KWA HABARI ZA MICHEZO NA BURUDANI WASILIANA NASI KWA NAMBA 0719-153800 AU 0788-455808 AU EMAIL rashidzahor67@gmail.com '

Wednesday, October 27, 2010

K-One, msanii mwenye ndoto ya kufika mbali kimuziki


WASWAHILI wana msemo usemao, ‘Avumaye baharini papa, kumbe wengi wapo’. Hivyo ndivyo ilivyojidhihirisha kwa msanii chipukizi wa muziki wa kizazi kipya, Karim Othman, maarufu kwa jina la K-One.
Japokuwa jina lake si maarufu miongoni mwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, lakini umahiri wake wa kuimba na kutunga nyimbo zenye mashairi yenye mvuto umedhihirisha kwamba naye wamo.
K-One amedhihirisha ukali wake huo katika vibao vyake kadhaa, vikiwemo ‘Bila wewe’, ‘Sema baby’ , alivyowashirikisha wasanii nyota kama vile Ney wa Mitego na Pasha. Vibao hivyo viwili vimekuwa vikipigwa mara kwa mara kwenye vituo vya radio vya Times FM na Radio Uhuru.
Msanii huyo chipukizi amerekodi vibao hivyo katika studio za Brain Trust, zilizopo Temeke, Dar es Salaam kwa udhamini wa dada yake, ambaye hakupenda kumtaja jina.
Kwa mujibu wa K-One, amekuwa akipata sapoti kubwa ya kiusanii kutoka kwa familia yake, wakiwemo dada zake, ambao ndio wadhamini wake wakuu.
“Sio siri, naishukuru sana familia yangu, hasa bi mkubwa wangu (mama yangu) na dada zangu kwani wamekuwa wakinipa sapoti kubwa kiusanii. Japokuwa bado sijatoka kama ilivyo kwa wasanii wengine, lakini wamekuwa wakinipa moyo,”alisema msanii huyo.
Mbali na kurekodi vibao vyake, K-One pia amekuwa akishirikishwa kuimba viitikio katika nyimbo za wasanii mbalimbali maarufu wa muziki hao. Baadhi ya wasanii hao ni JB wa kundi la Mabaga Fresh na Mood Kibra.
Hivi sasa, K-One yupo katika hatua za mwisho za kukamilisha kibao chake kipya kinachokwenda kwa jina la ‘Valentine’. Amerekodi kibao hicho katika studio za Baucha Records.
Vibao vingine vilivyorekodiwa na msanii huyo, anayependa kutengeneza nywele zake kwa mtindo wa rasta ni ‘Kwa nini’, ‘Mpenzi sasa why’ na ‘Fau’. Amerekodi vibao hivyo kwenye studio za Brain Trust.
“Lengo langu ni kuwa na albamu moja ya nyimbo zangu zote. Naamini baada ya muda si mrefu, nitakuwa nimekamilisha albamu yenye nyimbo nane,”alisema msanii huyo.
Aliongeza kuwa, hadi sasa amekuwa akirekodi nyimbo zake kwa kutegemea msaada wa fedha kutoka kwa dada zake kwa vile bado hajapata wadhamini.
Ametoa mwito kwa wakuzaji wa vipaji vya wasanii nchini, kujitokeza kumsaidia kurekodi albamu yake na kusisitiza kuwa, hawatajutia uamuzi wao huo ama kupoteza fedha zao.
“Kipaji cha muziki ninacho na nimedhihirisha ukweli huo kupitia nyimbo zangu zilizofanikiwa kuzirekodi hadi sasa. Lakini ningependa kufika mbali zaidi, hivyo nawaomba mapromota wa muziki wa kizazi kipya wajitokeze kunidhamini,”alisema.
K-One alisema, muziki kwa sasa hapa nchini ni biashara na iwapo msanii atajiamini na kufanyakazi zake kwa umakini, ni rahisi kufaidi matunda ya jasho lake.
Kwa mujibu wa K-One, amepanga kukamilisha kazi ya kurekodi albamu yake kabla ya mwisho huu wa mwaka kumalizika. Alisema mambo yakienda vizuri, albamu yake hiyo itakuwa sokoni mwishoni mwa mwaka huu.
Je, ni kwa nini K-Onea aliamua kujitosa kwenye fani ya muziki wa kizazi kipya?
“Tangu nikiwa mdogo, nilipenda sana kushiriki katika maigizo na shughuli zozote zilizohusu mambo ya muziki. Ndipo nilipojigundua kwamba ninacho kipaji cha muziki kwani tangu nikiwa shule, niliweza kutunga mashairi ya wimbo,”alisema.
Kwa mujibu wa K-One, katika familia yake, hakuna ndugu yoyote aliyewahi kujihusisha na muziki huo. Ni yeye pekee, aliyejitosa kwenye fani hiyo baada ya kubaini kuwa, ana uwezo nayo.
“Lengo langu ni kuwaonyesha watanzania kwamba nina kipaji cha muziki. Pia nataka niutumie muziki kama ajira yangu kwa sababu ni biashara inayolipa,”alisema.
K-One ametoa wito kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, wapendane, kusaidiana na kuaminiana ili waweze kupiga hatua za juu zaidi kimaendeleo.
Alisema miongoni mwa sababu zinazochangia kuwakwamisha wasanii chipukizi wa muziki huo, ni kutokuwepo kwa umoja miongoni mwao, kuchukiana na kutosaidiana.
“Wasanii walio juu wanapaswa kukumbuka kuwa, kabla ya kufika huko waliko hivi sasa, nao walianzia chini, hivyo wasikwepe kuwasaidia wenzao wanaohitaji msaada kutoka kwao, hata kama wa kurekodi pamoja,”alisema.

Mwasiti kufyatua albamu mpya


BAADA ya ukimya wa muda mrefu, msanii Mwasiti Almasi ameibuka na kusema anatarajia kudondosha albamu yake mpya mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Akizungumza mjini Dar es Salaam wiki hii, Mwasiti alisema albamu yake hiyo itakuwa na vibao vinane, kikiwemo ‘Si kisa pombe’ alichokiimba kwa kumshirikisha rapa Quick Racka.
Albamu hiyo itakuwa ya pili kwa Mwasiti tangu alipoanza kung’ara katika muziki wa kizazi kipya, kutokana na tungo zake zenye mvuto na pia sauti maridhawa. Albamu yake ya kwanza inajulikana kwa jina la ‘Niambie’.
"Kwa sasa najiandaa kufyatua albamu yangu mpya ya pili, ambayo itakuwa na nyimbo nane na nimezirekodi kwenye studio tatu tofauti,” alisema mwanadada huyo.
Alizitaja studio alizorekodi vibao hivyo kuwa ni Ngoma Records, Fishcrab ya Lamar na Sound Crafters ya Enrico.
Licha ya maandalizi kuachia albamu hiyo kuendelea vyema, Mwasiti alisema hadi sasa bado hajaamua aiite jina gani kwa vile lengo lake ni kutafuta jina litakalowavuta mashabiki baada ya kuingia sokoni.
"Jina ndo bado naendelea kulitafuta, isipokuwa kila kitu kinaendelea vyema. Natumaini kila kitu kitakamilika mwezi ujao," alisema.
Mwanadada kutoka kundi la THT, alianza kutamba mara baada ya kuachia wimbo uliotamba wa 'Haooo' kabla ya kufyatua vibao vingine kama vile 'Niambie,' 'Huruma' na 'Nalivua pendo'.

Genevieve aendelea kuchemsha China

SANYA, China
MATUMAINI ya mrembo wa Tanzania, Genevieve Emmanuel kufanya vizuri katika shindano la kumsaka mrembo wa dunia mwaka huu, yamezidi kuota mbawa baada ya kuvurunda katika kinyang’anyiro cha kuwania mataji ya michezo na mitindo ya mavazi.
Katika kinyang’anyiro hicho, kilichowashirikisha warembo wote 119 wanaoshiriki kwenye shindano hilo, mrembo Lori Moore kutoka Ireland Kaskazini aliibuka mshindi wa taji la michezo wakati mrembo Mariann Birkedal kutoka Norway alitwaa taji la mitindo ya mavazi.
Mashindano ya kuwania mataji hayo pamoja na lile la vazi la ufukweni, hufanyika kabla ya fainali ya shindano hilo. Tayari Genevieve ameshachemsha katika taji la ufukweni, ambalo lilinyakuliwa na Yara Santiago kutoka Puerto Rico.
Washindi wa mataji hayo, wamefuzu moja kwa moja kuingia kwenye fainali ya shindano hilo, ambayo imepangwa kufanyika Oktoba 30 mwaka huu mjini Sanya.
Shindano la kuwania taji la michezo ndilo lililokuwa na mvuto wa aina yake kutokana na washiriki wote kuonyesha vipaji vyao katika michezo mbalimbali. Shindano hilo lilifanyika kwenye ufukwe wa hoteli ya Sheraton.
Mrembo Lori alishinda taji hilo baada ya kufanya vizuri na kutia fora katika michezo ya kuruka juu, mbio fupi na kuogelea. Alama alizozipata katika michezo hiyo ndizo zilizomwezesha kuibuka mshindi.
“Siwezi kuamini. Nimefuzu kuingia fainali,”alisema Lori, ambaye alizawadiwa medali.
Mshindi wa pili wa taji hilo alikuwa Marina Georgievo kutoka Slovakia wakati nafasi ya tatu ilinyakuliwa na Mariann wa Norway. Wote wawili pia walizawadiwa medali.
Katika kinyang’anyiro cha kuwania taji la mitindo ya mavazi, Mariann kutoka Norway aliibuka mshindi akifuatiwa na mrembo Irina Sharipova kutoka Russia na Alexandria Mills kutoka Marekani.
Katika kuwania taji hilo, washiriki walichuana kwa mavazi mbalimbali yaliyobuniwa na wabunifu maarufu wa mavazi wa China na kuwapa wakati mgumu majaji katika kuamua mshindi.
“Kwa kweli siwezi kuamini kwamba nimewashinda wasichana wengi na kuibuka mshindi wa taji hili,”alisema Mariann. “Ni heshima kubwa kwangu na bila shaka, nimefurahia kuingia fainali.”

