KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Thursday, May 30, 2013

YANGA KUTEMA NYOTA SABAKLABU ya Yanga inatarajia kuwatema nyota wake sita katika msimu ujao wa ligi kuu na michuano ya kimataifa.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, nyota hao wanatemwa kutokana na kushuka kwa viwango vyao.

Kwa mujibu wa habari hizo, miongoni mwa nyota hao sita, wamo watakaouzwa kwa mkopo kwa klabu zingine za ligi kuu.

Wachezaji hao ni pamoja na kipa Saidi Mohamed, mabeki Shadrack Nsajigwa, Godfrey Taita, Salum Telela, Ladslaus Mbogo, Stephano Mwasika na kiungo Nurdin Bakari.

Habari hizo zimeeleza kuwa, Mbogo anaachwa kutokana na kuwa mgonjwa kwa muda mrefu na hivyo kushindwa kuitumikia vyema timu hiyo katika ligi ya msimu uliopita.

Tangu alipojiunga na Yanga mwaka juzi, Mbogo ameshafanyiwa operesheni mara tatu kwa ajili ya kuondoa uvimbe kwenye shingo yake.

Wachezaji wanaotarajiwa kuuzwa kwa mkopo ni Nurdin na Saidi kwa vile bado wana mikataba ya kuitumikia Yanga.

Wakati huo huo, klabu ya Yanga imesema inatarajia kuwatangaza nyota wake wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao kabla ya timu hiyo kwenda Sudan.

Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga, Abdalla Bin Kleb alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, wachezaji hao ni wale waliopendekezwa na Kocha Ernie Brandts kutoka Uholanzi.

"Tayari tunayo majina ya wachezaji wapya tuliowasajili kutokana na mapendekezo ya kocha na tunatarajia kuyatangaza wakati wowote wiki ijayo,"alisema.

Bin Kleb alisema kwa sasa wapo katika hatua za mwisho za mazungumzo na baadhi ya wachezaji hao wapya kabla ya kuingia nao mikataba.

Miongoni mwa wachezaji wapya waliosajiliwa na Yanga ni pamoja na mshambuliaji Mrisho Ngasa, aliyekuwa akiichezea Simba kwa mkopo akitokea Azam.

TAIFA STARS YAIPA MCHECHETO SUDANMAZOEZI makali yanayofanywa na kikosi cha timu ya soka ya Taifa, 'Taifa Stars' nchini Ethiopia kimeifanya timu ya Taifa ya Sudan kuanza kuingiwa na hofu.

Taifa Stars inatarajiwa kumenyana na Sudan mwishoni mwa wiki hii katika mchezo wa kirafiki wa kimatifa utakaofanyika katika Uwanja wa Addis Ababa, Ethiopia.

Meneja wa Taifa Stars, Leopod Tasso Mukebezi alisema kwa njia ya simu jana kutoka Ethiopia kuwa, timu hiyo iliwasili nchini humo juzi na kuweka kambi katika hoteli ya Hilton kabla ya kuanza mazoezi jana asubuhi.

Tasso alisema baada ya Taifa Stars kuanza mazoezi, maofisa wa benchi la ufundi la Sudan walifika uwanjani kwa lengo la kufuatilia mazoezi hayo.

Meneja huyo alisema ujio wa Wasudan nchini Ethiopia umeonyesha wazi kuwa, wameingiwa na wasiwasi kuhusu mechi hiyo, ambayo ni sehemu ya maandalizi kwa Taifa Stars kabla ya kumenyana na Morocco.

Tasso alisema kambi ya timu hiyo inaendelea vizuri na wachezaji wote wapo katika hali nzuri wakiwa na hamu kubwa ya kuvaana na Morocco.

Taifa Stars inatarajiwa kumenyana na Morocco, Juni 8 mwaka huu mjini Marrakech katika mchezo wa marudiano wa kundi C wa michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014.

Wachezaji wa Taifa Stars waliokwenda Ethiopia ni nahodha Juma Kaseja, Aggrey Morris, Mwadini Ally, Ally Mustafa, Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Erasto Nyoni, Haroub Nadir na Mwinyi Kazimoto.

Wengine ni Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd, Haruni Chanongo na Zahoro Pazi.

NAMPENDA PENNY KULIKO WEMA-DIAMONDMSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Naseeb Abdul 'Diamond' amekiri kuwa anampenda zaidi mpenzi wake mpya, Penny Mungilwa kuliko ilivyokuwa kwa mpenzi wake wa zamani, Wema Sepetu.

Diamond alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, mapenzi yake kwa Penny yamemfanya ajione kama vile ameoza kwa binti huyo.

"Ni sawa na kusema treni imegonga mwamba maana kila ninapokuwa naye, nasikia raha ya ajabu, sijui ameniroga. Ananipenda mno,nami nampenda, kwake nimefika,"alisema Diamond.

Msanii huyo nyota wa bongo fleva alisema japokuwa udanganyifu katika mapenzi ni jambo la kawaida, lakini Penny hajawahi kuonyesha dalili hiyo kwake.

Alisema kwa kawaida, mwanamke anapofanya udanganyifu wa mapenzi, inakuwa aibu kwa mwanaume, lakini udanganyifu huo ukifanywa na mwanaume, inakuwa sifa kwake.

"Ni kweli Wema alinipenda, alinionyesha mapenzi ya dhati, lakini alifanya udanganyifu hadharani, alinivunjia heshima, alinivunja moyo, sikupenda kitendo alichokifanya,"alisema Diamond.

Diamond alikanusha madai kuwa, aliwahi kuhusiana kimapenzi na mcheza filamu nyota, Irene Uwoya lakini alikiri kuhusiana kimapenzi na Jokate Mwegelo na Jacqueline Wolper.

Alipoulizwa ni kwa nini amekuwa akipenda kuhusiana kimapenzi na wacheza filamu kuliko wasanii wa fani zingine, Diamond alisema ni kwa sababu amekuwa akikutana nao mara kwa mara sehemu mbalimbali.

"Huwezi kujitosa kimapenzi kwa mtu usiyemfahamu. Hawa ndio ambao nakutana nao mara kwa mara,"alisema.

Je, ni kwa nini wasichana wengi wamekuwa wakimpenda Diamond?

"Unajua mimi nampenda sana mama yangu. Huenda Mungu ananiona na ameamua kunirejeshea upendo huo kupitia kwa watoto wa kike kwa kuwajaza mapenzi kwangu,"alisema.

Diamond alisema yeye ni mstaarabu na amekuwa akijituma katika kazi zake ndiyo sababu hata anapogombana na mpenzi wake, atabaki kumpenda.

Hata hivyo, Diamond alikiri kuwa anajuta kukosana na mpenzi wake wa zamani, Jokate kwa vile ni mwanamke mstaarabu na asiyekuwa na doa.

"Kusema kweli, Jokate hakuwahi kunikosea. Ni mtoto asiye na kosa lolote. Nilimfuata mwenyewe, nikampenda, lakini nilimkosea,"alisema Diamond.

Aliitaja sababu kubwa iliyomfanya agombane na Jokate kuwa ni uamuzi wake wa kurudiana kimapenzi na Wema.

"Nilikuwa nimegombana na Wema, tukarudiana, Jokate hakuufurahia uamuzi huo, sijui nilirogwa, sijui ilikuwa ni utoto, maana ujana ukizidi sana ni matatizo! Hajawahi kunikosea. Ni mstaarabu na ana maisha mazuri,"alisema.

Diamond alisema hajawahi kumuomba msamaha Jokate kwa kosa hilo kwa sababu hadi sasa anajisikia aibu kufanya hivyo.

Wakati huo huo, Diamond amesema amekubali kucheza filamu na Wema kutokana na muandaaji wake kumlipa kiasi kikubwa cha pesa.

"Sidhani kama kuna mcheza filamu wa Tanzania aliyewahi kulipwa fedha nyingi kiasi hiki na tayari nimeshalipwa. Hata katika muziki, sijawahi kulipwa pesa nyingi kiasi hiki,"alisema.

Diamond alisema awali, alimueleza muandaaji wa filamu hiyo wasiwasi aliokuwa nao kuhusu kucheza filamu hiyo na Wema, lakini baadaye akagundua kwamba hiyo ni kazi.

"Kuna watu waliokuwa na uhusiano wa kimapenzi, wakatengana lakini baadaye wakaja kufanya shughuli nyingi pamoja,"alisema msanii huyo.

Katika hatua nyingine, Diamond amesema akaunti yake benki haijawahi kupungua sh. milioni 100.

Alisema akaunti yake inapopungua pesa, huwa anachanganyikiwa na kuongeza kuwa, alianza kuwa na kiasi hicho cha pesa benki tangu 2011.

"Ukipiga hesabu, huu sasa ni mwaka 2013. Hapa nazungumzia zaidi ya bilioni moja benki,"alisema.

MNIGERIA AFUNIKA SIMBAKIUNGO mkabaji Izdore Modebe kutoka Nigeria jana alikuwa kivutio kikubwa kwa makocha Abdalla Kibadeni na Jamhuri Kihwelo wa Simba wakati wa mazoezi yaliyofanyika kwenye uwanja wa Kinesi, Ubungo, Dar es Salaam.

Katika mazoezi hayo yaliyofanyika asubuhi na kushuhudiwa na mashabiki wachache wa Simba, Modebe alikuwa kivutio kikubwa kutokana na kuonyesha uwezo wa hali ya juu wa kumiliki mpira, kutoa pasi na kukaba.

Modebe amekuja nchini kufanya majaribio ya kusajiliwa na Simba, akitokea klabu ya Udense FC ya Benin. Kabla ya kwenda Benin, alikuwa akichezea klabu ya Kwao ya Nigeria.

Akizungumza wakati wa mazoezi hayo, Kocha Msaidizi wa Simba,Kihwelo alisema wametenga muda wa wiki moja kwa ajili ya kuwajaribu wachezaji wapya.

Kocha huyo, ambaye ni maarufu zaidi kwa jina la Julio alisema, wachezaji waliojitokeza ni wazuri na wapo katika kiwango kizuri, lakini alimmwagia sifa zaidi Modebe.

Alisema mchezaji huyo yuko katika kiwango kizuri na kama ataendelea hivyo katika kipindi chote cha majaribio, anaweza kulamba karata dume na kusajiliwa.

Hata hivyo, Julio alisema benchi la ufundi la Simba haliwezi kukurupuka katika kufanya usajili wa wachezaji wapya kwa vile baadhi yao hufanya vizuri wakati wa majaribio na kuvurunda baada ya kusajiliwa.

Julio alisema mazoezi hayo ni sehemu ya maandalizi ya Simba kabla ya kushiriki katika michuano ya Kombe la Kagame, inayotarajiwa kuanza Juni 18 hadi Julai 2 mwaka huu nchini Sudan.

Wachezaji wengine wanaofanyiwa majaribio na Simba ni Joe Fils, Fabian Tsshiyaz, Fabrice Baloko kutoka klabu ya Vita ya Lubumbashi na Patrick Milambo kutoka Nguena FC ya Lumbumbashi nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Wengine ni Mohamed Abdallah (Ferreviariode Nampula,Msumbiji), Adeyun Saleh (Miembeni), Shaaban Kondo (Mbagala Jack Sports Academy), Rashid Salum (New Boko ya Zanzibar), Ramadhan Kipiala (Buza), Shaaban Saidi (Boom FC) na Samuel Ngassa mchezaji wa zamani wa African Lyon.

Mbali na wachezaji hao, kuna habari pia kuwa, Simba imekamilisha mipango ya kumsajili mwanasoka wa kimataifa wa Uganda, Samuel Ssenkoomi anayechezea timu ya URA.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, Ssenkoomi ametia saini mkataba wa miaka miwili wa kuichezea klabu hiyo.

Beki huyo anakuwa mchezaji wa tano mpya kusajiliwa na Simba kwa ajili ya msimu ujao, baada ya awali kusajiliwa wachezaji wanne wazawa, kipa Andrew Ntalla kutoka Kagera Sugar, beki Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ kutoka Mtibwa Sugar, kiungo Twaha Shekuwe ‘Messi’ kutoka Coastal Union na mshambuliaji Zahor Pazi kutoka Azam FC aliyekuwa anacheza kwa mkopo JKT Ruvu.

FALCAO AWA MCHEZAJI GHALI MONACOPARIS, Ufaransa
MSHAMBULIAJI nyota wa klabu ya Atletico Madrid ya Hispania, Radamel Falcao, amekuwa mchezaji ghali wa klabu ya Monaco ya Ufaransa baada ya kununuliwa kwa bei mbaya.

Falcao alifuzu vipimo vya afya juzi na sasa ataichezea timu hiyo katika michuano ya Ligi Kuu ya Ufaransa msimu ujao akiwa na nyota wengine kama Zlatan Ibramovic, anayecheza Paris Saint Germain.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Colombia ametua Monaco kwa ada ya uhamisho wa pauni milioni 51 (sh. bilioni 110).

Monaco imezipiku klabu za Chelsea na Manchester United, ambazo zilikuwa zikimuwinda mchezaji huyo kwa udi na uvumba.

Falcao anatarajiwa kutia saini mkataba wa miaka minne au mitano wa kuichezea Monaco na atachuana na Ibrahimovic katika kuwania kiatu cha dhahabu.

