal.
Waliofunga mabao nane kila mmoja ni Tim Cahill wa Everton, Bobby Zamora wa Fulham, Matthew Taylor wa Bolton, David Dunn wa Blackburn, Kevin Doyle wa Wolves, Steven Fletcher wa Burnley, Kenwayne Jones wa Sunderland na Aruna Dindane wa Portsmouth.
Wakati huo huo, Chelsea imedhihirisha kuwa na washambuliaji wenye uchu zaidi wa kufunga mabao msimu huu, baada ya kupachika wavuni mabao 95.
Mabingwa watetezi Manchester United wanashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao 80, wakifuatiwa na Arsenal, iliyofunga mabao 78 na Manchester City iliyofunga mabao 72.
Tottenham inashika nafasi ya tano kwa kufunga mabao 64, ikifuatiwa na Liverpool iliyotikisa nyavu mara 61, Everton iliyofunga mabao 59, Sunderland iliyofunga mabao 47 na West Ham iliyofunga mabao 46.
Burnley ndiyo timu yenye ukuta mbovu kuliko zote baada ya kuruhusu mabao 80, ikifuatiwa na Hull City iliyofungwa mabao 73 na Wigan iliyofungwa mabao 69.
Bolton inashika nafasi ya nne miongoni mwa timu zenye ukuta mbovu baada ya kuruhusu lango lake kufungwa mabao 66, ikifuatiwa na Portsmouth na West Ham zilizofungwa mabao 65 kila moja na Wolves iliyofungwa mabao 55.
Kipa Edwin van der Sar wa Manchester United ndiye aliyedhihirisha kuwa kipa bora zaidi msimu huu baada ya kuruhusu lango lake kufungwa mabao machache. Kipa huyo hadi sasa amefungwa mabao 28.
Petr Cech wa Chelsea anashika nafasi ya pili kwa kufungwa mabao 28, akifuatiwa na Pepe Reina wa Liverpool aliyefungwa mabao 35 na Brad Friedel wa Aston Villa aliyefungwa mabao 38.

