KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, November 26, 2014

SAAD KAWEMBA MTENDAJI MKUU MPYA AZAM


KLABU bingwa ya Tanzania Bara, Azam FC imemuajiri Mkurugenzi wa zamani wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Saad Kawemba kuwa Mtendaji wake Mkuu.


Mwenyekiti wa Azam FC, Sheikh Said Muhammad amemtambulisha rasmi leo Kawemba mbele ya wachezaji na viongozi, makao makuu ya klabu Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, baada ya mazoezi ya asubuhi.

“Nafurahi kupata nafasi hii, ni fursa nyingine tena ya kupata uzoefu mwingine katika uongozi wa soka baada ya kufanya kazi kwa mafanikio TFF,”amesema Kawemba.

Bodi ya Ukurugenzi ya Azam FC imefikia hatua ya kuajiri Mtendaji Mkuu, ili kurahisisha uendeshaji ndani ya klabu kwa lengo la kutafuta ufanisi zaidi.

Kawemba amesema anatarajia kupata ushirikiano mzuri kutoka kwa Bodi, Menejimenti na wafanyakazi wote wa klabu hiyo bingwa Tanzania Bara. “Nimekuja hapa kusaidia kusukuma mbele gurudumu la maendeleo la Azam FC, natarajia ushirikiano wa wote,”amesema.

Tuesday, November 25, 2014

PONDAMALI AMCHANACHANA KASEJA
KOCHA wa makipa wa Yanga, Juma Pondamali 'Mensah' amemtaka kipa nguli nchini, Juma Kaseja, kuacha kutafuta mchawi baada ya kukosa namba katika kikosi hicho.

Kauli ya Pondamali imekuja siku chache baada ya Kaseja kukaririwa na vyombo vya habari akidai kocha huyo ni chanzo cha kukosa namba Yanga.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Pondamali, alisema kuwa kipa huyo amekosa namba mbele ya Deogratius Munishi 'Dida' baada ya kiwango chake kuporomoka.

Alisema nahodha huyo wa zamani wa Simba alikosa namba baada ya kuzembea katika mazoezi, hivyo hana sababu ya kutafuta mchawi.

Pondamali, alisema mchezaji huyo anatakiwa kuondoka kwa amani Yanga kurejea katika klabu yake ya zamani Simba.

Simba imeanza mazungumza ya kumsajili Kaseja katika usajili wa dirisha dogo lililofunguliwa Novemba 20 hadi Desemba 20, mwaka huu.

Kipa huyo wa zamani aliyekuwa na mbwembwe uwanjani, alidokeza kuwa Kaseja, alianza kupoteza namba Yanga ilipokuwa chini ya kocha Hans van der Pluijm.

"Nashangaa sana kwanini nahusishwa na sakata hili wakati anayepanga timu ni kocha (Marcio) Maximo, yeye ndiye msimamizi mkuu wa mazoezi," alisema Pondamali.

Alisema muda mfupi baada ya Maximo kujiunga na Yanga kuchukua nafasi ya Pluijm, alitaka kufahamu sababu za kipa huyo kutokuwemo katika kikosi cha Taifa Stars.

Kocha huyo alisema msingi wa swali la Maximo, lilikuwa ni kutaka kujua kwanini Kaseja hachezi timu ya taifa kwa kuwa hadi anaondoka nchini kurejea Brazil alikuwa kipa namba moja.

Maximo, aliwasili nchini mwaka 2006 kuinoa Taifa Stars hadi 2010 ambapo mkataba wake ulimalizika kabla ya kurejea kuifundisha Yanga mapema mwaka huu.

Katika kipindi hicho Kaseja, aliwahi kuingia matatani na Maximo, baada ya Maximo kudai alishangilia mabao manne aliyofungwa hasimu wake, Ivo Mapunda kwenye moja ya mechi za kimataifa.

Maximo, alimuengua Kaseja katika kikosi cha kwanza na kumpa nafasi Ivo katika mechi za kimataifa za Taifa Stars.

Hivi karibuni mchezaji huyo ameibua mzozo na Yanga akidai alipwe sh. milioni 20 zilizobaki katika usajili ambazo Yanga ilitakiwa kumlipa Januari, mwaka huu.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Yanga, Benno Njovu, amedai mchezaji huyo haidai Yanga fedha za usajili.

KIEMBA: NIMEKUJA AZAM KUTAFUTA MAISHA
MSHAMBULIAJI wa zamani wa klabu ya Simba, Amri Kiemba, amesema  kwenda kwake Azam ni kwa ajili ya kutafuta maisha yake kwani maisha popote sio sehemu moja.


Kiemba ameyasema hayo baada ya kusaini mkataba wa kuitumikia Azam na kudai kuwa ataitumikia kwa moyo mmoja timu hiyo.

Akizungumza na mwandishi wetu kiemba alisema, japokuwa ameichezea simba kwa muda mrefu lakini amepiti changamoto nyingi kama kuambiwa kiwango kimeshikaa mara mzee.

"Changamoto zipo lakini nimeyavumuila mengi ila kwa sasa nashukuru kwamba nimeenda sehemu salama na nitahakikisha kuwa nitaonyesha ujuzi wangu wote na kuitumikia vyema timu yangu mpya,"alisema

Alisema kuwa kila mtu yupo kwa ajili ya kutafuta maisha kwa hiyo ikitokea nafasi kama hiyo hainahaja kuicha ukizingatia kwamba azam pia ni timu bora na inawachezaji bora.

Kiemba alisema kuwa timu kubwa zinakuwa na changamoto nyingi mno hivyo uvumilivu na ujasiri ndio ulio mfikisha hapo alipo.

Aliwataka mashabiki wake wasiwe na wasiwasi na yeye kwani ataendelea na kasi yae ileile pia atakuzidisha ili kuhakikisha kila mechi anapangwa katika kikosi cha kwanza.

"Nitajitahidi kufanya mazoezi kwa bidii ili kuwahakikisha kuwa napata nafasi ya kwanza katika kikosi cha mwalimu,"alisema

KIIZA ATEMWA YANGA, NAFASI YAKE KUCHUKULIWA NA MZAMBIA


HATIMAYE Marcio Maximo, amekata mzizi wa fitina baada ya kumtema mshambuliaji wa kimataifa, Hamisi Kiiza katika kikosi hicho.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uganda ametemwa na nafasi yake inatarajiwa kujazwa na Mzambia Jonas Sakuwaha.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza dirisha dogo la usajili kuwa Novemba 20 hadi Desemba 20, mwaka huu.

Maximo, alitarajia kuwasili jana usiku kutoka Brazil alikokwenda kwa mapumziko baada ya michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kusimama kwa muda.

Habari za ndani kutoka Yanga zilidokeza kuwa kocha huyo amemuondoa, Kiiza, katika usajili wake kwa ajili ya kujiwinda na ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu.

Chanzo hicho cha uhakika kilisema, Sakuwaha, anatarajia kuwasili nchini wiki hii kufanya majaribio kabla ya kupewa mkataba endapo atamridhisha Maximo.

"Kocha ametoa maagizo kwa uongozi kumuengua (Hamisi) Kiiza na nafasi yake kujazwa na Mzambia wa TP Mazembe," alidokeza kigogo huyo.

Alisema ripoti ya Maximo ilitoa mapendekezo ya mchezaji huyo kutemwa kabla ya kuondoka nchini kwa mapumziko ya muda mfupi.

Sekuwaha, anatajwa kuwa mmoja wa washambuliaji hodari wa TP Mazembe, lakini Maximo, anataka kuona kipaji chake kwenye mazoezi kabla ya kumsajili.

Straika huyo anakuwa mchezaji wa pili wa kimataifa wa Yanga kuwania usajili katika dirisha dogo akiungana na Emerson De Oliveira Neves Rouqe kutoka Brazil.

Hivi karibuni Yanga ilisema Maximo anatarajia kuwasili nchini na siri nzito kuhusu mikakati yake ya usajili.

Sunday, November 23, 2014

JAJA AITOSA YANGA, YAMNASA MBRAZIL MWINGINE, KIUNGO MKABAJI EMERSONKiungo mkabaji raia wa Brazil Emerson De Oliveira Neves Rouqe anatarajiwa kuwasili siku ya jumanne mchana jijini Dar es salaam kwa ajili ya majaribio katika klabu ya Young Africans na endapo atafuzu moja kwa moja atajiunga na mabingwa mara 24 wa Ligi Kuu Tanzania bara.