"Sijui niwashukuru vipi mashabiki wa Atletico Madrid, sikutegemea kupata mafanikio haya. Siwezi kuwasahau, asanteni," alisema Falcao.

Mchezaji huyo alisema kuwa anaondoka Atletico Madrid akiwa na mafanikio makubwa kwa kuipa mataji matatu katika miaka miwili aliyokuwa akicheza soka Hispania.

Monaco inayonolewa na Claudio Ranieri, pia imewasajili nyota wengine kadhaa wakiwemo Joao Moutinho na James Rodriguez wa FC Porto ya Ureno na kumuongezea mkataba wa mwaka mmoja beki nguli duniani, Ricardo Carvalho.

MUUMIN MWINJUMA: NAJUTA KUTUNGA WIMBO WA CALL BOXMWANAMUZIKI nyota nchini, Muumin Mwinjuma amesema hakuna kitu anachokijutia katika maisha yake kimuziki kama kutunga wimbo wa Call Box.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Muumin alisema wimbo huo ulipoteza heshima yake kimuziki na kumfanya achukiwe na wanawake wengi kwa kuhisi alimtungia mkewe wa pili.

Muumin alisema hadi sasa bado anakuna kichwa ili kurejesha heshima yake kimuziki, hasa kwa wanawake, ambao alikiri kuwa ndiyo mashabiki wake wakubwa.

Alikanusha madai kuwa, alitunga wimbo huo kwa lengo la kusimulia mkasa uliomfanya aachane na mkewe wa pili baada ya kumfumania mara mbili.

"Huu wimbo nilipewa na rafiki yangu mmoja, ambaye ni mganga wa kienyeji, aliniomba niuimbe. Bahati mbaya sana, nilirekodi wimbo huu muda mfupi baada ya kuachana na mke wangu, ndio sababu mashabiki wengi walidhani nimemwimbia yeye,"alisema.

Muumin alisema mashabiki wake wengi ni wanawake kutokana na kuzipokea vizuri nyimbo zake za Mgumba namba moja na namba mbili pamoja na Kilio cha Yatima, hivyo kumchukulia kama mtetezi wao.

Mwimbaji huyo mkongwe alisema amekuwa akitunga nyimbo zake nyingi kutokana na hisia, lakini wakati mwingine hufanya hivyo kutokana na kushuhudia ama kusikia mikasa mbalimbali.

Akisimulia mkasa uliosababisha atengane na mkewe wa pili, Muumin alisema aliwahi kumfumania mara mbili akifanya mapenzi na rafiki zake wawili.

"Ni matukio yaliyonisikitisha na kuhuzunisha sana kwa sababu watu niliomkuta nao ni rafiki zangu wa karibu wa kufa na kuzikana. Ni watu, ambao wamekuwa wakinisaidia na hadi leo ni rafiki zangu,"alisema mwanamuziki huyo.

Aliongeza kuwa, hakutaka kugombana na rafiki zake hao kwa sababu alichobaini ni kwamba, mkosaji mkubwa alikuwa mkewe.

"Alikuwa akiwafahamu vizuri watu hawa kwamba ni rafiki zangu, hivyo hakuwa na sababu ya kuhusiana nao kimapenzi. Hiyo ndiyo sababu kubwa iliyonifanya niachane naye,"alisema.

Muumin alikiri kuwa, kwa sasa amefunga ndoa na mwanamke mwingine, ikiwa ni ndoa yake ya tatu, lakini hapendi ijulikane kwa hofu ya kusukamwa kwa maneno.

Mwimbaji huyo mwenye sauti yenye mvuto alisema, mara nyingi baadhi ya watu wamekuwa wakimsakama kila anapofanya jambo fulani, hivyo ameona ni vyema afanye mambo yake kimya kimya.

Kwa sasa, Muumin ni kiongozi wa bendi ya Victoria Sound, aliyoianzisha mwaka jana baada ya kujiengua katika bendi ya Twanga Pepeta International.

Muumin alisema bendi ya Victoria Sound sio mpya kwa sababu ilianzishwa miaka sita iliyopita. Alisema kilichofanyika ni kuisuka upya.

Kwa mujibu wa Muumin, tayari wameshatunga vibao vipya vinne na wameshaanza kuvipiga kwenye kumbi mbalimbali wanazofanya maonyesho.

Alivitaja vibao hivyo kuwa ni Shamba la Bibi na Utafiti wa mapenzi, alivyovitunga yeye mwenyewe. Aliviita vibao hivyo kuwa ni moto wa kuotea mbali.

Vibao vingine ni Mama Bahati, kilichotungwa na mpiga gita la rythim, Yohana Mbatizaji na Mwisho wa siku, kilichotungwa na Waziri Sonyo.

Muumin alitamba kuwa, baada ya kuisuka upya bendi hiyo, wapinzani wao wakubwa kwa sasa watakuwa Twanga Pepeta na FM Academia.

Mbali na Muumin, Sonyo na Yohana, wanamuziki wengine wanaounda bendi hiyo ni Selemani Mumba, anayepiga gita la solo na Moshi Hamisi, anayepiga kinanda.

Wengine ni George Gama, anayepiga magita yote matatu, Januari Joseph, Ciana Jordan, Ramso Bushoke, Jonas Mlembuka na Mussa Kalenga, ambao ni waimbaji.

Wanamuziki wengine wanaounda bendi hiyo ni Kassim Mumba, anayepiga gita la besi, Abdalla Hussein anayepiga kinanda na Vaninga Swalehe,anayepiga tumba.

Bendi hiyo inakamilishwa na wacheza shoo, Omari Mussa 'Bokilo', Joha Juma, Mariam Othaman, Farida Omari, Lilian Wayanga, Nadia Benjamin na Sophia Ramadhani.

KIFO CHA MANGWAIR SIMANZI TUPU


KWA mashabiki wengi wa muziki wa kizazi kipya, taarifa za kifo cha msanii nyota wa muziki huo nchini, Albert Mangwair zilionekana kama ni za uzushi.

Hakuna aliyependa kuzisikia wala kuamini. Ilionekana kama vile ni utamaduni uliozoeleka wa watu kutumiana meseji za uzushi kupitia simu za mkononi kwa lengo la kutiana vihoro.

Kadri muda ulivyokuwa ukisonga mbele, taarifa hizo ziliendelea kutapakaa nchi nzima kupitia matangazo ya redio na kwenye mitandao ya kijamii na hatimaye kuthibitika kwamba ni kweli Mangwair amefariki dunia.

Mangwair, ambaye alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na umahiri wake katika kuimba nyimbo za muziki wa hip hop, alifariki dunia juzi nchini Afrika Kusini, ambako alikwenda mwezi mmoja uliopita.

Taarifa zilizopatikana kutoka Afrika Kusini zilieleza kuwa, Mangwair alifariki dunia kutokana na matatizo ya matumizi ya dawa za kulevya.

Kifo cha Mangwair kimezua simanzi kubwa miongoni mwa wasanii na mashabiki wa muziki wa kizazi kipya, ambao baadhi yao walijikuta wakiangua vilio hadharani kwa huzuni.

Mama mzazi wa msanii huyo alisema, alipata taarifa za kifo cha mwanawe kutoka kwa dada wa marehemu, ambaye alipigiwa simu na mtu wa karibu wa msanii huyo.

"Wakati anaondoka, hakuniaga, lakini baada ya kufika huko, alinipigia simu na kuniambia kuwa yupo huko na aliniuliza kama sijambo, nikamwambia sijambo na aliniomba nimuombee na alishukuru kusikia tunaendelea vizuri," alisema mama huyo alipohojiwa na kituo cha redio cha Clouds FM.

"Hapa tunasubiri baba zake wadogo walikwenda Songea, wakirudi tutajua taratibu za mazishi zitakuwaje," aliongeza mama huyo.

Baba mdogo wa msanii huyo, ambaye anaishi Mbinga, Songea alisema wamekubaliana na kaka yake mkubwa, David Mangweha kukutana Mbezi, Dar es Salaam kwa ajili ya kupanga mipango ya mazishi ya mtoto wao.

Japokuwa bado haujatolewa uamuzi wowote kuhusu wapi atakapozikwa msanii huyo, David alisema huenda mazishi yakafanyika Morogoro, ambako baba yake mzazi alizikwa.

Alisema taratibu za kuurejesha nyumbani mwili wa Mangwair zinafanywa na baadhi ya ndugu zake kwa kushirikiana na ubalozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.

Akihojiwa na kituo cha redio cha East Africa jana asubuhi, mwanamuziki nyota wa muziki huo, Judith Wambura 'Lady Jaydee' alishindwa kuzungumza maneno mengi zaidi ya kuangua kilio.

Jaydee alisema amekuwa mtu wa karibu na Mangwair na kuongeza kuwa, taarifa za kifo chake zimemuhuzunisha.

Kutokana na kifo cha msanii huyo, JayDee aliamua kuahirisha onyesho lake la kutimiza miaka 13 katika muziki huo lililopangwa kufanyika kesho.

Onyesho hilo la Jaydee pia lilikuwa maalumu kwa ajili ya uzinduzi wa albamu yake mpya, uliotarajiwa kufanyika kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge.

JayDee alipanga kulitumia onyesho hilo kupiga nyimbo zake zote zilizowahi kutamba, ikiwa ni pamoja na zile alizowashirikisha wasanii mbalimbali nchini.

Naye Khamis Mwijuma (Mwana FA) alisema jana kuwa, amelazimika kusogeza mbele onyesho lake la kutimiza miaka 10 katika fani ya muziki lililopangwa kesho kutokana na kuguswa na kifo cha msanii huyo.

Mwana FA alipanga kufanya onyesho hilo kwenye ukumbi wa Makumbusho uliopo Kijitonyama, Dar es Salaam, akiwashirikisha wasanii mbalimbali maarufu nchini pamoja na bendi ya The Kilimanjaro 'Wana Njenje'.

Alisema kifo cha Mangwair ni pigo kubwa katika fani ya muziki wa kizazi kipya nchini kwa vile alikuwa na mchango mkubwa katika muziki huo.

"Siwezi kuendelea na onyesho langu siku mbili baada ya kifo cha mwenzetu na kaka yetu, naomba radhi kwa mashabiki wangu. Tutapanga tarehe nyingine ya kufanya onyesho hili,"alisema.

Mwana FA alisema alipata taarifa za kifo cha msanii huyo akiwa mazoezini na kujikuta akijawa na majonzi mengi kwa vile alikuwa mtu wake wa karibu.

"Nililazimika kuwaeleza wasanii wenzangu, ambao ningeshirikiana nao kufanya onyesho langu la Ijumaa (kesho) kwamba hatutaweza kuendelea nalo,"alisema Mwana FA.

Akielezea uhusiano wake na Mangwair, Mwana FA alisema walikuwa marafiki wa karibu, lakini walishindwa kuwa pamoja katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kila mtu kutingwa na shughuli zake.

Kiongozi wa kikundi cha Kikosi cha Mizinga, Karama Kalapina alisema jana kuwa, kifo cha Mangwair kimewafanya waamue kuahirisha onyesho lao la kusherehekea kutimiza miaka 13 lililopangwa kufanyika kesho kwenye ukumbi wa Msasani Beach Dar es Salaam.

Mtangazaji wa kituo cha redio cha Clouds FM, Boniventura Kilosa 'DJ Venture' alisema aliwahi kuishi gheto na Mangwair na kuongeza kuwa, alikuwa mtu wake wa karibu.

Kwa upande wake, P Funky, ambaye ndiye aliyemtoa Mangwair alisema ameamua kukizuia kituo cha redio cha Clouds FM kupiga nyimbo zote za msanii huyo aliyezirekodi kwenye studio yake.

Wakati huo huo, msanii M to the P aliyekwenda Afrika Kusini pamoja na marehemu Albert Mangwair, amefariki dunia.

Taarifa zilizopatikana jana kutoka Afrika Kusini zilisema kuwa, msanii huyo alipelekwa katika hospitali ya St Hellen iliyopo chini humo kwa matibabu baada ya kukutwa amepoteza fahamu akiwa na Mangwair aliyefariki dunia juzi.

Miili ya marehemu hao bado iko katika hospitali hiyo na mipango ya kuisafirisha kuirejesha Tanzania inaendelea kufanywa na watanzania wanaoishi nchini humo.

PELLEGRINI ATALIWEZA FUPA LILILOMSHINDA MANCINI?LONDON, England
KOCHA Mkuu wa Malaga ya Hispania, Manuel Pellegrini amethibitisha kuwa, Manchester City ya England ni miongoni mwa klabu zilizompa ofa nzuri na ambayo anaipa uzito mkubwa.

Pellegrini (59) amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi ya Roberto Mancini, ambaye alitimuliwa Manchester City kabla ya msimu huu kumalizika.

Hata hivyo, kocha huyo raia wa Chile, pia amekuwa akiwindwa kwa udi na uvumba na klabu za AS Roma, Napoli za Italia na Paris St Germain (PSG) ya Ufaransa.

Pellegrini aliwaambia waandishi wa habari wiki hii kuwa, anaondoka Malaga ili kutimiza ndoto aliyonayo katika mchezo wa soka na kuongeza kuwa, tayari ameshaanza kufanya mazungumzo na viongozi wa Manchester City.