Thursday, October 21, 2010

AZAM YAMKANA PHIRI


UONGOZI wa klabu ya Azam umesema, hauna mpango wa kumnyakua Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri katika mzunguko wa pili wa ligi kuu ya Tanzania.
Azam imesema, inauheshimu mkataba wa Phiri na Simba na kusisitiza kuwa, hauwezi kufanya mazungumzo na kocha huyo ama kufikiria kumwajiri wakati bado ana kibarua sehemu nyingine.
Msimamo huo wa Azam umekuja siku chache baada ya baadhi ya vyombo vya habari nchini kuripoti wiki hii kuwa, klabu hiyo imefanya mazungumzo na Phiri kwa lengo la kumwajiri.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Turiani mjini Morogoro jana, Mratibu wa timu hiyo, Mohamed King alisema hakuna kiongozi yeyote wa klabu hiyo aliyewahi kukutana na kufanya mazungumzo na Phiri.
"Ninachoweza kusema ni kwamba, habari hizo ni za uzushi kwa sababu hazina ukweli wowote. Sisi kama Azam tunaheshimu mkataba kati ya Phiri na Simba,”alisema.
Mratibu huyo alisema, kwa sasa Azam itaendelea kuwa chini ya kocha wake mkuu, Itamar Amorin kutoka Brazil akisaidiwa na Habibu Kondo.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa, Phiri huenda akajiunga na Azam siku chache zijazo baada ya kutokea hali ya kutokuelewana kati yake na viongozi wa Simba.
Hata hivyo, habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimeeleza kuwa, mkataba wa Phiri kuinoa timu hiyo unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi ujao.
Naye Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo amesema, taarifa za Phiri kwenda Azam sio za kweli kwa vile mkataba wa kocha huyo unatarajiwa kumalizika Januari mwakani.
"Phiri hawezi kuondoka Simba kwa sababu bado ana mkataba nahajawahi kuzungumza na viongozi wa Azam,"alisema Ndimbo alipozungumza kwa njia ya simu jana kutoka Mwanza.

BITEBO: Simba, Yanga zinashusha kiwango cha Stars

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MWANASOKA wa zamani wa timu ya Pamba ya Mwanza, Khalid Bitebo, amesema klabu za Simba na Yanga zimekuwa zikichangia kushuka kwa kiwango cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Akizungumza mjini hapa mwishoni mwa wiki iliyopita, Bitebo alisema uamuzi wa klabu hizo kongwe nchini kusajili wachezaji wengi wa kigeni, ndio unaosababisha kiwango cha Taifa Stars kushuka.
Bitebo, ambaye enzi zake alikuwa maarufu kwa jina la Zembwela alisema, kuwepo kwa wachezaji wengi wageni katika klabu hizo kunawanyima nafasi wanasoka wazalendo kuonyesha vipaji vyao.
“Mimi siku zote huwa nasema, Simba na Yanga ndio mhimili wa soka ya Tanzania. Klabu hizi mbili ndizo zinazotoa wachezaji wengi wa Taifa Stars, hivyo zinaposajili wachezaji wengi wa kigeni, zinawanyima nafasi wanasoka wazalendo kuonyesha vipaji vyao,”alisema.
Aliongeza kuwa, japokuwa wanasoka wa kigeni wanasaidia kuleta ushindani katika ligi, lakini wingi wao ndani ya Simba na Yanga unashusha ari ya wanasoka wazalendo.
Mkongwe huyo wa soka alisema ni vyema viongozi wa Simba na Yanga wabadili mwelekeo kwa kutoa kipaumbele zaidi katika kusajili wachezaji wazalendo badala ya wageni.
Bitebo pia alieleza kushangazwa kwake na kiwango duni cha soka kilichoonyeshwa na timu za Simba na Yanga zilipomenyana katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara iliyochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema kutokana na ukongwe wa timu hizo, uwezo zilionao kifedha na pia kuundwa na wanasoka wengi wageni, Simba na Yanga hazikupaswa kuonyesha kiwango duni.
Katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Yanga iliichapa Simba bao 1-0 na kuendeleza rekodi ya ushindi kwa watani wao hao.

MIMI NI YANGA DAMU!


HIVI ndivyo anavyoelekea kusema Kocha Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic wakati alipokuwa akiingia kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza kabla ya timu hiyo kumenyana na Simba katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara. Yanga ilishinda bao 1-0.

SIMBA YAIPUMULIA YANGA

Na Mwandishi Wetu, Mwanza
SIMBA jana ilizunduka katika michuano ya soka ya ligi kuu ya Tanzania Bara baada ya kuicharaza AFC mabao 3-1 katika mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Kwa matokeo hayo, Simba bado inashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi hiyo, ikiwa na pointi 18 baada ya kucheza mechi nane, nyuma ya vinara Yanga wanaoongoza kwa kuwa na pointi 19.
Yanga inaweza kuongeza tofauti ya pointi kati yake na Simba iwapo itaishinda JKT Ruvu leo katika mechi nyingine ya ligi hiyo, itakayochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.
Simba ingeweza kuifunga AFC mabao mengi zaidi, hasa kipindi cha pili, lakini papara za washambuliaji wake, Emmanuel Okwi, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Patrick Ochan zilikuwa kikwazo.
Pambano hilo halikuwa na mvuto katika kipindi cha kwanza kutokana na timu zote kucheza soka ya kiwango cha chini na kushindwa kugongeana pasi za uhakika.
Iliwachukua Simba dakika tatu kuhesabu bao la kwanza lililofungwa na Hillary Echesa kwa mpira wa adhabu baada ya Emmanuel Okwi kuangushwa na beki mmoja wa AFC nje kidogo ya eneo la hatari.
Dakika tano baadaye, Jerry Santo aliiongezea Simba bao la pili baada ya kumalizia pasi maridhawa aliyotanguliziwa na Amri Kiemba.
AFC ilipata nafasi nzuri ya kufunga bao dakika ya 25 wakati Abdalla Juma alipofumua shuti kali la umbali wa mita 20, lakini kipa Juma Kaseja alilipangua na kuwa kona isiyokuwa na matunda.
Dakika ya 28, Ochan alitengenezewa pasi safi na Haruna Shamte na kubaki ana kwa ana na kipa Azizi Simon, lakini shuti lake lilitoka pembeni ya lango.
Okwi aliipotezea Simba nafasi nyingine nzuri ya kufunga bao dakika ya 33 baada ya kuwatoka mabeki wawili wa AFC, lakini shuti lake lilitoka nje.
AFC ilijibu mapigo dakika ya 45 baada ya Bakari Kigodeko kupewa pasi na kubaki uso kwa uso na kipa Kaseja wa Simba, lakini shuti lake lilitoka nje. Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 2-0.
Mchezo ulichangamka katika kipindi cha pili baada ya AFC kupata bao la kujifariji dakika ya 54. Bao hilo lilifungwa na mshambuliaji Jimmy Shoji baada ya kuunganisha wavuni kona iliyochongwa na Kigodeko.
Dakika 10 baadaye, Mgosi aliiongezea Simba bao la tatu, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na Okwi na Azizi Gilla waliogongeana pasi nzuri pembeni ya uwanja kabla ya kutoa pasi kwa mfungaji.
AFC ilipata pigo dakika ya 71 baada ya beki wake, Amri Msumi kutolewa nje kwa kadi nyekundu kwa kosa la kumchezea rafu mbaya Okwi. Awali, Msumi alikuwa ameonyeshwa kadi ya njano.
Pamoja na kucheza ikiwa pungufu, AFC ilipata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao dakika ya 83 na 86, lakini zilipotezwa na Abdallah Juma na Shoji baada ya mashuti yao kuokolewa na kipa Kaseja.
Papara za Mgosi na Okwi ziliikosesha tena Simba bao dakika ya 90 baada ya kutokea piga nikupige kwenye lango la AFC. Shuti la kwanza la Mgosi lilimbabatiza kipa Azizi Simon wa AFC na lile la pili la Okwi lilitoka nje.
Simba: Juma Kaseja, Haruna Shamte, Juma Jabu, Kevin Yondani, Juma Nyoso, Hillary Echesa/ Mussa Mgosi, Jerry Santo, Amri Kiemba/Azizi Gilla, Rashid Gumbo, Patrick Ochani, Emmanuel Okwi.
AFC: Azizi Simon, Simon Mganga/Zahor Jairani, Andrew Carlos, Amri Msumi, Mohamed Upatu, Razaki Muhidin, Abdalla Juma, Kiworu Francis/Simon Nsajigwa, Juma Shoji, Bakari Kigodeko, Hilali Bigwa.