NI VITA YA CHELSEA NA MAN UTD

SIR Alex Ferguson

CARLO Ancelotti

Ancelloti atamba hakuna wa kuwazuia kutwaa ubingwa
Ferguson mambo mazito, ategemea mbeleko ya Wigan
Newcastle, West Bromwich zafuzu kucheza ligi kuu
LONDON, England
UNAWEZA kuielezea ligi kuu ya soka ya England msimu huu kuwa ni yenye ushindani mkali na wa aina yake kuliko ligi zilizopita kutokana na ukweli kwamba bingwa atajulikana siku ya mechi za mwisho zitakazochezwa Jumapili.
Kitendawili juu ya timu ipi itakuwa bingwa kimekuwa kigumu kuteguliwa, kufuatia vinara wa ligi hiyo, Chelsea na Manchester United kushinda mechi zake za mwishoni mwa wiki iliyopita.
Katika mechi hizo, Chelsea iliichapa Liverpool mabao 2-0 wakati mabingwa watetezi, Manchester United waliilaza Sunderland bao 1-0.
Matokeo hayo yaliiwezesha Chelsea kuendelea kuongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi moja kati yake na Manchester United, inayoshika nafasi ya pili.
Chelsea inaongoza kwa kuwa na pointi 83 baada ya kucheza mechi 37, ikifuatiwa na Manchester United yenye pointi 82 kutokana na idadi hiyo ya michezo. Arsenal ni ya tatu kwa kuwa na pointi 72 baada ya kucheza mechi 36.
Je, ni timu ipi itakayovikwa taji la ligi hiyo msimu huu? Swali hilo ndilo lililotawala kwenye vichwa vya mashabiki wa soka nchini England.
Matokeo ya mechi za Jumapili ndiyo yatakayojibu swali hilo. Katika mechi hizo, Chelsea itamenyana na Wigan kwenye uwanja wa Stamford Bridge wakati Manchester United itavaana na Stoke City kwenye uwanja wa Old Trafford.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya soka wanaipa Chelsea nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na kuwa na idadi kubwa ya magoli ya kufunga. Hii ina maana kwamba, hata kama Chelsea itatoka sare na Wigan na Manchester United kuishinda Stoke City, inaweza kuwa bingwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Hadi sasa, Chelsea imefunga mabao 95 na kufungwa 32 wakati Manchester United imefunga mabao 82 na kufungwa 28.
Lakini iwapo Chelsea itafungwa na Wigan na Manchester United kuibwaga Stoke City, taji la ligi hiyo litarejea tena kwa Mashetani Wekundu, ambao wataweka rekodi ya kulitwaa kwa mara ya tatu mfululizo.
Chelsea itaingia uwanjani Jumapili huku ikiwa na kumbukumbu ya kichapo cha mabao 3-1 ilichokipata kutoka kwa Wigan katika mechi ya mzunguko wa kwanza.
Lakini wachambuzi wa soka wanaamini kuwa, kutokana na makali ya Chelsea hivi sasa, si rahisi kwa Wigan kuhimili vishindo vya vijana hao wa mfanyabiashara bilionea, Roman Abramovich.
Wachambuzi hao wamesema, pambano hilo lingekuwa gumu kutabirika iwapo Wigan ingekuwa kwenye janga la kushuka daraja. Kwa sasa, Wigan inashika nafasi ya 16 katika msimamo wa ligi hiyo.
Kocha Mkuu wa Chelsea, Carlo Ancelotti alijigamba baada ya kuibwaga Liverpool kwamba, hakuna kitakachowazuia kutwaa taji hilomsimu huu.
Ancelotti alisema japokuwa bingwa atajulikana baada ya mechi za mwisho, kimahesabu, hakuna wasiwasi kwamba Chelsea ndiyo itakayolinyakua taji hilo.
“Huenda bado tunayo kazi ya kufanya, lakini huu ulikuwa mchezo muhimu katika kuwania ubingwa,”alisema. “Ulikuwa mchezo muhimu, na tulionyesha kiwango cha hali ya juu na kupata matokeo mazuri. Nina furaha kubwa.”
“Siku zote nimekuwa nikisema, ubingwa utapatikana katika mechi za mwisho, na hilo ndilo lililotokea,”aliongeza kocha huyo.
Ancellotti hakuwa tayari kueleza mustakabali wake katika klabu hiyo kwa madai kuwa, hana haraka ya kufanya hivyo. Alisema anatarajia kukutana na mwenyekiti wa klabu hiyo hivi karibuni kujadili juu ya suala hilo.
Alikiri kuwa, ligi ya msimu huu haikuwa bora kwa Chelsea kufuatia kufungwa mechi 11 na pia kujitokeza kwa matatizo mbalimbali. “Inaonekana, kocha amekuwa akibebeshwa lawama zote kwa kila kilichotokea miaka miwili iliyopita,”alisema.
Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson hakuwa tayari kuzungumzia kiundani ushindani wa taji hilo. Lakini alikiri kuwa, Chelsea inayo nafasi kubwa zaidi ya kuwa bingwa.
Hata hivyo, Ferguson alisema bado wanayo matumaini ya kutwaa tena taji hilo na kuongeza kuwa, watategemea zaidi kubebwa na Wigan.
Wakati Chelsea na Manchester United zikipigana vikumbo kuwania ubingwa, ushindani wa nafasi ya nne upo kwa timu za Tottenham na Manchester City, ambazo zinatofautiana kwa pointi moja.
Kabla ya mechi za jana, Tottenham ilikuwa ikishika nafasi ya tatu kwa kuwa na pointi 67 baada ya kucheza mechi 36 wakati Man City ni ya nne kwa kuwa na pointi 66 baada ya kucheza idadi hiyo ya mechi.
Hatma juu ya timu ipi itakayoshika nafasi ya nne, ilitarajiwa kujulikana jana usiku baada ya mechi kati ya timu hizo, iliyotarajiwa kuchezwa kwenye uwanja wa Light.
Iwapo Tottenham itashinda mechi hiyo, itajiweka kwenye nafasi nzuri zaidi ya kushika nafasi hiyo na kusubiri mechi yake ya mwisho dhidi ya Burnley, ambapo itahitaji sare ya aina yoyote.
Wakati huo huo, Hull City wiki hii iliungana na Portsmouth na Burnley kushuka daraja la kwanza baada ya kulazimishwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Wigan.
Matokeo hayo yaliifanya Hull City iwe na pointi 29 baada ya kucheza mechi 37 na hivyo kutokuwa na uwezo wa kufikisha pointi 34 ilizonazo West Ham, hata kama itashinda mechi yake ya mwisho dhidi ya Liverpool.
Portsmouth ilikuwa ya kwanza kupata tiketi ya kushuka daraja kutokana na kuwa na idadi ndogo ya pointi kuliko timu zingine zinazoshiriki ligi hiyo. Timu hiyo inayofundishwa na Kocha Avram Grant, inazo pointi 19 baada ya kucheza mechi 37 ikifuatiwa na Burnley yenye pointi 27.
Katika hatua nyingine, timu za Newcastle na West Bromwich zimefuzu kucheza ligi kuu ya England msimu ujao, baada ya kushika nafasi ya kwanza na ya pili katika ligi daraja la kwanza msimu huu.
Nafasi ya tatu ya kupanda daraja bado inawaniwa na timu za Nottingham Forest, Cardiff, Leicester City na Blackpool, ambazo zitalazimika kucheza mechi za mtoano ili kupata bingwa.
MECHI ZA MWISHO ZA
LIGI KUU JUMAPILI
Arsenal v Fulham
Aston Villa v Blackburn
Bolton v Birmingham
Burnley v Tottenham
Chelsea v Wigan
Everton v Portsmouth
Hull v Liverpool
Man Utd v Stoke
West Ham v Man City
Wolverhampton v Sunderland