Emerson mwenye umri wa miaka 24 ambaye kwa sasa anachezea timu ya Bonsucesso FC iliyopo ligi daraja la pili nchini kwao Brazil, msimu uliopita alikuwa akicheza soka la kulipwa nchini Poland katika timu ya Piotrkow Trybunalski FC iliyopo Ligi Daraja la pili nchini humo.

Ujio wa Emerson kuja kufanya majaribio nchini unakuja kufuatia mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Brazil pia Geilson Santos "Jaja" kushindwa kurejea nchini baada ya kwenda kwao Brazil na kutoa taarifa kwamba hataweza kurejea tena nchini kutokana kukabiliwa na matatizo ya kifamilia.

Awali ilikua familia ya Jaja ije nchini katika kipindi cha mapumziko, lakini waliomba yeye Jaja ndio aende Brazil na mara baada ya kufika huko matatizo ya kifamilia aliyokutana nayo yamepelekea kushindwa kurejea nchini kuitumikia klabu yake na kuomba abakie kwao kwa ajili ya kutatua matatizo hayo.

Kuondoka kwa Jaja kunafanya klabu ya Young Africans kubakia na wachezaji wanne tu wa kimataifa ambao ni Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima, Hamis Kizza na Andrey Coutinho hivyo endapo Emerson atafuzu atakua anakamilisha idadi ya wachezaji watano wa kimataifa

Endapo Emerson atafuzu majaribo pamoja na vipimo atajiunga na kikosi cha kocha mbrazil Marcio Maximo katika nafasi ya kiungo mkabaji ikiwa ni sehemu ya kuboresha timu kuelekea kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom pamoja na mashindano ya kimataifa.

Aidha kikosi cha Young African baada ya kuwa mapumzikoni kwa takribani wiki mbili, kinatarajiwa kuanza mazoezi siku ya jumatatu katika Uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo wa Nani Mtani Jembe pamoja na mzunguko wa nane wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara.

Thursday, November 20, 2014

BURIANI SWAHIBA WANGU INNOCENT MUNYUKU
HAIKUWA rahisi kuamini, lakini ukweli ni kwamba mwandishi maarufu wa habari za michezo nchini, Innocent Munyuku, amefariki dunia.

Munyuku alifariki dunia jana alfajiri nyumbani kwake Kimara Kibo Dar es Salaam. Alifariki akiwa usingizini.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia yake, mwili wa marehemu Munyuku unatarajiwa kusafirishwa kesho kwenda Mazimbu mkoani Morogoro kwa ajili ya mazishi. Mazimbu ndiko anakoishi mama yake mzazi, ambaye ni mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.

Taarifa za kifo cha Munyuku zilipokelewa kwa mshtuko mkubwa. Wafanyakazi wenzake wa Kampuni ya New Habari, inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Rai, Dimba na Bingwa, hawakuamini masikio yao baada ya kupata taarifa hizo.

Wapo waliozungumza na kuchati naye kwa simu hadi saa nne usiku juzi. Pia aliposti ujumbe wa aina mbalimbali kwenye mtandao wa facebook, ukiwemo ujumbe unaohusu masuala ya dini ya kikristo. Katika ujumbe wake wa mwisho, aliandika 'Usiku mwema'.

Mmoja wa wafanyakazi wenzake, Jimmy Chika, ambaye ni Mhariri wa gazeti la Dimba, anasema alitumiwa ujumbe na Munyuku, akimueleza kwamba amepata fedha alizoomba ofisini hivyo mambo yake yalikuwa safi.

Karibu kila mmoja aliyezungumza ama kuchati na Munyuku juzi, alisimulia kile walichozungumza naye. Zilikuwa simulizi za kuhuzunisha na kusikitisha. Hakuna anayeweza kutabiri ni lini ataondoka hapa duniani. Ni siri kubwa, ambayo imefichwa na Mwenyezi Mungu.

Mwanahabari mkongwe Abubakar Liongo aliandika kwenye mtandao wa facebook jana akisema:
" Japo lazima sote siku tutaipa kisogo dunia hii ya manani, lakini hakika habari za kifo cha comrade Innocent Munyuku, zimenistua sana. Si zaidi ya wiki nikiwa Dodoma, tulikuwa tukichati kupitia FB,tukitaniana kama kawaida yetu. Hakika kifo hakina hodi.Munyuku au Gaitanoama, tulivyokuwa tukiitana, umeondoka mapema ndugu yangu kama walivyoondoka Conrade Dunstan (kiona mbali) na Dan Mwakiteleko (mullah) na kuiachia pengo tasnia ya habari.".

Mwani Nyangasa naye aliandoka: "Ni vigumu kuamini, naona shida kuzungumzia kwa kuwa ni kitu ambacho sikiamini. Eti leo kaka zangu Innocent Munyuku na Baraka Karashani hatunao, wamekufa siku moja. Juzi nilipata taarifa za kuumwa Baraka, jana nikaenda hospitali na dada yangu Grace Hoka kumuangalia, tulitokwa na machozi. Baraka hakuwa na hali nzuri, tukajipa moyo atapona na tukamfariji mkewe kuwa asife moyo, Baraka atakuwa na nguvu, nikaondoka, Leo asubuhi naamshwa na simu eti Innocent amefariki nilipigwa na butwaa."

Kwa upande wake, Charles Mateso, alisimulia jinsi alivyokwenda ofisini kwa Munyuku, akamkosa, wakakutana siku inayofuata, wakazungumza mambo mbalimbali na kupanga kuyatekeleza jana, lakini Mungu hakupenda. Amemchukua Munyuku.

Binafsi nilipata taarifa za kifo cha Munyuku kupitia kwa Grace Hoka, Mhariri wa gazeti la Bingwa. Alinipigia simu saa 1.30, asubuhi na kuzungumza maneno matatu. Alisema: "Kaka Zahor, Munyuku amefariki." Akakata simu huku akiangua kilio.

Sikuamini masikio yangu. Nikakaa na kutafakari kwa sekunde kadhaa. Baada ya muda, nikaamua kupiga namba ya simu ya Munyuku. Ilipokelewa na mwanamke mmoja, ambaye naye alitamka maneno machache. Alisema: "Mwenye simu hii amefariki."

Nikamuuliza: "Amefariki lini?"
Akasema: "Leo alfajiri."
Nikaendelea kumuuliza: "Wewe ni nani?"
Akajibu: "Mimi mpangaji mwenzake."

Baada ya maneno hayo, yule dada alikata simu. Nadhani alichoshwa kupokea simu kutoka kwa watu mbalimbali waliokuwa wakiulizia taarifa za kifo cha mwanahabari huyo.

Nilipata uthibitisho zaidi wa kifo cha Munyuku baada ya kuelezwa na baadhi ya wafanyakazi wenzake kwamba, maofisa wa New Habari walikwenda nyumbani kwake na kuukuta mwili wake ukiwa bado kitandani kama alivyokuwa amelala. Wakauchukua na kuupeleka hospitali, bila shaka kwa lengo la kutaka kujiridhisha kuhusu sababu za kifo chake.

Hivyo ndivyo taarifa za kifo cha Munyuku zilivyoanza kusambaa katika vyombo mbalimbali vya habari. Taarifa zilizopokelewa kwa majonzi makubwa na wanahabari wengi waliomfahamu, hasa kutokana na ucheshi na vituko vyake, achilia mbali utendaji wake mzuri wa kazi.

Nilianza kumfahamu Munyuku tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000. Wakati huo alikuwa akiandikia magazeti mbalimbali. Alipenda kuniita kaka na mimi nilipenda kumwita 'kamanda'. Tuliitana hivyo kila tulipozungumza kwa simu au tulipokutana, hasa katika vikao vya nje ya kazi.

Nilianza kuwa naye karibu mwaka 2006, wakati yeye na swahiba wake mkubwa, Charles Mateso, walipoajiriwa na Kampuni ya Uhuru Publications Ltd, inayochapisha magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Burudani. Kuajiriwa kwao kulilenga kuliendesha gazeti la Burudani.