Genevieve aanza vibaya Miss World


SANYA, China
MREMBO wa Tanzania, Genevieve Emmanuel ameanza vibaya mashindano ya mwaka huu ya kuwania taji la dunia baada ya kutolewa mapema katika kinyang’anyiro cha vazi la ufukweni.
Genevieve hakuwa miongoni mwa warembo 40 waliovuka mchujo wa awali wa kuwania taji hilo. Alikuwa miongoni mwa warembo 79 waliotolewa mapema.
Taji hilo lilinyakuliwa na mrembo Yara Santiago kutoka Puerto Rico, ambaye sasa ataingia moja kwa moja katika hatua ya nusu fainali ya shindano hilo.
Katika shindano hilo lililofanyika juzi kwenye ufukwe wa mji wa Sanya, mrembo Alexandria Mills kutoka Marekani alishika nafasi ya pili akifuatiwa na Mariann Bincedal kutoka Norway.
Warembo 40 waliofuzu kuingia hatua ya nusu fainali ya shindani hilo walitoka katika nchi za Argentina, Australia, Bahamas, Barbados, Botswana, Bolivia, Bosnia & Herzegovina, Cape Verde, Cayman Islands, China PR, Jamhuri ya Czech, Ufaransa, French Polynesia, Ghana, Guadeloupe na Hong Kong China.
Wengine ni kutoka nchi za Hungary, India, Israel, Italia, Lithuania, Luxembourg, Martinique, Moldova, Mongolia, Uholanzi, New Zealand, Norway, Paraguay, Puerto Rico, Russia, St Lucia, Scotland, Sri Lanka, Thailand, Trinidad & Tobago, Uturuki, Ukraine, Marekani na Zimbabwe.
Kwa mujibu wa taratibu za shindano hilo, katika hatua za awali, washiriki huchuana katika kuwania taji la vazi la ufukweni, vipaji vya michezo na mrembo anayependeza kwenye picha (miss photogenic).
Fainali ya mashindano ya mwaka huu imepangwa kufanyika Oktoba 30, ambapo washiriki kutoka nchi 119 wanatarajiwa kupanda jukwaani kuwania taji hilo.
Katika mashindano hayo, bara la Afrika litawakilishwa na warembo kutoka nchi 18. Nchi hizo ni Angola, Botswana, Ivory Coast, Misri, Ethiopia, Ghana, Kenya, Lesotho na Malawi.
Zingine ni Mauritius, Namibia, Nigeria, Sierra Leone, Afrika Kusini, Uganda, Zambia, Zimbabwe na Tanzania.
Pamoja na kushindwa kufanya vizuri katika shindano la vazi la ufukweni, mrembo Emma Wareus kutoka Botswana ametajwa kuwa ni miongoni mwa wanaopewa nafasi kubwa ya kutwaa taji la dunia mwaka huu.
Shirika la Habari la OLBG limemwelezea Emma kuwa, ni mrembo mwenye sifa na vigezo vyote vinavyostahili kumfanya ashinde taji hilo, akifuatiwa na Kamilla Salgado kutoka Brazil na Laura Restrepo kutoka Colombia.
Emma amekuwa kivutio kikubwa tangu washiriki walipowasili mjini Sanya kutokana na uzuri wake wa sura na umbo na pia mambo mbalimbali, ambayo amekuwa akiyafanya.
Shirika hilo liliwataja warembo wengine wa Afrika wanaopewa nafasi ya kufanya vizuri kuwa ni Samantha Tshuma kutoka Zimbabwe, Ivaniltan Jones kutoka Angola na Zindaba Hanzala kutoka Zambia.

ROONEY: Bye bye Man Utd


LONDON, England
HATIMAYE Kocha Mkuu wa Manchester United, Sir Alex Ferguson amefichua kuwa, mshambuliaji Wayne Rooney anataka kuondoka katika klabu hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa juzi, Ferguson alikiri kuwa alipatwa na mshtuko na kukatishwa tamaa kusikia habari hizo, lakini alikanusha kuwepo na hali ya kutokuelewana kati yake na mchezaji huyo.
“Tumechanganyikiwa kama inavyoweza kutokea kwa yeyote, lakini hatuwezi kuelewa kwa nini anataka kuondoka,”alisema kocha huyo raia wa Scotland. Hata hivyo, Ferguson alisema milango ipo wazi kwa Rooney iwapo atabadili uamuzi wake huo. Rooney alishindwa kuichezea Manchester United jana katika mechi ya ligi ya mabingwa wa Ulaya dhidi ya Bursaspor kutokana na kuwa majeruhi.
Hatima ya Rooney kuendelea kuwepo Manchester United ilikuwa shakani, kufuatia kuwepo na habari kwamba aligoma kutia saini mkataba mpya wa kuichezea klabu hiyo. Mkataba wa sasa wa Rooney unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu wa 2011/12.
Akihojiwa na kituo cha televisheni cha MUTV kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari juzi, Ferguson alisema Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, David Gill alimweleza kuhusu uamuzi huo wa Rooney kutosaini mkataba mpya.
“Nilikuwa ofisini Agosti 14 na David alinipigia simu kunieleza kwamba Rooney hatasaini mkataba mwingine,”alisema Ferguson.
“Miezi michache iliyopita alisema yupo kwenye klabu kubwa dunia na anataka kubaki hapa maisha yake yote. Hatuelewi nini kimebadili msimamo wa kijana huyu,”aliongeza.
Mara baada ya kupata taarifa hizo, Ferguson alisema aliomba kuzungumza na mchezaji huyo, ambaye alimuhakikishia kuhusu uamuzi wake huo.
Ferguson alisema amesikitishwa na uamuzi huo wa Rooney kwa sababu alifanya kila analoweza kumsaidia tangu alipojiunga na klabu hiyo mwaka 2004 akitokea Everton.
“Hatuna tulichokifanya zaidi ya kumsaidia tangu alipowasili katika klabu hii,”alisema Ferguson, ambaye bado hajakata tamaa ya kumzuia mchezaji huyo asiondoke.
Wakati huo huo, Rooney amewadokeza wachezaji wenzake wa Manchester United kuwa, huenda akafikiria kujiunga na mahasimu wao, Manchester City.
Rooney alielezea msimamo wake huo siku chache baada ya kuieleza Manchester United kwamba, hatarajii kuongeza mkataba mpya na klabu hiyo.
Tayari Manchester City imeshaonyesha dhamira ya kumsajili mchezaji huyo wakati wa usajili wa dirisha dogo Januari mwakani na ipo tayari kumlipa mshahara wa pauni 230,000 (sh. milioni 529) kwa wiki.
Iwapo Manchester City itafanikiwa kumsajili Rooney, atakuwa ndiye mchezaji ghali kuliko wote wanaocheza katika ligi kuu ya England hivi sasa.
Baadhi ya wachezaji wa Manchester United wamelieleza gazeti la Daily Mail kuwa, uamuzi wa Rooney kuondoka klabu hiyo unatokana na masuala ya pesa na si kutokuelewana kwake na Kocha Sir Alex Ferguson.
Mke wa mwanasoka huyo, Coleen ameshamweleza wazi mumewe kuwa, hawezi kwenda nje ya England, hasa katika kipindi hiki, ambacho dada yake, Rosie ni mgonjwa.
Msimamo huo wa Coleen umemfanya Rooney akubali kubaki England na kujiunga na moja kati ya klabu za Manchester City na Chelsea, ambazo ndizo pekee zenye uwezo wa kumlipa mshahara mnono na kumudu ada ya uhamisho.
Rooney amewaeleza wazi wachezaji wenzake kuwa, hatafikiria mara mbili kujiunga na Manchester City iwapo klabu hiyo itawasilisha maombi ya kumsajili kabla ya Januari mwakani.
Kwa mujibu wa sheria za Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), Rooney anaruhusiwa kulipa pauni milioni tano kwa ajili ya kuvunja mkataba wake, iwapo utakuwa umesalia mwaka mmoja kabla ya kumalizika.
Kipengele hicho ndicho kilichozua hofu kwa viongozi wa Manchester United, ambao wana wasiwasi kuwa, wasipomuuza Januari mwakani, huenda akavunja mkataba wake ama kuhama bila kulipiwa ada.
Kocha Mkuu wa Chelsea, Carlo Ancelotti alisema juzi kuwa, atafikiria kumsajili mshambuliaji huyo wakati Kocha Mkuu wa Manchester City, Roberto Mancini bado anafuatilia hatma ya mchezaji huyo katika klabu ya Manchester United.
“Kwa sasa, Chelsea haitarajii kumsajili Rooney kwa sababu bado ni mchezaji wa Manchester United na nafikiri bado wanaweza kumaliza tatizo lililojitokeza,”alisema Ancelotti.
“Kama Rooney atawekwa sokoni, si Chelsea pekee itakayotaka kumsajili, bali na klabu zingine kubwa duniani,”aliongeza.
Klabu nyingine iliyoonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa England ni Real Madrid ya Hispania. Lakini kocha wake, Jose Mourinho alikuwa mwangalifu kuzungumzia suala hilo kwa hofu ya kumchefua Ferguson.
“Sifikirii iwapo atahama. Nafikiri kocha wake atamshawishi abaki,”aliongeza.
Mkurugenzi wa Real Madrid, Jorge Valdano alifichua juzi kuwa, anavutiwa na mchezaji huyo, lakini hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo.
Real Madrid imekuwa ikihusishwa na mipango ya kumsajili Rooney tangu msimu uliopita, ambapo rais wake wa zamani, Ramon Calderano alidai mapema mwaka huu kuwa, mrithi wake, Florentino Perez naye anavutiwa na mchezaji huyo.
Valdano alilieleza gazeti la Telemadrid: "Navutiwa sana na Rooney, lakini swali la kujiuliza ni je, kama Rooney atakuja, nani tutamwondoa kwenye timu. Tunao wachezaji wazuri wa safu ya ushambuliaji, akina Ronaldo, Higuain, Ozil na Di Maria.”
Rais huyo wa zamani wa Real Madrid alisema pia kuwa, klabu hiyo ina hazina ya wachezaji wengi chipukizi, ambao wataifanya isiwe na tatizo la kusajili wachezaji nyota kutoka nje kwa kipindi cha miaka kumi ijayo.
Taarifa za Rooney kutaka kufuata nyayo za Carlos Tevez, aliyejiunga na Manchester City msimu uliopita akitokea Manchester United, huenda zikawashtua mashabiki wa klabu hiyo.
Uhusiano wa Rooney na Kocha Ferguson umekuwa mbovu tangu mchezaji huyo alipokumbwa na kashfa ya kufanya mapenzi na changudoa.
Kocha Ferguson amekuwa akimweka benchi Rooney katika mechi kadhaa za ligi kuu ya England huku akitoa taarifa kwamba, mchezaji huyo ni majeruhi.
Hata hivyo, Rooney amezikana taarifa hizo za Ferguson na kusisitiza kuwa, yupo fiti na hajawahi kuumia tangu msimu huu ulipoanza.
Tayari Manchester United imeshaeleza wazi kuwa, haina mpango wa kumuuza Rooney wakati wa dirisha dogo na imeziita taarifa hizo kuwa ni za uzushi.
Katika hatua nyingine, kiungo wa zamani wa Manchester United, Roy Keane amemwonya Rooney awe makini katika kufikia uamuzi wa kuihama klabu hiyo.
Keane alisema juzi kuwa, kutokuelewana kwa Rooney na Ferguson hakupaswi kuwa kigezo cha yeye kuhama kwa vile wachezaji na makocha kukorofishana mara kwa mara ni jambo la kawaida katika maisha ya soka.

