KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Monday, March 20, 2017

MAVUGO AIPELEKA SIMBA NUSU FAINALI KOMBE LA SHIRIKISHO


MSHAMBULIAJI Laudit Mavugo jana aliivusha Simba katika hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho, baada ya kuifungia bao la pekee ilipoichapa Madini FC bao 1-0.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha, Madini ilionyesha kiwango safi cha soka na kuwapa wakati mgumu wachezaji wa Simba.

Mavugo, mchezaji wa kimataifa wa Burundi, alifunga bao hilo la pekee dakika ya 55 kwa kichwa, baada ya kupigwa krosi kutoka pembeni ya uwanja.

Simba sasa inaungana na Mbao FC ya Mwanza, iliyowatoa wenyeji, Kagera Sugar kwa mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa juzi kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Mechi nyingine mbili mbili za robo fainali kati ya Azam FC na Ndanda FC na Yanga SC na Prisons zitapangiwa tarehe nyingine.

AZAM YATUPWA NJE KOMBE LA SHIRIKISHO


WAWAKILISHI wengine wa Tanzania katika michuano ya Afrika, Azam jana walitupwa nje katika michuano ya Kombe la Shirikisho, baada ya kuchapwa mabao 3-0 na Mbabane Swallows.

Kipigo hicho kimeifanya Azam itolewe nje ya michuano hiyo kwa jumla ya mabao 3-1, kufuatia kushinda mechi ya awali mjini Dar es Salaam kwa bao 1-0.

Kabla ya pambano hilo, kulikuwepo na vitendo visivyo vya kiungwana, ambavyo polisi na mashabiki wa Swaziland waliwafanyia viongozi na wachezaji wa Azam.

Pengine kitendo kibaya zaidi kilikuwa wakati wachezaji wa Azam waliposhindwa kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo kwa madai kuwa wenyeji walivipulizia dawa kali ya sumu.

Sunday, March 19, 2017

YANGA YATUPWA NJE LIGI YA MABINGWA WA AFRIKA


MABINGWA wa Tanzania Bara, Yanga jana walitupwa nje ya michuano ya ligi ya mabingwa Afrika, baada ya kulazimishwa kutoka suluhu na Zanaco ya Zambia.

Katika mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya pili iliyochezwa kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Lusaka, Yanga ilikuwa ikihitaji ushindi au sare ya mabao zaidi ya mawili ili iweze kusonga mbele.

Kwa matokeo hayo, Yanga imetolewa kwa faida ya bao la ugenini, ambalo Zanaco ililipata wiki iliyopita, timu hizo zilipotoka sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kutokana na kutolewa katika michuano hiyo, Yanga sasa imeangukia kwenye kapu la michuano ya Kombe la Shirikisho, ambapo sasa itavaana na timu nyingine iliyotolewa katika michuano hiyo ili kupata timu 16 zitakazofuzu kucheza hatua ya 16 bora.

Wawakilishi wengine wa Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho, Azam watashuka dimbani leo kurudiana na Moroka Swallows ya Swaziland mjini Mbabane.

Katika mechi ya awali, Azam ilishinda bao 1-0 hivyo inahitaji sare ya aina yoyote ili iweze kusonga mbele.

Friday, March 17, 2017

PLUJM SASA AJIUNGA NA SINGIDA UNITED


ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa Yanga na baadaye Mkurugenzi wa Ufundi, Mholanzi Hans Van der Pluijm amejiunga na klabu ya Singida United, itakayocheza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu ujao.

Aliyefanikisha dili la Pluijm kujiunga na timu hiyo ya Singida ni Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya timu hiyo na Mbunge wa Singida, Mwigulu Nchemba ambaye, pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi.Na Pluijm anaamua kwenda Singida United baada ya kusitishiwa mkataba wa Ukurugenzi wa Ufundi wa Yanga wiki iliyopita.