Walifanyakazi pamoja kwa kipindi kisichopungua miaka miwili. Baada ya muda huo, wote wawili waliamua kuacha kazi kwa pamoja. Sababu za kufanya hivyo walizijua wenyewe.

Kwa uchapakazi, Munyuku alikuwa na sifa za aina yake. Hakutaka utani katika kazi. Na kila alipokuwa 'bize', hakupenda usumbufu kutoka kwa mtu yeyote. Akiona unamsumbua, atakwambia 'kamanda niache kwanza nimalize kazi, tutaongea baadae.'

Munyuku pia alikuwa mbunifu mzuri. Nakumbuka yeye na Mateso walifanikiwa kubadili sura ya gazeti la Burudani hadi likawa na mvuto wa aina yake. Walianzisha 'kolamu' nyingi zenye kusisimua na ambazo zinapendwa na vijana. Waliliweka gazeti hilo kwenye matawi ya juu.

Hatimaye Munyuku ametutoka. Ametangulia kwenda kule ambako, sisi viumbe wote wa Mwenyezi Mungu lazima tutakwenda. Maana yamenena maandiko matakatifu kwamba, 'Kila chenye roho, lazima kitaonja mauti.'

Buriani Innocent Munyuku. Tunamuomba Mwenyezi Mungu akupe mapumziko mema.

Wakati huo huo, habari zingine za kusikitisha zilizopatikana jana jioni zimeeleza kuwa, mwanahabari mwingine maarufu wa michezo, Baraka Karashani, amefariki dunia.

Baraka alifariki jana mchana kwenye hospitali ya Jeshi ya Lugalo, Dar es Salaam, alikokuwa amelazwa kwa siku kadhaa.

LIGI YA SDL KUANZA KUTIMUA VUMBI DESEMBA 6


Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) msimu huu iliyokuwa ianze kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu kwa mechi kumi katika viwanja vitano tofauti imesogezwa mbele hadi Desemba 6 mwaka huu.

Mechi hizo zimesogezwa ili kutoa fursa ya kukamilisha maandalizi mbalimbali ya ligi hiyo inayoshirikisha timu 24 kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara.

Mikoa yenye timu katika ligi hiyo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Katavi, Kigoma, Lindi, Mara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida na Tabora.

MASHINDANO YA TAIFA U12 YASOGEZWA
Mashindano ya Taifa kwa vijana wenye umri chini ya miaka 12 yanayoshirikisha kombaini za mikoa yote ya Tanzania yatafanyika jijini Mwanza kuanzia Desemba 30 mwaka huu hadi Januari 5 mwakani.

Awali mashindano hayo yalipangwa kuanza Desemba 6 mwaka huu, lakini yamelazimika kuyasogeza ili kutoa fursa ya kukamilika kwa matengenezo ya viwanja vitatu ambayo vitatumika.

Kila timu ya mkoa inatakiwa kuwa na ujumbe wa watu 16, wakiwemo wachezaji 14 na makocha wawili katika mashindano hayo ya timu yenye wachezaji saba (7 aside).

Timu zinatakiwa kuwasili jijini Mwanza kuanzia Desemba 28 mwaka huu tayari kwa ajili ya uhakiki wa umri na taratibu nyingine za mashindano. Timu zote zitafikia katika shule ya Alliance (Alliance Schools).

Wachezaji wanaotakiwa kushiriki mashindano hayo ni wenye umri chini ya miaka 12, hivyo ni wale waliozaliwa kuanzia Januari 2003 na kuendelea.

TASWA YATUMA RAMBIRAMBI VIFO VYA MUNYUKU, KARASHANI

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko vifo vya waandishi wa habari Innocent Munyuku na Baraka Karashani vilivyotokea jana (Novemba 19 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.

Msiba huo ni mkubwa katika familia ya mpira wa miguu, na tasnia ya habari nchini kwa ujumla kutokana na mchango mkubwa waliotoa katika ustawi wa mpira wa miguu nchini kupitia kalamu zao.

Munyuku alikuwa mmoja wa waandishi waanzilishi wa gazeti la Mwanaspoti wakati Karashani kwa nyakati tofauti alifanya kazi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwemo kampuni ya New Habari 2006 akiripoti habari za mpira wa miguu.

Tunatoa pole kwa familia za marehemu, Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA), na kampuni ya New Habari 2006 na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.

Bwana alitoa, Bwana ametwaa. Jina lake lihimidiwe.

Monday, November 17, 2014

TFF YAIPONGEZA SAFAShirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa pongezi kwa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kufuatia timu yake ya Taifa (Bafana Bafana) kufuzu kucheza fainali zijazo za AFCON nchini Equatorial Guinea.


Afrika Kusini iliifunga Sudan mabao 2-1, hivyo kufuzu kabla ya kukamilisha michezo yote. Bafana Bafana bado imebakiza mchezo mmoja katika hatua hiyo.

Wakati huo huo, TFF imeipeleka barua ya shukrani kwa Chama cha Mpira wa Miguu Afrika Kusini (SAFA) kwa kufanikisha kambi ya Taifa Stars nchini humo kabla ya kwenda kucheza Swaziland.

SAFA ilitoa viwanja vya mazoezi kwa Taifa Stars na usafiri wa basi la kisasa kutoka Johannesburg kwenda Swaziland na kurudi, hivyo kuokoa zaidi ya dola 15,000 ambazo TFF ingetumia kama ingegharamia yenyewe safari hiyo au kuweka kambi ya timu hiyo nyumbani.

Awali Benchi la Ufundi la Taifa Stars chini ya Kocha Mart Nooij lilipendekeza timu kufika Swaziland mapema au kuweka kambi nchini Afrika Kusini. SAFA ikajitolea kusaidia kambi hiyo.

Pia TFF inakanusha madai ya gazeti moja la kila siku lililodai kuwa wakaguzi wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) wamevamia/wamefanya ukaguzi wa siri kukagua fedha za udhamini wao kwa Taifa Stars.

Ukaguzi wa hesabu ni utaratibu wa kawaida wa kila robo ya mwaka wa fedha. TFF ndiyo huwaalika TBL kutuma wakaguzi wao ili kuhakiki vitabu vya fedha. Uhusiano kati ya TFF na TBL ni mzuri, na kila kinachofanyika ni kwa nia njema kwa makubaliano ya pande zote mbili.

NGASA AFUNGA NDOA NA LADHIA


MSHAMBULIAJI wa Taifa Stars na Yanga SC, Mrisho Ngassa mwishoni mwa wiki iliyopita alifunga ndoa ya pili na Ladhia Mngazija eneo la Tegeta jijini Dar es Salaam.

STARS YATOKA SARE NA SWAZILANDTIMU ya soka ya Taifa, Taifa Stars jana ilitoka sare yabao 1-1 na Swaziland katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyochezwa kwenye uwanja wa Somhlolo mjini Mbabane.

Katika mechi hiyo iliyokuwa kwenye kalenda ya Shirikisho la Soka Tanzania (FIFA), Swaziland ilikuwa ya kwanza kupata bao kipindi cha kwanza kabla ya Thomas Ulimwengu kuisawazishia Taifa Stars kipindi cha pili.

Taifa Stars ilifanikiwa kupata penalti dakika 10 za mwisho wakati beki mmoja wa Swaziland alipounawa mpira wa krosi uliopigwa na Oscar Joshua, lakini shuti la Ulimwengu lilitoka pembeni ya lango.

Thursday, November 13, 2014

KASEJA RUDI SIMBA- ZACHARIA HANSPOPE


KIPA nguli wa zamani wa Simba, ambaye kwa sasa yupo kikosi cha Yanga, Juma Kaseja, ameitwa kwenye timu yake hiyo ya zamani.

Simba imeamua kumuita Kaseja kutokana na kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga, inayonolewa na Mbrazil, Marcio Maximo.

Klabu hiyo imetoa baraka kwa nahodha wake huyo wa zamani kurejea mtaa wa Msimbazi, endapo mambo yataendelea kuwa magumu kwake Yanga.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alisema jana kuwa, Kaseja ni mtoto wa Msimbazi na alikwenda Yanga kutafuta maisha.

Hanspope alisema kipa huyo ana mapenzi makubwa na Simba, licha ya kuichezea Yanga katika vipindi viwili tofauti.

