KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, August 29, 2013

USAILI WAGOMBEA TFF, BODI KUANZA KESHOUsaili kwa wanaoomba kuteuliwa kuwa wagombea uongozi katika uchaguzi wa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na ule wa Bodi wa Ligi Kuu (TPL Board)
unaanza kesho (Agosti 30 mwaka huu).

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Agosti 30 mwaka
huu ni usaili kwa waombaji uongozi wote katika Bodi ya Ligi Kuu pamoja na waombaji
uongozi wa TFF kwa kanda namba 11 (Morogoro na Pwani), kanda namba 12
(Kilimanjaro na Tanga) na kanda namba 13 (Dar es Salaam).

Agosti 31 mwaka huu ni kanda namba sita (Rukwa na Katavi), kanda namba saba
(Mbeya na Iringa), kanda namba nane (Njombe na Ruvuma), kanda namba tisa
(Lindi na Mtwara) na kanda namba kumi (Dodoma na Singida).

Usaili kwa kanda namba moja (Geita na Kagera), kanda namba mbili (Mara na
Mwanza), kanda namba tatu (Simiyu na Shinyanga), kanda namba nne (Arusha na
Manyara) kanda namba tano (Kigoma na Tabora), na nafasi za Rais na Makamu
wa Rais wa TFF utafanyika Septemba Mosi mwaka huu.

Waombaji wote wamepangiwa muda wao wa usaili. Kwa mujibu wa ratiba usaili
ufanyika kuanzia saa 3 kamili asubuhi hadi saa 2 usiku. Wasailiwa wote wanatakiwa
kuzingatia muda waliopangiwa.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

COPA COCACOLA KANDA KUANZA SEPT 2Michuano ya Copa Coca-Cola kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15
inayoshirikisha mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani inaanza kutimua vumbi
Septemba 2 mwaka huu katika vituo sita tofauti.

Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa leo (Agosti 29 mwaka huu), kituo cha Mwanza
mechi zake zitachezwa katika viwanja vya Alliance ambapo timu zitakazofungua
dimba ni Kagera vs Kigoma, Mara vs Tabora, Simiyu vs Geita na Mwanza vs
Shinyanga.

Kituo cha Mbeya ambapo mechi zitachezwa viwanja vya Iyunga ni Katavi vs
Njombe, na Ruvuma vs Mbeya. Kituo cha Pwani ni Ilala vs Kaskazini Unguja, na
Lindi vs Pwani.

Ufunguzi katika kituo cha Arusha ambapo mechi zake zitachezwa Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta AMri Abeid ni Manyara vs Kilimanjaro, na Arusha vs
Singida.

Uwanja wa Jamhuri ambapo utatumika kwa mechi za kituo cha Morogoro, Tanga
itacheza na Dodoma wakati Morogoro itaumana na Temeke. Mjini Zanibar kwenye
Uwanja wa Chuo cha Amaan ni kati ya Kaskazini Pemba na Mjini Magharibi, na Kusini
Pemba dhidi ya Kusini Unguja.

YANGA, COASTAL ZAINGIZA MIL 152/-


Mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa
jana (Agosti 28 mwaka huu) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh.
152,296,000.
 
Watazamaji 26,137 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 14 ya VPL msimu
wa 2013/2014 iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.
 
Viingilio katika mechi hiyo vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000
huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 36,947,427.45 wakati Kodi ya Ongezeko la
Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 23,231,593.22.
 
Mgawo mwingine ni asilimia 15 ya uwanja sh. 18,786,827.52, tiketi sh. 3,818,890,
gharama za mechi sh. 11,272,096.51, Kamati ya Ligi sh. 11,272,096.51, Mfuko wa
Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 5,636,048.26 na Chama cha Mpira wa
Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 4,383,593.09.

YANGA YABANWA, MABOMU YARINDIMA


MABINGWA watetezi Yanga jana walilazimishwa kutoka sare ya bao 1-1 na Coastal Union katika mechi ya ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga itabidi ijilaumu kwa kushindwa kutoka uwanjani na ushindi kwani ilikuwa ikiongoza kwa bao 1-0 hadi dakika ya 87 wakati Coastal Union ilipopata adhabu ya penalti na kusawazisha.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbagu aliifungia Yanga bao la kuongoza dakika ya 67 kwa shuti kali baada ya kupokea pasi kutoka kwa beki David Luhende.

Coastal ilisawazisha kwa njia ya penalti kwa bao lililofungwa na Jerry Santo baada ya kutokea madhambi kwenye lango la Yanga.

Katika mchezo huo, mwamuzi Martine Saanya wa Pwani aliwatoa nje kwa kadi nyekundu Simon Msuva wa Yanga na Crispine Odula dakika ya 73 kwa mchezo mbaya.

Licha ya timu zote mbili kuchuana vikali dakika 45 za kipindi cha kwanza, hakuna iliyoweza kupata bao. Kila timu ilipata nafasi nzuri za kufunga, lakini umaliziaji mbovu ulikuwa kikwazo.

Coastal ilianza mchezo kwa kasi dakika ya kwanza baada ya Uhuru Selemani, kuchomoka na mpira na kupiga krosi iliyoshindwa kuunganishwa na Christipine Odula aliyepiga shuti nje.

Yanga ilijibu shambulizi hilo dakika ya nane lakini Msuva alishindwa kufunga baada ya kupiga mpira wa kichwa dhaifu licha ya kupata pasi nzuri ya kiungo, Salum Telela.

Haruna Moshi 'Boban' alishindwa kuipa Coastal Union bao dakika ya 67 baada ya kuzembea na mpira akiwa ndani ya eneo la hatari kabla ya mabeki wa Yanga kuokoa hatari.

Dakika ya 69 Deo Lyanga wa Coastal Union alishindwa kufunga baada ya kupiga shuti juu.
Mbali na kutoa kadi nyekundu, Saanya aliwaonya kwa kadi za njano wachezaji Kavumbagu wa Yanga na beki Juma Saidi 'Nyoso' wa Coastal kwa mchezo wa rafu.

Baada ya pambano hilo kumalizika, mashabiki wa Yanga walizingira eneo la mlango wa kuingilia uwanjani wakitaka kumpiga mwamuzi Saanya. Pia walirusha mawe kwenye basi lililowabeba wachezaji wa Coastal Union na kusababisha mchezaji mmoja ajeruhiwe kichwa.

Polisi walilazimika kufyatua mabomu ya machozi kuwatawanya mashabiki hao.

Yanga: Ali Mustapha, Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub, Mbuyu Twite, Salum Telela/Hamis Thabit, Simon Msuva, Frank Domayo, Didier  Kavumbagu, Jerry Tegete/Hussein Javu, Haruna Niyonzima.

Coastal:  Shaaban Kado,  Juma Hamad, Abdi Banda, Marcus  Ndeheli, Juma Nyoso, Jerry Santo, Uhuru Selemani/ Selemani Kassim, Christipine Odula, Yayo Tutimba, Haruna Moshi na Danny Lyanga.

SIMBA YACHANUA, AZAM YAUANa Shaban Mdoe, Arusha

SIMBA jana ilivuna pointi tatu za kwanza katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuichapa JKT Oljoro bao 1-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.

Ushindi huo ulileta ahueni kubwa kwa mashabiki wa Simba, kufuatia kulazimishwa kutoka sare ya mabao 2-2 na Rhino Rangers katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa mjini Tabora.

Kwa upande wa JKT Oljoro, kipigo hicho kilikuwa cha pili baada ya kuchapwa mabao 2-0 na Coastal Union kwenye uwanja huo wiki iliyopita.

Katika mechi hiyo, Simba iliwachezesha kwa mara ya kwanza beki Gilbert Kaze na mshambuliaji Hamisi Tambwe kutoka Burundi, ambao walishindwa kucheza mechi ya awali kutokana na kukosa hati za uhamisho wa kimataifa na vibali vya kufanyakazi nchini.

Kaze alicheza vizuri kwa kushirikiana na Joseph Owino kwenye nafasi ya ulinzi wa kati, lakini Tambwe alishindwa kuonyesha cheche zake kutokana na kukosa nafasi mbili nzuri za kufunga mabao.

Bao pekee na la ushindi la Simba lilifungwa na mshambuliaji Haruna Chanongo dakika ya 34 kwa shuti la umbali wa mita 25 lililotinga moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa Shaibu Issa wa JKT Oljoro akiwa hana la kufanya.

Kabla ya kufunga bao hilo, Chanongo aliunasa mpira kutoka katikati ya uwanja na kusogea nao karibu na lango la JKT Oljoro. Kipa Shaibu hakuhangaika kuufuata mpira akidhani ungetoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0.

JKT Olojoro ilipata adhabu ya penalti dakika ya 50 baada ya Issa Kandulu kuchezewa rafu na beki Joseph Owino ndani ya eneo la hatari. Hata hivyo, shuti la Babu Ally lilipanguliwa na kipa Abel Dhaira wa Simba.

Babu alipata nafasi nyingine nzuri ya kuifungia bao JKT Oljoro dakika ya 58 alipopewa pasi ndani ya eneo la hatari la Simba na kubaki ana kwa ana na kipa Dhaira, lakini shuti lake lilikwenda moja kwa moja mikononi mwa kipa huyo.

Simba: Abel Dhaira, Nasoro Masoud 'Cholo', Idrisa Rashid, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Abdulrahim Humud, Betram Mombeki, Hamisi Tambwe, Haruna Chanongo.

JKT Oljoro: Shaibu Issa, Yusuf Machogote, Napho Zuberi, Nurdin Mohamed, Shaibu Nayopa,Babu Ally, Swalehe Iddi, Hamisi Swalehe, Amri Omary, Sabri Ally, Esau Sani.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Mbeya City na Ruvu Shooting zilishindwa kutambiana baada ya kutoka sare ya bao 1-1.

Mbeya City ilikuwa ya kwanza kupata bao  dakika ya saba lililofungwa na Paul Nongwa baada ya kuwazidi maarifa mabeki wa Ruvu Shooting.Shaban Suzan aliisawazishia Ruvu Shooting dakika ya 25 baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la Mbeya City.

Bao la pili na la ushindi la Mbeya City lilifungwa na mkongwe Steven Mazanda dakika ya 90 kwa kiki kali ya chini iliyotinga moja kwa moja na kuamsha shangwe kwa wenyeji.

Azam FC ilitoka uwanjani kifua mbele dhidi ya Rhino Rangers baada ya kuichapa mabao 2-0 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

ETO'O HUYOOO CHELSEALONDON, England
KOCHA Mkuu wa Chelsea, Jose Mourinho ameamua kuongeza kasi ya kumsajili mshambuliaji, Samuel Eto'o kutoka klabu ya Anzhi Makhachkala ya Russia.

Mourinho ameamua kumuongezea kasi baada ya mipango yake ya kumnasa mshambuliaji, Wayne Rooney kutoka Manchester United kukwama.

Kocha huyo kutoka Ureno amefikia uamuzi huo baada ya saa 48 alizotoa kwa Rooney, akimtaka aamue moja, kumalizika bila mchezaji huyo kutoa tamko lolote.

Mourinho alitoa saa 48 kwa Rooney ili aamue iwapo atabaki Manchester United ama atatua Chelsea.
Chelsea iliwasilisha ofa mara mbili kwa Manchester United ikitaka kumsajili Rooney, lakini mashetani hao wekundu wamekuwa wakigoma kumuuza mchezaji huyo.

Awali, Rooney alionyesha nia ya kutaka kuondoka Manchester United baada ya Kocha David Moyes kusema, chaguo lake la kwanza katika nafasi ya mshambuliaji wa kati ni Van Persie.

Mourinho amesema atakamilisha usajili wa mshambuliaji huyo wa Anzhi Makhachkala ndani ya saa 24 zijazo ili kujenga upya safu yake ya ushambuliaji.

Chelsea tayari imemsajili winga, Willian kutoka Anzhi na Eto'o ni mchezaji wa pili kufuata baada ya klabu hiyo ya Russia kukumbwa na mzozo wa kimasilahi.

Habari za awali, zimedokeza kuwa Eto'o anaweza kutia saini mkataba wa mwaka mmoja.
Nguli huyo aliwahi kufanya kazi na Mourinho katika klabu ya Inter Milan. Pia amewahi kuzitumikia klabu za Mallorca na Barcelona za Hispania.

GURUMO: MUZIKI WA KIZAZI KIPYA UNALIPA KULIKO DANSIMWANAMUZIKI mkongwe wa bendi ya muziki wa dansi ya Msondo Ngoma, Muhidin Gurumo, ametangaza kustaafu kazi ya muziki, aliyoifanya kwa miaka 53.

Gurumo (73), alitangaza uamuzi huo Agosti 22, mwaka huu, alipozungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO), mjini Dar es Salaam.

Mkongwe huyo wa muziki alisema ameamua kustaafu kutokana na umri wake mkubwa.
Licha ya kujihusisha na muziki katika sehemu kubwa ya maisha yake, Gurumo alisema hana mafanikio makubwa kimaisha, licha ya kujenga nyumba anayoishi na familia yake, iliyoko Ubungo Makuburi, Dar es Salaam.