Yanga ilimhamishia Pluijm kwenye Ukurugenzi wa Ufundi Novemba mwaka jana, baada ya kumleta Mzambia, George Lwandamina awe kocha Mkuu.

Pluijm amefundisha Yanga kwa awamu mbili tangu mwaka 2014 alipoanza kwa kufanya kazi kwa nusu msimu, akimpokea Mholanzi mwenzake, Ernie Brandts kabla ya kwenda Uarabuni.

Alikwenda Al Shoalah FC ya Saudi ya Arabia na nafasi yake ikachukuliwa na Mbrazil, Marcio Maximo ambaye naye alifanya kazi kwa nusu msimu kabla ya Pluijm kurejeshwa Januari mwaka jana.

Saudi Arabia ambako alikwenda na aliyekuwa Msaidizi wake, Yanga SC, Charles Boniface Mkwasa – Pluijm  aliondoka baada ya kutofautiana na uongozi wa timu uliotaka kumsajilia wachezaji asiowataka.

Kabla ya kuhamishiwa kwenye Ukurugenzi wa Ufundi, Pluijm aliiongoza Yanga katika jumla ya mechi 128, akishinda 80, sare 25 na kufungwa 23.

Katika mechi 19 za nusu msimu mwaka 2014, alishinda 11, sare sita na kufungwa mbili, wakati katika mechi 110 za tangu mwaka jana, alishinda 69, sare 19 na kufungwa 21.

Msimu uliopita ulikuwa mzuri zaidi kwake, akibeba mataji yote matatu, Ngao ya Jamii, Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), maarufu kama Kombe la Azam Sports Federation (ASFC).

Pluijm pia aliiwezesha Yanga kufika hatua ya makundi ya michuano ya Afrika (Kombe la Shirikisho) kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1998 na mara ya pili kihistoria. Yanga ilifika hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho mwaka huu baada ya mwaka 1998 kufika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Na kwa mafanikio hayo, haikuwa ajabu Pluijm akishinda tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwishoni mwa msimu uliopita.

Mapema wiki hii, Singida United ilimsajili kiungo Tafadzwa Kutinyu kutoka Chicken Inn Fc ya Zimbabwe kwa mkataba wa miaka miwili.

Singida United imerejea Ligi Kuu msimu huu baada ya msoto wa zaidi ya miaka 15 tangu ishuke Daraja.

Thursday, March 16, 2017

BREAKING NEWWWWSSSSS, AHMAD WA MADAGASCAR ACHAGULIWA KUWA RAIS MPYA CAF


SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF), limemchagua Ahmad Ahmad kutoka Madagascar, kuwa rais wake mpya, baada ya kumbwaga Rais wa zamani, Issa Hayatou.

Katika uchaguzi huo uliofanyika leo mjini Addis Ababa, Ethiopia, Ahmad aliibuka mshindi kwa kupata kura 34 dhidi ya 20 alizopata Hayatou.

Hayatou anaondoka madarakani baada ya kuliongoza shirikisho hilo kwa miaka 27. Aliingia madarakani mwaka 1988 na ndiye Rais wa  CAF aliyetawala muda mrefu zaidi, akifuatiwa na Yidnekatchew Tessema wa Ethopia, aliyetawala kwa miaka 15.

BREAKING NEWSSSSSS. ZANZIBAR YAPATA UANACHAMA CAF


HATIMAYE Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), limekubali kuipatia Zanzibar, uanachama wa shirikisho hilo.

Uamuzi huo umefikiwa leo, wakati wa mkutano mkuu wa CAF, uliofanyika mjini Addis Ababa, Ethiopia.

Zanzibar sasa inakuwa mwanachama wa 55 wa CAF na itaanza kushiriki katika michuano ya Mataifa ya Afrika na ile ya vijana wa umri mbalimbali.

Aidha, Zanzibar sasa itaanza kupata mgawo wa CAF kwa nchi wanachama wa shirikisho hilo kwa ajili ya shughuli mbalimbali, ikiwemo kuendeleza soka.