Kocha huyo alisema anapaswa kuwa makini katika kuamua wapi pa kwenda, lakini alisisitiza kuwa, anaipa uzito mkubwa ofa kutoka kwa Manchester City.

Pellegrini aliiongoza Malaga katika mechi ya mwisho Jumapili iliyopita wakati timu hiyo ilipomenyana na Deportivo la Coruna katika mechi ya ligi kuu ya Hispania na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.

Kocha huyo alisema anaona fahari kuondoka Malaga akiwa ameiacha timu hiyo katika hali nzuri. Malaga imemaliza ligi ya Hispania ikiwa nafasi ya sita.

"Hupaswi kuuliza sherehe nzuri ya kuagwa. Nilitaka kuondoka hapa na ushindi na hivyo ndivyo nilivyofanya. Naondoka hapa timu ikiwa inashiriki michuano ya Ulaya kwa mara ya pili mfululizo. Nitayakumbuka mafanikio haya kwa muda mrefu,"alisema kocha huyo.

"Lengo letu lilikuwa kucheza michuano ya Ulaya kwa sababu klabu hii inastahili. Miaka yangu miwili na nusu hapa imekuwa ya kihistoria. Kuna siku ambazo kamwe siwezi kuzisahau,"aliongeza.

Staili ya ufundishaji soka ya Pellegrini na uongozi wake ni miongoni mwa vitu vilivyotarajiwa kumwongezea thamani kocha huyo atakapoanza kibarua cha kuinoa Manchester City.

Manchester City iliamua kukatisha mkataba wake na Mancini, kufuatia timu hiyo kupokonywa taji la ubingwa wa ligi kuu ya England na mahasimu wao, Manchester United na pia kufungwa na Wigan katika fainali ya Kombe la FA.

Kuna habari kuwa, iwapo Pellegrini atatua Manchester City, huenda akamnyakua kiungo nyota wa Malaga, Isco.

Tayari uongozi wa Manchester City umeshampa mtihani mgumu Pellegrini kwa kumweleza kuwa, anatakiwa kuiongoza klabu hiyo kutwaa mataji matano katika misimu mitano.

Pellegrini anatarajiwa kutangazwa rasmi kuwa kocha wa Manchester City, Juni 3 mwaka huu.

Mtendaji Mkuu wa Manchester City,Ferran Soriano alisema licha ya Manchester City kutwaa taji la ligi kuu ya England msimu uliopita, haijapata mafanikio makubwa chini ya Mancini.

"Nadhani msimu ujao utakuwa bora zaidi kwetu. Nashawishika kuamini hivyo,"alisema Soriano.

"Haimaanishi kwamba tutashinda taji moja au mawili, lakini katika mpangilio wa vitu, tukitazama miaka mitano ijayo, na ninaweza kupanga hivyo, naweza kusema nataka kushinda mataji matano katika kipindi cha miaka mitano ijayo,"aliongeza.

Akifafanua, Soriano alisema iwapo watashindwa kutwaa taji lolote katika msimu mmoja, wanapaswa kutwaa mataji mawili katika msimu utakaofuata.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa lengo lao ni kushinda taji moja kila msimu, yakiwemo mataji ya ligi ya mabingwa wa Ulaya, ligi kuu ya Englandn na Kombe la FA.

"Kama mwaka ujao hatutashinda taji lolote, lakini tutaendelea vyema na mchezo wetu na kufuzu kucheza nusu fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya, kushika nafasi ya pili katika ligi kuu ya England na kufungwa kwenye fainali ya Kombe la FA, haitakuwa mbaya,"alisema.

"Tunachotaka kocha wetu mpya akifanye ni kujenga kikosi, ambacho kinaweza kudumu na kufanya vizuri katika miaka 10 ijayo,"aliongeza kocha huyo.

Soriano alimpongeza Mancini kwa kazi nzuri aliyoifanya alipokuwa akiifundisha Manchester City, ambapo aliiwezesha kufuta ukame wa miaka 35 kwa kutwaa Kombe la FA, 2011 na taji la ligi kuu ya England msimu wa 2012.

Alisema Mancini alifanyakazi nzuri kwa kuibadili klabu hiyo kutoka isiyoshinda taji lolote na kuwa klabu ya ushindi. Alikiri kuwa kazi hiyo ilikuwa ngumu.

Mtendaji huyo wa Manchester City alisema uamuzi wa kumtimua Mancini ulifanywa kwa muda mrefu na umakini mkubwa ili kuepuka kuivuruga timu hiyo.

"Kamwe tusingeweza kumbadili kocha kutokana na matokeo ya mechi moja au mbili. Unapotaka kufanya mabadiliko, unapaswa kuwa na hakika na kile unachokifanya,"alisema Soriano.

Hata hivyo, alisema kikosi walichonacho sasa kina uwezo wa kushinda taji la ligi kuu ya England na siyo kikosi cha kutolewa hatua ya makundi katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya.

Soriano, ambaye aliteuliwa kuwa mtendaji mkuu wa Manchester City, 2012, alisema bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo ilitafakari mambo mengi kabla ya kufikia uamuzi wa kumtimua Mancini, aliyedumu klabu hiyo kwa miaka mitatu na nusu.

Alitoa mfano wa tukio la kocha huyo kurushiana ngumi na mshambuliaji, Mario Balotelli, ambaye aliuzwa kwa klabu ya AC Milan mwanzoni mwa mwaka huu.

Alisema tukio hilo lilileta picha mbaya kwa Manchester City duniani na kuongeza kuwa, hawako tayari kuliona likitokea tena.

"Kutokana na kikosi tulichonacho, tunataka kuwa na kocha mtu mzima. Tunataka kuwa na kocha, anayefahamu kuhusu soka na uongozi. Haitawezekana kwetu kushinda ubingwa wa Ulaya kama hatutakuwa na kundi linalojiona kama familia moja,"alisema Soriano.

Mtendaji huyo alisema pia kuwa, wanataka kuwa na kikosi ambacho nusu ya wachezaji ni wazawa kama ilivyo kwa klabu za Manchester United na Barcelona ya Hispania.

WASIFU WA PELLEGRINI
KUZALIWA: Septemba 16, 1953
UMRI: Miaka 59
URAIA: Chile
NCHI ALIZOFUNDISHA SOKA: Hispania, Argentina na Chile

NEYMAR DA SILVA SANTOS: NIMEACHA PESA BRAZIL, NAFUATA SOKA HISPANIASAO PAULO, Brazil
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Brazil, Neymar da Silva Santos amesema uamuzi wake wa kujiunga na klabu ya Barcelona ya Hispania umelenga kukuza zaidi kipaji chake cha soka.

Neymar alisema wiki hii mjini hapa kuwa, ameacha pesa nyingi katika klabu yake ya Santos na kufuata soka Hispania.

"Nakwenda Barcelona kukuza kiwango changu cha soka, sifuati pesa,"alisema Neymar, ambaye kwa sasa ni mwanasoka anayelipwa pesa nyingi nchini Brazil.

Mbali na malipo ya mshahara na posho katika klabu yake ya Santos, picha za Neymar zimekuwa zikitumika kwenye matangazo mbalimbali na hivyo kumwingizia mamilioni ya pesa.

Neymar alitangaza rasmi kujiunga na Barcelona mwishoni mwa wiki iliyopita kabla ya kumwaga wino Jumatatu wiki hii. Chipukizi huyo mwenye umri wa miaka 21 ameingia mkataba wa kuichezea Barcelona kwa miaka mitano.

Mbrazil huyo alikuwa akiwindwa na klabu mbalimbali za Ulaya, wakiwemo mahasimu wakubwa wa Barcelona, Real Madrid na Chelsea ya England.

"Nina masikitiko makubwa kuondoka Santos, lakini ni heshima kubwa kuingia mkataba na klabu kama Barcelona na kupata nafasi ya kucheza na baadhi ya wachezaji nyota duniani,"alisema Neymar.

Neymar ataungana na nyota kadhaa wa dunia, akiwemo mwanasoka bora wa dunia wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), Lionel Messi, Xavi Hernandez na Andres Iniesta.

Hata hivyo, klabu za Barcelona na Santos hazijatangaza kiwango cha malipo ya ada ya uhamisho wa mchezaji huyo, lakini baadhi ya vyombo vya habari vya Brazil vimeripoti kuwa, uhamisho wake umeigharimu klabu hiyo ya Hispania pauni milioni 38.7.

Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya habari, Santos ilikuwa imepokea ofa za kumsajili mchezaji huyo kutoka Barcelona na Real Madrid na lilikuwa jukumu la mchezaji kuamua wapi anapotaka kwenda kucheza.

Neymar aliandika ujumbe kupitia kwenye Twitter akielezea uamuzi wake wa kuondoka Santos, ambayo alianza kuichezea tangu 2009 alipokuwa mdogo kiumri.

"Asante kwa kila kitu. Nitatunza kumbukumbu hii katika maisha yangu yote,"alisema.

Neymar aliipatia Santos umaarufu mkubwa tangu mwanasoka nyota wa zamani wa dunia, Pele alipoichezea klabu hiyo miaka ya 1970. Aliiwezesha Santos kutwaa Komeb la Brazil 2010, Copa Libertadores 2011 na ubingwa wa Jimbo la Sao Paulo mara tatu mfululizo.

Mchezaji huyo kipenzi wa Pele, ameweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa Santos kwa kufunga mabao 138 katika mechi 230.

Baba wa mwanasoka huyo, Silva Santos alisema waliingia mkataba na Barcelona, Jumatatu wiki hii ukihusisha malipo ya mshahara na ada ya uhamisho wake.

Mzee huyo alisema pia kuwa, Neymar ameamua kujiunga Barcelona badala ya Real Madrid kwa sababu staili yake ya uchezaji inafanana na ya klabu hiyo.

Neymar alitarajiwa kujiunga na kikosi cha Brazil, Jumanne iliyopita kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya Kombe la Mabara kabla ya kwenda Hispania kwa ajili ya utambulisho kwa mashabiki wa Barcelona, unaotarajiwa kufanyika Juni 2 mwaka huu.

Mwanasoka huyo anatarajiwa kuwemo katika kikosi cha Brazil kitakachocheza mechi ya kirafiki dhidi ya England, itakayopigwa kwenye uwanja wa Maracana.

Alipoulizwa kuhusu namba ya jezi anayotarajiwa kuivaa atakapokuwa Barcelona, mwanasoka huyo wa Brazil alisema hatajali iwapo atapewa namba yoyote.

Neymar amekuwa akivaa jezi namba 11 katika klabu yake ya Santos na timu ya taifa ya Brazil.

"Acha tuone namba itakayopatikana, hilo halitakuwa tatizo kwangu,"alisema Neymar.

Mwanasoka huyo alisema pia kuwa, hana hakika iwapo familia yake itahamia Barcelona au la.

Mtandao wa Barcelona umemwelezea Neymar kuwa ni mshambuliaji na mfungaji mabao wa aina yake, anayetumia mbinu za uchezaji zenye mvuto.

"Wengi wanaamini kuwa ndiye mrithi wa Pele,"ulieleza mtandao huo wiki hii.

Gazeti la Marca la Hispania liliripoti wiki hii kuwa, muunganiko wa Messi na Neymar utaunda safu tishio ya ushambuliaji. Neymar na Messi wanatarajiwa kucheza pamoja katika safu ya ushambuliaji.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Barcelona ilikuwa ikihitaji kwa muda mrefu kuwa na mshambuliaji mwenye staili ya uchezaji kama ya Messi ili kuifanya safu ya ushambuliaji ya timu hiyo iwe tishio zaidi.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka wanahoji iwapo Neymar, aliyeifungia Brazil mabao 32, ataweza kuimudu staili ya uchezaji soka ya Ulaya.

Sunday, May 26, 2013

TAIFA STARS KWENDA ETHIOPIA LEOTimu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inatarajia kuondoka leo (Mei 26 mwaka huu) usiku kwenda Addis Ababa, Ethiopia ambapo itaweka kambi na kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya kwenda Morocco.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itaondoka saa 5 usiku kwa ndege ya EgyptAir ikiwa na kikosi cha wachezaji 21 chini ya nahodha wake kipa Juma Kaseja.

Timu hiyo ikiwa Ethiopia, Juni 2 mwaka huu itacheza mechi ya kirafiki dhidi ya Sudan ambapo siku inayofuata itaondoka kwenda Marrakech, Morocco kwa kupitia Cairo, Misri. Mechi hiyo ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji Morocco itachezwa Juni 8 mwaka huu jijini Marrakech.

Mbali ya nahodha Kaseja, wachezaji wengine wanaoondoka katika kikosi hicho ambacho kina wiki sasa tangu kingie kambini jijini Dar es Salaam ni Mwadini Ally na Ally Mustafa ambao wote ni makipa.

Wengine ni Shomari Kapombe, Kevin Yondani, Aggrey Morris, Haroub Nadir, Mwinyi Kazimoto, Frank Domayo, Mrisho Ngasa, Khamis Mchana, Amri Kiemba, Salum Abubakar, Simon Msuva, John Bocco, Vicent Barnabas, Mudathiri Yahya, Athuman Idd na Haruni Chanongo.