Katika kipindi alichopiga muziki katika bendi za NUTA, JUWATA, OTTU na Mlimani Park, Gurumo anasema ametunga nyimbo  zaidi ya 200.

Alijiunga na NUTA 1964 akiwa mmoja wa waanzilishi kabla ya kuhamia Mlimani Park 1978 na Orchestra Safari Sound (OSS) kuanzia 1985 hadi 1990.

Gurumo ana kipaji cha kutunga nyimbo zenye ujumbe kuhusu masuala mbalimbali ya kijamii. Alikuwa gwiji katika uimbaji na jina la Gurumo halikuwa la utani kwa sababu ya kuimba kwa sauti nzito, bali ni jina lake halisi.

Aliposimama jukwaani kuimba katika bendi za Msondo Ngoma, OSS na Mlimani Park Orchestra, mashabiki waliburudika kutokana na sauti yake nzito, ambayo ilikolezwa na nyingine za Hassan Bitchuka, marehemu Moshi William, Thobias Chidumule, hayati Hamisi Juma na Maxi Bushoke.

Katika wimbo wa Kassim aliouimba akiwa Mlimani Park, Gurumo akishirikiana na Hamisi Juma (sasa marehemu), aliimba na kutoa picha halisi ya mlevi wa pombe aliyeanza kufilisika na kubana matumizi, wakati Hamisi aliimba kama mwanamke, aliyezoea kupewa ofa na Gurumo.

“Na mie moja Kassim,” anaimba Hamisi katika wimbo huo.

“Sina hela ya mchezo,” anajibu Gurumo.

Wimbo mwingine uliompa sifa Gurumo ni Celina aliouimba akiwa na Mlimani Park. Katika wimbo huo, Gurumo anasikika akiimba: ‘Na kwa sababu imekuwa hivyo Celina, sioni haja ya kutaka ujiue kwa ajili yangu”. Wimbo huo ulitungwa na marehemu Joseph Mulenga, aliyekuwa akipiga gitaa la solo.

Akiwa OSS, alipata umaarufu kupitia wimbo wa Chatu mkali. Katika wimbo huo, sauti yake nzito inasikika alipoimba: ‘Natoa onyo kwa yeyote anayemchezea chatu ni hatari, atakuwa asipate lolote la manufaa, na ajali imkute bila ya kutegemea, atakuja adhirika ajute na dunia.

Nyimbo zingine, ambazo zinakumbusha kazi ya Gurumo tangu alipojitosa kwenye fani ya muziki ni ‘Salima’, ‘Bwana Abdul’, ‘Dada Fatuma’, ‘Kulima Hadeka’ (umelima bondeni) na ‘Agweti Chole’ (Mwenzangu Twende) zilizoimbwa kwa lugha ya Kizaramo. Alitunga nyimbo hizo alipokuwa Kilwa Jazz.

Gurumo alizaliwa 1940 katika kijiji cha Masaki, Kisarawe mkoani Pwani. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Sungwi na kumaliza darasa la saba 1956. Pia alipata mafunzo ya dini ya Kiislamu katika madrasa ya kijiji alichokuwa akiishi.

Baada ya kumaliza shule, aliamua kujiunga na bendi ya Kilimanjaro Chacha iliyokuwa na maskani Ilala, Dar es Salaam. Alifanya kazi na bendi hiyo hadi 1961 alipojiunga na Rufiji Jazz pia ya Dar es Salaam.

Alidumu na bendi hiyo hadi 1963 alipojiunga na Kilwa Jazz, iliyokuwa maarufu enzi hizo chini ya uongozi wa marehemu Ahmed Kipande. Bendi hiyo ilikuwa na makundi mawili, Kilwa A na B, Gurumo alikuwa kundi B.

Gurumo hakupendezwa na uamuzi wa marehemu Kipande kumuweka katika kundi B, wakati alijiona ana uwezo mkubwa wa kuimba kuliko baadhi ya wanamuziki waliokuwa wakiunda kundi A. Hali hiyo ilimfanya ajiunge na NUTA Jazz 1964.

Bendi hiyo ilikuwa ikiundwa na Jumuia ya Wafanyakazi Tanzania na baadaye ilibadili majina na kuitwa JUWATA na OTTU Jazz. Baada ya jumuia hiyo kujitoa katika kuendesha bendi, ilikabidhi vyombo kwa wanamuziki, ambao waliamua kuibadili jina na kuiita Msondo Ngoma.

Akiwa OTTU hadi Msondo Ngoma, alitunga nyimbo nyingi ukiwemo wa ‘Wosia kwa Watoto’.
Gurumo ndiye muasisi wa mitindo ya muziki ya Msondo, akiwa na NUTA, JUWATA na OTTU Jazz, Sikinde akiwa na Mlimani Park na Ndekule akiwa na OSS, ambayo ilizipatia umaarufu mkubwa bendi hizo.

Mitindo hiyo ya muziki ilitokana na majina ya baadhi ya ngoma za kabila la Wazaramo na huchezwa kama ilivyo ngoma ya Vanga.

Tofauti ni kwamba, wachezaji wa ngoma hizo huvaa mavazi ya asili, wakati wale wa muziki wa dansi huvaa mavazi ya kawaida.

Kabla ya uamuzi wa kustaafu muziki, Gurumo alishauriwa na daktari aliyekuwa akimtibu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam, kujiweka kando na masuala ya muziki baada ya kuugua ugonjwa wa moyo na kulazwa hospitali mara kadhaa.

Ugonjwa wa moyo hutokana na kupungua damu inayoingia kwenye mishipa ya moyo, ambao haukumpata Gurumo kwa sababu ya kuimba.

“Sijapatwa na ugonjwa huu kwa sababu ya kuimba kwa miaka mingi. Baada ya kupata tiba, madaktari walinishauri nipumzike kwa sababu ya umri kubwa mkubwa, siwezi tena kusimama jukwaani kwa muda mrefu na kuimba,” anasema. Alianza kusumbuliwa na maradhi mwaka 2011.

Gurumo ni mmoja wa wanahisa wa bendi ya Msondo. Wengine ni Saidi Mabela, Saidi Kibiriti (meneja), Ramadhani Zahoro, Abdul Ridhiwani, Roman Mng'ande na Huruka Uvuruge.
Wanamuziki hao wanamiliki kiwango sawa cha hisa na malipo yao kwa mwezi ni makubwa ikilinganishwa na waajiriwa.

Hata hivyo, Meneja wa Msondo Ngoma, Saidi Kibiriti, hakuwa tayari kutaja viwango vya malipo wanavyolipana.

Kwa Gurumo, muziki wa dansi, ambao wanamuziki hutumia ala mbalimbali, kama vile magitaa, tumba, ngoma, tarumbeta na vinanda katika kuupamba na kuufanya uwe na mvuto wa aina yake, utatoweka iwapo vituo vya redio na televisheni nchini vitaendelea kuacha kupiga nyimbo hizo.

"Ukifungua televisheni yoyote, kuanzia asubuhi hadi jioni, nyimbo zinazopigwa ni za bongo fleva tu. Huwezi kusikia nyimbo za muziki wa dansi. Hii maana yake ni kwamba, vyombo hivi vinaua muziki wetu makusudi," anasema.

Hata hivyo, Gurumo anasema wapo watunzi na waimbaji wengi wazuri wa nyimbo za muziki wa dansi na anavutiwa na Hassan Bitchuka wa Mlimani Park na Hussein Jumbe wa Talent Band.

Mkongwe huyo anasema muziki wa kizazi kipya, ambao hutengenezwa studio kwa kutumia kompyuta, na  kuimbwa katika miondoko mbalimbali kama vile, hip hop, R&B na Zouk, ukichezwa kwa kurukaruka na kujinyonganyonga mwili,  ni mzuri kwa wakati uliopo, hususan kwa vijana.

Hata hivyo, anasema hauwezi kudumu kwa vile wasanii wanatumia zaidi kompyuta kuutengeneza.
Gurumo anasema wasanii wa muziki huo wanapata mafanikio tofauti na zama zao, kwani hivi sasa sheria ya hatimiliki inawalinda.

Anasema muziki umemwezesha kujuana na kufahamiana na watu wengi, wakiwemo viongozi wa serikali. Anatoa mfano wa Rais Jakaya Kikwete, ambaye alikwenda kumjulia hali alipokuwa amelazwa Muhimbili.

Mke wa mwanamuziki huyo, Pili Kitwana, anasema mumewe ana jina kubwa kimuziki, lakini maisha yake ni ya kawaida. Pili na Gurumo walifunga ndoa mwaka 1967 na wana watoto wanne.

Mpiga gita la solo wa Msondo Ngoma, Mabela, anasema Gurumo ameshiriki kuimba nyimbo na pia kutunga zingine, zikiwemo Shaba imelia, Kilimo cha kufa na kupona, Ikiwa kama hunitaki,  Nimuokoe nani, Heko Mwalimu Nyerere na Baba nipeleke kwa mama.

Kwa mujibu wa Mabela, watunzi wa nyimbo nyingi za bendi hiyo walikuwa yeye, marehemu Joseph Lusungu, Khalfan Mabruki na Hassan Bitchuka.

Kwa upande wake, Bitchuka anasema Gurumo alikuwa kiongozi msikivu na alitoa ushauri kwa wanamuziki wenzake.

"Gurumo hakuwa mtu wa kuchezewa. Kama hujui muziki, hawezi kuwa rafiki yako na kama unaujua, atakuwa rafiki yako mkubwa," anasema.

Bitchuka anasema Gurumo alikuwa kiongozi jasiri, asiyeyumba, mwenye msimamo na alitunga nyimbo nyingi, hususan akiwa bendi za Mlimani Park na OSS.

Kiongozi wa bendi ya Extra Bongo, Ally Choki, anasema Gurumo ni mwanamuziki aliyekuwa makini katika kazi yake.

"Kwa mtu wa umri wake, isingekuwa rahisi kupanda jukwaani hadi sasa na kuimba. Ni wa kupigiwa mfano na vijana wanaochipukia kimuziki," anasema.

Anasema alihamasika kurekodi albamu na Gurumo kutokana na kuvutiwa na uwezo wake kimuziki.
Albamu hiyo ina nyimbo sita, tatu zimetungwa na Gurumo na tatu za Choki. Albamu hiyo inajulikana Choki/Gurumo remix.

Nyimbo za Gurumo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Nipeleke kwa baba, Ikiwa kama hunitaki na Nimuokoea nani.

BONGO FLEVA ALMASI INAYONG'ARISHA VIJANAMUZIKI wa kizazi kipya upo juu ikilinganishwa na muziki wa dansi, kutokana na idadi ya mashabiki wanaohudhuria maonyesho ya muziki huo.

Si hilo tu, hata maisha ya wasanii wa muziki huo ni ya juu ikilinganishwa na ya wa muziki wa dansi.
Utofauti huo unatokana na malipo ya fedha nyingi wanayolipwa kwa kuuza albamu au kufanya onyesho.

Muziki wa kizazi kipya, hutengenezwa studio kwa kutumia kompyuta, hupigwa na kuimbwa katika miondoko mbalimbali kama vile, hip hop, R&B na Zouk na unapendwa zaidi na vijana.  Uliingia nchini miaka ya mwanzoni mwa 1990 muasisi akiwa Saleh Jabir, ambaye kwa sasa anaishi nje ya nchi.

Wasanii wengi wa muziki huo wanamiliki magari ya kifahari, yakiwemo Toyota Land Cruiser, yenye thamani ya mamilioni ya shilingi na wengine wamemudu kujenga nyumba bora za kuishi, ambazo zimejengwa kwa matofali na wengine kuezeka kwa vigae.

Kutokana na malipo ya fedha nyingi wanayolipwa, baadhi wanaishi maisha ya anasa, ya kustarehe kwenye hoteli zenye hadhi ya juu, kama vile Serena au kutembelea kumbi maarufu za burudani kama vile Billicanas na Maisha Club, zilizoko Dar es Salaam.

Wapo wasanii wanaolipwa kati ya sh. milioni moja na sh. milioni 10 kwa onyesho moja, wakati bendi za muziki wa dansi zenye idadi kubwa ya wanamuziki, zinakodiwa kwa kati ya sh. 400,000 na sh. milioni moja kwa onyesho.

Muziki wa dansi, wanamuziki wake hutumia ala mbalimbali, kama vile magitaa, tumba, ngoma, tarumbeta na vinanda katika kuupamba na kuufanya uwe na mvuto wa aina yake. Ni tofauti na bongo fleva.

Zipo baadhi ya bendi ambazo kutokana na kukosa mashabiki, zinalazimika kufanya maonyesho bure kwa mashabiki, kwa kuingia makubaliano maalumu na wamiliki wa kumbi za burudani.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, bendi hulipwa kati ya sh. 50,000 na sh. 200,000 kwa onyesho moja, huku mmiliki wa baa akiongeza bei kwa kila kinywaji ili kufidia malipo anayotoa kwa bendi husika. Utaratibu huu  umelenga kuwaongezea mapato wamiliki wa baa.

Wasanii chipukizi katika muziki wa kizazi kipya, hulipwa kati ya sh. 100,000 na sh. 300,000. Malipo hayo bado ni makubwa ikilinganishwa na yale ya bendi za muziki wa dansi.