Kigogo huyo alisema Kaseja aliondoka Simba bila ya matatizo, hivyo anazo kila sababu za kurejea iwapo atapenda kufanya hivyo.

Alisema Simba ipo tayari kuzungumza na Kaseja kuhusu mpango huo, lakini mwenye uamuzi wa mwisho ni mchezaji mwenyewe.

"Kaseja ni kipa bora na Simba inatambua hilo, ana uwezo mkubwa wa kulinda lango. Kama anataka kurudi Simba, sisi hatuna tatizo wala pingamizi, hapa ni nyumbani kwake,"alisema.
Hivi karibuni, wakala wa kipa huyo, Abdulfatah Saleh, alitoa masharti kwa Maximo, akimtaka kumchezesha Kaseja kwenye kikosi cha kwanza, vinginevyo watavunja mkataba na Yanga.

Wednesday, November 12, 2014

SIMBA YAMNYEMELEA MSUVA, MKUDE ALAMBA MILIONI 40, AMWAGA WINO MIAKA MIWILIKIUNGO Jonas Mkude (katikati) akitia saini mkataba wa kuichezea Simba mbele ya Rais wa klabu hiyo, Evans Aveva (kulia) na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope
MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Evans Aveva (kushoto) akimpongeza Mkude baada ya kutia saini mkataba mpya na klabu hiyo.

KLABU ya Simba imetuma maombi kwa mahasimu wao Yanga, kutaka kuzungumza na mchezaji wao wa kiungo, Simon Msuva.

Simba imetuma salamu kwa mchezaji huyo wa timu ya taifa, Taifa Stars, ikitaka kumsajili katika usajili wa dirisha dogo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limetangaza kuwa, msimu wa usajili wa dirisha dogo utaanza rasmi keshokutwa hadi Desemba 15, mwaka huu.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope, alisema jana kuwa, barua ya maombi kwa Yanga ilitumwa juzi.

Hanspope alisema Simba inataka kufuata kanuni za usajili, hivyo imeamua kutuma maombi hayo kwa kuhofia kuvunja sheria.

"Unapotaka kufanya mazungumzo na mchezaji, ambaye bado hajamaliza mkataba na klabu yake, unatakiwa kwanza kuiomba klabu ndipo uzungumze naye,"alisema.

Alisema Msuva ni mchezaji mzuri, ambaye ataisaidia Simba, hivyo watahakikisha anavaa uzi wa klabu hiyo mwakani.

Hanspope alisema ana imani uongozi wa Yanga utaijibu barua hiyo ili waanze kufanya mazungumzo na Msuva, ambaye kwa sasa ni kipenzi kikubwa cha mashabiki wa klabu hiyo ya Jangwani.

Licha ya kuwa tegemeo kubwa la Yanga katika kufunga mabao, Msuva amekuwa akikosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza kutokana na kuanzia benchi.
Wiki iliyopita, Msuva aliifungia Yanga mabao yote mawili ilipoibwaga Mgambo JKT mabao 2-0 katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Alifunga mabao hayo kipindi cha pili akitokea benchi.
Hivi karibuni, mchezaji huyo alikarriwa akilalamikia kitendo cha Kocha Mkuu wa timu hiyo, Marcio Maximo kumwanzisha benchi wakati kiwango chake kipo juu.
Wakati huo huo, kiungo nyota wa Simba, Jonas Mkude, ameongeza mkataba wa kuichezea klabu hiyo kwa miaka miwili.
Mkude alimwaga wino Simba jana mbele ya Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspope, baada ya kupewa kitita cha shilingi milioni 40.
Kiungo huyo mkabaji amekubali kubaki Simba baada ya kuahidiwa kulipwa shilingi milioni 60. Fedha zingine zilizobaki atalipwa baadaye.

WAAMUZI 23 KUSHIRIKI SEMINA DAR


Waamuzi 23 wa daraja la kwanza wakiwemo wenye beji la Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) wameteuliwa kushiriki semina itakayofanyika Novemba 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Washiriki wa semina hiyo ambayo pia itakuwa na mtihani wa utimamu wa mwili (physical fitness test) wanatakiwa kuripoti Novemba 15 mwaka huu kwenye hosteli ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.

Wakufunzi wa semina hiyo wanaotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni Riziki Majala na Soud Abdi.

Waamuzi watakaoshiriki semina hiyo ni Ahmed Juma Simba (Kagera), Arnold Bugado (Singida), Charles Peter Simon (Dodoma), Dalila Jafari Mtwana (Zanzibar), Ferdinand Chacha Baringenge (Mwanza), Florentina Zabron (Dodoma) na Frank John Komba (Pwani).

Grace Wamara (Kagera), Hellen Joseph Mduma (Dar es Salaam), Israel Mujuni Nkongo (Dar es Salaam), Issa Bilali Ali (Zanzibar), Issa Haji Vuai (Zanzibar), John Longido Kanyenye (Mbeya), Jonesia Rukyaa Kabakama (Kagera) na Josephat Deu Bulali (Tanga).

Kudra Omary (Tanga), Martin Eliphas Saanya (Morogoro), Mary Kapinga (Ruvuma), Mfaume Ali Nassoro (Zanzibar), Mgaza Ali Kinduli (Zanzibar), Samwel Hudson Mpenzu (Arusha), Soud Iddi Lila (Dar es Salaam) na Waziri Sheha Waziri (Zanzibar).

TAIFA STARS YATUA SALAMA J'BURGKikosi cha wachezaji 23 wa Taifa Stars tayari kimewasili Johannesburg, Afrika Kusini tayari kwa maandalizi ya mechi dhidi ya Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Swaziland.


Mechi hiyo itafanyika Jumapili (Novemba 16 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa wa Somhlolo jijini Swaziland. Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwepo Johannesburg hadi Ijumaa itakapoondoka kwenda Mbabane.

Wachezaji wote walioitwa na Kocha Mart Nooij wapo kwenye msafara huo isipokuwa kiungo mshambuliaji Mrisho Ngasa ambaye amebaki Dar es Salaam kutokana na matatizo ya kifamilia.

Taifa Stars inatarajia kurejea nyumbani Jumatatu (Novemba 17 mwaka huu) saa 12.45 jioni kwa ndege ya South Africa Airways.

Wakati huo huo, kikosi cha maboresho cha Taifa Stars kitacheza mechi ya kirafiki na timu ya Taifa ya Rwanda kwa wachezaji wenye umri chini ya miaka 23. Mechi hiyo itachezwa Desemba 9 mwaka huu nchini Tanzania.

Kikosi cha maboresho cha Taifa Stars kinachoundwa na wachezaji wenye umri chini ya miaka 23 kitakuwa kinakutana mara moja kila mwezi hadi Mei mwakani kwa ajili ya mazoezi na kucheza mechi moja ya kirafiki.
Kocha Mart Nooij atatangaza kikosi kwa ajili ya mechi hiyo na programu nzima mara atakaporejea kutoka Swaziland.

Tuesday, November 11, 2014

MAMIA WAMZIKA AMIGOLAS, JK AMLILIA, WASANII WAANGUA VILIO MAKABURINI


RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.

Rais Kikwete ametuma salamu hizo kuomboleza kifo cha mwanamuziki mwasisi wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta', Hamisi Kayumbu 'Amigolas'.

Amigolas alifariki usiku wa kuamkia Jumapili saa 5:30 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa ugonjwa wa moyo.

“Nimehuzunishwa na kusikitishwa na taarifa za kifo cha mwanamuziki Hamisi Kayumbu kilichotokea tarehe 9 Novemba, 2014 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa moyo”, alisema Rais Kikwete katika Salamu zake.

Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Ikulu jana, ilisema Rais Kikwete anatambua mchango mkubwa wa marehemu Amigolas, katika kuhamasisha maendeleo ya nchi yetu.

Taarifa hiyo ilisema Kayumbu alitoa mchango wake kupitia sanaa ya muziki kuwafikishia wananchi ujumbe muhimu wa masuala mbalimbali ya kijamii na kiuchumi.

Alisema Kayumbu alikuwa mfano unaofaa kuigwa na wasanii wengine nchini. Amigolas alikuwa kiongozi wa bendi mpya ya Ruvu Stars baada ya kuhama Twanga Pepeta.