Wachezaji Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu ambao wako na timu yao ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo watajiunga moja kwa moja na Stars jijini Marrakech, Juni 4 mwaka huu wakitokea Maputo, Msumbiji mara baada ya mechi yao ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Liga Muculumana ya huko.

Katika msafara huo wa Ethiopia benchi la ufundi la Stars linaundwa na Kim Poulsen (Kocha Mkuu), Sylvester Marsh (Kocha Msaidizi),Juma Pondamali (Kocha wa makipa), Leopold Tasso (Meneja wa timu), Dk. Mwanandi Mwankemwa (Daktari), Frank Mhonda (Mtaalamu wa tibamaungo) na Alfred Chimela (Mtunza vifaa).

30 WAITWA KAMBINI TWIGA STARSKocha Mkuu wa timu ya Taifa ya wanawake ya mpira wa miguu (Twiga Stars), Rogasian Kaijage amewaita kambini wachezaji 30 ikiwa ni mwendelezo wa kuijenga na kuiimarisha timu hiyo.

Twiga Stars itakuwa na kambi ya siku kumi kuanzia Jumapili (Mei 26 mwaka huu) ambapo baadaye inatarajia kucheza mechi moja ya kirafiki kabla ya wachezaji kurudi kwenye klabu zao.

Kambi hiyo ni mwendelezo wa programu iliyopendekezwa na kocha kuijenga na kuiimarisha timu hiyo kwa vile haina mashindano mwaka huu, na itakuwa kambi ya pili baada ya ile iliyofanyika Machi mwaka huu.

Wachezaji walioitwa na klabu zao kwenye mabano ni Asha Rashid (Mburahati Queens), Aziza Mwadini (Zanzibar), Belina Julius (Lord Barden), Ester Chabruma (Sayari), Ester Mayala (TSC Academy), Eto Mlenzi (JKT), Evelyn Sekikubo (Mburahati Queens) na Fatuma Bushiri (Mburahati Queens).

Fatuma Hassan (Mburahati Queens), Fatuma Omari (Sayari), Flora Kayanda (Tanzanite), Hamisa Athuman (Marsh Academy), Hellen Peter (JKT), Maimuna Said (JKT), Mwajuma Abdallah (Tanzanite), Mwanahamisi Omari (Mburahati Queens), Mwanaidi Tamba (Mburahati Queens) na Mwapewa Mtumwa (Sayari).

Nabila Ahmed (Marsh Academy), Pulkeria Charaji (Sayari), Rehema Abdul (Lord Barden), Rukia Khamis (Uzuri Queens), Semeni Abeid (Tanzanite), Sharida Boniface (Makongo Sekondari), Sophia Mwasikili (Sayari), Therese Yona (TSC Academy), Vumilia Maarifa (Evergreen) na Zena Khamis (Mburahati Queens).

RCL KUENDELEA KUTIMUA VUMBI KESHO
Raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) inaendelea kesho (Mei 26 mwaka huu) kwa mechi sita za kwanza zitakazochezwa katika miji sita tofauti.

Abajalo ya Dar es Salaam na Kariakoo ya Lindi zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam wakati Machava FC ya Kilimanjaro itakuwa mwenyeji wa Mpwapwa Stars ya Dodoma kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Nayo Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida huku Polisi Jamii ya Bunda mkoani Mara ikimenyana na Biharamulo FC ya Kagera kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma.

Mjini Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika ni kati ya wenyeji Saigon FC na Katavi Warriors ya Katavi wakati Njombe Mji itaikaribisha Kimondo SC ya Mbeya kwenye Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe.

Leo (Mei 25 mwaka huu) Friends Rangers ya Kinondoni, Dar es Salaam inacheza na African Sports ya Tanga kwenye Uwanja wa Azam Chamazi. Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.

Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.

Friday, May 24, 2013

WENYEVITI FA WASIMAMIZI RCL

Wakati mechi za kwanza za raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zinachezwa wikiendi hii, Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imesisitiza kuwa wasimamizi wa mechi za ligi hiyo ni wenyeviti wa mikoa wa vyama vya mpira wa miguu.

Kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Ramadhan Nassib ilikutana jana (Mei 23 mwaka huu) kupitia ripoti za makamishna kwa mechi za raundi ya kwanza ya RCL iliyomalizika wikiendi ya Mei 18 na 19 mwaka huu.

Kuhusu viwanja vinavyotumika kwa ligi hiyo, Kamati imesema vitaendelea kuwa vile vya makao makuu ya mikoa, na kwa vile vilivyokuwa vimeombwa vifanyiwe marekebisho ili viweze kukaguliwa kwa ajili ya RCL msimu ujao. Pia imeitaka mikoa kuendelea kuboresha viwanja vinavyotumika sasa, lakini vina upungufu.

Vilevile Kamati imebaini kuwa zimekuwepo pingamizi kuhusu usajili wa wachezaji ambapo imesema haiwezi kujadili pingamizi hizo kwa vile mikoa yote haikuwasilisha usajili wa wachezaji wa klabu husika uliofanyika mikoani kama ilivyoagizwa na kuelekezwa na TFF.

Hata hivyo, Kamati imeitaka mikoa ambayo klabu zao zimefanikiwa kuingia raundi ya pili kuwasilisha usajili huo haraka.

Pia Kamati imebaini kuwa zipo baadhi ya klabu ambazo zimekata rufani kuhusu usajili wa baadhi ya wachezaji, na kusisitiza kilichowasilishwa ni pingamizi kwa vile kwa mujibu wa kanuni masuala ya uwanjani hayakatiwi rufani. Hivyo, Kamati imeshauri klabu zilizokata rufani zilirejeshewe ada zilizolipa kwa ajili hiyo.

Makamishna na waamuzi wanaosimamia mechi za RCL wamekumbushwa kuwa ili mchezaji aruhusiwe kucheza mechi ni lazima awe na leseni yake (kadi ya usajili), vinginevyo asiruhusiwe kucheza mechi husika.

Mechi za RCL zinaendelea wikiendi hii ambapo zote zitachezwa Jumapili (Mei 26 mwaka huu) isipokuwa mechi kati ya Friends Rangers ya Dar es Salaam na African Sports ya Tanga itakayochezwa Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi.

Nayo mechi kati ya Abajalo ya Dar es Salaam na Kariakoo ya Lindi iliyokuwa ichezwe Jumamosi kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam sasa itachezwa Jumapili kwa vile siku hiyo uwanja huo utatumika kwa mazoezi ya Taifa Stars.

Mechi nyingine za RCL zitakazochezwa Mei 26 mwaka huu ni Machava FC ya Kilimanjaro dhidi ya Mpwapwa Stars ya Dodoma kwenye Uwanja wa Ushirika mjini Moshi, Stand United FC ya Shinyanga itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa Namfua mjini Singida.

Polisi Jamii ya Bunda mkoani Mara na Biharamulo FC ya Kagera zitaumana kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma. Mjini Kigoma kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika ni kati ya wenyeji Saigon FC na Katavi Warriors ya Katavi.

Nayo Kimondo SC ya Mbeya itakuwa mgeni wa Njombe Mji ya Njombe katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe. Mechi za marudiano zitachezwa kati ya Juni 1 na 2 mwaka huu.

Timu zitakazofuzu kucheza raundi ya tatu zitacheza mechi za kwanza kati ya Juni 8 na 9 mwaka huu wakati mechi za marudiano zitakuwa kati ya Juni 15 na 16 mwaka huu.

SEMINA YA USAJILI- TMS KUFANYIKA MEI 25
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeandaa semina ya usajili kwa njia ya mtandao (Transfer Matching System-TMS) kwa klabu za Ligi Kuu ya Vodacom kwa ajili ya msimu wa 2013/2014.

Semina hiyo itafanyika Jumamosi (Mei 25 mwaka huu) kwenye ofisi za TFF saa 3 kamili asubuhi ikishirikisha watu wawili kutoka kila klabu ambao ni TMS Manager, na ofisa mwingine wa klabu.

Klabu za ligi hiyo zinazotakiwa kuhudhuria semina ya usajili ni Ashanti United, Azam, Coastal Union, JKT Ruvu, Kagera Sugar, Mbeya City, Mgambo Shooting, Mtibwa Sugar, Oljoro JKT, Rhino Rangers, Ruvu Shooting, Simba, Tanzania Prisons na Yanga.

KOCHA WA AZAM AKATAA OFA KUTOKA LIBYA NA CANADAKOCHA Mkuu wa Azam, Stewart Hall amesema amekataa ofa ya mamilioni ya fedha kutoka katika klabu mbalimbali za soka za Libya na Canada zilizokuwa zinamtaka.


Stewart aliwaambia waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana kuwa, alipokea ofa hizo muda mfupi baada ya kumalizika kwa michuano ya ligi kuu ya Tanzania Bara.

Kocha huyo kutoka Uingereza alisema, ameshindwa kuzikubali ofa hizo kwa sababu bado anataka kuendelea kuinoa Azam kwa muda mrefu ili aweze kutimiza malengo yake.

Stewart alisema viongozi wa Azam wamemtaka aendelee kuinoa timu hiyo kwa msimu mmoja zaidi.

"Hakuna kocha anayekataa ofa ya mamilioni ya fedha, lakini kitu kikubwa ninachoangalia kwa sasa ni uhuru na mazingira ya kazi,"alisema.

Stewart alianza kuinoa Azam, 2011na kuiwezesha kutwaa Kombe la Mapinduzi na nafasi ya pili katika Kombe la Kagame kabla ya kutimuliwa na kujiunga na Sofapaka ya Kenya.

Alirejea nchini Desemba mwaka jana na kuendelea kuinoa Azam, ambayo ilifuzu kucheza raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la Shirikisho na kushika nafasi ya pili katika ligi kuu.

KIKWETE AWAPA CHANGAMOTO WACHEZAJI TAIFA STARS

RAIS Jakaya Kikwete amesema ataweka historia ya kukumbukwa na wachezaji wa timu ya Taifa, Taifa Stars iwapo itafuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia 2014.
Rais Kikwete pia amesema atatoa zawadi nono kwa timu hiyo iwapo itashinda mchezo wake wa kufuzu kucheza fainali za kombe hilo dhidi ya Morocco.

Kikwete alisema hayo jana Ikulu mjini Dar es Salaam alipokutana na wachezaji wa timu hiyo pamoja na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Taifa Stars inatarajiwa kurudiana na Morocco, Juni 8 mwaka huu katika mechi itakayopigwa mjini Marrakech. Katika mechi ya awali iliyochezwa mjini Dar es Salaam, Taifa Stars iliichapa Morocco mabao 4-1.

Timu hiyo imepangwa kundi C pamoja na timu za Morocco, Ivory Coast na Gambia. Inashika nafasi ya pili katika kundi hilo ikiwa na pointi sita nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kwa kuwa na pointi saba.

Kikwete alisema kufuzu kwa Taifa Stars kucheza fainali za kombe hilo litakuwa tukio la kihistoria katika uongozi wake, hivyo atawapa zawadi nzito.

Alisema hatua iliyofikia sasa Taifa Stars ni nzuri hivyo wachezaji wanapaswa kucheza kufa na kupona ili kuandika historia mpya kwa Tanzania.

Kikwete alisema serikali itakuwa tayari kutoa msaada wa kila aina kwa timu hiyo ili iweze kufanikisha azma hiyo na kuongeza kuwa, jukumu la wachezaji ni kucheza mpira.

Alisema jambo la msingi kwa wachezaji ni kuhakikisha mawazo na akili zao wanazielekeza katika mechi zijazo za michuano hiyo.

"Sasa hivi elekezeni nguvu zenu katika michezo yenu na mhakikishe mnashinda, hayo mambo mengine niachieni mimi na Kamati ya Saidia Stars Ishinde,"alisema.

Rais Kikwete alisema mechi zilizobaki kwa Taifa Stars ni ngumu, lakini iwapo wachezaJi watajiamini na kujijenga kisaikolojia, haitakuwa migumu.

Thursday, May 23, 2013

ROONEY NA FAMILIA MPYA

Mshambuliaji Wayne Rooney wa klabu ya Manchester United akiwa amempakata mtoto wake aliyezaliwa wiki hii. Kulia ni mkewe, Coleen na mtoto wao wa kwanza, Kay


WASAUZI KUZIHUKUMU STARS, MOROCCO


SHIRIKISHO la Soka la Kimataifa (FIFA), limemteua mwamuzi Fraser Daniel Bennett kutoka Afrika Kusini kuchezesha mchezo kati ya timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' na Morocco.

Mchezo huo wa marudiano wa kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia za 2014, utafanyika Juni 8 mwaka huu Jijini Marrakech, Morocco.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema jana kuwa, Bennett atasaidiwa na Thusi Zakhele Siwela wa Afrika Kusini na Marwa Range kutoka Kenya.

Alisema mwamuzi wa akiba katika mechi hiyo, itakayochezwa kuanzia saa 2.30 usiku atakuwa Lwandile Mfiki wa Afrika Kusini.

Alisema Kamishna wa mechi hiyo ni Robert Mangollo-M’voulou wa Gabon wakati mtathimini wa waamuzi atakuwa Charles Masembe kutoka Uganda.

Stars ipo kundi C na timu za Ivory Coast, Morocco na Gambia, ikiwa inashika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi sita, nyuma ya Ivory Coast inayoongoza kwa kuwa na pointi saba.