Si hilo tu, wanamuziki wa taarab, ambao ni maarufu kwa mashairi na mipigo ya kinanda, waimbaji wakijimwaya kwa kutikisa miili yao, pia wanalipwa kiasi kikubwa cha fedha ikilinganishwa na wale wa muziki wa dansi.

Baadhi ya vikundi maarufu vya muziki wa taarab, kama vile Jahazi vimekuwa vikilipwa kati ya sh. milioni moja na sh. milioni 1.5 kwa onyesho moja, wakati vikundi vinavyochipukia hulipwa kati ya sh. 600,000 na sh. 800,000.

Msanii nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' ndiye anayeongoza kwa kulipwa fedha nyingi kwa kila onyesho. Msanii huyo amekuwa akilipwa dola za Marekani 10,000 (sh. milioni 16) anapofanya onyesho nje ya nchi.

Diamond anasema katika baadhi ya nchi, kiwango cha malipo kwa kila onyesho ni kati ya dola 15,000 (sh. milioni 24) na 25,000 (sh. milioni 42).

"Sifanyi shoo nje ya nchi chini ya dola 10,000. Katika nchi kama vile Muungano wa Falme za Kiarabu (UAE), kiwango changu ni dola 25,000. Wakati mwingine nalipwa hadi dola 30,000," anasema.

Diamond anasema kwa nchi kama vile Comoro, ambako alikwenda kufanya onyesho hivi karibuni, malipo kwa onyesho yalikuwa dola 25,000 (sh. milioni 42).

Hata hivyo, Diamond anasema wakati mwingine amekuwa akilipwa zaidi ya anavyotarajia, akitoa mfano wa Rwanda, ambako promota aliyemwalika alimlipa sh. milioni 180.

"Nina msimamo, ninapoalikwa nje ni lazima nifuatane na wacheza shoo wangu," anasema.
Diamond amezaliwa 1986 mkoani Dar es Salaam. Amesoma katika Shule ya Msingi Olympio na sekondari ya Loyola. Amehitimu kidato cha sita 2006.

Kabla ya kujitosa katika muziki, Diamond anasema aliwahi kufanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza mikoba kilichoko Mikocheni, Dar es Salaam kati ya 2008 na 2009 na kulipwa mshahara wa sh. 2,000 kwa saa nane.

Anasema mshahara huo ulikuwa mdogo, haukuweza kukidhi mahitaji yake ya kila siku kwa sababu alikuwa akitumia sh. 1,000 kwa nauli na sh. 1,000 kwa ajili ya chakula.

Licha ya malipo makubwa ya fedha katika maonyesho yake nje na ndani ya nchi, Diamond anasema hajawahi kulipa kodi kwa kuwa hakuna utaratibu wa kuwawezesha wasanii kulipa kodi.

Anasema anatarajia kuanza kulipa kodi kutokana na mauzo ya albamu baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuamua kuweka stempu kwenye kila kazi ya msanii.

Diamond anasema ana vitega uchumi ambavyo ni hoteli, nyumba, viwanja, magari na pikipiki anazozitumia kwa biashara. Anasema mali hizo zina thamani ya sh. bilioni moja.

Mratibu wa maonyesho katika ukumbi wa Dar Live, ulioko Mbagala, Dar es Salaam, Luqman Maloto, anasema wasanii wa muziki wa kizazi kipya ndio wanaoongoza kwa kupata idadi kubwa ya mashabiki kila wanapofanya maonyesho kwenye ukumbi huo.

Hata hivyo, Luqman anasema wingi wa mashabiki unategemea umaarufu wa wasanii husika na aina ya maonyesho yanayoandaliwa.

Amewataja wasanii wenye idadi kubwa ya mashabiki kuwa, Naseeb Abdul 'Diamond', Ally Kiba, Joseph Haule 'Profesa Jay', Ommy Dimples na kundi la TMK Wanaume Family linalopiga muziki wa kizazi kipya

"Kuna wakati tuliwahi kuandaa maonyesho ya usiku wa hip hop, usiku wa Sugu na old is gold ya bongo fleva, tulipata idadi kubwa ya mashabiki kuliko maonyesho mengine kama vile ya muziki wa dansi na taarab," anasema.

Usiku wa hip hop ni onyesho lililowahusisha wasanii wa muziki wa kizazi kipya wanaopiga aina hiyo ya muziki, usiku wa sugu ni onyesho lililomuhusisha msanii Joseph Mbilinyi, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Sugu (kwa sasa ni mbunge wa Mbeya Mjini kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na old is gold ya bongo fleva ni onyesho lililohusisha nyimbo za zamani za muziki wa kizazi kipya.

Maloto anasema bendi za muziki wa dansi hazina mashabiki wengi katika ukumbi huo. Anasema wamewahi kuandaa maonyesho ya bendi kama vile Extra Bongo, Mashujaa, Twanga Pepeta na FM Academia, lakini idadi ya mashabiki haikuwa kubwa.

Anasema hilo linatokana na mashabiki wengi wanaofika kwenye ukumbi huo ulioko Mbagala Zakhem, wilayani Temeke, Dar es Salaam, kuwa vijana, ambao wanaushabikia zaidi muziki wa kizazi kipya.

Mratibu huyo anasema vikundi vya muziki wa taarab vinashika nafasi ya pili kwa kuwa na idadi kubwa ya mashabiki, hususan kikundi cha Jahazi, ambacho hakijawahi kupata mashabiki wachache.

"Kuna wakati tuliwahi kuandaa onyesho la Mitikisiko ya Pwani, ambalo lilivihusisha vikundi vingi vya taarab. Onyesho hili lilivunja rekodi ya wingi wa mashabiki," anasema.

Meneja Uhusiano wa Kampuni ya Simu za Mkononi ya Airtel, Jackson Mmbando, anasema wamekuwa wakiwatumia wasanii wa aina zote katika kutangaza bidhaa zao kwa kuzingatia mazingira ya maeneo husika.

Hata hivyo, Mmbando anasema wamekuwa wakiwatumia zaidi wasanii wa muziki wa kizazi kipya, kwa kuwa wana mashabiki wengi.

"Hatubagui tunapofanya maonyesho kutangaza bidhaa zetu, tunawatumia wasanii wa aina zote, iwe muziki wa kizazi kipya au bendi za muziki wa dansi, lakini hilo linazingatia sehemu tunakofanya maonyesho hayo na watu wanapenda nini," anasema.

Mmbando anasema mara nyingi wamekuwa wakifanya utafiti wa maeneo wanakokwenda kufanya maonyesho ili kujua wakazi wa maeneo hayo wanataka nini.

Meneja wa hoteli ya Koyanga, iliyoko Kiwalani, Dar es Salaam, Twaha Mohamed, anasema vikundi vya taarabu ndivyo vinavyoongoza kwa kupata mashabiki kila vinapofanya maonyesho kwenye hoteli hiyo.

Wednesday, August 28, 2013

TAMU, CHUNGU YA MUZIKI WA KIZAZI KIPYA

Banana Zorro

Barnaba Elias
Pauline Zongo
 
MWANZONI mwa miaka ya 1990, fani ya muziki nchini ilipitia mabadiliko makubwa baada ya kuibuka muziki wa kizazi kipya, maarufu Bongo Fleva.

Muziki huu ulipachikwa jina la kizazi kipya kutokana na kupigwa zaidi na vijana ambao hawana elimu ya muziki au utaalamu wa kutumua ala za muziki. Ni muziki unaotengenezwa studio kwa kutumia kompyuta yenye programu maalumu ya kutengeneza midundo ya ala mbalimbali za muziki.

Asili ya muziki wa kizazi kipya ni barani Ulaya, ambako baadhi ya wasanii kwa kukwepa gharama za kurekodi nyimbo kwa kutumia ala za muziki, waliamua kutumia kompyuta. Vijana wa Kitanzania waliiga mtindo huo na kuufanya muziki huo uwe maarufu kuliko mitindo mingine.

Kazi kubwa inayofanywa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya ni kutunga mashairi na kwenda kwa mtayarishaji wa muziki, ambaye hutengeneza mipigo ya ala mbalimbali kwa kutumia kompyuta.

Wakati mwingine, watayarishaji wa muziki hutengeneza mipigo ya wimbo na kuwapatia wasanii ili wautengenezee mashairi na kuimba.

Muziki wa kizazi kipya hupigwa na kuimbwa katika miondoko mbalimbali kama vile, hip hop (muziki wa kufokafoka), R&B (muziki laini wenye kuchombeza) na Zouk na unapendwa zaidi na vijana. Uliingia nchini miaka ya mwanzoni mwa 1990 muasisi akiwa Saleh Jabir, ambaye kwa sasa anaishi nje ya nchi.

Saleh aliutambulisha muziki huo kwa kufanya maonyesho kwenye kumbi za burudani za mjini Dar es Salaam. Alitumia CD kupiga midundo ya muziki na yeye kushika kipaza sauti na kuimba. Alikuwa na uwezo wa kutunga mashairi yanayoelezea matukio mbalimbali yanayotokea katika jamii.

Kwa sasa yapo mabadiliko makubwa katika muziki huo kutokana na wasanii kutunga nyimbo zinazosisimua na kuamsha hisia, zikielezea masuala mbalimbali. Zipo nyimbo zinazozungumzia mapenzi, ukahaba, wizi, utumiaji wa dawa za kulevya, utumiaji mbaya wa madaraka na siasa.

Muziki huu ni tofauti na uliozoeleka wa dansi, ambao wanamuziki hutumia ala mbalimbali, kama vile magitaa, tumba, ngoma, tarumbeta na vinanda katika kuupamba na kuufanya uwe na mvuto wa aina yake.

Kutokana na muziki huo kuwa na mashabiki wengi, baadhi ya wasanii wanaamini  utadumu kwa muda mrefu, kama ilivyo kwa nyimbo za muziki wa dansi.

Selemani Msindi, maarufu Afande Sele, anasema wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya wanapenda kutengeneza nyimbo kwa kutumia kompyuta kutokana na gharama kubwa za kuwakodi wapiga ala za muziki.

“Dunia hivi sasa ni kama kijiji. Muziki wa kizazi kipya ni matokeo ya mabadiliko yanayotokea duniani. Ni sawa na kusema zamani tulikuwa na magari yanayotumia gia kuanzia moja hadi nne, lakini magari mengi hivi sasa ni automatiki," anasema.

Hata hivyo, Afande Sele anaamini watayarishaji wa muziki ni muhimu zaidi katika kutengeneza nyimbo za msanii au bendi kwa vile kazi yao huchukua takriban asilimia 20 au 30. Anasema mara nyingi kazi ya msanii ni kutunga na kuandika mashairi.

Msanii huyo mwenye maskani mjini Morogoro, anaamini muziki wa kizazi kipya utadumu kwa vile hata baadhi ya nyimbo zilizopigwa miaka saba hadi 10 iliyopita, kama vile wimbo wake wa Darubini Kali, Nikusaidieje wa Profesa Jay na Kamanda wa Daz Nunda bado zinapendwa.

"Wimbo kudumu kwa miaka mingi, inategemea ujumbe wake, upigaji wa ala na vionjo. Zipo nyimbo za baadhi ya bendi za zamani ukizisikiliza hivi sasa hazina mvuto kabisa," anasema.

Kiongozi wa B Band, Banana Zorro, ambaye ni mmoja wa wasanii nyota wa muziki wa kizazi kipya anasema aliamua kupiga muziki wa bendi baada ya kubaini kutegemea mauzo ya CD hakuwezi kumfikisha mbali.

"Faida ya muziki wa bendi ni kwamba, huwezi kutegemea mauzo ya CD. Unaweza kupata maonyesho sehemu mbalimbali ukaingiza fedha, lakini muziki ni muziki, uwe wa bendi au msanii mmoja, inategemea umejipanga vipi katika kuurekodi," anasema Banana.

Anasema wapo watayarishaji hodari katika kutengeneza muziki wa kizazi kipya, ambao wanaweza kumbadilisha msanii akaonekana mzuri na kwamba jambo la msingi ni kwa msanii kuwa mbunifu.

Akifafanua, Banana anasema mtayarishaji bora wa muziki anaweza kutambua kipaji cha msanii na kumwelekeza ni aina gani ya muziki inayomfaa na kumtayarishia nyimbo kulingana na aina hiyo ya muziki, hivyo kuwa utambulisho wake.

Barnaba Elias wa kundi la muziki la Tanzania House of Talent (THT), anasema kupiga muziki wa ala ni jambo muhimu katika kutafuta soko la muziki, lakini si kweli kwamba muziki wa kizazi kipya hauna mvuto.

“Hilo linategemea utunzi wa msanii na utengenezaji wa ala za muziki unaofanywa na mtayarishaji wa muziki," anasema msanii huyo.

Barnaba anasema binafsi aliamua kujifunza kupiga ala za muziki badala ya kutegemea muziki wa studio baada ya kusoma soko la muziki. Anasema muziki wa bendi ni mzuri na una mvuto zaidi ikilinganishwa na ule wa kompyuta.