Niliandika usia nikiwa kitandani-Cherly ColeLONDON, England
MWANAMUZIKI nyota wa Uingereza, Cherly Cole amefichua kuwa, aliandika usia juu ya kifo chake akiwa kitandani baada ya madaktari kumweleza kwamba, alikuwa hatarini kupoteza maisha kutokana na kuugua ugonjwa wa malaria.
Cherly (27), mke wa zamani wa beki Ashley Cole wa klabu ya Chelsea ya England amesema, alipewa saa 24 za kuendelea kuishi wakati alipokuwa akipambana na ugonjwa huo miezi minne iliyopita.
Mwanamuziki huyo wa kundi la zamani la muziki la Girls Aloud, amefichua hayo alipokuwa akihojiwa na kituo kimoja cha televisheni cha Uingereza kuhusu maisha yake.
“Niliandika usia juu ya kifo changu nikiwa kitandani,”alisema Cherly wakati wa mahojiano hayo.
Katika mahojiano hayo yaliyodumu kwa saa mbili, mwimbaji huyo pia alizungumzia kwa uwazi kuhusu kuvunjika kwa ndoa yake na Ashley Cole na kusisitiza kuwa, siku zote bado ataendelea kumpenda.
Alisema kuvunjika kwa ndoa yao kuliufanya moyo wake usononeke, lakini bado anamuheshimu na kumpenda mwanasoka huyo, ambaye pia anachezea timu ya taifa ya England.
Cherly alidokeza kuwa, bado amekuwa akiwasiliana mara kwa mara na Cole, licha ya kumsaliti katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya ndoa yao. Wanandoa hao walitengana rasmi Septemba mwaka huu.
Mwanadada huyo alidondokwa na machozi aliposema kuwa, bado anaamini Cole alikuwa mwanaume mwaminifu na kuongeza: “Kwa vile tumeshalimaliza tatizo hili, natumaini tunaweza kuwa tena marafiki. Siku zote nitaendelea kumpenda Ashley.”
“Nikitazama nyuma tulikotoka, najihisi kama niliyeganda. Tulikuwa na ndoa nzuri na yenye furaha na siku ya harusi yetu, ilikuwa ya aina yake, lakini sielewi nini kilichotokea. Hadi sasa, bado najiuliza swali hilo,”alisema mwanamuziki huyo.
Cherly, mzaliwa wa mji wa Newcastle wa Uingereza, alishindwa kushiriki katika maandalizi ya kipindi cha X Factor, kufuatia kuugua malaria Julai mwaka huu. Alijiunga na kipindi hicho mwishoni mwa wiki iliyopita kilipoanza kuonyeshwa laivu baada ya kuonekana yupo fiti.
Wakati wote wa mahojiano hayo, Cherly alikuwa karibu na mama yake mzazi, Joan pamoja na wanamuziki wenzake wa kundi la Girls Aloud, Kimberley Walsh na Nicola Roberts, ambao walitokwa machozi alipokuwa akizungumzia ugonjwa wa malaria.
Kwa mujibu wa Cherly, madaktari walimweleza kwamba alikuwa hatarini kufa baada ya kupatwa na ugonjwa huo alipokuwa ziarani nchini Tanzania.
Alikiri kwamba, alikunywa chupa tatu za vodka usiku, siku moja kabla ya kupiga picha za ziara yao nchini Tanzania na kujihisi kama aliyelewa kupita kiasi. Alisema huo ulikuwa ndio mwanzo wa kuugua kwake malaria.
Cherly alikiri kuwa, ni wakati alipokuwa akiugua ugonjwa huo, ndipo alipoamua kuandika wosia na kufikiria jinsi ya kugawanya mali zake kwa rafiki na familia yake.
“Nilifikiri ningekufa. Ukweli ni kwamba, nilifikiri nilikuwa nikikaribia kufa. Nilifikiri kama nilikaribia kufa, nataka nife haraka kwa sababu nilikuwa kwenye maumivu makali,”alisema.
Cherly, ambaye aliingiza pauni milioni 1.2 za Uingereza kutokana na vipindi vilivyopita vya X Factor, pia alizungumzia uhusiano wake na Simon Cowell.
“Ni mmoja wa watu muhimu katika maisha yangu,”alisema Cherly.
Hata hivyo, Cherly alikiri kuwa, kwa sasa, hapati nafasi ya kujihisi mwanamke wa kawaida kama ilivyokuwa zamani. “Baadhi ya wakati najihisi kama niliye mtegoni,”alisema Cherly. “Siwezi kurudi Newcastle na kuvaa suti za michezo na raba.
Katika hatua nyingine, Cherly ametunga wimbo unaoelezea maisha ya ndoa kati yake na Ashley Cole na yaliyojitokeza baada ya ndoa hiyo kuvunjika. “Niliuza almasi zote na kuchoma moto nguo zako zote,” ameimba Cherly katika moja ya beti za wimbo huo, alioupa jina la ‘Happy Tears’.
Maneno mengine yaliyomo kwenye wimbo huo ni kama ifuatavyo:
‘Nililia wakati niliposikia umetembea nje ya ndoa Nililia wakati niliposema naondokaNilikata nywele zangu na kuchora vidole gumba vyanguNililia wakati suti yako iliposhika motoNililia wakati moyo wangu uliposhindwa kuaminiLakini sasa sitokwi tena na machozi’
Wimbo huo ni miongoni mwa vibao vipya vya mwanamuziki huyo vilivyomo kwenye albamu yake ya ‘Messy Little Raindrops’, inayotarajiwa kuingia sokoni Novemba Mosi mwaka huu.
Katika albamu hiyo, Cherly ameonyesha uwezo mkubwa wa kuimba kwa hisia kali na imeelezwa kuwa, mahojiano yake na televisheni moja ya Uingereza huenda yakamsaidia kuongeza mauzo.
Cherly alisema, anataka albamu yake hiyo iwe na mvuto wa aina yake kwa mashabiki na ndio sababu kava yake imetengenezwa kwa utaalamu wa hali ya juu.
“Naifurahia albamu hii, lakini siwezi kuweka wazi kila kitu hadi wakati utakapowadia,”alisema mwanamuziki huyo mwenye mvuto na kuongeza kuwa, japokuwa hakuandika mashairi ya nyimbo zake yeye mwenyewe, lakini aliyapitia na kuridhika nayo.
Kibao kingine kilichomo kwenye albamu hiyo ni pamoja na ‘Promise This’, ambacho kimeshaanza kushika chati kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini Uingereza. Cherly anaamini ataongeza umaarufu wa kibao hicho wakati atakapofanya onyesho kwenye kipindi cha X Factor kitakachorushwa hewani Oktoba 24 mwaka huu.
000000

Jokha Kassim aipua albamu yake binafsi


MWIMBAJI nyota wa muziki wa taarab nchini, Jokha Kassim amekamilisha kazi ya kurekodi albamu yake binafsi, inayokwenda kwa jina la ‘Acha nijishebedue’.
Akizungumza mjini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Jokha alisema albamu hiyo itakuwa na vibao vinne, ambavyo alijigamba kuwa ni moto wa kuotea mbali.
Alivitaja vibao hivyo kuwa ni ‘SMS za nini’, ‘Kinyang’anyiro’, ‘Kelele za mlango’ na ‘Acha nijishebedue mke mwenzangu anijue’.
Uamuzi wa Jokha, mwimbaji wa kundi la Five Stars Modern Taraab kurekodi albamu hiyo, umekuja wakati mwimbaji mwenzake, Isha Ramadhani ‘Mashauzi’ akiendelea kutesa na albamu yake ya ‘Mama nipe radhi’.
Isha alirekodi albamu hiyo mapema mwaka huu na hadi sasa vibao vyake kama vile ‘Mama nipe radhi’, ‘Tugawane ustaatabu’ na ‘Kila mtu na mtuwe’ vikishika chati kwenye vituo mbalimbali vya radio na televisheni nchini.
"Nimeamua kutoka na albamu yangu ili kuonyesha kipaji na uwezo wangu katika fani hii ya uimbaji wa taarab. Naamini albamu hii itashika vilivyo,"alijigamba Jokha.
Mwimbaji huyo mwenye sauti yenye mvuto na sura jamali alisema, albamu hiyo inatarajiwa kuingia sokoni hivi karibuni na kuwataka mashabiki wake wajiandae kupata uhondo babu kubwa.
Jokha alisema uzinduzi wa albamu hiyo utafanyika katika jiji la Dar es Salaam na utasindikizwa na baadhi ya waimbaji nyota wa muziki huo nchini, wakiwemo Khadija Omar Kopa na Isha Mashauzi.
Kabla ya kujiunga na Five Stars Modern Taarab, Jokha aliwahi kutamba katika vikundi vya Zanzibar Stars, East African Melody na Jahazi.
Baadhi ya vibao vilivyomweka kwenye chati ya juu katika muziki wa taarab ni pamoja na 'Utakufa nacho’, ‘Alonacho kajaaliwa’, ‘Mtenda akitendewa’ na ‘Aso mtu ana Mungu’.
Katika hatua nyingine, kundi la muziki wa taarab la Five Stars linatarajiwa kufyatua albamu mbili kwa mpigo mwishoni mwa mwezi huu.
Rais wa kundi hilo, Ally Jay alisema wiki hii kuwa, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya uzinduzi wa albamu hiyo, utakaofanyika kwenye ukumbi wa klabu ya Msasani, Dar es Salaam, yamekamilika.
Alizitaja albamu hizo kuwa ni ‘Shukrani kwa mpenzi’ na ‘Ndio basi tena’, ambazo alitamba kuwa, zitakuwa moto wa kuotea mbali kutokana na mpangilio wa ala na mashairi.
Jay alisema uzinduzi wa albamu hizo utasindikizwa na waimbaji mahiri wa muziki huo nchini, akiwemo Fatuma Binti Baraka (Bi Kidude), Hashimu Saidi na kundi la Offside Trick 'Wazee wa Bata' kutoka Zanzibar.
Kiongozi huyo wa Five Stars alisema, mashabiki watakaohudhuria uzinduzi huo, watazawadiwa zawadi mbalimbali, zikiwemo kanda za kaseti zenye nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo. Kundi la Five Stars lilizinduliwa Juni mwaka jana na hivi sasa linatamba kwa albamu yao ya kwanza, inayojulikana kwa jina la 'Riziki mwanzo wa chuki'.