Kabla ya kupitishwa kwa uamuzi huo, Zanzibar ilikuwa ikiruhusiwa kushiriki katika mashindano ya klabu bingwa Afrika na Kombe la Shirikisho.


UPELELEZI KESI YA WEMA SEPETU HAUJAKAMILIKA
UPANDE wa Jamhuri  katika kesi ya kukutwa bangi na misokoto, inayomkabili msanii Wema Sepetu na wenzake, umeieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo uko hatua za mwisho kukamilika.

Kutokana na hilo, Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ameutaka upande huo kujitahidi kukamilisha upelelezi huo mapema.

Wakili wa Serikali, Constatine Kakula, alidai jana mbele ya Hakimu Simba, kuwa upelelezi haujakamilika, hivyo aliomba kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Baada ya kueleza hilo, Hakimu Simba aliutaka upande huo kujitahidi kukamilisha upelelezi mapema.

Wakili Kakula aliieleza mahakama kuwa, upelelezi huo uko hatua za mwisho kukamilika.

Kabla ya kuingia katika chumba cha mahakama, Wema aliyekuwa amevalia gauni refu, alielekezwa na askari kutafuta ushungi wa kufunika kifua chake, ambacho sehemu kubwa kilikuwa wazi.

Kutokana na hilo, mmoja wa wanawake waliokuwa wameongozana na Wema, alilazimika kutoa mtandio wake mweusi na kumpatia msanii huyo ambaye alijifunika sehemu iliyokuwa inaonekana.

Mbali na Wema, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Angelina Msigwa  na Matrida Abas.

Washitakiwa hao wanakabiliwa na shitaka la kukutwa na msokoto mmoja wa bangi na vipande viwili vidogo vya bangi, vyenye uzito wa gramu 1.08.

Washitakiwa hao wanadaiwa walikutwa na bangi na msokoto huo, Februari 4, mwaka huu, nyumbani kwao Kunduchi Ununio, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Wema na wenzake wako nje kwa dhamana.

Tuesday, March 14, 2017

KABUNDA MCHEZAJI BORA LIGI KUU YA VODACOMKIUNGO mshambuliaji wa Mwadui FC, Hassan Salum Kabunda ndiye Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwa mwezi Februari, mwaka huu.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Alfred Lucas Mapunda amesema leo katika Mkutano na Waandishi wa Habari mjini Dar es Salaam kwamba, Kabunda amewapiku washambuliaji wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo na mzalendo Ibrahim Hajibu baada ya mechi mechi tatu za Februari kushinda tuzo hiyo.
“Kabunda amecheza dakika 270 katika mechi tatu ambazo Mwadui wameshinda mbili na kupoteza mechi moja, hivyo kujikusanyia pointi 6 na kupanda kutoka nafasi ya nane hadi ya sita,”amesema Mapunda.
Aidha, Ofisa huyo wa TFF amesema mtoto huyo wa beki wa zamani wa Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, Salum Kabunda enzi zake akiitwa Ninja au Msudan, katika mechi hizo tatu alifunga mabao manne kati ya sita ambayo Mwadui ilifunga.
Na kwa ushindi huo, Kabunda atazawadia Sh. Milioni 1 na wadhamini wa Ligi Kuu, kampuni ya Vodacom.