KAMPUNI MBILI ZAIDI KUDHAMINI LIGI KUUKAMPUNI mbili zinazomiliki vituo vya televisheni zimeanza kufanya mazungumzo na kamati ya ligi kuu ya Tanzania Bara kwa ajili ya kudhamini ligi hiyo msimu ujao.

Hayo yalisemwa jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Wallace Karia alipokuwa akizungumza na gazeti hili mjini Dar es Salaam.

Wallace alisema katika makubaliano hayo, kampuni hizo zinataka kuonyesha mechi za ligi hiyo moja kwa moja kwenye luninga ili mashabiki wengi zaidi waweze kuzishuhudia.

Kwa mujibu wa Karia, katika makubaliano hayo, klabu za ligi kuu zitakuwa zikilipwa kutokana na mechi zao kuonyeshwa moja kwa moja kwenye luninga.

Hata hivyo, Karia hakuwa tayari kutaja majina ya kampuni hizo kwa madai kuwa ni mapema kufanya hivyo. Lakini alidokeza kuwa, kituo kimoja ni cha nje na kingine cha hapa nyumbani.

"Lengo la kamati yetu ni kuhakikisha kuwa, msimu ujao timu zote zitakazoshiriki katika ligi, zinapata udhamini wa uhakika kwa lengo la kuongeza ushindani,"alisema Karia.

Mbali na kampuni hizo, Karia alisema lengo la kamati yake ni kuhakikisha kuwa, ligi hiyo inakuwa na wadhamini wengi ili timu ziweze kunufaika.

Timu zinazotarajiwa kushiriki katika ligi kuu msimu ujao ni Yanga, Azam, Simba, Mtibwa, Ruvu Shooting, JKT Ruvu, Prisons, Coastal Union, JKT Mgambo, JKT Oljoro, Kagera Sugar, Ashanti,Rhino Rangers na Mbeya City.

Wakati huo huo, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom imeomba kusogeza mbele tarehe ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.

Mwenyekiti wa kamati ya ligi, Wallace Karia alisema jana kuwa, tarehe mpya ya utoaji wa zawadi hizo itatangazwa baadaye.

Awali, Vodacom ilipanga kukabidhi zawadi hizo kwa washindi mwishoni mwa wiki hii. Bingwa wa ligi hiyo atapata sh. milioni 70, wa pili sh. milioni 35, wa tatu sh. milioni 25 na wa nne sh. milioni 20.

Zawadi zingine ni ya kipa bora wa mwaka na mfungaji bora, ambao watazawadiwa sh. milioni tano kila mmoja wakati mwamuzi bora na kocha bora watapata sh. milioni 7.5 kila mmoja.

WACHEZAJI JANGWANI KUJAZWA MAMILIONI

KLABU ya Yanga imepanga kuwajaza mamilioni ya pesa wachezaji wake kutokana na timu hiyo kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara msimu huu.

Pesa hizo ni zile zinazotokana na zawadi ya ubingwa wa ligi hiyo kutoka kwa wadhamini, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Vodacom na zilizoahidiwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji.

Yanga itazawadiwa kitita cha sh. milioni 70 kutokana na kutwaa ubingwa wa ligi hiyo, ambao mwaka jana ulinyakuliwa na watani wao wa jadi Simba.

Naye Manji aliahidi kuwazawadia wachezaji wa timu hiyo sh. milioni 20 kwa kila mechi watakayoshinda katika mechi tano zilizokuwa zimesalia kabla ya ligi hiyo kumalizika kwa lengo la kuwaongezea hamasa.

Katika mechi hizo, Yanga ilishinda nne na kutoka sare moja, lakini uongozi umeamua kuwapa sh. milioni 50 bila kujali mechi moja waliyopata sare.

Uongozi wa Yanga pia uliahidi kuwapa wachezaji zawadi ya sh. milioni 50 iwapo wangeifunga Simba katika mechi ya mwisho ya ligi hiyo.

Katika mechi hiyo iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga iliichapa Simba mabao 2-0 na kunogesha sherehe za ubingwa.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alikiri jana kufanyika kwa kikao cha kujadili mgawo huo wa wachezaji, lakini hakuwa tayari kutaja kiwango watakachowapa kwa madai kuwa hiyo ni siri ya klabu.

YANGA YAITESA SIMBAKAMATI ya Usajili ya klabu ya Simba imepanga kufanya usajili wa wachezaji wake wapya msimu ujao kwa siri ili kuepuka kuingiliwa na wapinzani wao.

Mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, wamepania kufanya usajili wa nguvu msimu ujao kwa lengo la kurejesha taji la ligi kuu.

Hanspope alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha kamati ya utendaji ya Simba kilichofanyika mjini Dar es Salaam juzi.

Alisema usajili huo utafanyika kwa kuzingatia vigezo muhimu, ambavyo vitawekwa na kamati hiyo.

"Tulikutana jana (juzi) na kuamua kufanya usajili kwa staili ya pekee ili kukwepa hujuma kutoka kwa wapinzani wetu,"alisema.

Alisema Simba ilifanya usajili usiokuwa na viwango msimu uliopita baada ya kufanyiwa hujuma nyingi na kujikuta ikisajili wachezaji ambao hawakuwa chaguo lao.

Katika msimu huo, Simba ilizidiwa kete na Yanga kwa mchezaji wa zamani wa APR ya Rwanda, Mbuyu Twite, ambaye alikula fedha za Msimbazi, lakini akatua Jangwani.

Hanspope alisema kwa kuwa msimu uliopita walifanya makosa, hawaoni sababu ya kuyaduria msimu ujao na kusisitiza kuwa, kila kitu kitafanyika kwa kuzingatia viwango vitakavyowekwa.

"Napenda niwaambie kuwa, msimu uliopita tulifanya usajili, lakini umetugharimu na kutufikisha hapa tulipo, hivyo hatupaswi kurudia makosa," alisema Hanspope.

Mbali na kuzungumzia usajili, Hanspope alisema kikao hicho pia kilijadili masuala mengine mbalimbali, ikiwemo tathmini ya wachezaji wote wanaounda timu hiyo.

Aliongeza kuwa, mambo mengine waliyoyajadili yatabaki kuwa siri hadi utekelezaji wake utakapokamilika ili taarifa zisivuje na kuwafikia wapinzani wao.

Kamati ya usajili ya Simba inaundwa na Hanspope (mwenyekiti), Kasim Dewji (makamu mwenyekiti), Francis Waya, Crencesious Magori, Salim Abdallah, Collins Frisch na Gerald Lukumaya (wajumbe).

MESSI: HATUPASWI KUBADILI STAILI YETU YA UCHEZAJIMADRID, Hispania
MWANASOKA bora wa dunia, Lionel Messi ameitaka klabu yake ya Barcelona ya Hispania isibadili staili yake ya uchezaji.

Messi alisema mjini hapa juzi kuwa, wanapaswa kuendelea na staili hiyo licha ya kushindwa kufika mbali katika michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya msimu.

Barcelona ilitolewa katika hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kupata kipigo cha jumla cha mabao 7-0 kutoka kwa Bayern Munich ya Ujerumani.

Kutolewa mapema kwa Barcelona katika michuano hiyo, kumetafsiriwa kuwa, kumetokana na staili ya uchezaji ya timu hiyo kuzidiwa na ile ya Bayern Munich.

"Hatuwezi kupoteza vichwa vyetu. Hatuwezi kubadili staili yetu ya uchezaji," alisema mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 25.

"Huwezi kushinda siku zote. Tumekuwa tukicheza kwa kiwango cha juu kwa miaka kadhaa na makocha na timu zingine zimekuwa zikijifunza kutoka kwetu,"aliongeza mchezaji huyo.

Messi alisema wanapaswa kuwa watulivu na kujipanga upya kwa ajili ya michuano ya msimu ujao.

Makamu wa rais wa klabu hiyo, Josep Bartomeu alisema wanapaswa kuongeza wachezaji wapya wanne au watano kwa ajili ya kukiimarisha kikosi chao.

SUAREZ AZUA HOFU LIVERPOOLLONDON, England
KOCHA Mkuu wa Liverpool, Brendan Rodgers amekiri kuwa, anatarajia kukumbana na upinzani mkali katika kumzuia mshambuliaji, Luis Suarez asiondoke.

Rodgers alisema juzi mjini hapa kuwa, licha ya Liverpool kumuunga mkono mchezaji huyo wa kimataifa wa Uruguay, hali inaweza kubadilika iwapo ataamua kuondoka.

Wakati Rodgers alipokabidhiwa kibarua cha kuinoa timu hiyo msimu uliopita, jukumu lake la kwanza lilikuwa ni kuzikataa ofa kutoka klabu za Juventus ya Italia na Paris St Germain za kutaka kumsajili mchezaji huyo.

Suarez ametia saini mkataba mpya wa kuichezea Liverpool hadi 2017, lakini mustakabali wake katika klabu hiyo bado una utata.

Mshambuliaji huyo kutoka Uruguay alimaliza msimu uliopita kwa matatizo, ikiwa ni pamoja na kufungiwa mechi 10 kwa kumng'ata beki Branislav Ivanovic wa Chelsea.

Hadi sasa, mchezaji huyo ameshatumikia adhabu hiyo katika mechi nne na amekabisha mechi sita, ambazo atazitumikia msimu ujao.

Klabu ya Juventus imeshaonyesha tena nia ya kumsajili mshambuliaji huyo, ikiwemo Atletico Madrid ya Hispania. Suarez pia amekuwa akihusishwa na mipango ya kujiunga na Bayern Munich ya Ujerumani.

"Sina wasiwasi wa kupokea ofa kutoka klabu zingine kwa sababu yupo kwenye kiwango cha juu,"alisema Rodgers.

"Kuna asilimia chache ya wachezaji walioko kwenye kiwango cha dunia. Suarez yumo kwenye orodha hiyo. Lazima kuna klabu zitamuhitaji,"aliongeza.

Hata hivyo, Rodgers alijipa moyo kwa kusema kuwa, ana hakika Suarez anapenda kubaki katika klabu hiyo kwa vile anafurahia kucheza soka England.

LUIZ AZIGONGANISHA BARCA NA REAL MADRID


MADRID, Hispania
KLABU za Real Madrid na Barcelona za Hispania zimeanza kupigana vikumbo kwa ajili ya kumwania beki David Luiz wa Chelsea ya England.

Luiz huenda akawa mchezaji wa kwanza kuondoka Chelsea baada ya kutua kwa kocha mpya, Jose Mourinho, ambaye havutiwi na uchezaji wa beki huyo.

Beki huyo kutoka Brazil aliigharimu Chelsea pauni milioni 12 za Uingereza (sh. bilioni 19) na klabu hiyo inataka kumuuza kwa faida iwapo itapata ofa kutoka kwa klabu zingine.

Mourinho anataka kusajili beki mpya wa kati, kiungo mkabaji na mshambuliaji mmoja baada ya kurejea Stamford Bridge.

Luiz amekuwa akicheza nafasi ya kiungo mkabaji chini ya kocha Rafael Benitez, ambaye amefungashiwa virago baada ya ligi kuu ya England kumalizika.

Barcelona imepanga kumsajili Luiz kwa ajili ya kuimarisha safu yake ya ulinzi na huenda ikatumia kitita cha pauni milioni 25 (sh. bilioni 40) kumnyakua beki huyo.

Mabingwa hao wa Hispania pia walipanga kumsajili Thiago Silva kutoka Paris St Germain, lakini wameamua kubwaga manyanga kutokana na malipo ya ada ya uhamisho kuwa makubwa.

Barcelona pia imekuwa ikimuwinda beki chipukizi, Marquinhos kutoka AS Roma ya Italia, lakini ameamua kubaki nchini humo kwa msimu mmoja zaidi.

Mchezaji mwingine, ambaye Chelsea imeonyesha dhamira ya kumsajili ni beki Krygiakos Papadopoulos wa klabu ya Schalke ya Ujerumani, ambaye pia anawaniwa na Liverpool ya England.

Mourinho pia ni shabiki mkubwa wa mchezaji Raphael Varane wa Real Madrid ya Hispania, lakini huenda akakumbana na kikwazo katika kumsajili kutokana na uondokaji wake katika klabu hiyo kutawaliwa na mizengwe.

Real Madrid imepanga kukipangua kikosi chake kilichokuwa kikinolewa na Mourinho kwa kumuuza beki Pepe na kumbakisha Varane. Tayari Manchester City imeonyesha dhamira ya kumsajili Pepe.

REHEMA, SHILOLE WAJA NA MDUARA


MWANAMUZIKI mkongwe wa muziki wa dansi nchini, Rehema Tajiri anatarajia kurekodi wimbo mpya wa mduara kwa kushirikiana na msanii wa muziki wa kizazi kipya, Zuwena Mohamed 'Shilole'.

Akizungumza mjini Dar es Salaam juzi, Rehema alisema ameshaanza kufanya mazoezi na Shilole kwa ajili ya kurekodi wimbo huo.

Rehema alisema lengo la kurekodi wimbo huo ni kuwapa ladha tofauti ya muziki mashabiki wake.

"Bado hatujaupa jina wimbo huo, lakini nawahakikishia mashabiki wangu kwamba utakuwa moto wa kuotea mbali,"alisema Rehema.