Sunday, October 17, 2010

Tambo,mbwembwe, vituko vyatawala pambano la Simba na Yanga


"Kuloga wameloga wao, mechi tumeshinda sisi," hizo zilikuwa kelele za shangwe kutoka kwa mashabiki wa soka wa Yanga baada ya timu yao kushinda bao 1-0 dhidi ya Simba katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.
Mamia ya mashabiki wa klabu hiyo walikimbia mchakamchaka katika mitaa ya Kirumba, wakipita huku na kule na wengine walifurika kwenye baa wakinywa pombe na kushangilia kwa mbinde na staili tofauti ili kujipongeza baada ya ushindi huo.
Furaha ya mashabiki hao ilikuwa kubwa kupindukia kutokana na kushinda mechi, ambayo ilikuwa na homa kubwa kwa timu zote kutokana na kila upande kupania kushinda, ambapo kwa sababu hiyo, wanazi wa klabu hizo wa kutoka Dar es Salaam, waliopo Mwanza na mikoa mengine ya Kanda ya Ziwa, kutupiana makonde.
Hali kabla ya mchezo
Yanga waliwasili jijini Mwanza Ijumaa saa 5:30 asubuhi wakiwa na msafara wa watu 45, kati yao wakiwemo wachezaji 20 na wengine walikuwa viongozi na mashabiki wa klabu hiyo.
Kuwasili kwa timu hiyo kulilipua shangwe kwa mashabiki wao waliokuwa wametangulia na waliopo Mwanza, ambao walikwenda kuipokea timu kwa shangwe na kuisindikiza hotelini na baadaye kuingia uwanja wa CCM Kirumba kwa mazoezi ya siku moja kabla ya mechi.
Yanga, ambao walikuwa wageni wa Simba walipofika uwanjani, walizusha kizaazaa baada ya baadhi ya mashabiki wa Simba waliotaka kuingia kushuhudia mazoezi hayo, kukataliwa kufanya hivyo kwa madai kuwa, walikuwa wanataka kuiba mbinu za wapinzani wao.
Mashabiki wa Yanga walikaa milangoni na wengine majukwaani na walisikika wakiapa kuwa, bora afe mtu kuliko wenzao wa Simba kuingia ndani.
“Nyinyi hamuingii hata kwa nini, tutapigana hadi asubuhi, tokeni wauza chipsi na mayai tunawajua sana hapa, mnajidai babu kubwa," walisikika wakisema wanazi wa Jangwani.
Polisi wa kutuliza ghasia (FFU), ambao walikuwepo nje ya Uwanja wa CCM Kirumba kulinda fedha za tiketi, ambazo zilianza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo,walikaa kimya kutazama tambo hizo, lakini baadaye iliwalazimu kuingilia kati kwa kuwatawanya mashabiki wa Simba baada ya makonde kufumka.
Fujo zilikuwa kubwa na kusababisha wapenzi wengi kukimbia ovyo mitaani baada ya kundi la mashabiki wa Yanga maarufu kama 'Yanga Bomba' kuwasili Mwanza usiku na kwenda moja kwa moja uwanjani, ambako waliwaongezea nguvu wenzao na kufanikiwa kuwashinda manazi wa Simba, ambao baadhi yao waliumizwa.
Jumamosi ilikuwa siku ya mechi yenyewe na homa ilikuwa imepanda maradufu kwa sababu kila baa ilikuwa imefurika mashabiki wa timu hizo waliokuwa wanakunywa pombe na kutambiana hadi baadhi kuonyeshana nguo za ndani.
"Rangi ya kijani na njano haifai kuwa vazi, mimi mwanamke napenda kuvaa nyekundu na nyeupe," alitamba shabiki mmoja mbele ya wenzake wa Yanga wakati wanakula mlo wa mchana, ambapo baadaye alivua jeans na kuonyesha nguo aliyovaa kudhihirisha alichokuwa anakisema.
Walitambiana kwa muda na kisha wakazika tofauti za usimba na uyanga kwa kucheza pamoja nyimbo na ngoma zilizokuwa zinapigwa na mashabiki wa Yanga nje ya Hoteli ya Wendele.
"Wera wera...oya oya mwanangu," alisema Sofia, mwanachama maarufu wa Simba wakati akicheza na kukumbatiana kwa furaha na mashabiki wanawake wa Yanga kuonyesha upendo na kwamba, Simba na Yanga upinzani upo uwanjani, lakini katika mambo mengine wao ni ndugu!
Iliwadia zamu ya uwanjani, ambapo mashabiki wanaokaribia 20,000 walikuwa wamejaaa hadi mechi hiyo ilipoanza. Rangi za kijani, njano, nyekundu na nyeupe za miamvuli, bendera, fulana, trakisuti na mavazi ya aina tofauti zilipamba uwanja huo.
Mashabiki waliimba kwa zamu, Yanga walipokuwa wanacheza, wale wa Simba walijibu mapigo na mara nyingine wote walionekana kuishiwa tambo na kubaki kimya.
Saa 8:50 mchana, wachezaji wa Simba waliingia uwanjani bila ya gari wakitokea upande wa Kaskazini wakiongozwa na kipa Ali Mustafa 'Barthez'. Ilibidi mtu uwe mwepesi kuona 'utundu' wao baada ya kuingia huku wanageuka nyuma na kubadilisha kitendo hicho haraka.
Wote walipita uwanjani na kushangiliwa kwa nguvu kisha waliingia kwenye vyumba vya kuvalia nguo na mara Yanga nao waliwasili kwa mbwembwe. Timu hiyo ikiongozwa na msafara wa magari matatu, iliwasili uwanjani saa 9:22.
Dakika tano baadaye, mbinje kutoka kwa mashabiki wa Yanga zililipuka baada Kocha Mserbia, Kostadin Papic akiwa amevaa suti ya rangi nyeusi, kuingia uwanjani na kuonyesha skafu ya rangi ya kijani na njano iliyoandikwa Yanga. Uso wa kocha huyo ulikuwa umejaa tabasamu.
Saa 10:20 jioni, mechi ilianza na Simba walionekana kama wangeshinda mchezo huo baada ya kulishambulia lango la Yanga kama nyuki na kukosa mabao kutokana na kipa Yaw Berko kusimama imara langoni.
Emmanuel Okwi na Joseph Owino ni wachezaji, ambao hawataisahau mechi hiyo kutokana na kukosa mabao, ambayo yangeipa Simba uongozi wa ligi kuu na tambo dhidi ya wapinzani wao wa jadi.
Dakika ya pili na tatu, Okwi alionekana kuwa tishio kwa ngome ya Yanga baada ya kuuwahi mpira uliookolewa kwa kifua na beki Shadrack Nsajigwa na kupiga shuti, ambalo Berko alilipangua kwa ufundi na kuwafokea mabeki wake.
Berko alionyesha kuwa ni mchezaji bora wa mechi hiyo baada ya kubaki yeye na Okwi na kumfuata kama nyati aliyejeruhiwa na kuuondoa mkwaju wa Mganda huyo na mashabiki wa Simba kubaki wameshika vichwa wakiwa hawaamini kilichotokea.
Kipa huyo alionyesha kuwa habahatishi kuondoa michomo baada ya kuruka juu na kuudokoa mkwaju wa Patrick Ochan, ambao dhahiri ulikuwa unajaa wavuni. Mpira huo ulizaa kona tasa, ambazo Simba walipata tano na walishindwa kuzitumia.
Nafasi nyeti kuliko zote, ambazo Simba watakaa wazililie daima ni ya Owino, aliyepiga mpira nje wakati kipa Berko ameshaangukia upande mwingine huku zikiwa zimebaki dakika sita mtanange kumalizika.
Kwa ujumla, Simba walicheza vizuri dakika 20 za kwanza na ilifuata zamu ya Yanga kutawala mchezo, lakini tatizo kubwa la timu hiyo lilikuwa katika ushambuliaji kwa sababu Jerry Tegete na Nsa Job walishindwa kuwapenya Juma Nyoso, Owino na Maftah waliokuwa wamesimama imara kumlinda Kaseja asipate madhara.
Kupoteza nafasi za wazi za mwanzo kuliwagharimu Simba kwani kipindi cha pili kilikuwa cha Yanga, waliokuwa wanatafuta bao kwa udi na uvumba na kufanikiwa katika dakika ya 70 baada ya Tegete kupenyezewa pande refu na Ernest Boakye na kuitumia pasi hiyo kwa umakini.
Tegete alikimbia kama mashine na kubaki ana kwa ana na Kaseja, ambapo alifumua kiki iliyojaa wavuni kupitia nyavu za juu ya goli. Kwa mwonekano, Kaseja alidhani mpinzani wake angepiga pembeni.
Goli hilo liliwapa nguvu Yanga na kufanya mashambulizi mawili ya haraka, ambayo hayakuzaa matunda. Nsa Job kuna wakati aliwaweka roho juu mabeki wa Simba na Kaseja alicharuka na kumchezea rafu mbaya kwa kumrukia kichwani.
Alionyeshwa kadi ya njano na Simba walijipanga kuonyesha wanataka kushambulia na kupata bao la kusawazisha, lakini haikuwezekana tena baada ya mabeki wa Yanga kujipanga na kuondoa hatari zote.
Ilikuwa zamu ya butua butua kwa kila timu.Mabeki wa Yanga walipiga mpira mbele kwa nguvu na staili ya chogo chemba ilionekana katika mchezo huo kupitia beki Nadir Haroub 'Cannavaro', ambaye aliondoa shambulizi moja namna hiyo na kushangiliwa. Mchezo ulimalizika kwa Yanga kushinda bao hilo pekee la Tegete anayeonekana ni mwiba kwa Kaseja.
Nderemo za Yanga zimeendelea hadi jana kwa baadhi ya mashabiki wao waliotoka Dar es Salaam kubaki jijini Mwanza na kujipongeza kwa vinywaji, lakini mashabiki wachache wa Simba walionekana kukatiza mitaa ya jiji hilo.
Mashabiki wa Msimbazi wa kutoka Dar es Salaam waliobaki Mwanza walikuwa wanyonge, ingawa baadhi yao walionyesha kukomaa kisoka baada ya kuwapongeza wenzao kwa mafanikio hayo.
Yanga wamefikisha pointi 19 zinazowapa uhakika wa kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi kuu na Simba wamebaki nafasi ya pili baada ya kuwa wamejikusanyia pointi 14 katika mechi saba.
Kauli za makocha.
Patrick Phiri wa Simba alisema amesikitishwa kupoteza mechi hiyo muhimu na kufafanua kuwa, anakwenda kujipanga na wachezaji wake kwa ajili ya michezo mingine.
"Inauma maana tumepata nafasi nyingi, lakini tumeshindwa kuzitumia. Wenzetu Yanga wamepata moja na wameshinda, ndio mchezo ulivyo," alisema Phiri.
Akizungumzia waamuzi, kocha huyo alisema hawakuwa na tatizo bali walijitahidi kuhimili presha ya mchezo huo mkubwa.
Kostadin Papic hakuwa na raha kwani alichukizwa kutimuliwa kwenye benchi na mwamuzi wa pembeni. "Sijui nilikosa nini, mimi ni kocha ninayejua kazi yangu, inakuwaje mshika kibendera anitoe," alilalamika Papic na kusema anajua wajibu wa kazi yake kwani ameifanya miaka 24.
Kilichowasibu Simba
Japokuwa wengi walishindwa kujua kwa nini timu hiyo ya Msimbazi ilifungwa, ukweli ni kwamba walikuwa wamejikaza moyoni, kwani pengo la nyota wake Mussa Hassan 'Mgosi', Nico Nyagawa, Uhuru Selemani na Salum Kanoni, ambao ni majeruhi lilichangia kipigo hicho.
Hakuna kificho kwamba wachezaji hao wamekuwa tegemeo la Simba katika kikosi cha kwanza kwa misimu mingi. Uzoefu wa Kanoni haufanani na Haruna Shamte. Santo na Hilary Echesa ni wazuri, lakini Nyagawa naye bado lulu na mzoefu wa kutosha na siasa za Simba na Yanga. Vivyo hivyo kwa Mgosi na Ochan, aliyechezeshwa sehemu ya ushambuliaji. Mgosi amewiva zaidi ya Mkenya huyo.
Yango nao wana pengo la mshambuliaji wa kusaidiana na Tegete, lakini ipo haja ya kuutazama upya ukuta wao kwa vile Cannavaro na Isaack Boakye hawakuwa wanaelewana sana ikilinganishwa na alivyokuwa anacheza pamoja na Wisdom Ndlovu.
Ushirikina pia ni suala, ambalo lilitawala mchezo huo na ndio kilikuwa chanzo cha wanachama wa timu hizo kusukumiana makonde kabla ya mchezo, lakini kama kweli unafanya kazi, basi umeinufaisha Yanga.
Baadhi ya viongozi wa timu hiyo kwa kushirikiana na wanachama wenye uchungu na Yanga, walilinda uwanja wa Kirumba hadi asubuhi kuhakikisha 'dawa' zao hazichezewi na Simba ambao walionekana dhahiri kuchelewa kuzinduka!
Walijifunika shuka asubuhi wakati wenzao wametawala uwanja nao wakawa wanapambana kutaka kwenda kufanya vitu vyao. Wakiwa wenyeji, walikuwa na nafasi ya kuugeuza hata bahari kama walipenda kufanya hivyo.
Simba walikuwa na zaidi ya wiki moja ya kutembeza ‘ndumba’ uwanjani kwa sababu walifika Mwanza mapema wakitokea mikoa ya Tabora na Shinyanga, lakini walijisahau na kuwa bize katika mazoezi ya soka pekee.
Hiyo ni mara ya nane timu hizo kukumbana katika jiji la Mwanza.Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1974, Yanga iliposhinda mabao 2-1 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Nyamagana. Katika mechi za ligi pekee, ilikuwa mara ya nne kukutana. Mashindano mengine waliyokutana ni ya Kombe la Hedex, Tusker na mechi nyingine za kirafiki.