SERENGETI BOYS YAANZA MAZOEZI


TIMU ya taifa ya mpira wa miguu ya vijana wenye umri wa miaka 17 maarufu kwa jina la Serengeti Boys imeanza mazoezi rasmi Machi 12, 2017 kwenye Uwanja wa Karume, Ilala jijini Dar es Salaam.
Serengeti Boys itakuwa kambini Dar es Salaam hadi Machi 26, mwaka huu ambako itakwenda Bukoba mkoani Kagera kwa ajili ya mechi za kirafiki za kimataifa kujiandaa na michuano Afrika ambayo sasa itaanza Mei 14, 2017 badala ya Mei 21, mwaka huu.
Michezo ya kirafiki ya kimataifa itakuwa ni dhidi ya timu za vijana za Rwanda (Machi 28, 2017), Burundi (Machi 30, mwaka huu) na Uganda Aprili 2, mwaka huu). Michezo yote itafanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera.
Timu hiyo itarejea tena Dar es Salaam Aprili 3, mwaka huu ambako siku inayofuata itaagwa kwa kupewa bendera na mmoja wa viongozi wa nchi kabla ya kusafiri Aprili 5, mwaka huu kwenda Morocco kwa ajili ya kambi.

MAYANGA ATANGAZA KIKOSI CHA WACHEZAJI 26 WA TAIFA STARSKOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Salum Mayanga ameita wachezaji 26 kwa ajili ya maandalizi maandalizi ya michezo ya kufuzu michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Katika kikosi hicho, Mayanga hajawajumuisha mabeki wa Yanga, Juma Abdul, Kevin Yondan, Mwinyi Hajji na wa Azam, Aggrey Morris na David Mwantika.

Kuhusu Mngwali na wachezaji wengine wa Zanzibar, Mayanga amesema hajawaita kwa sababu anasubiri maamuzi ya kikao cha Shirikisho la Soka Afrika (CAF) Machi 16 kuhusu kuipa uanachama nchi hiyo.

"Kama Zanziabr itapewa uanachama CAF, ina maana hatutaendelea kuchanganyika na Zanzibar, lakini kama ikikwama, basi nitawarudisha wachezaji wa Zanzibar, nimeacha nafasi nne kwa ajili hiyo," amesema.

Mayanga aliyetaja kikosi hicho juzi katika Mkutano na Waandishi wa Habari ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ilala, Dar es Salaam - amewachukua washambuliaji chipukizi, Mbaraka Yussuf wa Kagera Sugar na Abdulrahman Juma wa Ruvu Shooting.

Kwa ujumla kikosi alichoteua Mayanga kinaundwa na makipa; Aishi Manula (Azam), Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).

Mabeki; Shomary Kapombe (Azam), Hassan Kessy (Yanga), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba), Gardiel Michael (Azam), Andrew Vincent (Yanga), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba) na Erasto Nyoni (Azam FC).

Viungo ni Himid Mao (Azam), Jonas Mkude (Simba), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam), Said Ndemla (Simba), Frank Domayo (Azam), Muzamil Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga), Shiza Kichuya (Simba), Farid Mussa (DC Tennerife) na Hassan Kabunda (Mwadui FC).

Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna, Sweden), Ibrahim Hajib (Simba), Mbarak Yussuf (Kagera Sugar) na Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting).

RAIS MAGUFULI APIGA SIMU CLOUDS, AZUNGUMZA NA DIAMOND, AAHIDI KUKUTANA NA WASANII


RAIS Dk. John Magufuli ameahidi kukutana na wasanii wa fani mbalimbali nchini kwa lengo la kuzungumza nao kuhusu maendeleo yao na changamoto zinazowakabili.

Alitoa ahadi hiyo leo, baada ya kupiga simu na kuzungumza na msanii Naseeb Abdul 'Diamond', kupitia kipindi cha Clouds 360, kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds.

Rais Magufuli aliamua kupiga simu baada ya kumsikia Diamond akimuomba asaidie sanaa ya muziki kama anavyosaidia katika mambo mengine.

”Mimi namuomba Rais Magufuli, kama anavyosaidia mengine kwa wepesi, kwenye sanaa uweke mkono wako Baba tunakutegemea,” alisema Diamond.