"Kwa vile nimeamua kurudi kwenye fani kwa nguvu zote, nawahakikishia mashabiki wangu kwamba nyimbo zote mpya nitakazozitoa, zitakuwa hatari. Lengo langu ni kuwapa burudani ya uhakika,"alisema.

Wakati huo huo, Rehema amesema video ya wimbo wake mpya wa Msikilize Mama imekamilika na inatarajiwa kuanza kuonekana kwenye vituo vya televisheni wakati wowote.

Rehema alisema juzi kuwa, video hiyo imerekodiwa kwa ubora wa kiwango cha juu na itakuwa na mvuto wa aina yake kwa watazamaji wa luninga.

Mwanamuziki huyo mkongwe aliyewahi kurekodi nyimbo zake nyingi kwa kushirikiana na baadhi ya wanamuziki wa Msondo Ngoma, amerekodi kibao hicho kwa kutumia miondoko ya zouk.

Katika wimbo huo, Rehema amemshirikisha msanii chipukizi wa muziki wa kizazi kipya, Dogo Sama kwa lengo la kuutia nakshi.

Wimbo huo unazungumzia masuala ya mapenzi kati yake mwanamke na mpenzi wake, huku kikwazo kikubwa kikiwa kwa mama mkwe.

"Nimesimulia jinsi mimi na mpenzi wangu tunavyopendana, lakini mkwe wangu (mama wa mpenzi wake) hanipendi, anataka niachane na mwanawe,"alisema.

Rehema amewataka mashabiki wake wakae mkao wa kula kwa vile amejipanga upya kuhakikisha anateka tena soko la muziki nchini.

Alisema ukimya wake wa muda mrefu ulitokana na kutingwa na matatizo ya kifamilia na pia kujipanga upya.

WANAHABARI KUKIPIGA NA WABUNGE JUNI MOSITIMU za soka na netiboli zinazoundwa na wachezaji kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini, zinatarajiwa kucheza mechi za kirafiki na wabunge Juni Mosi mwaka huu mjini Dodoma.

Timu hizo za vyombo vya habari zimeundwa na baadhi ya wachezaji walioshiriki katika michuano ya kuwania Kombe la NSSF iliyofanyika Machi mwaka huu mjini Dar es Salaam.

Ofisa Uhusiano Mwandamizi wa NSSF, Juma Kintu alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, mechi hizo mbili zinatarajiwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.

Kintu alisema mechi hizo zimelenga kujenga uhusiano wa kirafiki kati ya wabunge na wafanyakazi wa vyombo vya habari.

Alisema timu hizo mbili za waandishi wa habari zinatarajiwa kuondoka Mei 31 mwaka huu kwenda Dodoma na kurejea Dar es Salaam Juni 2 mwaka huu.

Kintu alisema wachezaji wa timu hizo wanatarajiwa kufanya mazoezi kwa siku tatu kabla ya safari hiyo kwa lengo la kujiweka fiti.

"Uteuzi wa wachezaji timu zote mbili za soka na netiboli umeshafanyika na ulitokana na viwango walivyovionyesha wakati wa michuano ya Kombe la NSSF,"alisema Kintu.

Aliwataja wachezaji 17 walioteuliwa kuunda timu ya soka kuwa ni Mzee Mfaume (NSSF), Mbozi Katala (TBC), Paul Urio (IPP Media), Majuto Omary (Mwananchi), Fred Mweta (BTL), Anwar Mkama (Mlimani TV), Julius Kihampa (Jambo Leo) na Nurdin Msindo (Tumaini Media).

Wengine ni Said Ambua (Uhuru Media), Mohamed Mharizo (New Habari), Mohamed Mkandemba (Free Media), Edward Mbaga (Sahara Media), Saleh Ally (Global Publishers), Mussa Abdalla (Habari Zanzibar), Ridhiwani Ramadhani (Changamoto), Heri Mselem (Redio Kheri) na Mgaya Kingoba (TSN).

Wachezaji walioteuliwa kuunda timu ya netiboli ni Pili Mogela (NSSF), Agnes Mbapu (TBC), Somoye Ng'itu (IPP Media), Imani Makongoro (Mwananchi), Lulu Habibu (BTL), Sophia Turuka (Mlimani TV), Charity James (Jambo Leo).

Wengine ni Monica Kinyemi (Tumaini Media), Sophia Ashery (Uhuru Media), Zuhura Abdulnoor (New Habari), Crecensia Tryphon (Free Media), Immaculata Kiluvya (Sahara Media), Glory Massawe (Global Publishers), Beshuu Abdalla (Habari Zanzibar) na Vicky Godfrey (Changamoto).

MICHO KOCHA MPYA THE CRANES


KAMPALA, Uganda
SHIRIKISHO la Soka la Uganda limemteua Milutin 'Micho' Sredojevic kuwa kocha mkuu mpya wa timu ya taifa ya nchi hiyo, The Cranes.

Micho (43) anachukua nafasi ya kocha wa zamani wa timu hiyo, Bobby Williamson, ambaye mkataba wake ulikatishwa mwezi uliopita.

Habari kutoka ndani ya shirikisho hilo zimeeleza kuwa, Micho ametia saini mkataba wa kuifundisha timu hiyo kwa miaka miwili.

Micho, ambaye alitimuliwa kuifundisha timu ya taifa ya Rwanda mwezi uliopita, alilieleza Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) juzi kuwa, amefurahi kurejea katika nchi, ambayo alianza kufundisha soka kwa mara ya kwanza barani Afrika.

"Ndoto yangu ya kufundisha soka Afrika ilianzia 2001 nchini Uganda katika klabu ya Villa na nilikaa kule kwa miaka mitatu. Katika miaka minane iliyopita, nilifundisha soka Ethiopia, Sudan, Afrika Kusini, Tanzania na Rwanda. Na sasa nimerejea nyumbani nilikoanzia,"alisema.

Micho alisema amejipanga vizuri kufanya kila analoweza kuipatia mafanikio Uganda katika michuano mbalimbali itakayoshiriki.

"Nataka kuendelea kukuza kiwango cha soka cha Uganda na kuiwezesha kufuzu kucheza fainali za Afrika. Nahisi nakwenda nyumbani, ambako wachezaji wananielewa vyema na kwenye utamaduni ninaoufahamu,"alisema kocha huyo.

Micho alisema anawaelewa vyema wachezaji wa Uganda kutokana na kucheza soka ya kiwango, hivyo anachohitajika kukifanya ni kuongeza kiwango chao.

Alisema Uganda haijafuzu kucheza fainali za Afrika tangu 1978 hivyo jukumu lake kubwa litakuwa ni kuwashawishi wachezaji wawe na dhamira hiyo.

Micho alisema haendi Uganda kutafuta pesa bali kuwasaidia wachezaji na timu ya taifa ya nchi hiyo katika kupata mafanikio na anaamini mchango wake utafanikisha azma yake hiyo.

Rais wa Shirikisho la Soka la Uganda, Lawrence Mulindwa alisema makocha 37 walituma maombi ya kutaka kuifundisha timu hiyo na kusisitiza kuwa, Micho atapewa kila anachokihitaji katika kufanikisha kazi yake.

Kwa mujibu wa Mulindwa, Micho atasaidiwa na Sam Timbe na Kefa Kisala wakati Fred Kajoba atakuwa kocha wa makipa.

Micho aliiongoza Villa kutwaa mataji matatu ya ligi kuu ya Uganda, aliiongoza St George ya Ethiopia kutwaa ubingwa wa nchi hiyo mara moja na pia kuiongoza Orlando Pirates kutinga nusu fainali ya ligi ya mabingwa wa Afrika 2006.

Kocha huyo pia aliiwezesha Al Hilal ya Sudan kufuzu kucheza hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho kwa miaka minne mfululizo.

AZAM: HATUNA MPANGO WA KUMTOSA UHURU SELEMANI

UONGOZI wa klabu ya Azam umesema hauna mpango wa kumtupia virago mshambuliaji Uhuru Selemani baada ya msimu huu wa ligi kuu kumalizika.

Kocha Msaidizi wa Azam, Kally Ongara alisema mjini Dar es Salaam juzi kuwa, Uhuru ataendelea kuwemo kwenye kikosi cha timu hiyo katika msimu ujao wa ligi.

Ongara alisema kukaa benchi kwa Uhuru katika msimu huu wa ligi, kulitokana na mpangilio wa uchezaji wa Kocha Stewart Hall katika kikosi cha kwanza.

"Si kweli kwamba Uhuru alikuwa hapangwi kwa sababu ya kushuka kwa kiwango chake. Bado Uhuru ni mchezaji mzuri, isipokuwa ulikuwa uamuzi wa kocha anavyotaka kikosi chake kicheze,"alisema.

Ongara alisema Uhuru bado ni mchezaji mzuri na ana uwezo wa kuendelea kuwemo kwenye kikosi cha Azam kwa zaidi ya mwaka mmoja.

Alisisitiza kuwa, kwa vile kocha ndiye mwenye uamuzi wa mwisho kuhusu upangaji wa kikosi katika mechi, Uhuru anapaswa kuwa mvumilivu na kuongeza bidii katika mazoezi.

"Nimesikia watu wakilalamika kwa nini Uhuru hachezeshwi katika mechi za Azam. Ninachofahamu ni kwamba Uhuru ni mchezaji mwenye sifa zote za kucheza soka, lakini bado kuna mtu mwenye mamlaka ya kuamua nani acheze na nani asicheze,"alisema.

Kauli ya Ongara imekuja siku chache baada ya kuwepo na taarifa kwamba, Uhuru anataka kurejea Simba kutokana na kuchoshwa kukaa benchi.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Coastal Union, alijiunga na Azam kwa mkopo wakati wa usajili wa dirisha dogo akitokea Simba, aliyoichezea kwa misimu miwili.

Alipoulizwa iwapo ni kweli anataka kuondoka Azam, mshambuliaji huyo alisema: "Hakuna mchezaji anayefurahia kuwekwa benchi."

Hata hivyo, Uhuru alisema amepanga kukitumia kipindi hiki cha mapumziko kufanya mazoezi ya nguvu ili aweze kurejea katika kiwango chake.

AZAM KUHAMIA ZANZIBARNa Salum Vuai, maelezo, Zanzibar
UONGOZI wa klabu ya Azam umesema upo katika mchakato wa kuunda timu nyingine ya soka itakayoshiriki katika michuano ya ligi kuu ya Zanzibar.

Katibu Mkuu wa Azam, Nassoro Idrisa alisema kwa njia ya simu juzi kuwa, uamuzi wao huo umelenga kuongeza ushindani katika ligi kuu ya Zanzibar.

Idrisa alisema pia kuwa, uamuzi wao huo umelenga kufanikisha jitihada za Kampuni ya SSB, inayomiliki Azam, kuwekeza katika soka ili kuongeza ajira kwa vijana.

Alisema walianza mchakato huo miezi sita iliyopita na iwapo sheria zitaruhusu, timu hiyo itaundwa mara moja.

Alipoulizwa timu hiyo mpya ya Azam itaanzia daraja lipi, Idrisa alisema lengo lao ni kushiriki moja kwa moja katika ligi kuu ya Zanzibar.

"Tunachoweza kufanya ni kununua mojawapo ya klabu zinazoshiriki ligi kuu ya Zanzibar, japokuwa inaweza kuwa kazi ngumu,"alisema Idrisa.

Hata hivyo, Idrisa alisema iwapo watashindwa kununua timu ya ligi kuu, watafanya hivyo kwa timu za madaraja ya chini, hasa daraja la pili.

Idrisa alisema mpango wao huo pia umelenga kujenga timu imara na itakayokuwa na miundombinu yote muhimu ili kuwavutia vijana wengi zaidi kucheza soka.

Alisema SSB ni kampuni kubwa, ambayo imeamua kujitangaza kibiashara kwa kutumia mchezo wa soka.

"Kwa kuwa tunao wigo mkubwa wa biashara Zanzibar, tunatarajia hatua hiyo itasaidia sana kuipa hadhi kampuni kama tulivyofanya kwa Tanzania Bara,"alisema.

NGASA: SIKUONGEZA MKATABA SIMBAMSHAMBULIAJI nyota nchini, Mrisho Ngasa mwanzoni mwa wiki hii alirejea rasmi katika klabu yake ya zamani ya Yanga baada ya kutia saini mkataba wa miaka miwili. Ngasa amerejea Yanga akitokea Simba, ambayo aliichezea kwa mkopo wa mwaka mmoja baada ya kuuzwa na Azam.

Katika makala hii ya ana kwa ana iliyoandikwa na ATHANAS KAZIGE, mshambuliaji huyo anaelezea mambo mbalimbali kuhusu mustakabali wake kisoka.

SWALI: Ni sababu ipi iliyokufanya uamue kurejea Yanga ukitokea Simba? Huoni kwamba utashusha kiwango chako kutokana na kuhama mara kwa mara?

JIBU: Niliichezea Simba kwa mkopo nikitokea Azam, ambayo ndiyo niliyokuwa na mkataba nayo. Yanga ilianza kunifuatilia miezi sita iliyopita, tukazungumza na kufikia makubaliano ndio sababu nimeamua kuondoka Simba.