PAPIC: Safari bado ndefu


KOCHA Mkuu wa Yanga, Kostadin Papic amesema licha ya timu yake kuibwaga Simba, bado safari ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu ya Tanzania Bara ni ndefu.
Papic alisema hayo juzi, muda mfupi baada ya Yanga kuichapa Simba bao 1-0 katika mechi ya ligi hiyo, iliyochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini hapa.
Kocha huyo kutoka Serbia alisema, licha ya timu yake kuibuka na ushindi, haikucheza vizuri na atalazimika kuzifanyiakazi dosari kadhaa zilizojitokeza katika mchezo huo.
Alisema kilichoiwezesha timu yake kuibuka na ushindi ni bahati aliyonayo kwa Yanga, lakini alikiri kuwa, wapinzani wao walicheza vizuri zaidi na kupata nafasi nyingi za kufunga mabao.
“Tumeshinda, lakini timu yangu haikucheza vizuri ikilinganishwa na Simba. Kilichotuwezesha kushinda ni bahati na kuitumia vyema nafasi tuliyopata kufunga bao,”alisema.
Naye mshambuliaji Jerry Tegete, aliyeifungia Yanga bao hilo la pekee alisema, kumtungua kipa Juma Kaseja ni kitu cha kawaida katika maisha yake ya soka.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Tegete alisema Kaseja ni kipa wa kawaida na hana jipya ama uwezo wa kuiokoa timu yake isifungwe kama anavyofikiriwa na mashabiki wengi.
"Mimi naona kawaida na wala sina dawa yoyote bali ni soka tu," alisema mchezaji huyo anayeongoza kwa kufunga mabao matano katika ligi kuu ya msimu huu baada ya Yanga kucheza mechi saba.
Tegete pia alitangaza hali ya hatari kwa wapinzani wao wote wa ligi hiyo, ambapo alisema kila timu watakayocheza nayo, watailamba mabao na salamu hizo zimeanzia kwa Simba.
Wakati huo huo, baba mzazi wa mchezaji huyo, John Tegete amesema amekoshwa na mtoto wake kwa kufunga bao katika mechi ya watani wa jadi, lakini alimtaka asibweteke na mafanikio hayo.
"Hakuna siku, ambayo nimefurahi kama leo, mwanangu kufunga goli ni mafanikio kwake, zawadi ninayompa ni kumuongezea upendo kwa sababu ndio kitu cha msingi katika maisha ya mtoto," alisema.
John Tegete ndiye meneja wa uwanja wa CCM Kirumba wa Mwanza na inaaminika ni mnazi wa kutupwa wa Yanga. Pia aliwahi kuchezea timu ya Pamba kabla ya kustaafu soka.

Simba, Yanga zavunja rekodi

MSHAMBULIAJI Jerry Tegete (kulia) wa Yanga akiwa na baba yake, John Tegete mara baada ya pambano la ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Simba kumalizika juzi mjini Mwanza. Yanga ilishinda bao 1-0.

PAMBANO la watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga lililochezwa juzi kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, limeingiza sh. milioni 138.
Akitangaza mapato hayo jana, Mkurugenzi wa Fedha wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Ahmed Naheka alisema, fedha hizo zilipatikana kutokana na idadi ya mashabiki 25,000 walioingia uwanjani kwa kulipa kiingilio.
Kufuatia kupatikana kwa kiasi hicho cha fedha, Naheka alisema kila klabu ilipata mgawo wa zaidi ya sh. milioni 33 wakati makato mengine yalikwenda TFF, Chama cha Soka cha Mwanza (MRFA) na uwanja.
Naheka alisema mapato hayo ni kadirio la juu kwenye uwanja huo na yamevunja rekodi ya mapato yaliyopatika mwaka 2007 kati ya timu hizo, ambapo sh. milioni 100 zilipatikana.
Mkurugenzi huyo wa fedha wa TFF alipongeza usimamizi mzuri wa mechi hiyo uliofanywa kwa pamoja na MRFA kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ambao alisema ndio uliowezesha kupatikana kwa mapato hayo.
Katika mechi hiyo iliyoshuhudiwa na maelfu ya mashabiki, Yanga iliendeleza ubabe wake kwa Simba baada ya kuichapa bao 1-0.
Ushindi huo ulikuwa wa pili kwa Yanga dhidi ya Simba katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Yanga pia iliichapa Simba mabao 3-1 katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani iliyochezwa Agosti mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena keshokutwa wakati Simba itakapomenyana na AFC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba; Mtibwa itavaana na Azam kwenye uwanja wa Manungu, Morogoro; Polisi itaikaribisha African Lyon mjini Dodoma wakati Ruvu Shooting itacheza na Majimaji mjini Morogoro.
Yanga wanatarajiwa kuteremka tena dimbani Alhamisi kumenyana na JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro.