“Kutokana na msiba huu, naomba upokee salamu zangu za rambirambi kwa kumpoteza mmoja wa wanamuziki mahiri hapa nchini, pia ziwafikie wanamuziki wengine kote nchini kwa kumpoteza mwenzao”, ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Rais Kikwete amemwomba Dk. Fenella, kumfikishia salamu zake za pole kwa familia ya marehemu Kayumbu kwa kupotelewa na kiongozi na mhimili madhubuti.

Wakati huohuo, wasanii mbalimbali jana walishindwa kujizuia kuangusha vilio, baada ya mwili wa mwanamuziki mahiri marehemu Hamisi Kayumbu 'Amigolas' kuwasili nyumbani kwake Mburahati, Dar es Salaam.

Amigolas alifariki usiku wa kuamkia Jumapili saa 5:30 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kwa ugonjwa wa moyo.

Mkurugenzi wa bendi ya Extra Bongo na mwimbaji hodari nchini, Ali Choki, alishindwa kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu kifo cha Amigolas.

Choki na Amigolas, walifanya kazi kwa karibu na pia waanzilishi wa bendi ya African Stars 'Twanga Pepeta' mwaka 1997.

Hata hivyo, baadhi ya wasanii walitoa maoni yao kuhusu kifo cha Amigolas aliyekuwa na sauti nzito jukwaani.

Kiongozi wa Twanga Pepeta, Luiza Mbutu, alisema Amigolas alikuwa mtu muhimu katik tasnia ya muziki na ametoa mchango mkubwa kwa wasanii chipukizi.

Naye Saidi Mabera 'Dokta' wa Msondo Ngoma alisema alimfahamu, Amigolas, tangu mwaka 1986 alipokuwa mwimbaji wa bendi ya Bicco Stars.

"Nilimfahamu marehemu Amigolas tangu mwaka 1986 akiwa Bicco Stars, naomba wanamuziki tumuenzi kwa kudumisha muziki wa asili," alisema Mabera.

Ramadhani Athumani 'Dogo Rama' wa Twanga Pepeta alisema, Amigolas, alikuwa kiungo muhimu na mmoja wa wasanii walimsaidia kukuza kipaji chake cha kuimba.

Naye Stara Thomas, alisema alianza kufahamiana na Amigolas akiwa bado kinda katika muziki, hivyo ametoa rai kwa wadau kumuombea.

"Tunamshukuru Mungu kwa sababu kifo hakikwepeki, jambo la msingi ni kumuombea ingawa alikuwa bado anahitajika,"alisema msanii wa maigizo nchini Steven Mengele 'Steve Nyerere'.

Kwa upande wake Hassani Mussa 'Super Nyamwela' wa Extra Bongo, alisema hakutarajia kama nguli huyo angefariki kwa ugonjwa wa moyo na amemtaja Amigolas alikuwa mhimili wa Twanga Pepeta.

Marehemu Amigolas alizikwa jana alasiri katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam na umati wa watu wakiwemo wasanii na watu mbalimbali maarufu.

Sunday, November 9, 2014

AMIGOLAS WA TWANGA PEPETA AFARIKI DUNIA
MWIMBAJI nyota wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta Internationa, Hamisi Kayumbu 'Amigolas', amefariki dunia.


Amigolas, alifariki dunia juzi saa 5.30 usiku katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, alikokuwa amelazwa kutokana na kusumbuliwa na ugonjwa wa moyo.

Mwanamuziki huyo alikuwa kiongozi mpya wa bendi ya Ruvu Stars baada ya kutamba kwa muda mrefu na Twanga Pepeta, ambapo pia aliwahi kuwa kiongozi.

Amigolas atakumbukwa kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika bendi ya Twanga Pepeta, ambapo alikuwa mmoja wa waimbaji wake mahiri, akishirikiana na Ally Choki, Luiza Mbutu, Khalid Chokoraa, Ramadhani Masanja 'Banza Stone'.
Akizungumzia kifo cha mwanamuziki huyo, Mkurugenzi wa Kampuni ya African Stars Entertainment, Asha Baraka, alisema marehemu Amigolas alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo kwa miaka minne iliyopita.
Asha alisema tasnia ya muziki imempoteza mtu muhimu, ambaye alisaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa wasanii wanaong'ara katika bendi mbalimbali.
Kwa mujibu wa Asha, Amigolas alijiunga na Twanga Pepeta mwaka 1998, wakati huo ikiwa inafanya maonyesho ya wazi kwenye baa kabla ya kuanza kupata umaarufu na kuteka soko la muziki nchini.
Marehemu Amigolas ameacha mke na watoto wanne na anatarajiwa kuzikwa leo kwenye makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam.

SIMBA YAFUTA MWIKO WA SARE, YAICHAPA RUVU SHOOTING 1-0BAO lililofungwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Emmanuel Okwi, jana liliiwezesha Simba kupata ushindi wake wa kwanza katika michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0.

Okwi alifunga bao hilo dakika ya 78 baada ya kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Rashid Abdalla wa Ruvu Shooting, kutokana na shuti kali la Elias Maguri.

Ushindi huo uliwapa ahueni kubwa mashabiki wa Simba baada ya kuishuhudia timu yao ikitoka sare mechi sita mfululizo na hivyo kuhatarisha kibarua cha Kocha wao, Patrick Phiri kutoka Zambia.

Sare hizo pia zilisababisha uongozi wa Simba kuwasimamisha wachezaji wake nyota watatu, Amri Kiemba, Haruna Chanongo na Shaaban Kisiga kwa tuhuma za utovu wa nidhamu.

Kwa matokeo hayo, Simba sasa inazo pointi tisa baada ya kucheza mechi saba na imechupa hadi nafasi za juu katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa nyumba ya Yanga kwa tofauti ya pointi tatu.

Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ilipata nafasi kadhaa nzuri za kufunga mabao, lakini umaliziaji mbovu wa washambuliaji wake ulikuwa kikwazo.

Kuingia kwa Elias Maguli katika kipindi cha pili, aliyechukua nafasi ya Saidi Ndemla, kuliiongezea uhai safu ya ushambuliaji ya Simba, ambayo ilifanya mashambulizi kadhaa kwenye lango la Ruvu Shooting.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Mtibwa Sugar ilitoka sare ya bao 1-1 na Kagera Sugar kwenye uwanja wa Manungu ulioko Turiani mjini Morogoro.

Awali, mechi hiyo ilichezwa juzi kwenye uwanja huo, lakini ililazimika kuahirishwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha uwanjani. Hadi mechi ilipovunjika, Mtibwa ilikuwa mbele kwa bao 1-0.

Saturday, November 8, 2014

YANGA, AZAM ZASHINDA LIGI KUU, MBEYA CITY HOIMABAO mawili yaliyofungwa na mshambuliaji Simon Msuva jana yaliiwezesha Yanga kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mgambo JKT katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Msuva, ambaye aliingia uwanjani kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Haruna Niyonzima,alifunga mabao hayo dakika ya 73 na 88.

Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa imefikisha pointi 13 baada ya kucheza mechi saba, ikiwa inakabana koo na Azam, inayoshika nafasi ya pili.

Azam ilitoka uwanjani kifua mbele baada ya kuichapa Coastal Union mabao 2-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Mabao ya Azam yalifungwa na beki Shomari Kapombe na mshambuliaji wa kimataifa wa Ivory Coast, Kipre Tchetche. Bao la Coastal Union lilifungwa na Rama Salim.

Timu ya soka ya Mbeya City jana ilipigwa mweleka wa bao 1-0 ba Stand United katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga.

Kipigo hicho ni cha tano kwa Mbeya City tangu ligi hiyo ilipoanza msimu huu, ambapo katika mechi saba ilizocheza, imeshinda moja na kutoka sare moja.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa jana, Prisons ya Mbeya ilichezea kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa maafande wa Polisi kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro.

Pambano kati ya Mtibwa na Kagera Sugar lililochezwa kwenye uwanja wa Manungu mjini Turiani, lilivunjika kipindi cha pili kutokana na mvua kubwa kuanza kunyesha.

Hadi pambano hilo lilipovunjika, Mtibwa ilikuwa mbele kwa bao 1-0. Pambano hilo sasa litachezwa leo.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo itakayochezwa leo, Simba itashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na Ruvu Shooting.