Baada ya Diamond kuyaomba hayo, Rais Maguli alipiga simu moja kwa moja kwenye kipindi hicho na kusema: “Nimemsikia Diamond na maombi yake nimeyapokea kwa mikono miwili. Nimefurahi kumskia siku ya leo, natafuta siku ambayo tutakaa pamoja. Nasikilizaga nyimbo zako hata wale wanaoigiza nawapenda sana na SHILAWADU,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza: “Hongera sana Diamond hongera sana kuwa na watoto, wakati wa kampeni ulikuwa na mtoto mmoja sasa una wawili.“

NUKUU ZA DIAMOND KATIKA MAHOJIANO HAYO:

Watu wanashangaa mimi kutangaza vivutio vya Afrika Kusini, sio kwamba nimekosa uzalendo, wameniona kupitia sanaa.

Tumeanzisha mtandao wetu wa kuuza na kusambaza nyimbo za wasanii online, tumeongea na mashabiki watuunge mkono

Nilishawahi kwenda TANAPA kuomba niwe balozi wa utalii nitangaze nchi yangu, lakini walitaka nijitolee bure tu

Msanii akihusishwa kwenye sakata la dawa za kulevya ni kuharibu brand, serikali itumie busara kuzilinda na kesi

Makonda ni mlezi wa WCB, kila mwanadamu ana mapungufu yake, tuangalie pia mazuri, ameonesha uthubutu kwenye kazi.

Tangu mwezi wa saba mpaka sasa sijapokea mauzo yangu, nimeyasusa, kinachofuata itakuwa ni hatua za kimahakama.

Mimi ni kielelezo ndani na nje ya nchi, watu wengi wameifahamu Tanzania kupitia sanaa yetu, lazima tujijenge.

Kipindi tunamuaga Rais Kikwete, nilipata nafasi ya kuzungumza na Rais Magufuli, nilimuomba tupate ukumbi wa kisasa

Watu walizungumza vibaya mimi kupewa benderĂ , ilisaidia sana kulitangaza taifa letu, nilimuomba Nape samahani

Tulilipa kodi ya TRA shilingi milioni 35, ni uthubutu, tunaweza kulipa kodi nyingi, serikali inabidi itulinde kwenye sanaa.

Nilikutana na Alikiba, Nairobi, tukazungumza, maneno yanasemwa na watu wa katikati, baadhi ya media zinachochea tu

Hili suala la Serengeti Boys ni jukumu letu kulibeba kama Taifa, tuunganishe nguvu ushindi wetu ushindi wao.

Naomba serikali iwasaidie vijana wa vibanda vya chipsi pamoja na bodaboda ishu ya muda wa saa sita wapewe ulinzi

Wakati huo huo, mwimbaji wa BongoFleva, Vanessa Mdee, ameachiwa na polisi kwa dhamana, baada ya kusota rumande kwa siku tano.

Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Simon Sirro, amethibitisha kwamba Vanessa, ameachiwa kwa dhamana.

“Ndio, tumempa dhamana wakati tunaendelea na uchunguzi, amepewa ataripoti kesho,” alisema.

Thursday, March 9, 2017

MAANDALIZI MECHI ZA YANGA NA ZANACO; AZAM NA MBABANE YAKAMILIKA


Maandalizi yote kwa michezo miwili ya kimataifa, yamekamilika.

Michezo hiyo ni kati ya Young Africans ya Tanzania na Zanaco ya Zambia utakaochezwa Jumapili kuwania taji la Ligi ya Mabingwa Afrika pia Azam FC ya Tanzania na Mbabane Swalows ya Swaziland kuwania Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Kwa upande wa Young Africans dhidi ya Zanaco, mchezo huo utafanyika Jumamosi Machi 11, mwaka huu. Waamuzi kutoka Djibouti ndio watakaochezesha mechi hiyo.

Waamuzi hao ni Djamal Aden Abdi ambaye atapuliza kipenga wakati wasaidizi wake ni Hassan Yacin na Farhan Salime ilihali mwamuzi wa akiba atakuwa Souleiman Djamal. Kamisha katika mchezo huo Na. 61 atakuwa Luleseged Asfaw kutoka Ethiopia.