Ukweli ni kwamba nina mapenzi makubwa na ya dhati kwa Yanga na ninachoweza kusema ni kwamba namshukuru Mungu kwa kuweza kupata nafasi hii. Ninawaomba viongozi na wachezaji wa Yanga wanipe ushirikiano wa kutosha ili niweze kutimiza malengo yangu.

SWALI: Ulipohama Yanga na kujiunga na Azam, 2009 uliondoka kwa mapenzi yako ama kulikuwa na shinikizo lolote kutoka kwa viongozi wa zamani wa klabu hiyo.

JIBU: Niliamua kuhamia Azam kwa mapenzi yangu mwenyewe kwa lengo la kutafuta maisha mazuri. Hakuna mtu yeyote aliyenishinikiza nifanye hivyo. Unajua mimi bado ni kijana na ninaendelea kupambana na maisha kwa ajili ya siku zijazo.

Kilichotokea ni kwamba, baada ya kutua Azam, nikagundua kwamba kuna baadhi ya mambo, ambayo kwa upande wangu hayakunifurahisha na niliyaona kama kikwazo.Nilipata wakati mgumu kuweza kutekeleza majukumu yangu. Nisingependa kuzungumza kiundani kuhusu suala hilo.

SWALI: Vipi ulipokuwa ukiichezea Simba kwa mkopo, kuna matatizo yoyote uliyokumbana nayo?

JIBU: Nilikwenda Simba kwa hiari yangu, nikiwa na lengo lingine la kutafuta maisha. Kilichotokea ni kwamba hawakuwa na imani na mimi. Kilichotokea ni kama ilivyokuwa kwa Azam. Lakini niliichezea kwa uwezo wangu wote kwa sababu mpira ndiyo kazi yangu.

SWALI: Hebu eleza kiundani, ni kwa nini viongozi wa Simba na Azam hawakuwa na imani na wewe?

JIBU: Tatizo kubwa lilikuwa likijitokeza wakati wa maandalizi ya mechi dhidi ya Yanga. Viongozi wa Simba na Azam walionekana kutokuwa na imani na mimi, sielewi kwa nini!

Kingine kilichokuwa kikionekana kuwakera viongozi wa Simba na Azam ni kuona mashabiki wa Yanga wakinishangilia na mimi kuonyesha mapenzi yangu kwao.

Lakini binafsi nilijitahidi kucheza kwa uwezo wangu wote kwa lengo la kuwaonyesha kwamba, mawazo yao yalikuwa tofauti na ukweli wa mambo ulivyo.

Kama ulivyoona, katika mechi ya mwisho kati ya Simba na Yanga, niliweza kufanya juhudi kubwa na hatimaye kuipatia Simba penalti iliyopigwa na Mussa Mudde, lakini alikosa.

SWALI: Hivi ni kwa nini ulikataa ofa ya kwenda kucheza soka ya kulipwa katika klabu ya El-Merreikh ya Sudan wakati ilikuwa tayari kukulipa fedha nyingi?

JIBU: Si kweli kwamba nilikataa ofa ya kwenda kucheza soka ya kulipwa Sudan. Kilichotokea ni kwamba viongozi wa Simba na Azam walianza kujichanganya kuhusu klabu ipi iliyostahili kulipwa ada ya uhamisho. Klabu zote mbili zilitaka kuniuza bila kuzungumza na mimi.

Hivi katika ulimwengu wa sasa, kuna mchezaji yeyote anayeweza kukataa kulipwa pesa nyingi kama zilizoahidiwa na El-Merreikh? Kama yupo, atakuwa mtu wa ajabu. Mimi nilikataa kwenda Sudan kwa sababu niliona kuna ujanja ulikuwa unataka kufanyika.

Kwa jumla ninachoweza kusema kwa sasa ni kwamba, namshukuru Mungu nimemaliza salama mkataba wangu wa mkopo Simba na sasa nipo huru. Kiwango changu kilipanda sana nilipokuwa Simba. Niliifungia mabao mengi na kutoa pasi zilizozaa mabao. Soka ndiyo kazi yangu.

SWALI: Kwa maana hiyo siyo kweli kwamba ulikuwa ukicheza chini ya kiwango ulipokuwa Simba na Azam kwa lengo la kuzihujumu?

JIBU: Hicho kitu kisingewezekana kabisa kwangu. Nilichokuwa nikikifanya ni kutimiza wajibu wangu. Ninapaswa kuheshimu mkataba kati yangu na klabu yoyote. Mchezo wa soka ndio ulionifikisha hapa nilipo.

SWALI: Unaweza kueleza ni kwa nini ulipokuwa Azam kiwango chako kilikuwa cha chini tofauti na ulipojiunga na Simba, ambapo ulionyesha kiwango cha juu?

JIBU: Sina jibu la swali hilo kwa sababu mimi nilijiona nacheza katika kiwango changu cha kawaida. Lakini ni kweli kwamba, nilicheza vizuri zaidi nilipokuwa Simba kwa sababu nilipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wachezaji wenzangu. Na nilikumbana na upinzani mkali kutoka kwa wachezaji wa timu pinzani.

SWALI: Je, ni kweli kwamba ulishatia saini mkataba mwingine na Simba kabla ya ligi kumalizika?

JIBU: Sikuwahi kuongeza mkataba mwingine na Simba kwa sababu nilikuwa na mkataba na Azam. Kule nilikwenda kucheza kwa mkopo. Sielewi kwa nini viongozi wa Simba wananizulia uongo huo. Mkataba wangu na Simba ulishamalizika na nimekubali kurejea Yanga kutokana na kupata ofa nzuri.

SWALI: Kabla ya kuzichezea Yanga, Azam na Simba, uliwahi kuzichezea timu za Toto African na Kagera Sugar. Umejifunza nini kutokana na kuzichezea timu zote hizo?

JIBU: Ninachoweza kusema ni kwamba nimejifunza mambo mengi sana,kuanzia kwa viongozi, wanachama na mashabiki wa soka nchini. Wanasoka wa Tanzania wanakwamishwa na mambo mengi.

Pengine tatizo kubwa linalowaathiri wachezaji wa Tanzania ni kutotimiziwa haki zao ipasavyo na viongozi wa klabu. Ni vyema kila upande utimize wajibu wake, vinginevyo soka ya Tanzania itaendelea kudumaa.

Binafsi nisingekuwa makini wakati wa kuingia mikataba na klabu, nadhani hivi sasa ningekuwa kwenye matatizo makubwa. Pengine ningekuwa nahangaika kule Sudan huku wanaofaidika kupitia mgongo wangu ni wengine kabisa. Nawaomba wanasoka wenzangu wawe makini kuhusu suala la mikataba.

SWALI: Iwapo utapata nafasi nyingine ya kwenda kucheza soka ya kulipwa nje hivi sasa, utakuwa tayari kufanya hivyo?

JIBU: Nipo tayari kwenda kufanyiwa majaribio nje wakati wowote, lakini itabidi nipate baraka za viongozi wa Yanga kwa vile tayari nimeshaingia nao mkataba wa miaka miwili.

MOYES AANZA KIBARUA MAN UNITEDLONDON, England
KOCHA Mkuu mpya wa Manchester United, David Moyes mwanzoni mwa wiki hii alianza kazi katika klabu hiyo, ikiwa ni siku 43 kabla ya tarehe rasmi ya kutakiwa kufanya hivyo.

Moyes (50) aliwasili kwenye uwanja wa mazoezi wa klabu hiyo uliopo Carrington, Jumatatu iliyopita kabla ya saa 3.20 asubuhi kwa ajili ya kuanza maisha mapya ndani ya Old Trafford.

Kocha huyo wa zamani wa Everton anatakiwa kuanza rasmi kibarua cha kuinoa Manchester United, Julai Mosi mwaka huu, akichukua nafasi ya Sir Alex Ferguson. Ametia saini mkataba wa miaka sita.

Ferguson alikuwa miongoni mwa watendaji wa Manchester United waliompokea Moyes baada ya kuwasili Carrington pamoja na mtendaji mkuu aliyemaliza muda wake, David Gill.

Ujio wa Moyes kwenye uwanja wa Carrington ulipokelewa kwa mshangao mkubwa na wafanyakazi wachache wa uwanja huo kwa vile hawakumtarajia. Ilikuwa ni siku ya mapumziko.

Ferguson alimtambulisha Moyes kwa wafanyakazi hao na kumtembeza kwenye maeneo mbalimbali ya uwanja huo kabla ya kufanya naye mazungumzo kwa saa moja kwenye ofisi za kocha huyo.

Kocha huyo mpya wa Manchester United pia alipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya maofisa wa benchi la ufundi, akiwemo kocha wa makipa, Eric Steele. Alitarajia kukutana na kocha msaidizi namba mbili, Mike Phelan juzi asubuhi.

Katika mazungumzo yake na maofisa hao, Moyes aliwaeleza kuwa anatarajia kutangaza mabadiliko atakayoyafanya kwenye kikosi cha timu hiyo kesho.

Kocha huyo pia alizungumza na bosi wa kituo cha vijana cha klabu hiyo, Brian McClair na baadhi ya wasaidizi wake wakati walipokuwa wakijiandaa kucheza mechi ya fainali ya ligi kuu kwa timu za vijana wa chini ya miaka 21 dhidi ya Tottenham.

Katika mechi hiyo, vijana wa Manchester United walikuwa nyuma kwa mabao 2-0 kabla ya kuzinduka na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Hakukuwa na nafasi yoyote kwa Moyes kutoa hotuba kwa maofisa wa klabu hiyo. Ilikuwa ni nafasi yake ya kutembelea mazingira mapya kabla ya kuanza kibarua cha kuinoa timu hiyo.

Moyes alikaa kwenye uwanja huo kwa saa tatu kabla ya kuondoka kwa kutumia gari aina ya Chevrolet 4x4 lililokuwa likiendeshwa na mtunza vifaa wa klabu hiyo, Albert Morgan.

Baadaye kocha huyo wa zamani wa Everton aliongozana na Ferguson katika sherehe za kuwazawadia makocha wa ligi kuu ya England, ambapo Ferguson alitangazwa kuwa kocha bora wa mwaka.

Moyes alikanusha madai kuwa, aliandaliwa mapema na Ferguson kwa ajili ya kurithi mikoba yake. Alisema hizo zilikuwa hisia kwa vile wapo makocha wengi waliokuwa wakitajwa kumrithi Ferguson kama vile Roy Keane, Mark Hughes na Steve Bruce.

Hata hivyo, Moyes alieleza kuvutiwa kwake na Ferguson na kumwelezea kuwa ni kocha bora duniani.

Swali kubwa, ambalo mashabiki wa soka wa Manchester United wamekuwa wakijiuliza ni iwapo Moyes ataweza kufuata nyayo za Ferguson, ambaye alidumu kwenye klabu hiyo kwa miaka 27 na kuiwezesha kutwaa mataji lukuki.

Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya soka wamemuelezea Moyes kuwa, anafanana kwa kiasi fulani kiutendani na Ferguson ndiyo sababu bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo ilimpa kipaumbele kuliko makocha wengine.

Watu walio karibu na Moyes wanaamini kuwa, ana uwezo wa kuiongoza klabu hiyo kwa utaratibu ule ule uliokuwa ukitumiwa na Ferguson na pia kama alivyofanywa kwa Everton katika kipindi cha miaka 11 iliyopita.

Chanzo cha habari kimeeleza kuwa, Moyes amechangia kwa kiasi kikubwa kumshawishi beki Rio Ferdinand kuongeza mkataba wa mwaka mmoja kwa ajili ya kuichezea Manchester United msimu ujao.

Baadhi ya wachezaji wa Manchester United wamesema wapo tayari kukabiliana na changamoto mpya kutoka kwa Moyes baada ya kuanza kuinoa timu hiyo.

Moyes alizaliwa Aprili 25, 1963. Ni raia wa Scotland. Aliwahi kushinda tuzo za kocha bora wa mwaka wa England, 2003, 2005 na 2009.

Aliwahi kuwa mchezaji wa klabu ya Celtic ya Scotland na kuichezea katika mechi 540 akiwa beki wa kati. Pia amewahi kuzichezea klabu za Dunfermline Athletic na Preston North End.

Alianza kazi ya ukocha katika klabu ya Preston, akiwa kocha msaidizi kabla ya kupandishwa na kuwa kocha mkuu 1998.

Aliteuliwa kuwa kocha wa Everton 2002 na chini yake ilifuzu kucheza michuano ya ligi ya mabingwa wa Ulaya 2005 na kufuzu kucheza fainali ya Kombe la FA 2009.

Wakati wa sherehe za kutimiza miaka 10 katika klabu hiyo, Moyes alipokea pongezi nyingi kutoka kwa makocha wenzake, wakiwemo Ferguson, Arsene Wenger na Kenny Dalglish kutokana na mafanikio yake.

Moyes ni kocha wa tatu katika historia ya ligi kuu ya England kudumu kwenye klabu moja kwa miaka mingi, akiwa nyuma ya Ferguson na Wenger.

Kocha huyo mpya wa Manchester United anao watoto wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume. Baba yake, David Sr ni mfuatiliaji wa vipaji vya wachezaji katika klabu ya Everton. Mama yake, Joan anafanyakazi katika duka la nguo.