Thursday, November 6, 2014

AZIM DEWJI AWATULIZA WANA SIMBA


MWANAMICHEZO maarufu nchini, Azim Dewji amewataka wanachama na wapenzi wa timu ya soka ya Simba kuamini timu yao bado ni bora, isipokuwa ipo katika kipindi cha mpito kuelekea katika mafanikio yatakayowashangaza wengi.

Kutokana na imani yake hiyo, ameshauri ni vyema wakatoa ushirikiano wa kila aina kwa viongozi, wachezaji na benchi lote la ufundi, vivyo hivyo akiwataka viongozi kushikamana na wachezaji na benchi la ufundi,badala ya kuanza kunyoosheana vidole.

Aliyasema hayo jana alipokuwa anazungumzia mwenendo wa klabu hiyoaliyowahi kuifadhili na kuipa mafanikio makubwa katika miaka ya 1990, lakini msimu huu ukionekana kuyumba, kwani tangu kuanza kwa ligi, imetoka sare katika mecho zake zote sita, hali inayowasonesha `wanazi’ wa klabu hiyo.
Alisema Simba inapitia mapito kama ya Manchester United ya England, ambayo tangu kuondoka kwa kocha wake wa zaidi ya robo karne, Sir Alex Ferguson iliyumba na hata kutemeshwa ubingwa kwa aibu, lakini sasa imeanza kurejesha makali.
“Sasa ukiangalia hata Simba si timu mbaya ndiyo maana ingawa haijashinda, haijapoteza mchezo pia. Haya yanatokana na mabadiliko mengi kwa wakati mmoja, kuanzia safu ya uongozi, benchi la ufundi na
hata wachezaji…hawa watu wanahitaji kupewa muda. Nakuhakikishia Simba hii itakuwa tishio
“Lakini wakati nikiwasihi wanachama na wapenzi kuwaunga mkono viongozi, wachezaji na kocha, naamini viongozi nao watumie busara ya kufanya kila linalowezekana kuwafanya wachezaji na makocha kujiamini na kujiona wana deni, lakini si kutishiana kila kukicha.
“Hii si sahihi na kwa mazingira ya vitisho, siku zote watabaki kuwa watu wa wasiwasi na kushindwa kuisaidia timu…tuwape nafasi, hakika mapinduzi ya kisoka yataonekana kwa sababu nimeona timu ina wachezaji wengi wenye vipaji,” alisisitiza Dewji.

Katika msimu huu wa ligi, Simba ilianza ligi kwa kutoka sare ya 2-2 na Coastal Union ya Tanga kabla ya kupata sare mbili za matokeo ya 1-1 mbele ya Polisi Moro na Wakuja katika ligi hiyo, Stand United ya Shinyanga. Haikufungana na Yanga iliyokuwa inaaminika ni mara zaidi tangu ilipomnasa kocha Mbrazil Marcio Maximo katikati ya mwaka huu, ikatoka pia sare ya 1-1 na Prisons ya Mbeya na pia na Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Wednesday, November 5, 2014

MPANDA UTD, UJENZI RUKWA KUANZA SDL
Michuano ya Ligi Daraja la Pili (SDL) inayoshirikisha timu 24 katika makundi manne ya timu sita sita kwa mtindo wa nyumbani na ugenini inaanza kutimua vumbi Novemba 22 mwaka huu ambapo Mpanda United itakuwa mwenyeji wa Ujenzi Rukwa.

Mechi hiyo ya kundi A itachezwa kwenye Uwanja wa Mandela mjini Sumbawanga. Siku hiyo hiyo katika kundi hilo kutakuwa na mechi kati ya Mvuvumwa FC na CDA (Lake Tanganyika, Kigoma), na Milambo dhidi ya Singida United kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Kundi B mechi za ufunguzi ni kati ya Pamba na JKT Rwamkoma kwenye Uwanja wa CCM Kirumba huku Bulyanhulu FC ikiwa mwenyeji wa AFC kwenye Uwanja wa Bulyanhulu mkoani Shinyanga.

Abajalo FC ya Dar es Salaam itaikaribisha Kariakoo FC ya Lindi kwenye mechi ya kundi C itakayochezwa Uwanja wa Karume. Nazo Kiluvya United na Transit Camp zitaoneshana kazi kwenye Uwanja wa Mabatini uliopo Mlandizi mkoani Pwani.

Kundi D mechi tatu za ufunguzi ni kati ya Town Small Boys na Volcano FC (Uwanja wa Majimaji, Songea), Njombe Mji na Mkamba Rangers (Uwanja wa Sabasaba, Njombe), na Wenda FC dhidi ya Magereza Iringa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

NOOIJ ATANGAZA KIKOSI CHA STARS KITAKACHOCHEZA NA SWAZILANDKocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij ametangaza kikosi cha wachezaji 24 kwa ajili ya mechi ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) dhidi ya Swaziland itakayochezwa Novemba 16 mwaka huu jijini Mbabane.


Akizungumza Dar es Salaam, leo (Novemba 5 mwaka huu), Nooij alisema kikosi hicho kitaingia kambini Novemba 10 mwaka huu saa 6 mchana kwenye hoteli ya Accomondia, na siku hiyo hiyo jioni kitafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana.

Novemba 11 mwaka huu, Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka kwenda Afrika Kusini ambapo itaweka kambi ya siku mbili kabla ya kuondoka Novemba 13 mwaka huu kwenda Swaziland.

Wachezaji walioitwa kwenye kikosi hicho ni makipa Aishi Manula (Azam) na Deogratias Munishi (Yanga). Mabeki ni Abubakar Mtiro (Kagera Sugar), Aggrey Morris (Azam), Emmanuel Simwanda (African Lyon), Hassan Isihaka (Simba), Kelvin Yondani (Yanga), Nadir Haroub (Yanga), Osacr Joshua (Yanga), Said Moradi (Azam), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar) na Shomari Kapombe (Azam).

Viungo ni Amri Kiemba (Simba), Erasto Nyoni (Azam), Haruna Chanongo (Simba), Himid Mao (Azam), Mwinyi Kazimoto (Al Markhiya, Qatar), Said Ndemla (Simba) na Salum Abubakar (Azam).

Washambuliaji ni Juma Luizio (ZESCO, Zambia), Mbwana Samata (TP Mazembe, DR Congo), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga) na Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, DR Congo).

Tuesday, November 4, 2014

KOCHA NOOIJ KUTAJA KIKOSI CHA STARSKocha Mkuu wa Taifa Stars, Mart Nooij keshokutwa (Novemba 5 mwaka huu) atatangaza kikosi cha timu hiyo kwa ajili ya mechi ya kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) itakayochezwa ugenini Novemba 16 mwaka huu.

Nooij atatangaza kikosi hicho mbele ya waandishi wa habari katika mkutano utakaofanyika saa 4.30 asubuhi kwenye ofisi za TFF zilizoko ghorofa ya tatu, Jengo la PPF Tower jijini Dar es Salaam.

Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Swaziland, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa wa Somhlolo jijini Mbabane.

MWAKIBINGI AONDOKA BODI YA LIGI KUU


Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), Silas Mwakibinga amemaliza mkataba wake tangu Oktoba 31 mwaka huu.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na TPLB wanamshukuru Mwakibinga kwa mchango wake kwa kipindi ambacho ameitumikia Bodi, na kumtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya huko aendako.

TPLB hivi sasa iko katika mchakato wa kupata Ofisa Mtendaji Mkuu mpya kwa ajili ya kuziba nafasi hiyo iliyoachwa wazi na Mwakibinga baada ya muda wa mkataba wake kumalizika.

Monday, November 3, 2014

ONYESHO LA MIAKA 50 YA MSONDO NGOMA LAFANA DAR Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo,Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akimkabidhi cheti cha heshima kwa kiongozi wa bendi ya Msondo Ngoma, Said Mabela.
 Kiongozi wa Msondo Ngoma, Saidi Mabela akionyesha umahiri wake wa kupiga gita la solo
 Rapa maarufu wa Msondo Ngoma, Roman Mng'ande akifanya vitu vyake
 Waimbaji wa Msondo Ngoma wakiwajibika jukwaani. Kutoka kushoto ni Athumani Kambi, Shabani Dede na Juma Katundu.
Mmoja wa wanamuziki waanzilishi wa Msondo Ngoma, Kepteni mstaafu, John Simon (katikati) akielezea historia ya bendi hiyo wakati wa onyesho hilo.