Kiingilio katika mchezo huo kwa mujibu wa Mratibu wa Mechi za Kimataifa wa Young Africans, Mike Mike ni Sh 20,000 kwa VIP ‘A’, Sh 10,000 kwa VIP ‘B’ na ‘C’ na Mzunguko (Viti vya Rangi ya chungwa, kijani na bluu) ni Sh 3,000.

Azam wao watacheza Jumapili Machi 12, mwaka huu na Mbabane Swallows ya Swaziland kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi, Dar es Salaam. 

Waamuzi watakochezesha mchezo huo wanatoka Benin ambao ni Mwamuzi wa kati, Addissa Abdul Ligali na wasaidizi ni Medegnonwa Romains Agbodjogbe na Babadjide Bienvenu Dina huku Mwamuzi wa akiba akiwa Moumouni Kiagou na kamisha wa mchezo atakuwa Mohamed Omar Yusud wa Kenya.

Kiingilio katika mchezo huo kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba ni Sh 10,000 kwa VIP, Jukwa Kuu itakuwa ni Sh 5,000 na Mzunguko itakuwa ni Sh 3,000.

Wakati huohuo, tiketi za waamuzi wa Tanzania walioteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), kuchezesha mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya timu za AS Porto Louis 2000 ya Mauritius na El Hilal ya Sudan wikiendi ijayo, wamepata tiketi zao za kusafiri.

Katika mchezo huo ambao utafanyika ama Machi 17, 18 au 19 Mwamuzi wa kati atakuwa Israel Mujuni Nkongo wakati wasaidizi wake watakuwa ni Samuel Hudson Mpenzu na Josephat Deu Bulali huku Mwamuzi wa akiba akiwa ni Hery Sasii. Kamisha katika mchezo huo Na. 78 atakuwa Jerome Kelvyn Damon kutoka Afrika Kusini.

SIMBA, MADINI KUKIPIGA MACHI 19


Mechi mbili za kwanza hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Azam (Azam Sports Federation Cup 2016/2017), zitachezwa Machi 18 na 19, mwaka huu kwenye viwanja viwili tofauti.

Mechi hizo ni kati ya Kagera Sugar itakayocheza na Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba mkoani Kagera wakati siku inayofuata Machi 19 Simba itacheza na Madini kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Awali Simba ilikuwa icheze Machi 18, mwaka huu, lakini siku hiyo uwanja huo utakuwa na shughuli za kijamii hivyo sasa utachezwa siku ya Jumapili Machi 19, mwaka huu.

Mechi nyingine zitapangiwa tarehe za baadaye. Mechi hizo ni kati ya Azam FC na Ndanda FC kadhalika Tanzania Prisons ya Mbeya itakayocheza na mshindi kati ya Young Africans ya Dar es Salaam na Kiluvya United ya Pwani.

Bingwa wa michuano hiyo kwa mujibu wa kanuni, atazawadiwa Tsh. 50 milioni.

Pia bingwa wa michuano hiyo, ndiye atakayeiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ya Total wakati Bingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara ndiye ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Total Ligi ya Mabingwa Afrika.

MWAMUZI AONDOLEWA LIGI KUU YA VODACOM


Kamati ya Bodi ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi za Tanzania (Kamati ya Saa 72), imemwondoa Mwamuzi wa kati, Ahmada Simba katika orodha wa waamuzi watakaochezesha mechi za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu wa 2016/2017.

Hatua hii imefikiwa baada ya utetezi wa Mwamuzi Simba kudai kwamba hakuona tukio la Mchezaji wa Young African, Obrey Chirwa ambaye alifunga bao ambalo hata hivyo, mwamuzi alilikataa na kumwonya mchezaji kwa kadi njano.

Tukio hilo lilitokea katika mchezo ambao Young Africans walikuwa wageni wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Taifa, Machi mosi, mwaka huu.