HAYNCKES: HAKUNA KAMA BAYERN MUNICH


KOCHA Mkuu wa Bayern Munich, Jupp Heynckes wiki iliyopita alionekana kujawa na furaha kubwa wakati timu yake ilipoichapa Augsburg mabao 3-0 na kukabidhiwa kombe la ubingwa wa Bundesliga.

Bayern Munich ilitwaa kombe hilo tangu Aprili 6 mwaka huu huku ikiwa imesaliwa na mechi sita mkononi. Imetwaa taji hilo baada ya kulikosa kwa miaka mitatu na mechi ya wiki iliyopita ilikuwa ya kukamilisha ratiba.

"Hakuna timu katika historia ya Bundesliga, ambayo imewahi kuonyesha kiwango cha soka kama tulichoonyesha sisi msimu huu,"alisema kocha huyo, ambaye mikoba yake inatarajiwa kurithiwa na Pep Guardiola mwishoni mwa msimu huu.

Guardiola anatarajiwa kuanza rasmi kibarua cha kuinoa Bayern Munich, Juni 26 na kusafiri nayo hadi katika mji wa Trentino nchini Italia kwa ajili ya kambi ya mazoezi inayotarajiwa kuanza Julai 4 hadi 12 mwaka huu.

"Tulicheza kwa kiwango cha juu na hilo limenifanya nione fahari kubwa," aliongeza kocha huyo, ambaye aliagwa na mashabiki wapatao 20,000 waliohudhuria mechi hiyo.

Taji hilo lilikuwa na maana kubwa kwa Bayern Munich kwa vile haikuwa imetwaa taji lolote tangu 2010 ilipotwaa ubingwa wa ligi hiyo na kombe la ligi.

"Furaha yenu inanieleza kwamba, mlikuwa na kiu kubwa ya kubeba taji hili na mmekuwa mkilisubiri kwa muda mrefu," kocha huyo aliwaeleza mashabiki wa Bayern Munich.

Heynckes aliwaahidi mashabiki hao kwamba, wanayo nafasi nyingine kubwa ya kutwaa taji la ligi ya mabingwa wa Ulaya wakati watakapomenyana na mahasimu wao, Borussia Dortmund katika mechi ya fainali itakayopigwa Mei 25 mwaka huu kwenye uwanja wa Wembley nchini England.

"Tutafanya kila tunaloweza kuhakikisha kwamba tunakipata kile, ambacho tumekuwa tukikiota kwa miaka mingi,"alisema kocha huyo.

Bayern Munich ilishindwa kutwaa taji hilo 2010 baada ya kufungwa na Inter Milan ya Italia katika mechi ya fainali kabla ya kulikosa tena msimu uliopita baada ya kufungwa na Chelsea.

Mbali na taji hilo, Bayern Munich pia inatarajiwa kumenyana na Stuttgart katika mechi ya fainali ya DFB-Pokal itakayochezwa Juni Mosi mwaka huu kwenye uwanja wa Olimpiki mjini Berlin.

Kwa upande wake, nahodha wa Bayern Munich, Philipp Lahm alisema bado kazi waliyoianza haijamalizika kwa sababu wamepania kuongeza mataji mawili zaidi.

"Kombe hili limerejea Munich, ambako ndiko mahali pake. Ni ndoto kuona idadi kubwa ya mashabiki hapa uwanjani,"alisema nahodha huyo alipokuwa akizungumzia ubingwa wa Bundesliga.

Lahm ndiye aliyepokea kombe la ubingwa kutoka kwa Rais wa Ligi ya Soka ya Ujerumani (DFL), Reinhard Rauball kwenye uwanja wa Allianz Arena.

Nahodha huyo wa Bayern Munich alisema lengo lao kubwa ni kuweka rekodi ya kutwaa mataji matatu msimu huu na kuendelea hivyo kwa miaka michache ijayo.

Lahm alisema anaona fahari kubwa kuwa nahodha wa Bayern Munich iliyotwaa ubingwa wa Bundesliga msimu huu na pia kuendelea kuwa katika kiwango cha juu.

"Kutwaa ubingwa wa ligi siku zote ni kitu muhimu na ni mafanikio makubwa kwa sababu mnakuwa mmecheza kwa kiwango bora katika mechi 34. Na msimu huu tumevunja rekodi chache,"alisema nahodha huyo.

Lahm alilielezea benchi la ufundi la klabu hiyo kwamba limefanyakazi nzuri na kumfanya kila mchezaji ajione muhimu katika timu.

Alisema kufuzu kwa Bayern Munich na Dortmund kucheza fainali ya ligi ya mabingwa wa Ulaya ni mafanikio makubwa katika soka ya Ujerumani na kuongeza kuwa, hawatakuwa tayari kuipoteza nafasi hiyo.

"Ni mechi itakayozikutanisha timu zenye kiwango cha juu. Na siku zote, timu itakayocheza kwa kiwango cha chini ama kufanya makosa ndiyo itakayopoteza mchezo,"alisema.

"Tutalazimika kuwa makini katika safu yetu ya ulinzi, kama ambavyo tumekuwa tukifanya msimu wote. Na tunayo safu nzuri ya ushambuliaji na siku zote imekuwa ikitafuta magoli kwa bidii,"aliongeza nahodha huyo.

Kwa mujibu wa Lahm, Bayern Munich itaendelea kuwa na mafanikio makubwa katika kipindi cha miaka michache ijayo, ndani na nje ya nchi hiyo.

JAYDEE: NITASAMBAZA ALBAMU YANGU KWA KUTUMIA MAX MALIPOMSANII nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura 'JayDee' amesema anatarajia kuuza albamu yake mpya ya Nothing but the Truth kwa kutumia wakala wa Max Malipo.

Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, JayDee alisema amefikia uamuzi huo kwa lengo la kudhibiti wizi wa kazi za sanaa na pia kuboresha soko la kazi zake.

JayDee alisema Max Malipo itaitumia Kampuni ya Posta yenye ofisi zake kote nchini kwa ajili ya kusambaza albamu hiyo.

"Naamini kwa kutumia wakala wa Max Malipo, albamu yangu itaweza kupatikana kote nchini na kwa muda mfupi,"alisema msanii huyo aliyewahi kushinda tuzo kadhaa za muziki nchini.

"Nataka nijaribu na kujifunza, nikifanya hivi itakuwaje au nifanyeje ili kuboresha soko la muziki wangu,"aliongeza.

Kwa mujibu wa msanii huyo, onyesho la uzinduzi wa albamu yake hiyo mpya limepangwa kufanyika Mei 31 mwaka huu kwenye ukumbi wa Nyumbani Lounge.

JayDee alisema katika onyesho hilo, atamshirikisha msanii Juma Kassim 'Nature', mwanamuziki mkongwe nchini, Hamza Kalala, Grace Matata na Joseph Haule 'Profesa Jay', ambaye ameshirikiana naye kuimba kibao cha Joto la hasira.

Msanii huyo anayemiliki bendi ya Machozi alisema, ameamua kuandaa onyesho la uzinduzi wa albamu hiyo kwa ajili ya kusherehekea kutimiza miaka 13 katika fani ya muziki.

Alisema katika kipindi hicho, ameweza kujifunza mambo mengi kuhusu muziki ikiwa ni pamoja na kupata uzoefu mkubwa wa fani hiyo.

Mwanadada huyo alisema alisimama kwa muda mrefu kutoa nyimbo mpya kutokana na kuelekeza nguvu zake zaidi katika bendi yake ya Machozi.

"Unajua usipotoa nyimbo kwa muda mrefu, si rahisi kupata maonyesho. Lakini kwa upande mwingine, bendi ina manufaa makubwa zaidi katika muziki,"alisema.

JayDee alikiri kuwa, muziki wa kizazi kipya kwa sasa umekuwa na mabadiliko makubwa, ikiwa ni pamoja na kutoa ajira nyingi kwa vijana na kuwabadilisha kimaisha.

Hata hivyo, alisema soko la muziki huo lilikuwa zuri miaka ya nyuma kutokana na kuwepo kwa wasanii wachache, tofauti na sasa, ambapo idadi ya wasanii wa muziki huo imekuwa kubwa na hivyo kusababisha mauzo yapungue.

Aliitaja changamoto nyingine inayowakabili wasanii wa muziki huo kuwa ni kukithiri wa wizi wa kazi za sanaa, ambapo baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakiendelea kudurufu nyimbo za wasanii na kutengeneza albamu bila ridhaa yao huku wengine wakifanya biashara ya kuingiza nyimbo za wasanii kwenye simu za mkononi bila kuwalipa chochote.

"Ninachowaomba watanzania ni kuendelea kuwaunga mkono wasanii wa muziki huu ili kuongeza ajira kwa vijana,"alisema msanii huyo mkongwe wa muziki wa kizazi kipya.

Pamoja na kupatikana kwa mafanikio hayo, JayDee alisema bado maonyesho yanayofanywa na wasani wa Tanzania katika baadhi ya nchi za Ulaya ni ya kiwango cha chini.

Alisema mara nyingi maonyesho hayo yamekuwa yakihudhuriwa na watanzania wachache wanaoishi katika nchi hizo za Ulaya, ama raia wengine kutoka nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda na zile zinazozungumza lugha ya kiswahili.

"Ninachoweza kusema ni kwamba, faida pekee wanayoipata wasanii wa Tanzania wanapokwenda Ulaya ni kusafiri, kujifunza mambo tofauti na kukutana na watu wengi,"alisema.

JayDee alisema binafsi amekuwa akitembelea baadhi ya nchi za Ulaya kwa ajili ya shughuli zake binafsi na ni mara chache amewahi kualikwa kufanya maonyesho.

Msanii huyo alisema amefurahi kukamilisha ndoto yake ya kurekodi wimbo na mwanamuziki mkongwe wa Zimbabwe, Oliver Mutukuzi na kwamba kwa sasa, ndoto nyingine aliyonayo ni kurekodi na mwanamuziki Dr. Dre wa Marekani.

Msanii huyo alisema pia kuwa, ndoto nyingine aliyonayo katika maisha yake ni kuanzisha kituo cha redio, ambacho kitakuwa kikifanyakazi kwa ajili ya watanzania wote.

Aliongeza kuwa, yupo tayari kutoa mchango wa mawazo kwa wasanii wanaochipukia wa muziki huo kuhusu nini la kufanya kwa lengo la kuendeleza vipaji vyao, lakini si kuwapa pesa kwa vile hana uwezo huo kwa sasa.

WASIFU WA JAYDEE
ALIZALIWA: Juni 15, 1979
KAZI: Mwanamuziki
NDOA: Ameolewa na mtangazaji wa redio, Gardner Habbash
TUZO ALIZOSHINDA: Msanii bora wa kike wa R&B (2002)
Albamu bora ya R&B (2004)
Video bora ya msanii wa kike nchini Afrika Kusini
(2005)
Wimbo bora wa mwaka wa Tanzania (2008)
Mwimbaji bora wa kike (2010)
Mwimbaji bora wa kike (2012)/
Mwimbaji bora wa kike anayechipukia Afrika Mashariki (2003, 2004 na 2005).

Tuesday, May 21, 2013

NGASA ATUA YANGA KWA MIL 30/-
HATIMAYE mshambuliaji Mrisho Ngasa wa klabu ya Simba ametia saini
mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia klabu yake ya zamani ya Yanga
kwa ajili ya michuano ya ligi kuu na kimataifa.

Japokuwa viongozi wa Yanga hawakuwa tayari kutaja kiwango cha pesa
walichomlipa mchezaji huyo, kuna habari kuwa, Ngasa amechota zaidi
ya sh. milioni 30 na atakuwa akilipwa mshahara wa sh. milioni tatu
kwa mwezi.

Mara baada ya kutambulishwa kwa waandishi wa habari jana makao
makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam,
Ngasa alisema amefurahi kurudi nyumbani.

Ngasa alisema amekubali kutia saini mkataba na Yanga kwa sababu ana
mapenzi na klabu hiyo, aliyokuwa akiichezea kabla ya kujiunga na
Azam.

"Nimefurahi kurejea katika klabu, ambayo naipenda. Nilicheza Simba
kwa ajili ya kazi tu na nilicheza kwa nguvu zangu zote ili kupata
ushindi, lakini hawakuwa na imani na mimi,"alisema.

Ngasa aliwasili makao makuu ya Yanga akiwa amefutana na Mwenyekiti
wa Yanga, Yussuf Manji, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Abdalla
Bin Kleb, mjumbe wa kamati ya usajili, Seif Ahmed 'Magari' na
mjumbe wa baraza la wadhamini, Francis Kifukwe.

Bin Kleb alisema ujio wa mchezaji huyo utaiongezea nguvu Yanga na
kwamba walimsaka mchezaji huyo kwa miezi sita kabla ya kufanikiwa
kumshawishi arejee nyumbani.

Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga, Lawrence Mwalusako alisema Ngasa ni
mchezaji mahiri nchini hivyo kurejea kwake Yanga ni faraja kubwa
kwa klabu hiyo.

Ngasa alijiunga na Yanga kwa mara ya kwanza 2006 akitokea Kagera
Sugar, ambayo ilimsajili kutoka Toto Africans. Mshambuliaji huyo
alikwenda kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa katika klabu
ya West Ham, 2009 kabla ya kwenda kujaribiwa Seattle Sounders ya
Marekani.