JK AIBARIKI SUNDERLAND KUJENGA KITUO CHA MICHEZO KIDONGO CHEKUNDU MNAZI MMOJA

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Profesa Jakaya Mrisho Kikwete (kulia) akiwaonyesha jezi yenye jina la Tanzania kwa wageni waalikwa pamoja na wananchi waliohudhuria hafla ya kutoa Kibali kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Umma uliopewa jina la Rais Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park. Tukio hilo limefanyika leo 1 Novemba, 2014 eneo la Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Profesa Jakaya Mrisho Kikwete akiwahutubia wageni waalikwa, wafanyakazi mbalimbali wa Kampuni ya Symbion pamoja na wananchi wakati wa hafla ya kutoa Kibali chake kwa Chuo cha Michezo cha Sunderland kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Umma uliopewa jina la Rais Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park. Tukio hilo limefanyika leo 1 Novemba, 2014 eneo la Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam


Mkurugenzi wa Biashara wa Chama cha Michezo cha Sunderland, Bi. Gary Hutchinson akimkabidhi zawadi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Profesa Jakaya Mrisho Kikwete wakati wa hafla ya kutoa Kibali chake kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Umma uliopewa jina la Rais Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park. Tukio hilo limefanyika leo 1 Novemba, 2014 eneo la Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam

Mtoto akimsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Profesa Jakaya Mrisho Kikwete kuweka maji katika shina la mche wa mnazi wakati wa hafla ya kutoa Kibali kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa Michezo wa Umma uliopewa jina la Rais Jakaya Mrisho Kikwete Youth Park. Tukio hilo limefanyika leo 1 Novemba, 2014 eneo la Kidongo Chekundu jijini Dar es Salaam.PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA, MAELEZO-DSM

Sunday, November 2, 2014

DK. SHEIN AAHIDI KUINUA MICHEZO ZANZIBARRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha inaiendeleza sekta ya michezo sambamba na kuimarisha miundombinu yake ili Zanzibar iweze kurejesha hadhi yake katika sekta hiyo.

Dk. Shein aliyasema hayo, leo katika hotuba yake aliyoitoa kwenye sherehe za ushindi wa michezo mbali mbali ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo KMKM, zilizofanyika huko katika viwanja vya Maisara mjini Zanzibar ambazo pia,zimehudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, viongozi mbali mbali wa serikali wanamichezo na wananchi.

Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein alisema kuwa katika kufanya hivyo, Serikali inapitia upya Sera ya Michezo ili iweze kufikia malengo ya Serikali katika kuinua sekta ya michezo hapa nchini.

Alisema kuwa wakati mchakato wa kuipitia upya Sera ya Michezo ukiendelea aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali inaendelea na juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya michezo ikiwemo ujenzi wa viwanja mbali mbali vya michezo Unguja na Pemba.

Dk. Shein alisema kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa viwanja vitatu vya Kimataifa hapa Zanzibar vinaimarishwa ambapo hivi sasa tayari uwanja wa Amaan uliopo mjini Unguja uko tayari na kiwanja cha Gombani Pemba tayari kimeshajegwa ambacho ndani ya mwaka huu wa fedha uwanja huo utawekwa tatan katika eneo la kukimbilia.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali imeshafikia makubaliano na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China ya ujenzi wa uwanja wa Mao-te-tung ili nao uweze kutumika sambamba na viwanja vya Amaan na Gombani huku akieleza azma ya kuviimarisha viwanja vyengine mbali mbali vya Unguja na Pemba kwa lengo la kuendeleza michezo pamoja na kutoa fursa nzuri kwa wananchi waweze kuendeleza michezo kwa ufanisi zaidi hapa Zanzibar

Dk. Shein alipendekeza kuongezwa kwa mashindano ya mpira wa miguu ili kuleta ushindani katika vilabu vya mpira vya hapa Zanzibar pamoja na kuvishirikisha vilabu vyengine kadhaa.

Alisema kuwa hatua hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuzijengea uwezo timu za Zanzibar ili ziweze kushiriki mashinadano ya ndani na nje ya nchi na kupata mafanikio na kusisitiza kuwa wakati umefika Zanzibar kuwa mshindani katika mashindano na kuchukua vikombe katika mashindano mbali mbali.

Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ina vipaji vya kutosha na wanamichezo wa kufanya vizuri wapo, kinachotakiwa ni maandalizi bora na kuondoa migogoro katika uongozi wa vilabu na vyama vya michezo hapa Zanzibar.

Kwa kusisitiza hilo, Dk. Shein alitoa mfano wa mgogoro wa Chama Cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) katika uongozi uliopita ambapo ulisababisha wanamichezo wa timu ya Taifa ya Zanzibar walioshiriki katika mashindano ya 'Challange Cup' mwaka juzi kushindwa kuwakabidhi zawadi aliyowaandalia kutokana na migogoro kadhaa ndani ya chama hicho.

Alieleza kuwa iwapo mashirikiano mazuri yatakuwepo sekta ya michezo itapata mafanikio makubwa na kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa malengo yake ya kukuza sekta ya michezo nchini yanafanikiwa.

Dk. Shein alisema kuwa michezo ni afya, ukakamavu, inajenga udugu na kuleta ushirikiano na kwa hivi sasa, michezo ni ajira kwa hivyo ni vyema wananchi wote wakashiriki katika michezo japo ya vilabu vya mazoezi ili kuimarisha afya zao.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuridhishwa sana na mafanikio ya timu ya mpira wa miguu ya KMKM kwa kuwa mabingwa kwa misimu miwili mfululizo 2013-2014 na 2014-2015 pamoja na ushindi wa timu ya riadha pamoja na kupata ngao za hisani. "Naungana na nyinyi na wale wote wanaokupongezeni kwa mafanikio hayo", alisema Dk. Shein.

"Napenda kuwapongeza wanamichezo wa KMKM kwa kuchagua mbio hizi ambazo kwa kweli zinatukumbusha na sisi wengine enzi zetu katika michezo ya riadha hasa ya 'cross-country na field tract' tulishiriki vyema pamoja na mchezo huu wa kuvuta kamba ambapo mimi mwenyewe nilikuwa kocha", alisema Dk. Shein.

Alisema kuwa Uongozi wa Awamu ya Kwanza ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ulichukua jitihada za makusudi kujenga Uwanja wa Amaan uliofunguliwa mwaka 1970 na ule wa Gombani uliofunguliwa mnamo mwaka 1992 wakati wa uongozi wa Awamu ya Tano ambapo ujenzi wake ulianza katika uongozi wa Awamu ya Nne chini ya Marehemu Sheikh Idrisa Abdul Wakil.

Dk. Shein vile vile, alisisitiza haja ya kila timu hapa Zanzibar kuwa na Klabu yake na jengo lake na kuunga mkono azma ya klabu ya KMKM kutaka kujenga jengo maalum la ghorofa litakalokuwa na eneo la kufanyia mazoezi (GYM), ukumbi wa mikutano na maduka ya vifaa vya michezo.

Mapema Dk. Shein aliyapokea mashindano ya mbio za kilomita kumi katika viwanja hivyo vya Maisara yalioanzia huko Kibweni nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, na kuwashirikisha wakimbiaji zaidi ya 200 ambapo mkimbiaji Philip Jacob Mambo kutoka Kikosi cha Mafunzo aliibuka mshindi wa kwanza na Mohamed Ramadhan kutoka KMKM ambae aliibuka mshindi wa Pili.

Kwa upande wa wanawake mshindi wa kwanza alikuwa Albina Edward kutoka KMKM na mshindi wa pili alikuwa Nuru Nasib kutoka Kambi ya Mtoni. Mashindano hayo pia, yalijumuisha Makundi maalum ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na mkimbiaji Ali Abdalla na mshindi wa pili alikuwa Amina Daudi Simba.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Idara Maalum za SMZ Mhe. Haji Omar Kheir alitoa pongezi kwa Dk. Shein kwa kushirikiana pamoja na wanamichezo hao wa Kikosi cha KMKM katika sherehe zao hizo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa KMKM Komodoo Hassan Mussa alisema kuwa mbio za kilomita 10 ambazo zilishirikisha wanamichezo zaidi ya 200 zimefanyika kwa mara ya kwanza mwaka huu lakini zitafanyika kila mwaka katika siku itakayoteuliwa kuwa ya KMKM.