Katika hiyo ya njano ilikuwa ni ya kwanza kwa Chirwa ambayo hata hivyo kamati ya Saa 72 imeifuta kadi hiyo kwa mujibu wa kanuni ya 9 (8) baada ya Kamati ya Saa 72 haikupaswa kutolewa kwa Chirwa kwa sababu hakukuwa na kosa wala mazingira ya kuonywa.

Kadi hiyo ilikuwa ni msingi wa kadi nyekundu baada ya Chirwa kufanya faulo ambayo aliadhibiwa tena kwa kadi ya njano hivyo kutolewa nje kwa mujibu wa taratibu.

Kufutwa kwa kadi ya njano ya kwanza, kunapelekea kufutwa kwa kadi nyekundu ambayo msingi wa kadi hiyo ulisababisha kadi nyekundu hivyo mchezaji angempaswa kukosa mchezo mmoja. Hata hivyo, kadi ya pili ya njano inahesabiwa.

Kadhalika uamuzi mwingine ulikuwa ni kuipiga faini Young Africans iliyocheza na Simba Februari 25, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya Wanajwani hao kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi.

Kitendo hicho ni kwenda kinyume cha kanuni ya 14 (14) ya Ligi Kuu inayoelekeza kuwa timu zitaingia uwanjani kwa kutumia milango rasmi. Hivyo kwa kuzingatia Kanuni ya 14 (48) ya Ligi Kuu, Kamati imeipiga Young Africans fainali ya Sh 500,000 (lakini tano).

KUZIONA YANGA, ZANACO BUKU TATUKIINGILIO cha chini katika mchezo wa kwanza hatua ya 32 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kati ya wenyeji, Yanga SC na Zanaco ya Zambia Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa Sh. 3,000.
Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa ametaja viingilio vya mchezo huo juzi wakati akizungumza na wanahabari kwamba, VIP A itakuwa Sh. 20,000 na VIP B na C kote mashabiki watakaa kwa Sh. 15,000.
Mchezo huo utanyeshwa moja kwa na Televisheni ya Azam, jambo ambalo ni faraja kwa mashabiki wa timu hiyo ambao hawataweza kwenda uwanjani, hususan wa nje ya Dar es Salaam.

Yanga ilifuzu hatua ya 32 bora ya michuano hiyo, baada ya kuitoa Ngaya Club de Mde ya Comoro kwa jumla ya mabao matano kwa mawili, ikishinda matano kwa moja mjini Moroni na kulazimishwa sare ya bao moja kwa moja Dar es Salaam, wakati Zanaco iliitoa APR ya Rwanda kwa bao moja bila, ililoshinda Kigali kufuatia sare ya bila bila mjini Lusaka.

Monday, March 6, 2017

YANGA YABANWA MBAVU NA MTIBWA, MSUVA AKOSA PENALTI


MABINGWA watetezi Yanga jana walibanwa mbavu na Mtibwa Sugar baada ya kulazimishwa kutoka nayo suluhu katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Iwapo Yanga ingeshinda pambano hilo, ingeweza kuiengua Simba kileleni mwa ligi kwa kuongoza kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa kwani zote zingekuwa na pointi 55 baada ya kucheza mechi 24.

Lakini kutokana na sare hiyo, Yanga imeendelea kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 53 huku Simba ikiendelea kuongoza kwa kuwa na pointi 55.

Yanga itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani ilipata penalti dakika ya 35, lakini shuti la Simon Msuva lilitoka nje ya lango.

Sunday, March 5, 2017

SIMBA YAVUTWA MKIA


KASI ya Simba katika kuwania taji la ligi kuu ya Tanzania Bara, jana ilipunguzwa baada ya kulazimishwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Mbeya City kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Licha ya kulazimishwa sare, Simba inaendelea kuongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 55 baada ya kucheza mechi 24, ikifuatiwa na Yanga yenye pointi 52 baada ya kucheza mechi 23.