"Muziki wowote ni mzuri, inategemea kazi yako. Wanaosema muziki wa kizazi kipya hauwezi kudumu wanakosea, ni kwa sababu tangu ulipoanza bado upo na umekuwa ukiipandisha chati Tanzania kimuziki," anasema.

Msanii Lucas Silas 'Dk. Leader' wa mkoani Tanga, anakiri muziki wa kizazi kipya umekusanya wasanii wengi wasio na vipaji, ambao baadhi wamepandikizwa au kujitosa kwenye fani kwa lengo la kupata umaarufu.

Akifafanua kauli yake, Dk. Leader anasema wasanii wasio na vipaji ni wale wasioweza kuimba kwa kufuata funguo za muziki, kwamba wapo ambao badala ya kuimba wanapayuka.
Ametaja aina nyingine ya wasanii wa aina hii kuwa ni wenye uwezo kifedha na wanalazimisha kuimba ili wapate umaarufu.

"Wengi wanatafuta pesa kwa sababu hawajui ala za muziki. Wakiimba ‘laivu’ inakuwa kichekesho. Teknolojia imerahisisha, lakini inatumaliza," anasema.

Msanii huyo anasema wasanii wengi wa muziki wa kizazi kipya wanashindwa kuimba wanapokuwa jukwaani (laivu) kutokana na kutokuwa na uzoefu huo na kwamba, muziki wa kompyuta umerahisisha kazi kwa sababu ni rahisi kwa msanii yeyote mwenye uwezo wa kuandika mashairi.

Msanii wa zamani wa kundi la Wagosi wa Kaya, John Evans 'Dk John' mwenye makazi mjini Tanga, anaamini muziki wa kizazi kipya umelenga biashara na ni wa kuiga kutoka kwa wasanii wa Marekani, ambao waliamua kutumia kompyuta ili kurahisisha kazi.

"Wasanii wengi hukimbilia kuandika mashairi na kuingia studio bila kuwa na ufahamu wowote kuhusu muziki. Tunapaswa kuwa wabunifu. Ndiyo sababu katika nyimbo zangu nimekuwa nikitumia zaidi ala za asili na kuimba kwa lafudhi ya Kidigo ili kuongeza mvuto," anasema.

Hata hivyo, Dk. John anasema wapo wanaoingia katika muziki kwa lengo la kujifunza na kuonyesha wanachokijua na kukipenda kwa mashabiki wa fani hiyo.

Licha ya kuwepo kwa kasoro hizo, Dk. John anaamini muziki huo utadumu kwa sababu ni biashara inayowaingizia baadhi yao mamilioni ya shilingi, ikiwa ni pamoja na malipo ya miito ya simu. Malipo hayo hufanywa na kampuni za simu kwa wasanii, ambao nyimbo zao hutumiwa na wateja kama miito ya simu.

Msanii nyota wa zamani wa kundi la East Coast, Pauline Zongo, anasema aliamua kuachana na muziki wa kizazi kipya na kujitosa kwenye dansi kwa lengo la kupima uwezo wake na kujiendeleza kimuziki.

Pauline anasema uamuzi wake wa kujiunga na bendi ya TOT Plus ulilenga kukuza kipaji chake cha muziki na pia kuwaonyesha mashabiki kwamba ana uwezo mkubwa katika fani hiyo.

"Huwezi kuwa mwanamuziki mzuri kama hujui kupiga ala yoyote ya muziki," anasema mwanamama huyo, ambaye ana uwezo wa kupiga gita, ngoma na kinanda.

Mwanamama huyo anasema hakujifunza muziki kutoka kwa mtu yeyote. Anasema kuna siku alilala akaota ndoto anapiga gita, ngoma, kinanda na kuimba.

Kwa mujibu wa Pauline, alipozinduka usingizini, aliamua kutimiza ndoto yake.
Pauline anasema awali, aliamua kujitosa katika muziki wa kizazi kipya baada ya kujitambua kwamba ana kipaji cha kuimba. Anakiri muziki huo unafanana na wa dansi, lakini unatofautiana katika uchezaji.

Muziki wa dansi huchezwa kwa kutingisha viungo vya mwili wakati wa kizazi kipya huchezwa kwa kuinyonganyonga mwili na wakati mwingine huongezewa nakshi kwa kuruka sarakasi.

Pauline anasema hivi sasa anaweza kupiga muziki wa miondoko tofauti, ikiwemo reggae, dansi na ragamuffin. Muziki wa reggae na ragamuffin huchezwa kwa kurukaruka.

"Kuna umuhimu kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya kujifunza kupiga ala za muziki, badala ya kutegemea muziki unaotengenezwa kwenye kompyuta," anasema mwimbaji huyo wa zamani wa kundi la Tanzania One Theatre (TOT).

Pauline anasema ameamua kutoa ushauri huo ili wasanii wa fani hiyo wawe na uwezo wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja, badala ya kutegemea kitu kimoja.
Anasema kubadilika kwa wasanii hakuwezi kuzifanya studio za kurekodi muziki zife au ajira hiyo kukoma.

Mtayarishaji wa muziki wa kizazi kipya, Ally Mohamed 'Baucha' anaamini gharama za kurekodi nyimbo studio kwa kutumia ala za muziki ndizo zinazowafanya wasanii wengi wakimbilie kurekodi nyimbo kwa kutumia kompyuta.

Gharama ya kurekodi wimbo  kwa kutumia kompyuta inatofautiana kati ya watayarishaji, ambapo kiwango cha chini ni sh. 100,000, tofauti na kutumia ala, ambapo gharama ziko juu kwani wapiga ala pia huhitaji kulipwa, hivyo kuwa zaidi ya sh. 500,000.

"Tatizo pekee kwa sisi watayarishaji wa muziki ni ubunifu wa mipigo ya ala. Kama mtayarishaji wa muziki atatengeneza ala nzuri, muziki utadumu kwa muda mrefu. Si watayarishaji wote wamesoma au wana ujuzi huo," anasema.

Baucha anasema kazi kubwa ya mtayarishaji wa muziki ni kwenye kuchanganya mipigo ya ala za muziki na sauti kwa lengo la kuunogesha wimbo. Anasema kinyume cha hilo, kazi ya msanii haiwezi kuwa na mvuto.

ATHUMANI IDDI 'CHUJI': YANGA MWENDO MDUNDOKIUNGO nyota wa klabu ya Yanga, Athumani Iddi Chuji amesema kikosi cha sasa cha timu hiyo kinatisha kutokana na kukamilika katika kila idara.

Akizungumza na Burudani mjini Dar es Salaam juzi, Chuji alisema kutokana na kukamilika huko, Yanga ina uwezo mkubwa wa kutetea ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.

"Mwendo wetu msimu huu ni wa ushindi tu, hakuna sare. Hatuna wasiwasi na ubingwa,"alisema kiungo huyo aliyewahi kuichezea Simba.

Chuji ameusifu uongozi wa Yanga kwa kutoa kipaumbele kwa vijana katika usajili wa msimu huu na kuongeza kuwa, watakuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo katika miaka michache ijayo.

Alisema katika mechi yao ya ufunguzi wa ligi dhidi ya Azam, kipa Ally Mustafa 'Barthez' na beki Kevin Yondan waliumia na kushindwa kuendelea na mchezo, lakini vijana walioingia badala yao waliweza kuziba vyema mapengo yao.

"Kusema kweli, timu ina mabadiliko makubwa. Karibu kila namba kuna wachezaji zaidi ya wawili.
Hakuna mapungufu. Yanga ya msimu huu ni bora zaidi kuliko ya msimu uliopita,"alisema.

Kiungo huyo wa Taifa Stars alisema viwango vya baadhi ya wachezaji vimepanda ikilinganishwa na msimu uliopita na alitoa mfano wa Didier Kavumbagu kutoka Burundi, ambaye aling'ara katika mechi dhidi ya Azam na Ashanti.

Chuji alisema pia kuwa kurejea kwa mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Mrisho Ngasa kutaiongezea nguvu zaidi Yanga kutokana na uwezo na uzoefu wake katika ligi na michuano ya kimataifa.

Hata hivyo, Ngasa amezuiwa kucheza mechi sita za ligi hiyo baada ya kubainika kuwa, alitia saini mkataba wa kuichezea Simba kwa mwaka mmoja wakati alipokuwa akiichezea timu hiyo kwa mkopo kutoka Azam.

"Ngasa ni mchezaji mzuri sana. Akicheza pamoja na akina Domayo, Niyonzima, Kavumbagu na Tegete, safu yetu ya ushambuliaji itakuwa tishio,"alisisitiza.

Chuji amemsifu kocha mkuu wa timu hiyo, Ernie Brandts kwa kutoa mafunzo mazuri kwa wachezaji wake na kuongeza kuwa, wamekuwa wakiyafuata vyema ili kuhakikisha wanatangaza ubingwa mapema.

Alisema kocha huyo amekuwa akipendwa na wachezaji, ambao wamekuwa wakifika mazoezini mapema na hakujawahi kutokea mgogoro wowote kati yao.

"Kocha wetu ni mzuri. Kungekuwa na tatizo, nadhani asingeelewana na wachezaji na wangeweza kufanya mgomo, lakini tunakwenda naye vizuri," aliongeza.

Chuji pia alimsifu kocha msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro kwa kuwaweka fiti wachezaji kutokana na kuwapa mazoezi ya kuwajaza stamina kwa saa tatu kila simu.

Licha ya Yanga kuanza ligi hiyo kwa kishindo kwa kuifunga Ashanti mabao 5-1 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wiki iliyopita, Chuji alisema timu hiyo ni nzuri.

"Sidhani kama kuna timu mbaya msimu huu. Hata hao Ashanti tumewafunga kwa sababu ya ugeni wao katika ligi, lakini ni timu nzuri. Nadhani baada ya mechi tatu zijazo watabadilika,"alisema.

Alizitaja timu zinazoweza kutoa upinzani mkali kwa Yanga msimu huu kuwa ni pamoja na watani wao wa jadi, Simba, Azam, Mtibwa Sugar na Coastal Union.

Kwa sasa Chuji ni majeruhi baada ya kuumia kifundo cha mguu katika mechi ya ufunguzi wa ligi hiyo dhidi ya Ashanti. Chuji alishindwa kumaliza mchezo huo na nafasi yake ilichukuliwa na Frank Domayo.

Kiungo huyo kwa sasa amekuwa akifanya mazoezi mepesi na daktari amemshauri aendelee kupumzika ili apone sawasawa kabla ya kuanza mazoezi na wenzake.

Chuji hakuweza kuichezea Yanga katika mechi nyingine ya ligi hiyo dhidi ya JKT Oljoro ya Arusha iliyochezwa jana mjini Dar es Salaam na huenda akakosa mechi zingine mbili zijazo.

Hata hivyo, Chuji anaamini kuwa atakuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars kitakachocheza mechi ya mwisho ya michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa mwezi ujao mjini Banjui.

SERIKALI YAVALIA NJUGA WIZI WA KAZI ZA WASANII


NA HAMIS SHIMYE, DODOMA

SERIKALI imesema imeshaunda tume ambayo imeazimia kuhakikisha inatatua tatizo la usambazaji wa nyimbo za msanii katika simu za mkononi.

Imesema maazimio ya tume hiyo ni kukiagiza Chama cha Hati Miliki Tanzania (COSOTA), kuzichukulia hatua kampuni za simu za mkononi nchini, ambazo zinawalipa wasanii chini ya kiwango kilichowekwa kisheria na chama hicho.

Hayo yalisemwa jana bungeni mjini hapa na Naibu Waziri wa Teknolojia, Sayansi na Mawasiliano, Januari Makamba, alipokuwa akijibu swali Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA), aliyetaka kujua ni lini serikali itatunga kanuni za kuweka wazi mapato ya kazi za wasanii kwa kampuni za simu.

Alisema serikali inatambua changamboto mbalimbali anazokutana nazo msanii ndiyo sabau iko nao bega kwa bega kuhakikisha inatatua matatizo yao, hasa katika suala la usambazaji wa kazi za wasanii kupitia simu za mkononi.

"Wizara ilikutana na wadau na kuunda kamati iliyoshirikisha Wizara ya Viwanda na Biashara, COSOTA, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), kampuni za simu na wawakilishi wa wasanii. Lengo lilikuwa ni kupata uvumbuzi wa tatizo,''alisema Makamba.

Makamba, alisema tume hiyo iliamua kutekeleza mambo mbali mbali ikiwemo malipo ya msanii yawe siyo chini ya kiwango kinachotajwa kwenye sheria ya COSOTA na isiwe kwa mawakala ili kuondoa dhuluma kwa wasanii.

Alisema pia tume hiyo, imepanga kuweka utaratibu wa kufanyia marekebisho sheria za COSOTA, BASATA na TCRA ili ziwe pamoja na kuondoa mwingiliano wa kimajukumu katika utekelezaji na uondoaji wa dhuluma kwa wasanii.

“Wizara yangu inaendelea kufuatilia utekelezaji wa maazimio haya, pia Wizara ya Viwanda na Biashara iko kwenye mchakato wa kuweka utaratibu wa wazi na haki wa kuwezesha wasanii kunufaika na kazi zao zinapopigwa kwenye radio na televisheni,” alisema Makamba.