Katika risala yao nao wanamichezo wa KMKM walieleza mikakati inayochukiliwa katika kuendeleza michezo katika kikosi chao sambamba na kupongeza jinsi Serikali inavyowaunga mkono katika kufikia malengo waliyojiwekea

Sherehe hizo ziliambatana na burudani kutoka vikundi mbalimbali vya sanaa vikiwemo Diamond Morden Taarab, Kidumbaki kilichoongozwa na Msani Makame Faki maarufu sauti ya zege, ngoma ya Kibati kutoka kikundi cha sanaa cha JKU, JKU Morden Taarab ambacho kiliimba wimbo maalum kwa ajili ya sherehe hiyo.

Pia, mchezo wa kuvuta kamba ulifanyika katika sherehe hizo ambao uliwashirikisha maafisa wa KMKM wanaofanya kazi pamoja na Wastaafu ambapo Wastaafu walipata ushindi na kukabidhiwa zawadi na Rais zikiwemo fedha taslim zilizotolewa na wapenda michezo.

YANGA, AZAM ZAPATA VIPIGO LIGI KUU, SARE YAZIDI KUIANDAMA SIMBA
MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Azam jana walikwaa tena kisiki baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Ndanda FC katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Nangwande mjini Mtwara.


Kipigo hicho kilikuwa cha pili kwa Azam baada ya wiki iliyopita kuchapwa bao 1-0 na JKT Ruvu kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Chamazi mjini Dar es Salaam.

Bao pekee na la ushindi la Ndanda lilifungwa na Jacob Massawe dakika ya 15 na kuifanya ipate ushindi wake wa pili tangu ligi hiyo ilipoanza.

Washindi wa pili wa mwaka jana, Yanga nao walionja joto ya jiwe baada ya kuchapwa bao 1-0 na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Bao pekee na la ushindi la Kagera Sugar lilifungwa na Paul Ngwai dakika ya 54 alipounganisha kwa kichwa krosi kutoka pembeni ya uwanja.

Katika mchezo huo, beki Nadir Haroub wa Yanga alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumpiga kichwa mchezaji mmoja wa Kagera Sugar.

Timu kongwe ya Simba nayo iliendelea kusuasua katika ligi hiyo baada ya kulazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Simba ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 35 kupitia kwa beki wake, Joseph Owino baada ya kuunganishwa wavuni kwa kichwa krosi kutoka kwa Emmanuel Okwi.

Mussa Hassan Mgosi aliisawazishia Mtibwa dakika ya 56 na kufuta ndoto za Simba za kutoka uwanjani na ushindi wa kwanza katika ligi hiyo.

Katika mechi hiyo, kipa Manyika Peter wa Simba alionyesha ushujaa wa aina yake baada ya kupangua penalti ya David Luhende baada ya beki Hassan Isihaka kumwangusha Ame Ali wa Mtibwa ndani ya eneo la hatari.

Katika mechi zingine za ligi hiyo zilizochezwa jana, Coastal Union iliichapa Ruvu Shooting bao 1-0, Polisi Moro iliilambisha JKT Ruvu mabao 2-1.

TFF YAJIBU SHUTUMA ZA NDUMBARO


Oktoba 31 mwaka huu kupitia vyombo vya habari Wakili Damas Ndumbaro alitoa shutuma mbalimbali dhidi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Tunapenda kuuleza umma wa Watanzania yafuatayo;

1.Hukumu dhidi ya Wakili Ndumbaro ilitolewa na chombo halali kwa mujibu wa Katiba ya TFF. Hivyo, TFF inatoa tahadhari kwa wanafamilia wa mpira wa miguu kutomhusisha Wakili Ndumbaro katika masuala ya mpira wa miguu katika kipindi hiki anachotumikia adhabu.

2.Hadi sasa TFF haijapokea rufani yoyote kutoka kwa Wakili Ndumbaro. Hii ni kwa kuwa kupitia barua yake kwa TFF aliagiza asikabidhiwe nyaraka yoyote kutoka TFF hadi Oktoba 30 mwaka huu, hivyo hukumu ya Kamati ya Nidhamu dhidi yake alikabidhiwa Oktoba 30 mwaka huu. Alichokifanya Wakili Ndumbaro ni kuleta TFF barua ya kusudio la kukata rufani.

3.Tuhuma za ubadhirifu wa TFF zilizotolewa na Wakili Ndumbaro si za kweli. TFF inatafakari hatua za kisheria na kikanuni za kuchukua dhidi ya tuhuma hizi.

4.Mkataba wa TFF na TBL:

TFF inapenda kuwahakikishia wadau wa mpira wa miguu kuwa hakuna ubadhirifu wa aina yoyote katika matumizi ya fedha za mkataba wa TFF/TBL. TFF ingependa itoe kwa umma ufafanuzi wa vipengele vya mkataba huo na jinsi unavyoendeshwa lakini masharti ya mkataba huo (confidentiality clause) yanatuzuia kufanya hivyo.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikutana na klabu za Ligi Kuu na kuzielekeza zikae na kujadili kanuni za Ligi, kisha zipendekeze maboresho ili yajadiliwe katika kikao kijacho cha Kamati ya Utendaji.

TFF inapenda kuchukue fursa hii kusisitiza umuhimu wa kufuata mifumo tuliyojiwekea katika kutatua matatizo/kero zetu mbalimbali, utulivu ni muhimu katika kuendeleza mpira wa miguu.

MAKOCHA 35 KUSHIRIKI KOZI YA LESENI C YA CAF


Makocha 35 wameteuliwa kushiriki kozi ya ukocha ya Leseni C ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) itakayofanyika mjini Morogoro kuanzia Novemba 5 hadi 19 mwaka huu.

Kozi hiyo itaendeshwa na Mkufunzi wa CAF, Sunday Kayuni na itafanyikia Mchikichini College ambapo washiriki wote wanatakiwa kuwasilisha vyeti vyao vya ukocha vya ngazi ya Kati (Intermediate) pamoja na vyeti vya kitaaluma vya elimu ya sekondari (academic).

Washiriki wa kozi hiyo ni Abdulmaliki Nemes (Airport FC), Ahmed Haule (Kilimanjaro Talented Youth Sports Centre), Ally Jangalu (Moro Kids), Amri Saidi (Mwadui FC), Athuman Kambi (Morogoro), Charles Mwakambaya (Burkina Faso FC), Damian Mussa (Alliance One) na Daudi Sichinga (Kasulu United).

Denis Maneva (Shule ya Msingi Logo), Edgar Juvenary (JUT- Mlale), Hamisi Mangolosho (Shule ya Msingi Mtimbwilimbwili), Henry Ngondo (Chalinze Academy), Issa Hamisi (Polisi Kilimanjaro), Jumanne Chale (Dar es Salaam), Kizito Mbano (Masasi Alliance), Martin Saanya (Magereza Morogoro) na Masoud Gumbwa (Sokoine University Academy).

Mbwana Makata (Oljoro JKT), Mrage Kabange (Kagera Sugar), Muhibu Muhibu (Stand United FC), Nsubuga Solomon (Kishoto FC), Nyamtimba Muga (Kizuka Secondary), Oscar Mirambo (Makongo), Rashid Abdallah (Tech Fort Academy), Renatus Shija (Rhino Rangers), Safari Nyerere (Elimu Sports Academy) na Said Lyakuka (Kizuka Stars).

Simeon Mwesa (Mtibwa Sugar U20), Simon Shija (Tabora), Suleiman Mtungwe (Ruvu Shooting), Swalehe Allawi Abdul (Alliance Academy), Yasin Bashiri (Kick Off Sports Academy) na Zuberi Katwila (Mtibwa Sugar).

Wakati huo huo, kutakuwa na kozi ya wiki mbili ya ukocha ya ngazi ya Kati (Intermediate) itakayofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Desemba 29 mwaka huu.

Makocha wote wanaotaka kushiriki kozi hiyo wanatakiwa kutuma maombi katika Chama cha Makocha wa Mpira wa Miguu Tanzania (TAFCA).