Thursday, October 14, 2010

DIDA' Mtangazaji wa radio aliyejitosa kwenye muziki wa mipasho


JINA la Khadija Shaibu 'Dida' si jina geni kwenye masikio ya mashabiki wa muziki wa taarab, hasa wanaosikiliza vipindi vya muziki huo kupitia kwenye vituo mbalimbali vya radio nchini.
Ni mtangazaji maarufu na mwenye mbwembwe nyingi kila anapotangaza kipindi cha muziki huo kupitia kituo cha radio cha Times FM. Na sasa ameamua kuwa mwimbaji wa muziki huo, ambao ulianza kumvutia tangu akiwa mdogo.
Umaarufu wa Dida, mama wa mtoto mmoja, mwenye umbo dogo,lugha ya tashtiti na yenye mvuto wa aina yake, tayari ameshaipua kibao kimoja cha muziki huo kinachojulikana kwa jina la ‘Waniache miaka 800’.
Dida alikizindua kibao hicho mwishoni mwa wiki iliyopita katika onyesho lililofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Travertine iliyopo Magomeni, Dar es Salaam, akisindikizwa na kundi maarufu la muziki huo la Jahazi.
Akizungumza na mwandishi wa makala hii hivi karibuni mjini Dar es Salaam, Dida alisema ameamua kujitosa kwenye muziki huo kutokana na mapenzi makubwa aliyonayo katika fani hiyo.
"Huwezi kuamini, katika utoto wangu nilikuwa sipendi kabisa taarab na ilikuwa haiko kwenye damu, lakini baada ya kuwa mtangazaji, hasa wa kipindi cha taarab, nimetokea kuupenda tu,”alisema Dida."Nimeona kwa vile nimepata uzoefu wa kutosha kutokana na kuutangaza kwa muda mrefu muziki huo, nami niachie tungo yangu ili kujipima uwezo wangu," aliongeza.Awali, Dida alipanga kumshirikisha kiongozi wa kundi la Jahazi, Mzee Yusuph katika kuimba wimbo huo, lakini mpango huo ulikufa kimya kimya na kuamua kuuimba yeye mwenyewe."Nilitaka kumshirikisha Mzee Yusuph kwa sababu bila ya unafiki,yeye yupo juu kwa sasa. Pia ndiye aliyenishauri mambo mengi hadi nikafanikisha kutunga wimbo huo," alisema.Dida alisema anaamini wimbo huo utafanya vizuri na unaweza kuwa wimbo bora wa mwaka wa taarab.Mtangazaji huyo alijigamba kuwa, wimbo huo umesheheni vionjo vingi na siku ya uzinduzi alisindikizwa na kundi zima la Jahazi linalotamba na albamu yao ya sita ya 'My Valentine'.Akizungumzia kazi yake ya utangazaji, Dida alisema kwake ni kipaji alichojaliwa kuwa nacho na Mwenyezi Mungu na alibaini kuwa nacho baada ya kumaliza masomo ya sekondari."Utangazaji kwangu ni kipaji nilichokipata ukubwani, nakumbuka nilipokuwa mdogo, sikuwa na kipaji chochote, hata mimi nashangaa, sielewi ilikuwaje," alisema.Amemtaja mmoja wa watangazaji waliomvutia na kumfanya ajitose katika fani huyo kuwa ni marehemu Amina Chifupa 'Mpakanjia', aliyejizolea umaarufu mkubwa enzi za uhai wake kupitia kituo cha radio cha Clouds.Kupitia kazi yake hiyo, Dida alisema amejikuta akipata maadui wengi, hasa wanawake wanaodhani kuwa anawapiga vijimbe anapokuwa akiendesha kipindi chake.Alisema baadhi ya wanawake hao humuandama kwa matusi kwa kumtumia ujumbe mfupi wa maneno kupitia simu yake ya mkononi, ambao anakiri kuwa, mara nyingi humuathiri kisaikolojia."Usione hivi, navumilia mambo mengi, tangu nianze kutangaza, nimejikusanyia maadui kibao, wengi ni wanawake wenzangu, lakini hiyo ni changamoto kwangu na nitazidi kusonga mbele," alisema.Dida alisema maneno yake wakati anapotangaza kipindi cha mipasho hayalengi kumchafua mtu ama kumpiga vijembe yeyote, isipokuwa ni katika kukiboresha na kuwapa burudani wasikilizaji wake.Mwanamipasho huyo amelitaja tukio ambalo hawezi kulisahau katika maisha yake kuwa ni la kuvumishiwa kuwa anajihusisha na dawa za kulevya, jambo ambalo amekana katakata kuhusika nalo."Siwezi kuusahau uvumi huo katika maisha yangu kwa sababu ulilenga kunichafua, lakini yote namuachia Mungu, najua atawabainisha wote walionienezea uvumi huo," alisema.Amewaasa waimbaji chipukizi wa taarab nchini kuwa, watunge nyimbo zenye maadili na zenye kuleta ujumbe kwa jamii na waachane na majungu ili waweze kusonga mbele.Amewashauri pia watangazaji wenzake, wawe na ushirikiano , wapendane na wasitupiane vijembe visivyo na msingi ili waweze kuendeleza taaluma yao hiyo.Dida alizaliwa mwaka 1982, katika Hospitali ya Ocean Road, mjini Dar es Salaam. Alipata elimu ya msingi katika shule ya Ubungo na sekondari ya Makongo, Dar es Salaam. Kidato cha tano na sita alisoma mkoani Tanga na baada ya hapo alijiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari cha Dar es Salaam (DSJ). Mwanamama huyo hajaolewa, lakini anaye mtoto mmoja na anaishi Kijitonyama, Dar es Salaam.

'Wasanii wa kiume wanawadhalilisha wenzao wa kike'


KIONGOZI wa bendi ya muziki wa dansi ya Twanga Pepeta International, Luiza Mbutu amedai kuwa, wasanii wa kiume wamekuwa chanzo kikubwa cha kudhalilishwa kwa wenzao wa kike nchini.
Luiza alitoa madai hayo wiki hii katika semina ya Jukwaa la Sanaa, iliyofanyika mwanzoni mwa wiki hii kwenye ukumbi wa ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Ilala, Sharrifu Shamba, Dar es Salaam.
Alisema hali hiyo imekuwa ikisababisha wasanii wa kike, hasa wacheza shoo wa bendi mbalimbali, waonekane hawana maadili mema katika jamii na washutumiwe kwa kuwadhalilisha wanawake wenzao.
Luiza alisema hali imekuwa mbaya kiasi kwamba wasanii wa kike wamejikuta wakifanya mambo kinyume cha maadili ili kukidhi matakwa ya wasanii wa kiume na baadhi ya wapenzi wa muziki wa dansi hapa nchini.
Akitoa mfano wa udhalilishaji huo, Luiza alizungumzia tabia chafu ya wapenzi wa muziki wa dansi kuwatuza fedha wanenguaji wa kike wawapo kwenye maonyesho kwa kuwawekea kwenye matiti yao au makalio, kitendo alichokiita kuwa ni cha kidhalilishaji.
“Wanenguaji wa kiume wamekuwa wakituzwa fedha kwa kupewa mikononi au mifukoni, lakini wale wa kike wamekuwa wakiwekewa kwenye matiti na makalio, kitu ambacho kimekuwa ni cha kiudhalilishaji sana,” alilalamika Luiza.
Aliitaja pia tabia ya wanamuziki wa kiume kwenye bendi kuponda mawazo ya wenzao wa kike, hasa wanapotaka kutunga nyimbo, hali ambayo imekuwa ikisababisha wawe wakipitisha nyimbo zao pekee na kuwaacha nyuma wanawake kimaendeleo.
Kiongozi huyo wa Twanga Pepeta pia alilalamikia baadhi ya wazazi, ambao wamekuwa wakiwakataza watoto wao wa kike kushiriki kwenye shughuli za sanaa, hivyo kuwafanya wawe wakitoroka usiku wa manane na kushindwa kurudi majumbani baada ya kuomba hifadhi kwa wanaume na hivyo kuishia kupata mimba zisizotarajiwa na watoto wa mitaani.
Wakichangia mada ya udhalilishaji, baadhi ya wachangiaji walilalamikia vitendo vya rushwa ya ngono, ambavyo walidai kuwa vimekuwa vimekithiri na kuwadhalilisha wasanii wa kike.
Walisema wasanii wengi wa kike kila wanapohojiwa na vyombo vya habari, wamekuwa wakilalamikia rushwa ya ngono, wanazoombwa na wenzao wa kiume waliokwishapata umaarufu nchini pamoja na wakuzaji wa muziki.