Hata hivyo, Makamba alisema hakuna taarifa za pato ghafi lililotokana na biashara ya kuuza milio ya simu kwa kuwa mauzo ya kampuni za simu hutokana na huduma mbalimbali kama ujumbe mfupi,  M Pesa, vifurushi vya 'Internet' ambayo huchanganywa kama pato la jumla.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini-CHADEMA, Joseph Mbilinyi, alisema serikali ifanye kila linalowezekana kuwasaidia wasanii na kuiomba iunde tume huru itakayosaidia kuondoa tatizo la wizi wa kazi zao.

Makamba alisema Rais Jakaya Kikwete na serikali yake wana dhamira ya kusaidia wasanii ndiyo maana ilitoa kiasi sh. milioni 16 kwa ajili ya kufanyika kwa utafiti wa wizi wa kazi za wasanii. Utafiti huo ulifanywa na Chuo Kikuu cha  Dar es Salaam (UDSM).

PINGAMIZI ZA WAGOMBEA TFF ZATUPWA


Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imeshindwa kusikiliza pingamizi mbili zilizowasilishwa mbele yake dhidi ya waombaji uongozi wawili baada ya kukosa sifa kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za TFF.

Kwa mujibu wa Ibara ya 11 (3) ya Kanuni za Uchaguzi za TFF, pingamizi ni lazima iwekwe na mwanachama wa TFF (vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu za Ligi Kuu) au kiongozi wa kuchaguliwa wa TFF.

Pia pingamizi yoyote ni lazima iwe kwa maandishi ikieleza wazi sababu za pingamizi pamoja ushahidi wa kuunga mkono pingamizi hilo, jina kamili, anuani ya kudumu na kusainiwa na mweka pingamizi au Mwenyekiti/Katibu  wa mwanachama husika.

Pingamizi hizo ziliwasilishwa na Shamsi Rashid Kazumari na Samwel Nyalla dhidi ya Wallace John Karia anayeomba kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF na Vedastus Kalwizira Lufano anayeomba kuwania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Mbili ya mikoa ya Mara na Mwanza.

Kwa upande wa Kazumari ambaye alikiri hata kutowahi kuiona Katiba ya TFF pamoja na Kanuni za Uchaguzi, pingamizi lake halikusikilizwa kwa vile si mwanachama wa TFF wala kiongozi wa kuchaguliwa wa TFF. Wakati pingamizi la Nyalla halikusikilizwa kwa vile hakukuwa na ushahidi wowote uliowasilishwa, hivyo kushindwa kukidhi matakwa ya Ibara ya 11(3) ya kanuni husika.

 Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF

Tuesday, August 27, 2013

MAANDALIZI UCHAGUZI MKUU TFF YAPAMBA MOTO, KARIA APINGWA


Sekretarieti ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) inaendelea na maandalizi ya Mkutano Mkuu wa Uchaguzi utakaofanyika Oktoba 26 na 27 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Awali mkutano wa uchaguzi ulikuwa ufanyike Februari 23 na 24 mwaka huu lakini tukauahirisha kusubiri maelekezo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), hivyo tayari wajumbe wana taarifa rasmi kuhusu mkutano huo.

Orodha ya wajumbe iliyotumwa awali kwa ajili ya Mkutano tunayo, isipokuwa kama kuna wanachama wetu wana mabadiliko ya majina ya wajumbe watakaohudhuria wanatakiwa kutuma majina hayo kabla ya Septemba 30 mwaka huu.

Wanachama wa TFF ni vyama vya mpira wa miguu vya mikoa, vyama shiriki na klabu 14 za Ligi Kuu ya Vodacom.

Wanamichezo wawili walioomba kuwania uongozi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) utakaofanyika Oktoba 27 mwaka huu wamewekewa pingamizi.

Waliopingwa ni Wallace John Karia anayeomba kupitishwa kuwania urais na Vedastus Kalwizira Lufano anayewania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Mbili ambayo ni mikoa ya Mara na Mwanza. Anyempinga Karia ni Shamsi Rashid Kazumari wa Dar es Salaam wakati Lufano anapingwa wa Samwel Nyalla wa Mwanza.

Pamoja na mambo mengine, Kazumari anampinga Karia kwa madai kuwa akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, aliwashawishi wajumbe wenzake kuingia mkataba na Azam Tv wakati akijua kamati hiyo ni ya muda, hivyo haina nguvu za kisheria kusaini mkataba huo.

Naye Nyalla ambaye pia ni mmoja wa wanamichezo waliojitokeza kuwania ujumbe kupitia Kanda hiyo anampinga Lufano kwa madai hana uzoefu wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.

Kamati ya Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake Hamidu Mbezeleni itakutana kesho (Agosti 28 mwaka huu) saa 4 kamili asubuhi kusikiliza pingamizi hizo ambapo wawekaji pingamizi na waliopingwa wanatakiwa kufika wenyewe ndani ya muda kwa vile uwakilishi hautakiwi.

KIVUMBI TAIFA KESHO, YANGA KUVAANA NA COASTAL UNIONLigi Kuu ya Vodacom (VPL) inaingia raundi ya pili kesho (Agosti 24 mwaka huu) kwa timu zote 14 kuwa viwanjani huku macho na masikio ya washabiki wengi yakielekezwa kwenye mechi kati ya Yanga na Coastal Union.

Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni kwa kiingilio cha sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro ndiye atakayepuliza filimbi wakati Kamishna atakuwa Omari Walii kutoka Arusha.

Mtibwa Sugar itaikaribisha Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro wakati Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora utakuwa mwenyeji wa pambano kati ya wenyeji Rhino Rangers na Azam.

Vumbi lingine litatimka kwenye Uwanja wa Mabatini ulioko Mlandizi mkoani Pwani wakati maafande wa JKT Ruvu watakapokwaruzana na wenzao wa Tanzania Prisons kutoka Mbeya. Mbeya City na Ruvu Shooting zitacheza kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Jiji la Tanga litakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Ashanti United itakayochezwa kwenye Uwanja wa Mkwakwani. Oljoro JKT itakuwa mwenyeji wa Simba kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha.

RATIBA COPA COCA COLA U-15 KUPANGWA KESHORatiba ya michuano ya U15 Copa Coca-Cola ngazi ya kanda mwaka huu itapangwa keshokutwa (Agosti 29 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Michuano hiyo ya kanda itaanza Septemba Mosi mwaka huu wakati mikoa inakumbushwa kuwa inatakiwa iwe imewasilisha usajili wa wachezaji wao kufikia Agosti 28 mwaka huu kupitia email ya TFF ambayo ni tanfootball@tff.or.tz na nakala kwa madadi_salum@ yahoo.com

Pia mikoa inakumbushwa kutowajumuisha wanafunzi wa darasa la saba katika timu zao katika ngazi ya kanda na fainali itakayochezwa Dar es Salaam kuanzia Septemba 7 mwaka huu kwa vile watakuwa katika mitihani ya kumaliza elimu ya msingi. Timu zinatakiwa kufika vituoni Agosti 30 mwaka huu.

Kanda hizo ni Mwanza itakayokuwa na timu za mikoa ya Geita, Kagera, Kigoma, Mara, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Tabora. Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Singida inaunda Kanda ya Arusha.

Zanzibar itakuwa na Kaskazini Pemba, Kusini Pemba na mikoa miwili ya Unguja wakati Kanda ya Dar es Salaam ina Ilala, Kinondoni, Lindi, Mtwara, Temeke na mkoa mmoja wa Unguja.

Kanda ya Mbeya inaundwa na Iringa, Katavi, Mbeya, Njombe, Rukwa na Ruvuma wakati Dodoma, Morogoro, Pwani na Tanga zinaunda Kanda ya Morogoro.

Mwanza itatoa timu nne kucheza hatua ya fainali wakati kanda nyingine za Arusha timu mbili, Zanzibar (2), Mbeya (3) na Kanda ya Morogoro itaingiza timu mbili.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Saturday, August 24, 2013

YANGA YAUA, SIMBA, AZAM ZACHECHEMEAYANGA leo imeanza ligi kuu ya Tanzania Bara kwa kishindo baada ya kuibamiza Ashanti mabao 5-1 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mshambuliaji Jerry Tegete aliibuka shujaa wa Yanga baada ya kuifungia mabao mawili kati ya matano. Mabao mengine yalifungwa na Simon Msuva, Haruna Niyonzima na Nizar Khalfan wakati bao la kujifariji la Ashanti lilifungwa na Shabani Juma.

Katika mechi nyingine ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora, Simba ilibanwa mbavu na wenyeji Rhino Rangers baada ya kulazimishwa kutoka nayo sare ya mabao 2-2.

Mabao yote mawili ya Simba yalifungwa na kiungo mchacharikaji, Jonas Mkude wakati mabao ya Rhino Rangers yalifungwa na Iman Niel na Saad Kipanga.

Katika mechi nyingine zilizochezwa leo, Mtibwa Sugar imelazimishwa sare ya 1-1 na Azam FC kwenye Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro.

Mtibwa ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Juma Luizio dakika ya nne kabla ya Aggrey Morris kuisawazishia Azam kwa penalti dakika ya 19.

JKT Mgambo ilishindwa kutamba kwenye uwanja wake wa nyumbani baada ya kupokea kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa JKT Ruvu, Coastal Union iliichapa JKT Oljoro mabao 2-0 mjini Arusha, Mbeya City ilitoka suluhu na Kagera Sugar mjini Mbeya, Prisons ilipokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa Ruvu Shooting

WACHEZAJI WATANO SIMBA WAPIGWA STOP KUCHEZA LIGI, WAWILI WAZUIWA YANGA


Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imezuia usajili wa wachezaji 37 wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kutokana na usajili wao kuwa na kasoro.

Klabu husika zimetakiwa kurekebisha kasoro hizo kabla ya kuanza kuwatumia wachezaji hao kwenye mechi za VPL ambazo zinaanza leo (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja mbalimbali nchini.

JKT Ruvu Stars inatakiwa kuwafanyia uhamisho (transfer) wachezaji Salum Machaku Salum aliyekuwa Polisi Morogoro na Emmanuel Leonard Swita (Toto Africans). Mgambo Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Mohamed Hussein Neto (Toto Africans), Kulwa Said Manzi (Polisi Morogoro) na Mohamed Ally Samata (African Lyon).

Pia Salum Aziz Gilla anaonekana bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Coastal Union huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa mchezaji mwenyewe, Coastal Union au Mgambo Shooting kama ulivunjwa au umenunulia na klabu anayotaka kuchezea msimu huu.

Tanzania Prisons inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji James Mjinja Magafu kutoka Toto Africans na Six Ally Mwasekaga (Majimaji). Nayo Coastal Union inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Kenneth Abeid Masumbuko kutoka Polisi Morogoro.


Kagera Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Suleiman Kibuta Rajab (Toto Africans), Godfrey Innocent Wambura (Abajalo), Eric Mulera Muliro (Toto Africans), Adam Juma Kingwande (African Lyon) na Peter Gideon Mutabuzi (Toto Africans).

Pia Kagera Sugar imepata Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Kitagenda Hamis Bukenya, lakini bado hana kibali cha kufanyia kazi nchini (work permit).

Kwa upande wa Ruvu Shooting inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Abdul Juma Seif (African Lyon), Lambele Jerome Reuben (Ashanti United), Juma Seif Dion (African Lyon) na Cosmas Ader Lewis (African Lyon).

Oljoro JKT inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Tizzo Charles Chomba kutoka Polisi Morogoro, lakini imekataliwa kumsajili mchezaji Damas Mussa Kugesha wa Mlale JKT kwa kigezo kuwa ni askari na amehamishiwa Arusha kwa ajili ya mafunzo ya kijeshi. Kama Oljoro JKT inamtaka mchezaji huyo ni lazima ifuate taratibu za usajili kwa kumfanyia uhamisho kutoka Mlale JKT.

 Nayo Mtibwa Sugar inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Ally Shomari Sharrif (Polisi Morogoro), Salim Hassan Mbonde (Oljoro JKT U20) na Hassan Salum Mbande iliyemsajili kwenye kikosi chake cha U20 akitokea Oljoro JKT U20.

Ashanti United haiwezi kumtumia Said Maulid Kalikula aliyekuwa akicheza Angola kwa vile hajapata ITC. Nayo Rhino Rangers inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji Ally Ahmad Mwanyiro (Mwadui FC), Laban David Kambole (Toto Africans) na Musa Boaz Chibwabwa (Villa Squad).

Klabu ya Simba inatakiwa kumfanyia uhamisho Betram Arcadi Mwombeki kutoka Pamba SC wakati wachezaji Gilbert John Kaze na Amisi Tambwe bado hawajapata ITC kutoka Burundi na hawana vibali vya kufanya kazi nchini. Mchezaji Joseph Owino tayari ITC imepatikana lakini hana kibali cha kufanya kazi nchini. Pia kipa Abel right Dhaila hana kibali cha kufanya kazi nchini.