Hata hivyo, Simba inaweza kuenguliwa kileleni iwapo Yanga itaifunga Mtibwa Sugar leo kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro. Iwapo itashinda, itakuwa mbele ya Simba kwa tofauti ya mabao ya kufunga.

Mbeya City ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 37 lililofungwa na Ditram Nchimbi, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Raphael Daudi. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.

Ibrahim Ajib aliisawazishia Simba dakika ya 65 kwa mpira wa adhabu ndogo, baada ya beki Bryson Raphael kuunawa mpira nje kidogo ya eneo la hatari.

Mbeya City ilipata bao la pili dakika ya 79 kupitia kwa nahodha wake, Kenny Ally kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba kwa njia ya penalti dakika ya 86.

YANGA YAFUFUA MATUMAINI YA UBINGWA


YANGA jana ilirejesha matumaini ya kutwaa tena taji la ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Ushindi huo uliiwezesha Yanga ifikishe pointi 52 baada ya kucheza mechi 23, ikiwa nyuma ya vinara Simba wenye pointi 54 kutokana na idadi hiyo ya michezo.

Yanga ilijikuta ikimaliza mchezo huo ikiwa pungufu baada ya mchezaji Obrey Chirwa kutolewa nje kwa kadi nyekundu, ambayo ilizua utata kutokana na mazingira ya kutolewa kwake.

Awali, Chirwa alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 44 baada ya kuifungia Yanga bao safi ambalo lingekuwa la pili kwa kichwa akimalizia krosi ya beki wa kulia, Hassan Kessy, lakini refa Ahmada Simba wa Kagera akalikataa na kumuonyesha kadi ya njano.

Na Mzambia huyo akaonyeshwa kadi ya pili njano dakika ya 45 baada ya kuudunda mpira chini na kutolewa kwa kadi nyekundu.

Iliwachukua Yanga dakika 47 kuhesabu bao la kwanza kupitia kwa Amissi Tambwe kabla ya Emmanuel Martin kuongeza la pili dakika za nyongeza.

Wednesday, March 1, 2017

NAPE: NITAHAKIKISHA TIMU ZA DODOMA ZINACHEZA LIGI KUUWaziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Nape Moses Nnauye amewahakikishia wapenzi wa mpira mjini Dodoma, kuwa timu za mpira mkoani humo zitashiriki Ligi Kuu ili kuwapa raha ya ligi hiyo mashabiki wa mpira na michezo kwa ujumla.

Amezungumza hayo mara baada ya kukutana na kufanya mazoezi na vijana kutoka Jogging Club mbalimbali mjini Dodoma, ikiwa ni ishara rasmi ya wizara yake kuhamia katika makao makuu ya nchi.

Nape amesema kuwa haitawezekana serikali ikahamia Dodoma na kusiwe na timu inayoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hivyo yeye kama waziri anayehusika na michezo kwa kushirikiana na wadau wa michezo atahakikisha timu zinafanya vizuri na kushiriki Ligi hiyo.

“Haiwezekani Rais akawa hapa na Makamu wa Rais na mawaziri tukakosa ladha na furaha ya Ligi kuu hapa Dodoma. Nitahakikisha timu za hapa zinashiriki Ligi kuu,” alisisitiza Nnauye.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu kazi Vijana na Ajira, Anthony Mavunde amewapongeza vijana wa Jogging Club na wakazi wa Dodoma kwa kushiriki michezo na kuhimiza kujituma zaidi
kwa timu za michezo hasa mpira wa miguu ili kushiriki Ligi kuu Tanzania Bara.

Katibu Mkuu Wizara wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel amewaomba wakazi wa Dodoma kufanya michezo kuwa ni Utamaduni wao wa kila siku ili kujenga Taifa la wapenda michezo kwa nia ya kuimarisha afya na kuendeleza michezo nchini.

Aidha, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Omary Singo amewahakikishia wakazi na wapenzi wa michezo, ushirikiano katika kuendeleza na kukuza michezo hasa katika makao makuu ya nchi Dodoma.