Simba, Yanga zaanza kuviziana nje ya uwanjaWAKATI homa ya pambano la watani wa jadi wa soka nchini, Simba na Yanga ikiwa imeshaanza kupanda, viongozi wa klabu hizo wamekuwa katika mikakati kabambe, kila upande ukipania kuibuka na ushindi.
Timu hizo kongwe nchini zinatarajiwa kuteremka dimbani keshokutwa katika mechi ya ligi kuu ya Tanzania Bara, itakayochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Homa ya pambano hilo ilianza kupanda wiki iliyopita baada ya viongozi wa klabu hizo kuwawekea ulinzi mkali wachezaji wao waliokuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kilichokuwa kikijiandaa kumenyana na Morocco.
Hofu ya viongozi wa klabu hizo ilikuwa huenda upande mwingine ungetinga kwenye kambi hiyo kwa lengo la kuwashawishi wachezaji wao wacheze chini ya kiwango.
Hilo lilijidhihirisha wakati wachezaji wa Yanga walipofika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kushuhudia mechi ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Afrika za mwaka 2012 kati ya Taifa Stars na Morocco. Katika mechi hiyo, Taifa Stars ilichapwa bao 1-0.
Viongozi wa Yanga waliwawekea wachezaji wa timu hiyo ulinzi mkali wakati walipokuwa wakiingia na kutoka kwenye uwanja huo ili kuhakikisha hawafanyi mazungumzo na mtu yeyote.
Ulinzi huo uliongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya klabu hiyo, Mohamed Bhinda, Meneja wa timu hiyo, Emmanuel Mpangala na Kocha Mkuu, Kostadin Papic. Kazi ya viongozi hao ilikuwa kuhakikisha wachezaji hao hawapati nafasi ya kuzungumza ama kuonyeshana idhara na mtu yeyote.
Mbali na kuwawekea ulinzi huo wachezaji wao, mzozo mkubwa ulizuka baina ya viongozi wa klabu hizo mbili baada ya mchezo huo, kila upande ukitaka kuwachukua wachezaji wao waliokuwemo kwenye kikosi cha Stars.
Bhinda alitaka kuwachukua Shadrack Nsajigwa, Stephano Mwasika na Nurdin Bakari wakati viongozi wa Simba walitaka kuwachukua Juma Kaseja,Mohamed Banka na Haruna Shamte.
Hata hivyo, mzozo huo ulizimwa na viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ambao waliwazuia wachezaji hao kuondoka hadi siku iliyofuata baada ya kambi ya Stars kuvunjwa.
Vituko vingine vilivyopamba moto kwa klabu hizo ni kuwepo kwa imani za ushirikina. Tayari klabu hizo mbili zimeshaunda kamati za ‘uchawi’ zinazoongozwa na wazee, kila upande ukipania kutumia imani hizo kuibuka na ushindi.
Wazee wa Yanga walikutana mwishoni mwa wiki iliyopita makao makuu ya klabu hiyo, mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es Salaam kwa lengo la kupanga mbinu za kuibuka na ushindi dhidi ya mahasimu wao.
Moja ya mikakati iliyoamualiwa na wazee hao wa Yanga ni kuwalisha yamini wachezaji wao, ili iwapo yeyote kati yao ataihujumu, adhurike. Mpango huo umepangwa kufanyika kabla ya timu kwenda Mwanza. Lakini bado haijajulikana iwapo tayari wachezaji hao wameshalishwa yamini.
Uamuzi wa wazee wa Yanga kuwalisha yamini wachezaji wao umekuja baada ya kubainika kuwa, baadhi yao wana uhusiano wa karibu na viongozi wa Simba, hasa wanachama wa kundi la Friends of Simba.
Yanga imeweka kambi Bagamoyo mkoani Pwani kwa ajili ya kujiandaa kwa pambano hilo. Kambi ya timu hiyo ipo chini ya ulinzi mkali wa baadhi ya wanachama maarufu kwa jina la ‘Makomandoo’.
Tayari baadhi ya wanachama na wafanyabiashara wenye mapenzi mema na Yanga wameahidi kutoa zawadi mbalimbali za fedha kwa wachezaji wao iwapo wataibuka na ushindi dhidi ya Simba.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alijigamba wiki hii kuwa, maandalizi yao kwa ajili ya pambano hilo yanakwenda vizuri na kusisitiza kuwa, hawaoni kitakachowakwamisha kuibuka na ushindi katika mechi hiyo.
“Iwe, isiwe lazima mnyama afe tena safari hii,” alijigamba msemaji huyo wa Yanga.
Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha alisema wameshabaini njia zote zilizokuwa zikitumiwa na Simba kuwaangamizi na kuziziba barabara.
“Ile janja waliyokuwa wakiitumia Simba kutufunga, tumeshaibaini, sasa kazi ni moja tu, lazima mnyama afe,”alisisitiza.
Kwa upande wa Simba, timu hiyo iliweka kambi mjini Tabora kwa ajili ya kujiandaa kwa pambano hilo kabla ya kwenda Shinyanga, ambako ilicheza mechi moja ya kirafiki dhidi ya Kahama United na kuibuka na ushindi.
Maandalizi ya Simba kwa ajili ya mechi hiyo yamekuwa yakifanyika kimya kimya huku wafadhili mbalimbali wakiwa wamewaahidi wachezaji kitita kikubwa cha fedha iwapo wataibuka na ushindi katika mechi hiyo.
Wafadhili hao, wakiongozwa na kundi la Friends of Simba wamepania kuiona timu yao ikishinda, baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Yanga katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani, iliyochezwa Agosti mwaka huu.
Hali ndani ya klabu hiyo kwa sasa ipo shwari baada ya awali kuripotiwa kuzuka kwa tofauti kati ya viongozi na kundi la Friends of Simba mara baada ya kumalizika kwa tamasha la ‘Simba Day’.
Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alitamba kuwa, maandalizi yao hadi sasa yanakwenda vizuri na kusisitiza kuwa, ushindi ni lazima katika mechi ya keshokutwa.
“Tulifungwa na Yanga katika mechi ya kuwania ngao ya hisani kwa bahati mbaya, lakini hilo halitatokea tena Mwanza, lazima tutoke uwanjani na pointi zote tatu,”alisema.

SIMBA: Tupo Gado!


KLABU ya Simba imetamba kuwa, haina wasiwasi na pambano lao la ligi kuu ya Tanzania Bara dhidi ya Yanga, litakalochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ alisema mjini Dar es Salaam jana kuwa, kikosi chao kimekamilika katika kila idara na kimejiandaa vyema kwa pambano hilo.
Kaburu alisema mchezaji mwingine aliyekuwa majeruhi, kipa Ali Mustafa ‘Barthez’, amesharipoti kambini mjini Mwanza baada ya kupona maumivu yaliyokuwa yakimsumbua.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema, nahodha Nico Nyagawa alitarajiwa kujiunga na kambi ya timu hiyo jana, ambayo imekuwa ikifanya mazoezi asubuhi na jioni kwenye Uwanja wa CCM Kirumba.
Alisema wachezaji pekee, ambao hawapo kambini ni beki Salum Kanoni na mshambuliaji, Uhuru Selemani wanaoendelea kupatiwa matibabu mjini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kaburu, baadhi ya viongozi wa klabu hiyo pamoja na wanachama wa kundi la Friends of Simba wanatarajiwa kuwasili Mwanza kesho kwa ndege kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye timu hiyo.
Kaburu alisema, mara baada ya kutua Mwanza, kundi hilo la viongozi na wanachama hao watakutana na wachezaji kwa ajili ya kupanga mikakati ya ushindi katika mechi hiyo.
Naye Ofisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo alitamba kuwa, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mechi hiyo yamekamilika na kinachosubiriwa na kuwashikisha adabu wapinzani wao.
Wakati huo huo, habari zilizopatikana jana jioni zilieleza kuwa, mchezaji Mussa Hassan ‘Mgosi’ ameumia mazoezini na anapatiwa matibabu kwenye hospitali ya Sekou Toure ya mjini Mwanza.

Vibopa Yanga watenga mil 40 kuiua Simba
WAKATI homa ya pambano la watani wa jadi wa soka nchini ikizidi kupamba moto, baadhi ya wafanyabiashara matajiri wa klabu ya Yanga wametenga sh. milioni 40 kwa ajili ya kuiua Simba.
Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa, fedha hizo zitatolewa kwa wachezaji wa timu hiyo iwapo watashinda Simba katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara kati yao utakaochezwa keshokutwa.
Mechi hiyo inayosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka nchini, inatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, Simba wakiwa wenyeji.
Kwa mujibu wa habari hizo, wafanyabiashara hao walikutana na viongozi wa klabu hiyo pamoja na wachezaji wa Yanga Jumatatu iliyopita kwenye hoteli ya Kiromo Resort iliyopo Bagamoyo mkoani Pwani.
Katika mkutano huo, viongozi pamoja na wafanyabiashara hao, waliwaeleza wachezaji umuhimu wa kushinda mechi hiyo na pia kuwapatia kitita hicho cha fedha iwapo watawabwaga watani wao.
Ujumbe wa wafanyabiashara hao wenye mapenzi na Yanga, uliongozwa na Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Davis Mosha na mwanachama, aliyejulikana kwa jina la Majid Seif.
Kufuatia ahadi hiyo, wachezaji wa Yanga waliwahakikishia viongozi na wafanyabiashara hao kuwa, watapigana kufa au kupona uwanjani ili kuhakikisha wanashinda mechi hiyo na kupata pointi zote tatu.
Hata hivyo, hadi jana haikuweza kufahamika iwapo mfadhili mkuu wa klabu hiyo, Yusuf Manji atatoa zawadi yoyote ya pesa kwa wachezaji iwapo watashinda mechi hiyo.
Lakini habari za uhakika kutoka kwa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo zimeeleza kuwa, Manji huenda akaenda Mwanza keshokutwa asubuhi kwa ajili ya kushuhudia mechi hiyo.
Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kutua Mwanza kati ya kesho na keshokutwa asubuhi kwa ajili ya mechi hiyo, kikiwa chini ya ulinzi mkali wa wanachama wanaojulikana kwa jina la ‘makomandoo’.
Yanga imeweka kambi Bagamoyo kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo na imekuwa ikifanya mazoezi asubuhi na jioni kwenye uwanja wa Mbegani.
Ofisa Habari wa klabu hiyo, Louis Sendeu alisema jana kuwa, kikosi chao chote kipo fiti na hakuna mchezaji majeruhi. Alitamba kuwa, ushindi katika mechi hiyo ni muhimu na wa lazima kwao.
Kufuatia wachezaji wote kuwa fiti, Sendeu alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Kostadin Papic ameshindwa kikosi kipi kianze katika mechi hiyo kwa vile kila mchezaji ana uchu wa kucheza.
Sendeu alisema mashabiki kadhaa wa timu hiyo wanatarajiwa kuondoka Dar es Salaam kwa mabasi kati ya leo na kesho kwenda Mwanza kwa ajili ya kushuhudia pambano hilo.
Pambano hilo litakuwa la pili kuzikutanisha Simba na Yanga katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Zilipokutana Agosti mwaka huu katika mechi ya kuwania Ngao ya Hisani, Yanga iliichapa Simba kwa penalti 3-1.