Vilevile Simba inatakiwa kuwafanyia uhamisho wachezaji wawili iliyowasajili katika kikosi chake cha U20. Wachezaji hao ni Twaha Shekue Ibrahim kutoka Coastal Union 20 na Adeyun Saleh Seif (Oljoro JKT U20).

Nayo Yanga inatakiwa kumfanyia uhamisho mchezaji Rajabu Zahir Mohamed kutoka Mtibwa Sugar U20 wakati Hussein Omari Javu bado ana mkataba wa mwaka mmoja na Mtibwa Sugar huku kukiwa hakuna vielelezo vyovyote kutoka kwa mchezaji mwenyewe, Mtibwa Sugar au Yanga kama mkataba huo ulivunjwa au umenunulia na klabu anayotaka kuchezea msimu huu.

Wachezaji waliosajiliwa kutoka nje ambao ITC zimefika na pia wana vibali vya kufanya kazi nchini ni Crispine Odula Wadenya kutoka Bandari ya Kenya na Yayo Wasajja Fred Lutimba kutoka URA ya Uganda waliojiunga na timu ya Coastal Union. Pia Mtanzania Hamis Thabit Nyige aliyejiunga na Yanga kutoka Ureno naye tayari na ITC.

Kwa mujibu wa kanuni, wachezaji wote wa ridhaa (wa madaraja ya chini ikiwemo Daraja la Kwanza) wanatakiwa kufanyiwa uhamisho (transfer) kwa klabu husika kujaza fomu za uhamisho na kulipia ada Chama cha Mpira wa Miguu cha Wilaya, Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa na TFF.

Pia TFF inakumbusha kuwa wachezaji wanaotajwa kuwa wamesajiliwa kama wachezaji huru (free agent) ni lazima waoneshwe kama huko walipokuwa mikataba imekwisha au la.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

FILAMU YA FOOLISH AGE YA LULU KUREKEBISHWABODI ya Ukaguzi wa Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini imezuia kufanyika kwa uzinduzi wa filamu ya Foolish Age iliyochezwa na msanii Elizabeth Michael 'Lulu'.

Bodi imeikataa filamu hiyo iliyopangwa kuzinduliwa Agosti 30 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam hadi irekebishwe.

Taarifa kutoka ndani ya bodi hiyo zimeeleza kuwa, filamu ya Foolish Age imezuiliwa kutokana na waigizaji walioshiriki kuicheza, kuvaa nguo fupi.

Bodi hiyo imeagiza kuwa, sehemu hizo zote zifutwe na kufanyiwa marekebisho na kupitiwa tena kabla ya kuzinduliwa kwake.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, iwapo filamu hiyo haitarekebishwa na kufikia vigezo vya madaraja vilivyowekwa na bodi hiyo, haitaonyeshwa.

MANJI AJITOA KUGOMBEA UONGOZI BODI YA LIGI KUUKamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imebandika rasmi kwenye ubao wa matangazo majina ya waombaji uongozi kwenye uchaguzi wa TFF na Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) ili kutoa fursa kwa pingamizi.

Hata hivyo, katika majina hayo, jina la Yussuf Manji ambaye katika uchaguzi uliosimamishwa aliomba kuwania uenyekiti wa Bodi ya Ligi halimo.

Uamuzi wa Manji kujitoa kwenye uchaguzi huo, umetafsiriwa kuwa ni kukwepa kufanyiwa mizengwe kutokana na msimamo wake wa kuigomea Azam TV kuonyesha laivu mechi za Yanga.

Kipindi cha pingamizi kinaanza leo (Agosti 24 mwaka huu) hadi sa 10 kamili jioni ya Agosti 26 mwaka huu ambapo waweka pingamizi wanaruhusiwa kupitia taarifa za wale wanaokusudia kuwawekea pingamizi kabla ya kuwasilisha pingamizi husika.

Kwa mujibu wa tangazo la uchaguzi, Agosti 27 hadi 29 mwaka huu ni wawekaji pingamizi na wawekewa pingamizi kufika mbele ya Kamati ya Uchaguzi kwa ajili ya kusikiliza pingamizi.

Waombaji kuwania uongozi katika TFF ambao majina yao yamebandikwa ni Athuman Jumanne Nyamlani, Jamal Emil Malinzi, Omari Mussa Nkwarulo na Richard J. Rukambura (urais). Nafasi ya Makamu wa Rais ni Imani Omari Madega, Ramadhan Omari Nassib na Walace John Karia.

Walioomba nafasi za ujumbe kuwakilisha kanda ni Kanda Namba Moja (Kagera na Geita) ni Abdallah Hussein Mussa na Kaliro Samson. Kanda Namba Mbili (Mara na Mwanza) ni Jumbe Odessa Magati, Mugisha Mujwahuzi Galibona, Samwel Nyalla na Vedastus Kalwizira Lufano.

Kanda Namba Tatu (Shinyanga na Simiyu) ni Epaphra Amana Swai, Mbasha Matutu Mong’ateko na Stanslaus Haroon Nyongo. Kanda Namba Nne (Arusha na Manyara) ni Ally Mtumwa, Elley Simon Mbise na Omari Walii Ali.

Kanda Namba Tano (Kigoma na Tabora) ni Ahmed Idd Mgoyi na Yusuf Hamisi Kitumbo. Kanda Namba Sita (Katavi na Rukwa) ni Ayoub Nyaulingo, Blassy Mghube Kiondo, Nazarius A.M. Kilungeja. Kanda Namba Saba (Iringa na Mbeya) ni Ayoub Shaibu Nyenzi, Cyprian Charles Kuyava, David Samson Lugenge, Elias Lusekelo Mwanjala, Eliud Peter Mvella na John Mwachendang’ombe Kiteve.

Waombaji wa Kanda Namba Nane (Njombe na Ruvuma) ni James Patrick Mhagama, Kamwanga Rajabu Tambwe na Stanley William Lugenge. Kanda Namba Tisa (Lindi na Mtwara) ni Athuman Kingome Kambi, Francis Kumba Ndulane na Zafarani Mzee Damoder.

Kanda Namba Kumi (Dodoma na Singida) ni Charles Komba, Hussein Zuberi Mwamba na Stewart Ernest Masima. Kanda Namba 11 (Morogoro na Pwani) ni Farid Salum Mbarak, Geoffrey Irick Nyange, Juma Abbas Pinto, Riziki Juma Majala na Twahil Twaha Njoki.

Wanaowania kuteuliwa kugombea kupitia Kanda Namba 12 (Kilimanjaro na Tanga) ni Davis Elisa Mosha na Khalid Abdallah Mohamed wakati Kanda Namba 13 (Dar es Salaam) ni Alex Chrispine Kamuzelya, Muhsin Balhabou, Omar Isack Abdulkadir, Shaffih Dauda Kajuna na Wilfred Mzigama Kidao.

Kwa upande wa TPL Board waliotangazwa kuomba kuwania uongozi wa juu ni Hamad Yahya Juma (Mwenyekiti) na Said Muhammad Said Abeid (Makamu Mwenyekiti).

Wajumbe wa Kamati ya Uendeshaji ni Kazimoto Miraji Muzo, Michael Njunwensi Kaijage, Omari Khatibu Mwindadi, Salum Seif Rupia na Silas Masui Magunguma.

LIGI KUU BARA KUANZA KUTIMUA VUMBI LEOMichuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu wa 2013/2014 inaanza kutimua
vumbi leo (Agosti 24 mwaka huu) katika viwanja saba tofauti huku mabingwa
watetezi Yanga wakianza kutetea ubingwa wao kwa kuikaribisha Ashanti United
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro utakuwa mwenyeji wa mechi
kati ya Azam ya Dar es Salaam na wenyeji Mtibwa Sugar. Oljoro JKT itaikaribisha
Coastal Union kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini
Arusha.

Mgambo Shooting itaoneshana kazi na JKT Ruvu ambayo hivi sasa iko chini ya
Kocha Mbwana Makata. Mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wakati
Rhino Rangers itakwaruzana na Simba katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini
Tabora.

Mbeya City iliyopanda VPL msimu huu itapimana ubavu na Kagera Sugar kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya huku Ruvu Shooting ikiialika
Mabatini, Mlandizi timu ya Tanzania Prisons kutoka Mbeya.

Mzunguko wa pili wa ligi hiyo utachezwa Agosti 28 mwaka huu. Baada ya hapo ligi
itasimama kupitisha mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Gambia na
Tanzania (Taifa Stars) itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu jijini Banjul. VPL
itaingia mzunguko wa tatu Septemba 14 mwaka huu.

TIKETI ZA ELEKTRONIKI KUANZA MZUNGUKO WA NNE
Tiketi za elektroniki zitaanza kutumika katika mzunguko wa nne wa Ligi Kuu ya
Vodacom (VPL) utakaoanza Septemba 18 mwaka huu. Tayari benki ya CRDB
ambayo ndiyo ilishinda tenda hiyo imeshakamilisha ufungaji wa vifaa kwa ajili ya
matumizi ya tiketi hizo katika viwanja vyote.

Hivi sasa Serikali ambayo ndiyo inamiliki Uwanja wa Taifa, Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) pamoja na CRDB zinashughulikia mfumo wa tiketi hizo kwenye
uwanja huo ambao ndiyo ulikuwa haujakamilika kwa matumizi katika upande huo.

Mfumo (system) iliyoko kwenye uwanja huo inapishana na ule utakaotumiwa na
CRDB, hivyo pande husika zinashughulikia suala hilo ili mifumo hiyo iweze kuingilia.

Pia mashine za kuchapia (printer) kwa ajili ya tiketi ambazo CRDB wameziagiza
kutoka nje ya nchi zinatarajiwa kuwasili mwishoni mwa mwezi huu.

Hivi sasa CRDB inashughulikia ufungaji wa vifaa vya matumizi ya tiketi za elektroniki
iwemo turnstiles kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ambao mwanzoni hakuwemo
kwenye mpango huo kutokana na Mkoa wa Tabora kutokuwa na timu ya Ligi Kuu.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Friday, August 23, 2013

KAPOMBE AUZWA KWA MKOPO AS CANNES YA UFARANSA


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI


Ndugu wana habari.

MWENYEKITI wa klabu ya Simba, Mhe; Ismail Aden Rage, anapenda kuwatangazia wana Simba na wapenzi wa soka kwa ujumla kwamba klabu imefanikiwa kumuunganisha mchezaji wake, Shomari Salum Kapombe, na klabu ya soka ya AS Cannes ya Ufaransa.

Katika mkataba huo mpya na wa aina yake kuwahi kufanywa na klabu yoyote ya Tanzania, Simba imekubali mchezaji huyo achezee timu hiyo iliyo katika ligi daraja la nne la Ufaransa kwa makubaliano ya kumtafutia timu ya kucheza ndani ya miaka miwili kutoka sasa.

Timu hiyo itamgharimia Kapombe kwa kila kitu wakati atakapokuwa nchini Ufaransa. Endapo Kapombe atauzwa kwenda katika timu nyingine yoyote, Simba itapata gawio lake kupitia mauzo hayo na lengo la mchezaji huyo kubaki Ufaransa ni pia kumtengeneza awe bora zaidi kuliko alivyo sasa.

“Kwenye makubaliano hayo, Simba haitapata chochote kwa sasa. Isipokuwa endapo Kapombe atapata timu, Simba itapata mgawo wake kutoka katika mauzo hayo. Makocha wa Ulaya wamebaini kwamba Shomari ni mchezaji mzuri sana lakini anahitaji kuboreshewa vitu vichache kabla hajawa mchezaji mkubwa wa kutumainiwa na vilabu vikubwa,” alisema Rage.

Rage alisema katika mkataba huo mpya wa Kapombe, Simba imeangalia zaidi maslahi ya taifa na ya mchezaji kuliko ya klabu kwa vile kama mchezaji huyo atapata nafasi Ulaya, hilo litafungua milango kwa wachezaji wengi wa Kitanzania ambao kwa sasa hawapati fursa Ulaya.

Wakala wa Kapombe, Denis Kadito, alisema ingawa Kapombe ameonekana kuwa mchezaji mzuri, kutofahamika kwa jina la Tanzania kumekuwa kikwazo kikubwa kwa kupata kwake nafasi ya moja kwa moja na ndiyo maana imebidi aanzie kwenye hatua ya chini.

“Ofa hii ya Cannes ni nzuri kwa sababu timu hiyo huwa inacheza na timu za akiba za vilabu vyote vinavyoshiriki katika Ligi Kuu ya Ufaransa na hivyo atakuwa anaonwa na mawakala wa timu kubwa kila wiki. Hii itamsaidia kupata timu kubwa mapema ndani ya msimu mmoja kutoka sasa,” alisema Kadito.

AS Cannes ni mojawapo ya vilabu vikubwa nchini Ufaransa na ni maarufu kwa kuibua vipaji vikubwa. Miongoni mwa nyota maarufu wa Ufaransa waliowahi kupita katika klabu hiyo ni Patrick Vieira, Zinedine Zidane na Luis Hernandez.

Klabu hiyo inafahamika kwa kuwa na miundombinu imara ya kumwezesha mwanasoka kijana kukuza uwezo wake na ni matarajio ya Simba Sports Club, Kadito, Cannes na Kapombe mwenyewe kwamba atakuwa mchezaji bora zaidi kuliko sasa katika kipindi cha mwaka mmoja kutoka sasa.

Kutokana na mkataba huo wa Kapombe na Cannes, Simba sasa imeongeza mkataba wake na mchezaji huyo kwa muda wa miaka mitatu zaidi, kwa vile mkataba wake wa sasa unamalizika Aprili mwakani. Kama Kapombe hatafanikiwa kupata timu katika kipindi cha miaka miwili kutoka sasa, atarejea katika klabu ya Simba kuendelea na majukumu yake.

Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC

LULU ATANGAZA VIINGILIO VYA FOOLISH AGEMSANII Elizabeth Michael 'Lulu' ametangaza viingilio katika onyesho la uzinduzi wa filamu yake mpya, inayokwenda kwa jina la Foolish Age. Filamu hiyo inatarajiwa kuzinduliwa Agosti 30 mwaka huu kwenye ukumbi wa VIP wa Mlimani City mjini Dar es Salaam. Lulu ameeleza kupitia mtandao wa facebook kuwa, kiingilio kitakuwa sh. 30,000 kwa mtu mmoja na sh. 300,000 kwa watu watakaolipia meza maalumu. Kwa mujibu wa Lulu, uzinduzi wa filamu hiyo utapambwa na burudani ya muziki kutoka kwa bendi ya Machozi, inayoongozwa na Judith Wambura 'LadyJaydee' na wasanii Barnaba Elias na Amin kutoka kundi la THT. Filamu hiyo ni ya kwanza tangu Lulu alipotoka gerezani na imetengenezwa na Kampuni ya Proin Promotion Limited ya Dar es Salaam. "Nina kila sababu ya kumshukuru Mungu.. Ninayo furaha ya kuwafahamisha kuwa Agosti 30 ndiyo siku nitakayozindua movie yangu mpya iitwayo Foolish Age. Hatimaye narudi kazini,"ameeleza Lulu. "Nahitaji sapoti ya mashabiki wote wa Lulu na wale wa Bongo Movi,"ameongeza msanii huyo mwenye mvuto mbele ya luninga.

BANANA ATAKA WASANII WAWE WABUNIFU


MWANAMUZIKI nyota wa muziki wa dansi nchini, Banana Zorro amewataka wasanii wa muziki wa kizazi kipa wawe wabunifu na kwenda na mabadiliko ya wakati.


Banana amesema wasanii wa muziki huo wanapaswa kuboresha kazi zao ili ziweze kuwa katika kiwango cha kimataifa na hivyo kukubalika sehemu mbalimbali duniani.

Kiongozi huyo wa B Band alisema hayo hivi karibuni katika mazungumzo maalumu na gazeti hili yaliyofanyika mjini Dar es Salaam.

Banana alisema binafsi aliamua kujitosa katika muziki wa dansi kutokana na kukua kimuziki na pia kubadili mfumo wa muziki wake.

"Huwezi kutegemea mauzo ya CD kwa miaka yote. Unapaswa kuwa mbunifu zaidi. Inapobidi, unapaswa ujitegemee,"alisema mwanamuziki huyo, ambaye kipaji chake kilianza kuchomoza alipokuwa katika bendi ya In Africa.

Banana alisema msanii anayetumia na kutegemea CD kufanya maonyesho yake, hawezi kupata mafanikio makubwa kimuziki kwa vile kuna wakati anaweza kutakiwa kupiga nyimbo zake laivu, akashindwa.

Kutokana na mfumo mbovu uliopo sasa, Banana alisema mauzo ya CD si mazuri kwa vile baadhi ya watu wamekuwa wakitengeneza CD feki na kuziuza kwa wingi bila ya ridhaa ya wasanii na hivyo kuwafanya waendelee kuwa masikini.

"Ukiweza kupiga muziki laivu, ni rahisi kupata tenda na kupata shoo. Biashara ya kuuza CD kwa sasa ni ngumu,"alisema mwanamuziki huyo, ambaye bendi yake imekuwa ikifanya maonyesho katika hoteli mbalimbali za kitalii mjini Dar es Salaam.

Banana alisema si kweli kwamba maprodyuza wa muziki nchini hawatimizi wajibu wao ipasavyo kutokana na kutengeneza mipigo ya ala isiyokuwa na mvuto. Alisema msanii ndiye mtu wa kwanza, anayepaswa kubuni mipigo ya ala anayoitaka.

Alisema sehemu kubwa ya nyimbo zake zimekuwa zikitengenezwa na prodyuza Allan Mapigo, lakini baada ya kumpa maelekezo ya nini anachokitaka. Alimsifu Mapigo kuwa ni mtaalamu aliyebobea katika fani hiyo na mwenye uwezo wa kumbadili msanii kimuziki.

Licha ya serikali kuanza kutoza kodi kazi za wasanii, Banana alisema bado baadhi ya watu wanaendelea kutengeneza CD feki za nyimbo za wasanii na hivyo kujipatia fedha kwa njia haramu.

"Uamuzi huu wa serikali unaweza kuongeza umakini katika kudhibiti wizi wa kazi za sanaa, lakini wapo watu wanatengeneza CD na kuweka nembo feki za TRA (Mamlaka ya Kodi ya Mapato),"alisema Banana, ambaye ni mtoto wa mwanamuziki mkongwe nchini, Zahir Ally Zorro.

Mwanamuziki huyo ametoa mwito kwa serikali kuiongezea nguvu sheria ya hatimiliki kwa vile inayotumika sasa imeshindwa kudhibiti wizi wa kazi za wasanii kwa vile wahusika wamekuwa wakitozwa faini kidogo.

Amesema ni vyema serikali ishirikiane na wasanii katika kulinda kazi zao na za wasanii wa nje ili iwe rahisi kukabiliana na biashara hiyo haramu, ambayo imekuwa ikiwafaidisha watu wachache na kuwaacha wasanii wakiteseka.

Alisema kuna wakati msanii mmoja kutoka nje ya nchi aliwahi kufika nchini na kukuta kazi zake zinauzwa holela mitaani bila wahusika kuchukuliwa hatua yoyote.

"Ni vyema watu waache kununua CD feki, wanunue CD halali. Naamini wakati utafika udhibiti utakuwa mzuri na CD feki hazitakuwepo kwenye soko la muziki,"alisema Banana.

KASEJA: MIMI SI MCHAWI, SIJAWAHI KUIHUJUMU SIMBA


KIPA wa zamani wa klabu ya Simba, Juma Kaseja amesema tangu alipoanza kuichezea timu hiyo miaka tisa iliyopita, hakuwahi kujihusisha na masuala ya ushirikina au kuihujumu ifungwe na timu pinzani.

Kaseja amesema kucheza soka ndio kazi yake, hivyo isingekuwa rahisi kutumiwa na mtu yeyote kuihujumu Simba kwa maslahi yake binafsi.

"Uchawi? Sijawahi kujihusisha nao kabisa japokuwa Kaseja ndiye mtuhumiwa mkubwa. Tatizo ni kwamba wengi wanamjua Kaseja, hawamjui Juma," alisema Kaseja alipohojiwa katika kipindi cha Mkasi kilichorushwa hewani na kituo cha televisheni cha East Africa mwanzoni mwa wiki hii.

"Mwenyezi Mungu amenijalia kipaji cha kucheza soka. Tangu nilipokuwa sekondari ya Makongo, nilikuwa kipa namba moja, kwa nini isiwe Simba au Taifa Stars," alisema Kaseja, ambaye pia amewahi kuzidakia timu za Yanga na Moro United.

Kipa huyo aliyeachwa na Simba katika usajili wa msimu ujao amesema, katika kipindi chote alichoichezea timu hiyo, hakuwahi kutumiwa na kiongozi yeyote ama mfadhili kuihujumu ili ifungwe.

Alisema asingekuwa tayari kucheza chini ya kiwango ili kuihujumu Simba kwa vile angefanya hivyo, angejishushia hadhi yake kisoka na asingeweza kudumu kwenye klabu hiyo kwa miaka yote tisa.

Kaseja alisema hajawahi kuhongwa fedha ili aihujumu timu yake na kwamba ugomvi wa viongozi hauwezi kumshawishi acheze chini ya kiwango kwa lengo la kuunga mkono upande mmoja.

"Mimi ni mchezaji, sitaki kujua malumbano, kazi yangu ni kucheza soka. Watu wasingemjua Kaseja kama ningejihusisha na mambo hayo. Hayo ni maneno ya kawaida tu katika soka,"alisema kipa huyo, ambaye pia ameichezea Taifa Stars kwa zaidi ya miaka saba.Kaseja amekiri kuwa, nafasi ya kipa ni nyeti katika timu ya soka na kwamba anapofanya makosa, anafungwa kirahisi, lakini kosa hilo hilo linapofanywa na beki, kipa anaweza akaokoa.

Akizungumzia kuachwa kwake na Simba kwenye usajili wa msimu huu, Kaseja alisema kulitokana na mkataba wake kumalizika na si kweli kwamba aliachwa kwa makusudi.

Alisema baada ya mkataba wake kumalizika, yeye na viongozi wa Simba walishindwa kuelewana kuhusu mkataba mpya na ndio sababu aliamua kuachana nayo na kutafuta timu nyingine.

"Mpira ni kazi, mkataba umekwisha, hakuna maelewano, inawezekana mmoja kati yenu hakuridhika, basi mnaachana,"alisema Kaseja.

Aliongeza:" Simba si mali ya mtu, ni ya watu wengi. Nawapenda sana viongozi, wanachama na mashabiki wa Simba kwa sababu nimeishi nao kwa miaka mingi. Kuna kitu wao walikipata kutoka kwangu na mimi nimefaidika. Tumeachana kwa heri."

Kaseja alisema inasikitisha kuona kuwa, viongozi wa soka nchini hawapendi kuona mchezaji akicheza soka kwa miaka mingi katika timu moja kwa hofu kwamba atajua siri nyingi na pengine kuwatia maneno wachezaji wapya.

"Wenzetu Ulaya, mchezaji anapocheza soka kwa miaka mingi katika klabu moja, anapewa heshima kubwa. Hapa kwetu ni tofauti. Ukicheza soka kwa miaka mingi, unaitwa mzee,"alisema.

Kaseja alikanusha madai kuwa, hakuwa akipata namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Taifa Stars, ilipokuwa chini ya Kocha Marcio Maximo kwa sababu alifurahia ilipofungwa idadi kubwa ya mabao na Senegal katika michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika za 2008.

"Si kweli kwamba nilicheka kwa lengo la kufurahia kipigo kile. Hayo yalikuwa maneno ya watu tu. Mimi ni mchezaji, siwezi kufurahia kitu kama hicho ndio sababu niliamua kukaa kimya tu,"alisema.

"Inawezekana kuna watu walimtia maneno ya uongo kocha ili nionekane mbaya, lakini nisingeweza kufanya kitu kama hicho,"aliongeza.

Alisema alianza kuichezea Taifa Stars tangu wachezaji walipokuwa wakilipwa posho ya sh. 1,500 hadi sasa wanapolipwa posho ya sh. 50,000 na kwamba amekuwa akiichezea kwa mapenzi yake yote na ushirikiano mkubwa na wachezaji wenzake.

Kaseja alisema katika klabu zote alizowahi kuzichezea, ikiwemo Yanga, hakuna anakoweza kujutia kwa vile zinafanana kwa kila hali. Alisema hakuna tofauti yoyote kwa mchezaji kuichezea Yanga au Simba.

Kipa huyo alisema ameshindwa kujiunga na FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kutokana na kushindwa kuelewana na viongozi wake kuhusu mkataba.

Alisema alishafikia makubaliano ya awali na wakala wa klabu hiyo, lakini lilipokuja suala la mkataba, ndipo mambo yalipokwenda mrama.

Kwa mujibu wa Kaseja, awali lengo la FC Lupopo lilikuwa ni kumsajili kipa namba moja wa Mtibwa Sugar, lakini viongozi wake walishindwa kuelewana kuhusu malipo ya ada ya uhamisho na kiwango cha mshahara wa mchezaji huyo.

"Walipoona hivyo na baada ya kusikia habari zangu kwamba sina timu, ndipo waliponifuata mimi kwa kujua kwamba kusingekuwa na malipo ya ada ya uhamisho, lakini tumeshindwa kuelewana kuhusu mkataba,"alisema kipa huyo.

Kipa huyo mahiri alisema ni vigumu kutabiri timu ipi itatwaa ubingwa wa ligi kuu msimu huu kwa vile timu nyingi zimefanya maandalizi mazuri. Alisema japokuwa watu wengi wanazipa nafasi Simba na Yanga, lakini Azam inaweza kuonyesha maajabu kutokana na kuwekeza fedha nyingi katika mchezo huo.

Kaseja alisema wachezaji wengi wa Tanzania wanashindwa kucheza soka kwa miaka mingi kutokana na kubweteka baada ya kupata sifa. Alisema vyombo vya habari vimekuwa vikichangia kuua vipaji vya wachezaji kutokana na kuwapa sifa wasizostahili.

Kipa huyo alisema pia kuwa, hajutii kukosa nafasi ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi, hasa barani Ulaya kwa sababu, kimaumbile, makocha wa Ulaya hupenda zaidi kuwapa nafasi hiyo makipa warefu.

"Inaniuma sana kuona nimecheza soka kwa miaka mingi hapa nyumbani. Nilitamani ninapoitwa Taifa Stars, ningekuwa natokea nje ya nchi. Lakini pengine Mungu hakuwa ameniandikia bahati hiyo. Pengine aliniandikia nipate riziki yangu hapahapa nyumbani,"alisema.

Kaseja alisema pia kuwa, hajawahi kutumia dawa za kuongeza nguvu katika soka ama kuvuta bangi. Alisema kwake, vitu hivyo viwili ni mwiko kwa vile anaamini kipaji alichopewa na Mungu kinatosha na hahitaji kitu kingine cha ziada.

Je, nini malengo ya Kaseja baada ya kustaafu soka?

"Nitakapostaafu soka, nimepanga kuwa mfanyabiashara. Mazingira ya soka ya Tanzania ni mazito na ndiyo yamenifanya nifikie uamuzi huo mapema. Sitapenda kujihusisha tena na soka,"alisema.

GURUMO ASTAAFU RASMI MUZIKI

MWANAMUZIKI mkongwe wa bendi ya Msondo Ngoma Mzee Muhidin Gurumo amestaafu rasimi kazi ya muzika alioifanya kwa muda wa miaka 53.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo Mzee Gurumo mwenye umri wa miaka 73 amesema ameamua kustaafu kazi hiyo kwa hiari yake mwenyewe kutokana na umri wake kuwa mkubwa.

“Muziki kwangu umekuwa kama asili yangu na kazi yangu lakini nimeamua kustaafu kutokana na umri wangu na nitabaki kuwa mshauri tu kwa mwanamuziki yeyote atakayetaka ushauri wangu,”alisema Mzee Gurumo.

Pamoja na kufanya kazi ya muziki Gurumo alisema kuwa hakupata mafanikio makubwa zaidi ya kujenga nyumba anayoishi na familia yake.

“Mimi nimeimba kwa muda mrefu sana lakini hata baiskeli sina,”alisema Mzee Ngurumo. Hata hivyo alisema nashukuru kuwa ana nyumba ya kuishi na familia.

Vilevile Mzee Gurumo amewaasa vijana kuwa wabunifu na kuupenda mziki wa zamani kwani ndio chimbuko la bongofleva na kuwashauri wanamuziki wa sasa kuwa wavumilivu kukaa muda mrefu kwenye bendi moja ili hata wanapoondoka mchango wao uthaminiwe.

Mzee Gurumo ambaye ana mke na watoto wanne alisema kuwa katika maisha yake ya muziki alifanikiwa kutunga nyimbo 60,000 na anavutiwa zaidi na mwanamziki Hussein Jumbe na Hassani Lehan Bichuka na kwa wanamuziki wa kizazi kipya anavutiwa na Nassibu Abdul ’Diamond’.

Mwanamuziki huyo mkongwe alianza kufahamika katika tasnia ya muziki wa dansi kwenye miaka ya 1960 ambapo mwaka 1964 alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa bendi ya Nuta Jazz na Mlimani Park.

Alidumu na Mlimani Park mpaka mwaka 1985 na kuhamia Safari Sound aliyofanya nayo kazi mpaka mwaka 1990 na kujiunga na Msondo Ngoma mpaka sasa alipoamua kutangaza rasmi kustaafu kazi hiyo ya Kimuziki.

Tuesday, August 20, 2013

POULSEN AITA 24 WATAKAOIVAA GAMBIA


Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Kim Poulsen ameita kambini wachezaji 24 kujiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Gambia itakayochezwa Septemba 7 mwaka huu nchini humo.

Wachezaji hao wanatakiwa kuripoti kambini Agosti 29 mwaka huu kabla ya saa 1 kamili usiku. Kambi ya Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itakuwa kwenye hoteli ya Accommondia jijini Dar es Salaam.

Makipa walioitwa katika timu hiyo Juma Kaseja (Simba), Mwadini Ali (Azam), Ally Mustafa (Yanga) na Aishi Manula (Azam). Mabeki ni Aggrey Morris (Azam), Kelvin Yondani (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Erasto Nyoni (Azam), Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar) na David Luhende (Yanga).

Viungo Khamis Mcha (Azam), Salum Abubakar (Azam), Said Dilunga (Ruvu Shooting), Frank Domayo (Yanga), Athuman Idd (Yanga), Haruna Chanongo (Simba), Amir Kiemba (Simba), Mrisho Ngasa (Yanga), Simon Msuva (Yanga), John Boko (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) na Juma Liuzio (Mtibwa Sugar).

TWIGA STARS U-20 KUANZA NA MSUMBIJITimu ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania ya umri chini ya miaka 20 inaanzia moja kwa moja raundi ya kwanza Kanda ya Afrika kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Canada.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana (Agosti 18 mwaka huu) na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Tanzania imepangiwa kucheza na Msumbiji ambapo mechi ya kwanza itachezwa Dar es Salaam kati ya Oktoba 25, 26 au 27 mwaka huu.

Mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili baadaye nchini Msumbiji. Mechi hiyo inatakiwa kuchezwa kati ya Novemba 8,9 au 10 mwaka huu. Iwapo itafanikiwa kuitoa Msumbiji itacheza raundi ya pili na mshindi wa mechi kati ya Botswana na Afrika Kusini.

Raundi ya Tatu ambayo ndiyo ya mwisho, mechi zake za kwanza zitachezwa kati ya Januari 10, 11 au 12 mwakani wakati zile za marudiano zitakuwa kati ya Januari 24,25 au 26 mwakani.

Sudan Kusini na Uganda ndizo timu pekee kwa Kanda ya Afrika zinazoanzia raundi ya mchujo ambapo katika mechi ya kwanza zitapambana kati ya Septemba 13,14 au 15 mwaka huu na kurudiana kati ya Septemba 27, 28 au 29 mwaka huu.

Nchi 17 za Afrika zimeingia kwenye michuano hiyo. Nchi hizo ni Afrika Kusini, Botswana, Burkina Faso, Equatorial Guinea, Ghana, Guinea Bissau, Ivory Coast, Misri, Morocco, Msumbiji, Namibia, Nigeria, Sudan Kusini, Tanzania, Tunisia, Uganda na Zambia.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

WAGOMBEA 25 WACHUKUA FOMU UCHAGUZI MKUU TFFWanamichezo 25 wamechukua fomu kuwania nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) unaotarajiwa kufanyika Oktoba 27 mwaka huu.

Fomu hizo zilianza kutolewa juzi (Agosti 16 mwaka huu) ambapo wawili wamechukua nafasi ya Rais na wengine wawili Makamu wa Rais wakati waliobaki wanaomba ujumbe wa Kamati ya Utendaji wakiwakilisha kanda mbalimbali.

Waliochukua fomu za kuomba kuteuliwa kuwa wagombea urais ni Jamal Malinzi na Omari Musa Nkwarulo wakati umakamu wa rais hadi sasa umewavutia Wallace Karia na Ramadhan Nassib.

Waliochukua fomu za ujumbe ni Athuman Kambi, Charles Komba, Davis Mosha, Elias Mwanjala, Eliud Mvella, Epaphra Swai, Farid Nahdi, Hussein Mwamba, Jumbe Magati, Kamwanga Tambwe na Khalid Mohamed.

Wengine ni Muhsin Balhabou, Omari Abdulkadir, Omari Walii, Samwel Nyalla, Shaffih Dauda, Stanley Lugenge, Twahir Njoki, Vedastus Lufano, Venance Mwamoto na Wilfred Kidao.

Kwa upande wa Bodi ya Ligi Kuu aliyechukua fomu mpaka sasa ni Hamad Yahya anayeomba kuteuliwa kugombea nafasi ya uenyekiti.

Fomu za maombi pia zinapatikana kupitia tovuti ya TFF ambayo ni www.tff.or.tz Mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu ni saa 10 kamili jioni ya Agosti 20 mwaka huu.

Fomu zikiambatanishwa na risiti ya malipo (receipt) au malipo ya benki (deposit slip) kupitia akaunti ya TFF namba 01J1019956700 iliyoko CRDB tawi la Holland House zirejeshwe kwa Katibu Mkuu wa TFF kwa mkono au kwa barua pepe (email) ambayo ni tanfootball@tff.or.tz .

MECHI YA NGAO YA JAMII YAINGIZA MIL 208

Mechi hiyo ya Ngao ya Jamii (Community Shield) kuashiria ufunguzi wa msimu mpya wa 2013/2014 iliyochezwa jana (Agosti 17 mwaka huu) Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 208,107,000. Washabiki 26,084 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Yanga kushinda Azam bao 1-0.

Mgawanyo wa mapato ya mechi hiyo uliokuwa kama ifuatavyo; asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) sh. 31,745,135.59, asilimia 10 ya mchango wa kusaidia jamii sh. 20,810,700, gharama ya tiketi sh. 7,309,866.

Uwanja sh. 22,236,194.76, gharama za mchezo sh. 13,341,716.86, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 5,188,445.44, TFF sh. 13,341,716.86 na Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 6,670,858.43. Kila klabu imepata mgawo wa sh. 43,731,183.03.

Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Saturday, August 17, 2013

YANGA YAONYESHA NIA YA KUTETEA UBINGWA WA LIGI KUU, YAICHAPA AZAM 1-0


MABINGWA watetezi wa ligi kuu ya soka ya Tanzania Bara, Yanga leo wameonyesha nia yao ya kutetea taji hilo msimu ujao baada ya kuichapa Azam bao 1-0 katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo huchezwa kila mwaka kabla ya kuanza kwa ligi kuu, ikizikutanisha bingwa wa ligi ya msimu uliopita na mshindi wa pili.

Kipigo hicho kilikuwa ni mwendelezo wa ubabe wa Yanga kwa Azam baada ya msimu uliopita kushinda mechi zote mbili za ligi kuu. Katika mechi ya kwanza, Yanga ilishinda mabao 2-0 na katika mechi ya pili ilishinda bao 1-0.

Kiungo Salum Telela aliibuka shujaa wa Yanga baada ya kuifungia bao hilo la pekee na la ushindi dakika ya pili baada ya kupokea pasi kutoka kwa Didier Kavumbagu.

Yanga ilipata pigo dakika ya 11 baada ya beki wake kisiki, Kevin Yondani kuumia kufuatia kugongana na mshambuliaji John Bocco wa Azam. Beki huyo wa zamani wa Simba alitibiwa kwa dakika kadhaa, lakini alishindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikachukuliwa na Mbuyu Twite.

Yanga ilipata pigo jingine dakika ya 11 baada ya kipa wake, Ally Mustapha Barthez kuumia kufuatia kugongana na Kipre Tchetche wa Azam alipokuwa katika harakati za kuzuia mashambulizi kwenye lango lake. Nafasi yake ilichukuliwa na Deo Munishi 'Dida'

Yanga SC: Ally Mustafa ‘Barthez’/Deo Munishi ‘Dida’ , Juma Abdul, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan/Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Salum Telela, Jerry Tegete/Hussein Javu, Didier Kavumbangu na Haruna Niyonzima.

Azam FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni/Joackins Atudo, Waziri Salum, David Mwantika, Aggrey Morris, Himid Mao, Kipre Tchetche, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco ‘Adebayor’/Gaudence Mwaikimba , Kipre Balou/Ibrahim Mwaipopo na Khamis Mcha.

Friday, August 16, 2013

TFF YAMCHINJA NGASAKamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imepitia usajili wa wachezaji wa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom na kumuidhinisha Mrisho Ngasa kuchezea timu ya Yanga baada ya kukamilisha usajili wake.

Hata hivyo, Kamati hiyo chini ya Mwenyekiti wake Alex Mgongolwa imebaini kuwa Ngasa alisaini mkataba mwingine Simba (katika kipindi ambacho alikuwa na mkataba na Azam) ambapo anatakiwa kurejesha fedha alizopokea (sh. milioni 30) pamoja na fidia ya asilimia 50 (sh. milioni 15) ya fedha hizo kwa Simba.

Kamati pia imemfungia mechi sita za mashindano (kuanzia mechi ya Ngao ya Jamii), na anatakiwa awe amelipa fedha hizo ndani ya kipindi hicho cha kukosa mechi hizo. Akishindwa, hataruhusiwa kucheza hadi atakapolipa fedha hizo.

Vilevile Kamati imepitia pingamizi zote zilizowasilishwa kuhusu usajili wa wachezaji, kukatiza mikataba ya wachezaji na kuzitaka klabu husika ziwe zimetatua masuala hayo hadi Alhamisi (Agosti 22 mwaka huu).

Kwa upande wa wachezaji wa kigeni, Kamati imeagiza wasiruhusiwe kucheza hadi watakapopata Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) pamoja na vibali vya kufanya kazi nchini (work permits).

Kamati hiyo itakutana tena Ijumaa (Agosti 23 mwaka huu) ili kupata ripoti za pingamizi ilizoagiza ziwe zimefanyiwa kazi hadi Agosti 22 mwaka huu na kutoa uamuzi kwa pande ambazo hazikuafikiana